Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g93 10/22 kur. 12-16
  • Kitumbuizo Kilikuwa Mungu Wangu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kitumbuizo Kilikuwa Mungu Wangu
  • Amkeni!—1993
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Kuanza Maisha ya Sarakasi
  • Kugeukia Mchezo wa Vaudeville
  • Ndoa
  • Kutoa Maonyesho Katika Nchi Nyinginezo
  • Kurudi Australia
  • Mwito wa Dini
  • Pigano Langu Dhidi ya Kweli
  • Kusaidiwa na Mkristo Halisi
  • Baraka Tele
  • Baraka za Yehova Zimenitajirisha
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2015
  • Maisha Yangu Katika Sarakasi
    Amkeni!—2004
  • Je! Ilifaa Nijitahidi Kushinda Watu Wote?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1977
  • Niliacha Kupiga Watu Barabarani Nikawa Mhudumu Mkristo
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1977
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1993
g93 10/22 kur. 12-16

Kitumbuizo Kilikuwa Mungu Wangu

VIFIJO vyenye sauti kubwa vilivyoendelezwa vilinipendeza sana. Vilinichangamsha sana, vikifanya ule muda wa saa nyingi za mazoezi ufae. Nilikuwa mrukaji wa vifito vya kupembea katika mchezo wa mazoezi ya viungo, na nilisisimuliwa sana na ufanisi.

Sehemu ya wonyesho wangu ilikuwa pia kuruka na kupinduka hewani juu ya ndovu, kusimama kwa kichwa changu kwenye ufito unaosimamia mgongo wa mtu mwingine kwa njia iliyo hatari, ili nifanye wonyesho mgumu wa kiinimacho, na kusababisha mpasuko wa vicheko kutoka kwa watazamaji nikicheza nikiwa mcheshi.

Hayo yalitukia zaidi ya miaka 45 iliyopita, nilipokuwa mwenye umri wa miaka 17 tu. Sasa nastaajabia mambo ambayo mwili mwepesi ulio mchanga waweza kufanya kwa mazoezi makali na utaratibu hususa wa maisha yenye uangalifu. Basi kitumbuizo kilikuwa kimekuwa maisha yangu yote, mungu wangu, na kikabaki hivyo kwa zaidi ya miaka 20.

Kuanza Maisha ya Sarakasi

Nilizaliwa katika Kempsey, New South Wales, Australia. Tulikuwa maskini—nyumba yetu ilikuwa na kuta za magunia yaliyopakwa chokaa na paa yenye vipande vya mabati vilivyochakaa. Miaka michache baadaye, tulihamia sehemu ya kusini zaidi, kwenda Taree. Familia yetu haikuwa ya kidini, ingawa kwa jina tulikuwa washiriki wa kanisa la Church of Christ.

Katika 1939 baba yangu alijiunga na jeshi. Basi mama akapakia vitu pekee tulivyokuwa navyo, nguo zetu, na akiwa na dada zangu watatu pamoja nami akahamia Sydney. Huko nilihudhuria shule ya michezo ya viungo vya mwili na kwa kushangaza nikaonyesha uwezo wa asili. Kwa miezi michache tu, nikawa mstadi wa mchezo wa viungo vya mwili. Kisha, katika 1946, nilipewa kazi katika sarakasi ya kujifunza jinsi ya kuwa mrukaji katika wonyesho wa fito zenye kubembea.

Sarakasi hiyo ilikuwa ikitoa maonyesho katika mji tofuati-tofauti kila usiku. Umati mwingi ulikuwa ukija kuona uvutio wa sarakasi, lakini, bila shaka, hawakujua juu ya mapigano na magomvi ya ulevi yaliyokuwa yakiendelea bila wao kujua. Wala hawakujua juu ya mwenendo usio wa adili wa watumbuizaji wengi waliowavutia sana.

Nilikuwa nikiwa katika karamu nyakati zote na ilionekana kwamba nilikuwa nikihusika katika mapigano kila wakati. Ninashukuru kwamba sikupendezwa kamwe na kunywa pombe kupindukia. Pia nilikuwa nikiepuka tabia ya kutumia lugha chafu na nisingeweza kuvumilia kusikia mtu akiapa kwa maneno machafu mwanamke akiwapo. Hilo lilikuwa sababu ya mapigano yangu mengi.

Katika kila mji wenye ukubwa wa kadiri ambamo tulifanya wonyesho, mtu alitumwa aende kwa kasisi wa Katoliki wa hapo akampatie tikiti za kuingia bure na upaji kwa kanisa. Eti hilo lingeleta bahati nzuri na kuhakikisha kwamba sarakasi ingehudhuriwa na watu wengi.

Kugeukia Mchezo wa Vaudeville

Katika 1952, niliambiwa na watumbuizaji fulani wa mchezo wa vaudeville (wimbo pamoja na maonyesho mengi tofauti-tofauti) kwamba njia ya kuchuma fedha nyingi zaidi na kupata mafanikio zaidi ilikuwa ni kufanya maonyesho ya vaudeville. Kwa hiyo nilianza kusafiri sana nikitoa maonyesho ya vaudeville. Kisha nikaanza kutoa maonyesho katika klabu moja ya usiku hadi nyingine na hatimaye nikawa natoa wonyesho katika majumba ya michezo yaliyo mashuhuri zaidi katika Australia na New Zealand. Nilikuwa nikitoa wonyesho pamoja na watumbuizaji mashuhuri, ingawa, kwa wakati uo huo, nikijifanyia mwenyewe jina zuri katika mchezo wa kiinimacho na wa viungo vya mwili.

Nilihisi kwamba badiliko la kufanya mchezo wa vaudeville lilikuwa uamuzi mzuri, lakini nilivunjika moyo kwamba karamu, ukosefu wa adili, na unywaji wa kupindukia ulikuwa mbaya zaidi katika vaudeville kuliko katika sarakasi. Sasa nikakutana na wagoni wa jinsia-moja wa kiume na wa kike. Dawa za kulevya pia zikaanza kuonekana, lakini nafurahi kwamba sikujihusihisha kamwe pamoja nao.

Mimi nilifikiria tu kujifanyia mwenyewe jina zuri na kufanyia maendeleo wonyesho wangu. Kitumbuizo na sifa nilizopokea yalikuwa mambo pekee niliyotaka. Yalinipa hisia zote za ubora nilizohitaji. Hata niliamua kwamba sitaoa kamwe. Sikuwa na daraka lolote—nilikuwa na wakati mzuri sana. Kitumbuizo kilikuwa mungu wangu. Lakini hata mipango bora zaidi huharibika.

Ndoa

Siku moja, nilipokuwa nikitafuta mchezaji wa kike mwenye kipawa wa kujiunga na wonyesho wa vaudeville wenye kusafiri-safiri, nilikutana na mmoja wa wasichana warembo zaidi niliopata kuona. Jina lake lilikuwa Robyn. Hakuwa tu mchezaji hodari wa baleti bali pia alikuwa na kipawa katika mchezo wa viungo vya mwili. Nilifurahi sana alipokubali kazi hiyo mara hiyo na akawa mwenzi wangu katika wonyesho wa watu wawili uliofanikiwa. Miezi mitano baadaye, katika Juni 1957, tulifunga ndoa. Kwa miaka mitatu iliyofuata, tulikuwa tukitoa wonyesho katika klabu mbalimbali, tukitembelea maonyesho, na kuonekana katika televisheni.

Baada ya kufunga ndoa, tulijitenga kwa kadiri tulivyoweza, tukiepuka kuchangamana na watumbuizaji wengine kwa mambo ya kawaida kwa kadiri ilivyowezekana. Hata tulipokuwa tukitoa maonyesho katika vilabu, nilihakikisha kwamba Robyn alikaa katika chumba cha kubadili mavazi hadi tulipoenda jukwaani. Wacheshi hao walikuwa wakisema mizaha michafu kimchezo, na baadhi ya wanamuziki walikuwa wakilewa dawa za kulevya. Wengi wao walikuwa wakinywa pombe kwa kuendelea na kutumia lugha chafu.

Kutoa Maonyesho Katika Nchi Nyinginezo

Katika 1960 tulipewa kandarasi ya kutoa maonyesho katika nchi za kigeni. ‘Hii ndiyo nafasi yetu ya kufanikiwa,’ nikawaza. Lakini, kufikia sasa tulikuwa na binti mdogo, Julie, wa kushughulikiwa. Hata hivyo, niliburuta familia yangu kuzunguka Mashariki ya Mbali, nikiishi kwa vitu tu tulivyoweza kubeba katika masanduku yetu, nyakati nyingine tukifanya kufikia maonyesho matano kwa usiku mmoja. Hilo liliendelea kwa muda unaozidi mwaka mmoja, na kisha tukarudi Australia.

Sasa kwa kuwa tulikuwa tumefikia kiwango cha kutoa maonyesho ya kimataifa, wonyesho wetu ulitakiwa sana na watu. Lakini kulikuwa na fursa ndogo katika Australia kwa sababu ya idadi yayo ndogo ya watu kwa kulinganisha. Kwa hiyo katika 1965 tulienda ng’ambo tena. Wakati huu hatukuwa na Julie pekee yake bali tulikuwa na binti mwingine mdogo, Amanda. Wakati wa miaka mitano iliyofuata, tulitoa maonyesho katika nchi tofauti-tofauti 18.

Yale magumu niliyofanya familia yangu ipitie kwa sababu ya tamaa yangu ya kuwa bora zaidi yalikuwa mabaya sana. Pindi moja nilimlipa mtu mmoja alinde kwa bunduki watoto wetu, waliokuwa umbali wa meta 60 tu kutoka mahali tulipokuwa tukitoa wonyesho. Mara nyingi nilibishana na wenye vilabu waliotaka Robyn aketi na wateja ili awatie moyo wanywe zaidi, lakini wanywaji hao wenye makelele walitazamia mambo yasiyo ya adili. Tulitoa maonyesho katika vilabu vyenye watumbuizaji wenye kuvua mavazi yao, makahaba, na wagoni wa jinsia-moja, baadhi yao wangenidokezea au kumdokezea mke wangu mambo ya kingono. Na wanamuziki wa beni za roki walikuwa wakilewa dawa za kulevya mara nyingi.

Katika pindi za safari zetu, nilikuwa na wakati mwingi mchana wa kutazama vitu. Nyakati zote nilikuwa nikizuru hifadhi za wanyama, misikiti, mahekalu, makanisa, au sherehe za kidini. Nilikuwa nikizuru sehemu hizo kwa sababu ya udadisi tu kwa kuwa sikuwa hasa na mwelekeo wa kidini. Nilishangaa kwamba vitu vingi tofauti-tofauti vilikuwa vikiabudiwa. Kulikuwa na mifano ya watu wenye vichwa vya wanyama, na wanyama wenye vichwa vya wanaume au wanawake. Katika nchi moja, watu hata waliabudu viungo vya uzazi vya wanaume na wanawake, kwa wazi wakiamini kwamba kufanya hivyo kungemwongezea nguvu uwezo wa kingono na wa uzazi wa mwabudu huyo.

Katika nchi nyingine, wavulana na wanaume walikuwa wakijipiga mgongoni na visu vyenye makali matatu mpaka damu imwagike. Siku niliyokuwa hapo, watu watatu walipoteza uhai wao kwa sababu ya kupoteza damu nyingi mno. Katika kathedrali moja ijulikanayo sana, nilichukizwa kuona masanduku ya kuungama yakiwa na ishara hii: “Ungamo mmoja, franc 1 [fedha]; maungamo mawili, francs 2; maungamo matatu, francs 2.50.” Nikawaza: ‘kama dini iko hivyo, basi sitaki!’

Kurudi Australia

Katika 1968 tulimtuma Julie nyumbani, lakini ilituchukua miezi mingine 18 ili tuweze kuweka akiba ya fedha za kutosha kulipia nauli zetu sisi sote ili kurudi. Katika 1970 tulifika nyumbani bila fedha wala umashuhuri wa kuonyesha kazi yetu yote yenye jasho. Fedha zetu nyingi zilikuwa zimetumika katika mavazi ya maonyesho, muziki, gharama ya usafiri, sehemu za kulala, na wawakilishi wenye ufisadi. Vitu tulivyokuwa navyo pekee vilikuwa vitu vya jukwaa na vitu vyote ambavyo tungeweza kubeba katika masanduku yetu.

Baada ya kurudi Australia, nilieneza utendaji wangu na nikawa pia mwakilishi wa michezo ya jukwaa. Nilipata kandarasi ya kucheza nikiwa mtu mcheshi katika kipindi cha televisheni kilichoendelea muda mrefu kilichoitwa The Yellow House. Niliandika na kutokeza maonyesho ya michezo ya kuigiza ya watoto na ya ucheshi ya kutumiwa katika vilabu kadhaa, huku nikiendelea na Robyn katika maonyesho yetu. Kitumbuizo kingali kilikuwa mungu wangu. Robyn na watoto wakaanza kuumia; ilikuwa ni kana kwamba sikuwa mume wala baba.

Mwito wa Dini

Siku moja mama-mkwe wangu, aliyekuwa akiishi nasi, alionyesha Robyn kitabu Kweli Iongozayo Kwenye Uzima wa Milele. “Soma hiki,” akasema. “Kinahusu dini, lakini ni tofauti.” Robyn alikataa, akisema kwamba baada ya yale tuliyoyaona ng’ambo, hakupendezwa na dini. Hata hivyo, mama yake hakuchoka. Alimfuata Robyn huku na huku kwa juma moja, akisisitiza kwamba akisome kitabu hicho. Hatimaye Robyn alikubali, ili tu ampendeze mama yake.

Ilikuwa ni kana kwamba macho ya Robyn yalikuwa yamefumbuliwa kwa ghafula, alieleza hivyo baadaye. Alivutiwa sana na majibu ya maswali yake mengi hivi kwamba alitaka kujua zaidi. Majuma mawili baadaye mama yake alipanga ili Mashahidi wa Yehova wawili waje nyumbani kwetu. Baada ya ziara kadhaa, walitualika tuhudhurie moja ya makusanyiko yao yaliyokuwa karibu na hapo. Nilikubali kwenda shingo upande. Kwa kweli, nilivutiwa sana hivi kwamba tukaanza kuhudhuria mikutano katika Jumba la Ufalme.

Lakini, kitumbuizo kingali kilikuwa mungu wangu, kwa hiyo nikang’amua upesi kwamba nisingeweza kuendelea na Mashahidi. Hata hivyo, Robyn alitaka kuendelea kujifunza kweli za Biblia hata kama mimi sikutaka. Nilighadhabika sana. ‘Ni haki gani,’ nikahisi, ‘watu hawa wana haki gani ya kuingilia kati yangu na mke wangu, wakijaza akili yake kwa takataka za kidini?’

Hata matisho yangu ya kuvunja ndoa yetu hayakufua dafu. Robyn alisimama imara na kuendelea kujifunza. Hata akaanza kwenda nje kuongea na watu mlango kwa mlango juu ya itikadi zake. Nilipata pigo kubwa zaidi aliponiambia kwamba alitaka kubatizwa na kuwa Shahidi aliyejiweka wakfu. Hata hivyo, alishauriwa angojee mpaka aache kazi yake ya kitumbuizo.

‘Aha!’ nikawaza. ‘Nimeshinda. Hawatampata. Hawezi kuacha wonyesho wake.’ Lakini nilikosea. Robyn alinipa mwaka mmoja, ambapo baada ya muda huo alisema angeacha. Mimi nilicheka, nikiamini kwamba hangeweza kuacha kutoa wonyesho aliopenda sana. Lakini nilikosea tena. Mwaka mmoja baadaye aliacha kazi ya kutumbuiza na kubatizwa. Binti yetu Julie na mama ya Robyn vilevile walibatizwa.

Pigano Langu Dhidi ya Kweli

Baadaye nilimtenda vibaya Robyn kwa maneno makali, nikimwambia kwamba amenifanyia vibaya, kwamba hakunijali. “Kitumbuizo kilikuwa maisha yangu yote. Hakuna kitu kinginecho niwezacho kufanya,” nikalalamika. “Matatizo yangu yote yameletwa na wewe.” Hata nilitisha kupiga Mashahidi, ambao niliwalaumu kwa kuvunja wonyesho wetu na kusababisha matatizo yetu yote.

Robyn alianza kuacha magazeti ya Biblia huku na huku nyumbani mwetu, akitumaini kwamba ningeyasoma. Hilo halikufaulu, kwa hiyo hatimaye akaacha kufanya hivyo. Lakini hakuacha kamwe kusali kwa Yehova kwamba angalau kwa njia fulani nijifunze kweli na kwamba sisi sote tuwe pamoja tukiwa familia katika ulimwengu mpya.

Baada ya muda, nikaanza kuvumilia Mashahidi walipozuru nyumba yetu, na mara kwa mara nilikubali watoto wanibembeleze niende nao mkutanoni. Lakini nilikuwa mwenye uchambuzi wa mambo yote niliyoyasikia huko. Lakini, nilikiri ndani yangu kwamba watu waliokuwa katika Jumba la Ufalme, waliotia ndani watu wa kutoka mataifa mengi—watu wa Kiarabu, Wagiriki, Waitalia, Waingereza, na vilevile Waaustralia—wote walionekana wakisikilizana vizuri. Nyakati zote walikuwa wenye urafiki, na hakuna mtu aliyetumia lugha chafu au kujiingiza katika mazungumzo yasiyo ya adili.

Kusaidiwa na Mkristo Halisi

Hatimaye nilikubali funzo la Biblia la kawaida pamoja na Ted Wieland, mtu mwenye fadhili na unyenyekevu kwa njia yenye kutokeza sana. Alitumika katika Betheli, ofisi ya tawi ya Mashahidi wa Yehova. Katika pindi moja nilipokuwa hasa nikimsumbua sana Robyn, Ted aliniita kwenye gari lake, akaingiza mkono kwenye sehemu ya mzigo, na kunipa kibumba chenye maembe. Ikawa kwamba nilipenda sana maembe, lakini sidhani kama Ted alijua hilo. Matendo hayo yaliendelea kwa majuma: kibumba chenye maembe kila wakati Ted alipokuja kuzuru. Siku moja aliingiza mkono katika sehemu ya mzigo kuchukua kitu kile nilichodhania kuwa ni kile kibumba cha kawaida chenye matunda, kisha akageuka kwa utulivu na kusema hivi: “Je! wafikiria waweza kukiangika kitu hiki ukutani?” Lilikuwa ni andiko la mwaka la Biblia, ambalo Mashahidi huonyesha katika nyumba zao. Nisingeweza kukataa, nikaliangika ukutani.

Funzo la Biblia na Ted lilipoendelea, alinionyesha kutoka kwenye Biblia kwamba kitumbuizo hakikunitolea wakati ujao halisi. Tumaini la pekee la wakati ujao wenye furaha, yeye akaeleza, liko katika utimizo wa unabii mbalimbali wa Biblia kuhusu Ufalme ambao Kristo alitufundisha tusali juu yao. (Mathayo 6:9, 10) Ingawa nilikuwa ningali na kandarasi za vitumbuizo kutimiza, nilianza kuhudhuria mikutano ya kutaniko kwa ukawaida. Nilijiandikisha katika Shule ya Huduma ya Kitheokrasi na hata nikaanza kushiriki katika huduma ya nyumba kwa nyumba.

Nikaanza kuona kwamba kitumbuizo hakingenitolea kitu chochote. Sikuwa nimepata kitu chochote cha kimwili katika miaka yote ambayo nilikuwa nimetumia kwa kile ambacho kilikuwa mungu wangu. Familia yangu ilikuwa imeumia—ikiburutwa kuzunguka ulimwengu na kuishi kwa vitu pekee tulivyobeba katika masanduku yetu. Kwa kweli kitumbuizo kilikuwa karibu kivunje ndoa yetu. Lakini sasa Aliye Mkuu Zaidi wa ulimwengu wote mzima alikuwa akinitolea fursa ya kuishi milele katika dunia-paradiso chini ya utawala wa Ufalme wake.

Kwa hiyo nilifanya uamuzi mzito zaidi maishani mwangu. Nilipokuwa nimemaliza kandarasi zangu za vitumbuizo, nilikatisha kabisa mahusiano yote na ulimwengu wa vitumbuizo. Sikurudi tena kamwe kilabuni wala sikushirikiana tena na wale watu waliofanya vitumbuizo kuwa njia yao ya maisha. Ted alipitia nami maswali ambayo wanaotaka kubatizwa hupitia. Hata hivyo, Ted akafa, na muda mfupi baadaye nilibatizwa, katika Julai 26, 1975. Ninatazamia kukutana na mtu huyo mzuri ajabu katika ulimwengu mpya atakapokuwa amefufuliwa.—Yohana 5:28, 29.

Baraka Tele

Yehova ametuandalia sisi zaidi ya yale yote tuliyopokea katika miaka yote tuliyotumia katika kitumbuizo. Amenifungua kutoka katika ulimwengu wa kitumbuizo wenye ufisadi na usio na uadilifu. Amethawabisha sala za mke wangu mwaminifu, aliyeshikamana nami bila kuacha kamwe. Ametubariki kwa kiasi cha kwamba mama ya mke wangu na binti zetu wawili wakubwa pamoja na waume zao wote ni wenye utendaji katika huduma ya Kikristo. Binti yetu mchanga zaidi, Letitia, na mjukuu mkubwa zaidi ya wajukuu wetu watatu, Micah, wote ni wapigaji mbiu ya habari njema wasiobatizwa. Yehova amenibariki pia na pendeleo la kutumika nikiwa mzee katika kutaniko la Kikristo.

Robyn na mimi hatuwezi kamwe kumlipa Yehova kwa mambo yale ambayo ametufanyia. Hata hivyo, twaweza kuonya wengine—hasa vijana—juu ya hatari za ulimwengu wa vitumbuizo na aina mbaya ya kitumbuizo. Twaweza kuwaonya, kutokana na maono yetu wenyewe, juu ya huzuni ifuatayo ukosefu wa adili, dawa za kulevya, unywaji wa kupindukia, aina mbaya ya muziki, nyimbo zenye kusisitiza ngono haramu, na hatari zilizoko mtu anapoenda kwa kawaida kwenye vilabu au maonyesho ya muziki wa roki. Mambo hayo yote ni sehemu ya ulimwengu unaotawalwa kabisa na Shetani Ibilisi.—2 Wakorintho 4:4.

Ni rahisi kunaswa katika ibada ya Shetani bila kujua, jinsi nilivyokuwa nilipoweka kitumbuizo kuwa mungu wangu. Hata hivyo, sasa mimi na mke wangu tunafurahi kutia moyo vijana wamwabudu Yehova, yule Mungu mmoja anayeweza kuridhisha tamaa zote za moyo—yule Mungu anayetujali kwa kweli katika kila njia.—Kama ilivyosimuliwa na Vivian A. Weekes.

[Picha katika ukurasa wa 14]

Msichana niliyemwoa alikuwa mchezaji wa viungo vya mwili

[Picha katika ukurasa wa 15]

Robyn na mimi leo

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki