Kuutazama Ulimwengu
Utata Watokea Wapi?
Wanamageuzi wengi hudhani kwamba viumbe vya kale vilivyokuwa hai vilikuwa sahili lakini vilipata msukumo wa uteuzi wa asili na vikatatanika zaidi na zaidi kupitia muda wa wakati. Uchunguzi wa karibuni umeshindwa kupata msukumo kama huo kuelekea utata wa juu zaidi. Dakt. Dan McShea, mtaalamu wa biolojia ya masalio ya viumbe vya kale, alichunguza masalio ya uti wa mgongo wa mamalia wengi; uchunguzi mwingine ulizingatia masalio ya jamii ya konokono. Hakuna uchunguzi uliopata uthibitisho wowote wa msukumo wa kimageuzi wenye kuelekea utata mkubwa zaidi. Wala uchunguzi huo haukupata kwamba utata mkubwa zaidi ulileta mafaa kwa kuokoka. Kulingana na The New York Times, wastadi wasema kwamba magunduzi hayo “yatashangaza wanabiolojia wenye kupendelea kufikiri kwa mielekeo hiyo.” Times lasema hivi: “Kulingana na Dakt. McShea, wazo la misukumo kuelekea utata yaweza kuwa zaidi wonyesho wa tamaa ya wanasayansi ya kuona maendeleo fulani katika mageuzi badala ya wonyesho wa ukweli wa kibiolojia.”
Mazoezi na Umri
Je! kwaweza kuwa ni kuchelewa mno kuanza mazoezi? Si kulingana na uchunguzi uliofanywa hivi karibuni katika mashariki mwa United States. Uchunguzi wa watu zaidi ya 10,000 ulipata kwamba watu waliongezea wastani wa kuishi kwao hata wawe walikuwa na umri gani walipoanza mazoezi “yenye nguvu kidogo.” Wale waliokuwa na umri wa kati ya miaka 45 na 54 walipoanza mazoezi walinufaika zaidi, wakiendeleza wastani wa kuishi kwao kwa miezi yapata kumi. Kile kikundi cha miaka 65 hadi 74 kiliongeza miezi sita kwa maisha yao, na wale wa 75 hadi 84 walifanya maendeleo ya miezi miwili. Dakt. Ralph S. Paffenbarger, aliyeongoza uchunguzi huo, alikazia kwamba hayo yalikuwa wastani; kwa hiyo, watu fulani mmoja-mmoja walinufaika sana kutokana na mazoezi hayo kuliko wengine. Manufaa kubwa ilionekana kuwa ni kuzuia maradhi ya moyo. Hata hivyo, wale waliofanya mazoezi hawakuwa na mwelekeo sana wa kufa kutokana na matatizo mengine vilevile.
Mifupa ya Simba-Milia
Uhitaji mkubwa wa mifupa ya simba-milia ya kutumiwa katika dawa za kienyeji za Mashariki unatisha idadi ya simba-milia inayoendelea kupunguka ulimwenguni, lasema gazeti la kitiba la Uingereza The Lancet. Zijapokuwa jitihada za kimataifa za kukomesha biashara ya viungo vya simba-milia, mifupa ya simba-milia inauzwa sana katika divai, dawa, na dawa za kunywa (dawa za unga-unga zilizochanganywa na asali au maji ya sukari). Katika 1991 pekee, inasemekana kwamba nchi moja ya Esia ilisafirisha nje katoni 15,079 za tembe, kilogramu 5,250 za dawa za kunywa, na chupa 31,500 za divai zenye mifupa ya simba-milia. Idadi inayobaki ya simba-milia ulimwenguni pote inakadiriwa kuwa 6,000 pekee.
Tatizo la Jinsia
“Mara nyingi katika Ulimwengu wa Tatu, haifai hata kuishi maisha ya mwanamke,” ukaanza mfululizo mmoja wa ripoti katika The Washington Post. Maripota wa Post, baada ya kuhoji makumi ya wanawake katika sehemu maskini katika Afrika, Esia, na Amerika ya Kusini, walipata kwamba “utamaduni, dini na sheria mara nyingi huwanyima wanawake haki za kibinadamu za msingi na nyakati nyingine huwashusha kuwa nusu-binadamu.” Kwa kielelezo, katika kijiji kimoja cha Himalaya, wanawake walifanya asilimia 59 ya kazi, wakifanya kazi ngumu kufikia muda wa saa 14 kwa siku na mara nyingi wakibeba mizigo yenye uzito wa kushinda uzito wao wenyewe mara 1.5. Uchunguzi mmoja ulipata kwamba “baada ya kushika mimba . . . mara mbili au tatu, nguvu zao huisha, huwa wanyonge, na wakifikia miaka ya mwisho-mwisho ya thelathini wao hukwisha kabisa, huwa wazee, na kuchoka, na hufa upesi baadaye.” Mara nyingi wasichana hupewa chakula kidogo, huondolewa shuleni na kufanyizwa kazi katika umri wa mapema, na kutoshughulikiwa kiafya jinsi wavulana wanavyoshughulikiwa. Wanawake wengi huua vitoto vya kike, wakiviona kuwa vyenye gharama kubwa. Maripota hao walitaja kwamba katika sehemu za mashambani za kusini mwa India, njia ya kawaida ya kuua watoto ni kumwaga mchuzi moto ndani ya umio wa mtoto. Ofisa mmoja wa polisi alijibu hivi alipoulizwa kama uhalifu kama huo ulitozwa adhabu: “Kuna mambo yenye umuhimu zaidi. Visa vichache sana huripotiwa kwetu. Ni watu wachache sana wanaojali.”
Mwezi Ulio Muhimu
Kwa ile orodha yenye kuvutia ya mambo yanayofanya Dunia-sayari ifae kabisa kwa uhai, inaonekana wanastronomia watalazimika kuongeza kitu kingine: Mwezi. Kimulikaji hicho chetu chafanya mambo mengi zaidi ya kuandaa tu nuru nzuri ya usiku angani na kusababisha kujaa na kupwa kwa bahari. Kulingana na uchunguzi wa kompyuta uliofanywa na wanastronomia Wafaransa, mwezi husaidia pia kudhibiti mwinuko wa dunia, yaani kadiri ya mwinuko wa dunia katika mhimili wayo unaozunguka. Mars (Mihiri), ambayo haina kimulikaji kikubwa hivyo, kwa wazi imesonga kidogo katika kadiri ya mwinuko kati ya digrii 10 na 50 kwa muda ambao umepita. Ukosefu huo wa uthabiti labda umesababisha mabadiliko ya msiba sana ya hali ya hewa, ncha zayo zikiyeyuka kisha kuganda tena. Uchunguzi huo wa kompyuta ulifunua kwamba bila mwezi, ambao una uvutano wenye kuzuia, mwinuko wa dunia huenda ungesonga kufikia digrii zapata 85 hivi. Kwa hiyo, wanastronomia Wafaransa wanakata kauli kwamba: “Mtu aweza kuona mwezi kuwa kisawazisha hali ya hewa kwa ajili ya Dunia.”
Afrika Kusini Yashughulikia Tatizo la Kutenda Watoto Vibaya Kingono
Kwa miaka mitano tu, idadi ya watoto walionajisiwa katika Afrika Kusini iliongezeka zaidi ya mara mbili, hiyo ni kulingana na gazeti la Johannesburg The Star. Gazeti hilo laripoti kwamba kulikuwa na visa 1,707 vya kunajisi watoto vilivyoripotiwa katika 1988; kufikia 1992 hesabu hiyo ilikuwa imeongezeka sana kufikia 3,639. Waziri wa Sheria Kobie Coetsee alitaja tarakimu hizo alipokuwa akifungua mahakama ya kwanza ya nchi hiyo iliyokusudiwa ishughulikie kimahususi kesi za unajisi, iliyo katika Wynberg, Cape Town. Alitaja kwamba alitumaini mahakama hiyo ingeshughulikia kesi hizo haraka na kwa njia yenye huruma. Naibu wa Mkuu wa Sheria Natalie Fleischack alisema kwamba jambo hilo jipya litaondoa baadhi ya aibu na tahayari ambazo walionajisiwa hupata mara nyingi wakati wa mashtaka na pia litasaidia katika “kupona kisaikolojia.”
Kasoro za Kuzaliwa Zenye Kutilika Shaka Katika Hangari
Katika mji mdogo ulioko kusini-magharibi mwa Hangari, idadi kubwa ya watoto walizaliwa wakiwa na kasoro zilizo mbaya sana katika 1989 na 1990. Kwa kweli, watoto 11 kati ya 15 waliozaliwa katika kipindi hicho waliugua magonjwa kama ugonjwa wa Down na kasoro za mapafu, moyo, na njia ya uyeyushaji wa chakula. Kiwango hicho kilikuwa mara 223 kuliko sehemu nyingine zote za nchi. Andrew Czeizel, akiwa na kikundi cha wanasayansi Wahangari na Wajerumani, walizingatia kitu ambacho kingeweza kuwa kisababishi: triklorfoni, dawa ya kuua wadudu. Inaonekana kwamba katika 1988 shamba la kufuga samaki la kijiji hicho lilianza kutumia njia mpya ya kutumia triklorfoni: samaki walichovywa ndani ya kemikali isiyochanganywa na maji na kurudishwa majini wakiwa na dawa hizo kwa kiwango cha mara elfu moja kuliko kiasi cha juu zaidi kilichodokezwa. “Ni sumu,” asema Czeizel kuhusu triklorfoni. Kulingana na gazeti New Scientist, hiyo hubadilika polepole kuwa kemikali nyingine ambayo ni hatari zaidi mara mia moja na huweza kupitia kondo ya nyuma ya mama na kuingia katika kijusi.
Yatafsiriwa na Kompyuta
Katika jambo lililotajwa kuwa la kwanza, kompyuta hivi karibuni iliandaa tafsiri ya mazungumzo ya simu kati ya watafiti katika Japani, Ujerumani, na United States. Walipokuwa wakisema, wanasayansi katika Kyoto, Munich, na Pittsburgh walitumia tu msamiati wao kwa maneno 550 yatumiwayo kila siku na maneno zaidi 150 ya kipekee yanayotoka katika uwanja wa mikutano na kujiandikisha katika hoteli. Hayo ndiyo maneno ya pekee ambayo programu ya kompyuta iwezayo kuelewa na kutafsiri. Gazeti Süddeutsche Zeitung la Munich laripoti kwamba wanasayansi “wanafanya kazi pamoja kuunda kompyuta ya tafsiri itakayoshughulikia kuandikishwa kwa mikutano kwa washiriki wanaotoka nchi mbalimbali na kujibu maswali rahisi.”
Baa ya Wabuddha
Katika jitihada ya kurudisha Ubuddha kwa kundi lao lenye kutangatanga, makuhani wa Buddha wamefungua baa katika Osaka, Japani. “Katika nyakati za kale,” Asahi Evening News lilimnukuu mmoja wa makuhani akisema, “watu wa aina zote walikuwa wakikusanyika katika mahekalu wakiongea huku wakila na kunywa. Mamia ya miaka ilipopita, Ubuddha ukajitenga na watu.” Makuhani kumi na watano, wengi wao wakiwa wachanga, huchukua zamu wakiwa wauzaji katika baa na kunywa pamoja na wateja. “Baa yetu ni hekalu halisi ambako unaweza kuongea kinaga-ubaga na kuhani,” asema meneja. Uvumba wafukizwa na ishara za kidini zaning’inia ukutani. Kuna muziki wa roki unaocheza kichini-chini.
Divai Kidogo kwa Moyo Wako
Matumizi ya kiasi ya divai nyekundu yaweza kupunguza hatari ya kupatwa na maradhi ya moyo. Kwa muda fulani wanasayansi wameshangazwa na jambo ambalo limekuja kuitwa “Tamathali ya Ufaransa.” Ingawa ulaji wa Mfaransa wa kawaida huwa na mafuta mengi ambayo hutokeza maradhi ya moyo, Wafaransa wana mojapo viwango vidogo zaidi vya vifo vinavyotokana na maradhi ya moyo katika nchi zenye kuendelea kiviwanda za Magharibi. Kulingana na gazeti la Paris Le Figaro, lililokuwa likirejezea ripoti zilizokuwa zimechapishwa katika jarida la kitiba la Uingereza The Lancet, wanasayansi waamini kwamba jambo hilo laweza kuhusika na divai nyekundu ambayo Wafaransa kwa kawaida hunywa pamoja na milo yao. Mifanyizo ya asidi ambayo huwa katika divai nyekundu, inayoitwa fenoli, imeonyeshwa kuwa huzuia ile inayoonwa kuwa kolesteroli mbaya (LDL) isizibe mishipa ya arteri kwa kujaza mafuta yanayotokeza maradhi ya moyo. Le Figaro laongezea kwamba fenoli hizo ni sehemu ya divai isiyolevya na kwamba kiasi cha kileo kinachopita robo ya lita kila siku hutokeza madhara zaidi kuliko mazuri.