Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g93 10/22 kur. 17-19
  • Kutafuta Siri za Mkunga

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kutafuta Siri za Mkunga
  • Amkeni!—1993
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Fumbo la Chanzo Chake
  • Wachukua Njia Tofauti-Tofauti
  • Maisha Katika Maji Yasiyo ya Chumvi
  • Mabadiliko na Uhamiaji
  • Kuutazama Ulimwengu
    Amkeni!—1998
  • Unapokuwa Mgonjwa kwa Kula Samaki
    Amkeni!—2006
  • Kutembelea Chemchemi za Maji ya Moto za Japan
    Amkeni!—2004
Amkeni!—1993
g93 10/22 kur. 17-19

Kutafuta Siri za Mkunga

Na mleta habari za Amkeni! katika Ailandi

MIKUNGA walimstaajabisha sana Aristotle, yule mwanafalsafa Mgiriki wa kale. Hata alipochunguza kwa kadiri gani samaki hao wenye ngozi laini wafananao na nyoka, hakuweza kupata viungo vyao vya uzazi wala mayai. “Mkunga,” akasema, “si wa kiume wala si wa kike, na hawezi kutokeza jinsia.” Yeye alikata kauli hivi: “Mikunga hutokana na ‘nyuzi za ardhi’ ambazo hukua zenyewe tu katika matope na udongo wenye unyevu.”

Watafiti wa kisasa wamefumbua fumbo hilo hasa kuhusu mkunga. Christopher Moriarty wa Idara ya Maisha ya Majini katika Ailandi aeleza kwamba ingawa samaki wengi huwa na mayai yanayoonekana waziwazi, mkunga haonyeshi dalili yoyote ya hata yai dogo. “Kifuko cha yai cha mkunga,” yeye asema, “hakionekani waziwazi—karibu kisiweze hata kuonekana kabisa katika mikunga wachanga, na hufanyiza tu kitepe kidogo cheupe-cheupe chenye kupinda-pinda katika mikunga wakomavu.”

Na kwa sababu hakuna mkunga yeyote anayetaga mayai ambaye amepata kushikwa, hata kufikia nyakati zetu za kisasa, waweza kuelewa ni kwa nini Aristotle alishangazwa. Bila kuwa na darubini, hakuwa na njia yoyote ya kupata kujua mahali mikunga walipotoka.

Ingawa wanasayansi wamefumbua fumbo hilo la mkunga, wamefumbua mafumbo mengine ambayo bado hayaeleweki. Kwa kielelezo, ebu tazama maisha ya mkunga wa Ulaya wa maji yasiyo ya chumvi, na uone kama hayakushangazi vilevile.

Fumbo la Chanzo Chake

Katika kila majira ya masika, mamilioni ya mikunga midogo-midogo wenye urefu wa sentimeta 5-8—wanaoitwa elvers (vitoto)—hufika karibu na ufuko wa Ulaya Magharibi na Afrika Kaskazini. Wao hutokea wapi? Kufikia miaka ya 1920, hakuna mtu yeyote aliyejua.

Hata hivyo, karibu na mwisho wa karne ya 19, uvumbuzi wenye kustaajabisha uliochangia kufumbuliwa kwa fumbo hilo ulifanywa. Ilionekana kwamba mkunga, kama walivyo chura na kipepeo, huanza maisha akiwa katika hali tofauti. Wanabiolojia walifahamu kwa mara ya kwanza kwamba yule samaki mwembamba, awezaye kupenyezwa na nuru aitwaye leptocephalus, mwenye kichwa kidogo sana na mwili kama majani membamba ya mti uitwao willow, alikuwa akibadilika kuwa buu dogo sana awezaye kupenyezwa na nuru anayeitwa mkunga-kioo.

Mara uhusiano kati ya leptocephalus na mkunga-kioo ulipogunduliwa, iliwezekana kufuata chanzo cha mabuu ya mkunga. Katika 1922, mstadi wa bahari Mdenmark, Johannes Schmidt alivumbua kwamba mahali mikunga wote wa Atlantiki hutaga mayai palikuwa ni bahari ya Sargasso, sehemu kubwa yenye magugu katika bahari iliyoko Atlantiki ya Kaskazini. Mikunga wote wa Amerika na wa Ulaya hutaga mayai huko, na humo kuna fumbo jingine.

Wachukua Njia Tofauti-Tofauti

Mabuu ya mikunga wa Amerika na Ulaya hufuata njia zao tofauti katika sehemu fulani karibu na Bermuda. “Jinsi wanavyojua njia ya kufuata wakati hakuna mmoja wao amepata kuona ‘nyumbani’ ni swali ambalo halijajibiwa,” chasema kitabu The Fresh & Salt Water Fishes of the World. Kitabu hicho chaendelea kusema: “Kwa mikunga wa Amerika, safari hiyo ni karibu [kilometa 1,600]; safari hiyo huchukua karibu mwaka mmoja. Mkunga wa Ulaya husafiri [kilometa 5,000] au zaidi, safari yao ikichukua karibu miaka mitatu. Jambo la kushangaza vilevile ni uhakika wa kwamba kiwango cha ukuzi wa mikunga hao wawili [ambao ni vigumu sana kutenganisha] hutofautia-na ili kwamba kila mmoja huwa amekuwa karibu na ukubwa sawa kufikia wakati wanapofikia mwisho wa safari yao.”

Silika fulani za ajabu huelekeza aina hizo mbili za mikunga kwenda njia zao tofauti-tofauti. Juu ya tukio hilo la kifumbo, kitabu Fishes of Lakes, Rivers & Oceans chasema hivi: “Jinsi wanavyotimiza safari hiyo na sababu inayowafanya waichukue safari hiyo ya ajabu ni fumbo sana kama vile chanzo chao kilivyokuwa fumbo katika wakati wa Aristotle.”

Maisha Katika Maji Yasiyo ya Chumvi

Vitoto hivyo vinavyokua, sasa vikiwa na rangi ya kimanjano-hudhurungi, vinapomaliza kuvuka bahari, hivyo hupanda mito kisilika ili kufikia maziwa, vidimbwi, na vijito ambako vitakua kufikia ukomavu kwa miaka ifuatayo 15 na zaidi. Wao hushinda vizuizi vyote ili wafikie mradi wao.

Kitabu The Royal Natural History chaeleza juu ya “kando-kando ya mito zikiwa nyeusi katika sehemu fulani zikiwa zimejaa samaki hao wadogo-wadogo wanaohama.” Chaendelea kusema hivi: “Mikunga hao wachanga wameonekana wakipanda malango ya kuzuia mafuriko ya maziwa, kupanda mabomba ya maji au ya kuondoa takataka . . . na hata watapitia udongo wenye tope ili kupata mahali pafaapo.”

Katika Mto Bann katika Ailandi ya Kaskazini, wavuvi wameweka ngazi za vitoto vya mikunga zilizotengenezwa kwa majani katika sehemu ya mto iliyo ngumu zaidi kupanda. Hapa, vitoto hivyo hupanda kamba hizo na kuingia ndani ya matangi ya pekee ambako wanahesabiwa—20,000,000 kila mwaka!

Mabadiliko na Uhamiaji

Mikunga wanapofikia ukomavu, jambo jingine lenye fumbo sana hutokea. “Mfululizo wa mabadiliko makubwa yanayohusika na ukomavu huanza kutokea,” chasema kitabu Fishes of the Sea. “Jicho hupanuka na kupata uwezo wa kuona vizuri zaidi katika vina vya chini zaidi vya bahari; utumbo huanza kupotea na matezi hupanuka. Rangi pia hubadilika kutoka rangi ya kimanjano-hudhurungi hadi rangi ya kijivu kinachometa-meta.”

Kila majira ya vuli, mikunga wakomavu huanza uhamiaji wa kilometa 5,000 kurudi bahari ya Sargasso. Hakuna mtu ajuaye jinsi wanavyotimiza safari hiyo ya ajabu. Wao huacha kulisha na wakati wa miezi sita ya safari yao wao hutegemea akiba za mafuta ambazo zimewekwa mwilini.

Wanabiolojia husema kwamba mara mikunga hao wafikapo katika maji yenye vina ya bahari ya Sargasso, mkunga wa kike hutaga mayai kutokea milioni 10 hadi 20, na mkunga wa kiume huyatungisha. Kisha mikunga wakubwa hufa. Mayai hayo yaliyotungishwa huelea juu ya maji na kuangua na kutokeza leptocephalus wenye umbo la majani, na mzunguko huo wamalizwa.

Ni kwa nini mkunga anayetaga mayai hajapata kushikwa? “Wao huwa hawali tena, kwa sababu viungo vyao vya kusaga chakula huwa vimenyauka, kwa hiyo hawawezi kushikwa kwa ndoana zenye chambo,” asema Christopher Moriarty. “Wao hutaga mayai katika vina vya chini sana,” aendelea kusema, “na kwa sababu eneo la Bahari Sargasso ni lenye kina kuliko kina cha Visiwa vya Uingereza, na mikunga ni viumbe vya kuepa, mara nyingi watakuwa na nafasi nzuri ya kuepa nyavu zenye kuenda kasi.”

Labda siku moja mafumbo yote yanayohusu kiumbe hiki cha ajabu yatafumbuliwa. Kwa wakati huu, kulingana na mtafiti Moriarty, ikiwa kuna samaki mwenye kushangaza, ‘kwa kweli mkunga ni mwenye kutokeza sana.’

[Sanduku katika ukurasa wa 18]

Mapishi ya Mkunga

Ingawa wengi hukirihishwa kwa wazo la kula mikunga, hao huonwa kuwa chakula kitamu katika sehemu nyingi za ulimwengu. Je! ungependa kujaribu mkunga? Amkeni! liliuliza mpishi mmoja mkuu katika Ailandi Kaskazini jinsi ya kupika samaki huyo. Hapa pana mawili ya madokezo yake:

Mtokoso wa Mkunga: Utahitaji mikunga wawili wenye umbo la kadiri wenye urefu unaokaribia sentimeta 50. Wanahitaji kuambuliwa ngozi na kutolewa mifupa na kukatwa katika vipande vya sentimeta 5. Pia utahitaji kipimo cha vijiko vikubwa vinne vya mafuta ya halzeti (mafuta ya zeituni); vitunguu saumu kadhaa vilivyopondwa; shada moja la mchanganyiko la vikolezo; maji ya chungwa moja; kaka la chungwa lililosagwa; kiasi kidogo sana cha pilipili hoho; kiasi kidogo sana cha chumvi; kikombe kimoja cha divai nyekundu.

Weka mafuta ya halzeti katika chungu au sufuria yenye sehemu ya chini iliyo nzito yenye ukubwa wa kutosha viungo vyote vya upishi. Ongeza kitunguu saumu kilichopondwa, shada la mchanganyiko wa vikolezo, maji na kaka ya chungwa, na pilipili hoho. Tia chumvi katika vipande vya mkunga, na uviweke katika maziga. Mwaga divai juu yazo, ongeza maji ya kutosha kufunika mikunga hao. Ipike bila kufunika kwenye moto wa kadiri kwa muda wa dakika 30 hivi mpaka nyama ya mkunga iive. Pakua kwenye sahani zilizopashwa moto.

Jeli ya mkunga: Weka angalau kipimo cha kikombe kimoja cha mikunga walioambuliwa ngozi, kutolewa mifupa, na kukatwa-katwa ndani ya sufuria. Ongeza kitunguu kilichokatwa-katwa, karoti, kifungo cha selari, jani la loreli, mboga ya pasli, chumvi na pilipili, na maji ya kutosha, divai nyeupe, au maji ya tunda (sida) ya kufunika viungo vya upishi. Yachemshe polepole, na uache yachemke polepole kwa karibu muda wa saa moja. Weka vipande vya mkunga ambavyo vimepikwa katika chombo kimoja. Chemsha viungo vya upishi vilivyobaki mpaka vipungue kwa kiasi cha robo, kisha uchuje maji yaliyobaki juu ya vipande vya mkunga. Poesha vipande hivyo vya mkunga na yale maji ili kufanyiza jeli. Ukile pamoja na maji ya limau na tosti ya mkate iliyopakwa siagi, uipake kama siagi.

[Sanduku katika ukurasa wa 19]

Je! Ulijua?

Kwamba mkunga wa Ulaya wa kike aliyekomaa anafikia urefu wa meta 1, lakini wa kiume hufikia nusu tu ya ukubwa huo.

Mikunga wengine wanaoishi katika vidimbwi au maziwa yaliyozingirwa na ardhi huwa hawahami. Wanaweza kuishi katika mahali kama hapo kwa miaka 50 au zaidi.

Mikunga wanaweza kuishi kwa muda wa saa 48 nje ya maji.

Mkunga mwenye umri mkubwa zaidi aliyepata kurekodiwa alikuwa wa kike aliyeitwa Putte. Alikufa katika 1948 katika tangi la maji la Denmark akiwa na umri wa miaka 85.

Mikunga wana hisi ya kunusa ya hali ya juu sana, angalau wenye hisi kama ya mbwa.

[Picha katika ukurasa wa 17]

Mto Bann wa Ailandi hujaa mamilioni ya mikunga

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki