Kuutazama Ulimwengu
Uhuru wa Kidini Watishwa Ulaya
Kwenye mkutano baina ya waandishi wa habari wa hivi karibuni katika Washington, D.C., Marekani, Massimo Introvigne, ambaye ni msomi wa Katoliki ya Kiroma kutoka Turin, Italia, alisema kwamba orodha zinazopinga madhehebu zinakusanywa katika nchi kadhaa. Dini zinazotajwa kuwa “madhehebu hatari” zinatia ndani Baptist, Wabudha, vikundi fulani vya Katoliki, Wayahudi wa Hasidi, Mashahidi wa Yehova, dini ya Friends, na chama cha Young Women’s Christian Association (YWCA). Ripoti ya Ujerumani yataja kwamba kuna vikundi 800; ripoti ya Ubelgiji yataja vikundi 187; na ripoti ya Ufaransa yataja vikundi 172. Introvigne aliandika kwamba katika Ufaransa “walimu wameachishwa kazi katika shule za umma baada ya kutumikia kwa miaka mingi ya uaminifu eti kwa sababu walikuwa Mashahidi wa Yehova.” Kama ilivyoripotiwa na shirika la habari la Compass Direct, Introvigne alisema anahangaika kwamba umma unadhamini vikundi hivyo vya kupinga madhehebu. Alisema hivi: “Ni wazi kabisa kwamba vikundi hivyo vinaeneza habari za uwongo hasa dhidi ya dini ndogo-ndogo, na kueneza kotekote uhasama dhidi ya dini hizo.”
Madirisha Yenye Akili
Watafiti kwenye Chuo Kikuu cha Australia cha Sydney wametengeneza dirisha ambalo hujifunga lenyewe wakati ambapo ndege yenye kupaa kichinichini inapokaribia. Baada ya kelele yenye kuudhi ya ndege kuisha, dirisha hilo hujifungua tena. Mikrofoni moja iliyo nje, ikiwa na chombo fulani kilichotengenezwa dirishani, inaweza kutambua mawimbi fulani hususa ya kelele nyinginezo zenye kuudhi, kama vile kelele za lori. Majaribio yaonyesha kwamba madirisha hayo yaweza kupunguza kelele kwa karibu desibeli 20, angalau kwa kiwango cha kukuwezesha upate usingizi mnono. Gazeti New Scientist linasema hivi: “Mojawapo ya manufaa kubwa za mfumo huo ni kwamba majengo yaweza kujengwa yazuie sauti na wakati huohuo kuwe na hewa safi bila uhitaji wa kuweka mfumo ghali wa kusafisha hewa.”
Athari ya Televisheni kwa Watoto
“Katuni na michezo ya vidio huathiri tabia ya watoto wenye umri wa miaka 6 hadi 12 kuliko shule, kwa kuwa wao hutazama televisheni kwa muda wa saa 38 kila juma tofuati na muda wa saa 23 wanaotumia darasani,” laripoti gazeti la Mexico El Universal. Mtafiti Omar Torreblanca alisema kwamba televisheni huwafanya watoto waige tabia fulani katika hali fulani—lakini bila watoto hao kujua kama tabia hizo ni nzuri au mbaya. Alieleza hivi: “Mtoto akiona katuni au sinema ambamo mmoja wa wahusika afungwa kwa mafanikio, yaelekea mtoto huyo ataiga kitendo hicho.” Uchunguzi wa Torreblanca ulionyesha kwamba “watoto hutumia maishani kile wanachojifunza kila siku kwenye televisheni lakini si wanachojifunza shuleni, kwa kuwa wao huiona shule kuwa wajibu tu.”
Kutembea Kwaweza Kurefusha Maisha
Kutembea kila siku kwaweza kurefusha sana maisha ya mtu, lasema Asiaweek. Wanaume 707 wenye umri wa kati ya miaka 61 na 81, ambao hawavuti sigara na wawezao kutembea walifanyiwa uchunguzi mmoja uliochukua miaka 12. Wale ambao “walikuwa wanatembea kilometa 3.2 tu kwa siku—hata kwa mwendo wa polepole—walipunguza kwa nusu uwezekano wa kufa kunakosababishwa na hali zozote zile,” ripoti hiyo yasema. Wale ambao hawakuwa wakitembea walikuwa na uwezekano wa mara 2.5 zaidi wa kufa kwa kansa za aina zozote kuliko wale ambao walikuwa na mazoea ya kutembea kwa angalau kilometa 3.2 kwa siku. Uchunguzi huo, uliochapishwa katika The New England Journal of Medicine, ulipata kwamba hata kutembea mwendo mfupi kama nusu maili hivi kwa siku kulipunguza uwezekano wa kufa. Hapo awali, wataalamu fulani wa mazoezi ya mwili walitilia shaka mafaa ya mazoezi yasiyo makali. Sasa, uchunguzi huo mpya wakata kauli: “Kuwatia moyo wazee-wazee watembee huenda kukawanufaisha.”
Muziki Huwasaidia Watoto
Kufundisha watoto wenye umri wa miaka mitatu au minne kupiga muziki kwaweza kuwasaidia kusababu na kufikiri, asema Gordon Shaw, profesa wa fizikia kwenye Chuo Kikuu cha California, Irvine. Katika umri huo mchanga, miunganisho ya ubongo hufanyizwa haraka, na watafiti wameonyesha kwamba mazoezi ya kawaida ya hata dakika kumi kwa siku husaidia kutokeza “maendeleo makubwa kwa jinsi ambavyo mtoto husababu na kufikiri.” Katika jaribio la miezi tisa, watoto ambao walikuwa wamejifunza kupiga piano walilinganishwa na vikundi vya watoto ambao walikuwa wamefundishwa kompyuta au ambao hawakufundishwa jambo lolote. Wale ambao walikuwa wamejifunza kupiga piano waliboresha akili zao kwa asilimia 35, ilhali wale wa vile vikundi vingine viwili walifanya maendeleo kidogo au hawakufanya maendeleo yoyote, laripoti Sunday Times la London.
Mazingira ya Ufuo
Je, inawezekana kuharibu ufuo kwa kuuondolea takataka sana? Ndiyo, wasema uchunguzi mmoja uliofanywa kwenye Ghuba ya Swansea, Wales. Jambo linalofanya ufuo uwe mzuri ni kurundamana kwa uchafu mara mbili kila siku wakati wa kujaa kwa maji. Takataka zaweza kutia ndani miti, mbao, mwani, nyasi, na hata mizoga, zote zikiwa zimechangamana na magugu ya maji. Mchanganyiko huo una vijiumbe ambavyo husaidia kumeng’enya mimea inayooza, ambayo pia hutawanyishwa na upepo na mawimbi ili kushikanisha mchanga. Ufuo pia huwapa chakula ndege na wanyama kama panya, sungura na hata mbweha. Kupunguka kwa ndege wa ufuo ndiko kulikotahadharisha wataalamu wa hifadhi kwamba kuondoa takataka kwa ukawaida kwenye ufuo huharibu usawaziko wa mazingira. Wapenzi wengi wa ufuo hutamani ufuo safi isivyofaa. Gazeti The Times la London laripoti kwamba mgeni mmoja hata alitarajia vijiwe viondolewe kutoka kwenye mchanga.
Chakula Chetu Duniani
Je, umepata kujiuliza watu ulimwenguni hula kiasi gani cha chakula kila siku? Gazeti la Ugiriki To Vima liliripoti tarakimu fulani zenye kushangaza juu ya ulaji wa kila siku. Ulimwenguni pote, mayai bilioni 2 hutagwa na kuliwa! Ulimwengu hula tani milioni 1.6 za mahindi, na chakula chetu hukolezwa kwa tani 500,000 za chumvi. Viazi pia vinapendwa, tani 727,000 huliwa! Mchele ndio chakula kikuu cha watu wengi duniani, kwa kuwa tani milioni 1.5 huzalishwa kila siku. Kati ya hizo, Wachina hula tani 365,000 za wali. Tani 7,000 za chai hujaza vikombe bilioni 3. Watu wenye uwezo duniani hula tani 2.7 za mayai ya samaki. Mtu wa kawaida katika nchi za Magharibi hula kalori 4,000 kwa siku—zikilinganishwa na kalori 2,500 zinazopendekezwa kufaa afya—ilhali katika Afrika mtu wa kawaida hula kalori 1,800 pekee.
Mikunga Wafanyao Kazi
Mikunga wamepewa kazi ya kupima ubora wa maji nchini Japani, laripoti The Daily Yomiuri. Miaka mitano iliyopita Profesa Kenji Namba wa Chuo Kikuu cha Hiroshima aligundua kwamba mikunga huathiriwa na tofauti ndogo-ndogo katika maji. Vitu vyenye kudhuru kama vile cadmium au sianidi hufanya moyo wa mikunga udunde mara chache zaidi, ilhali kisababisha-kansa kiitwacho trichloroethylene huongeza haraka midundo ya moyo wake. Kuna mashine ambayo sasa inauzwa ambayo hutumia hali hiyo ya kipekee. Mkunga hulazwa katika bomba la acrylic la hiyo mashine. Maji yapitiapo bomba hilo, elektrodi ambazo zimeshikanishwa kwa bomba hilo ili kupima midundo ya moyo wa mkunga na mabadiliko yoyote hupelekwa kwa mtaalamu kupitia kidude chenye kengele. Mikunga wanaochaguliwa kufanya kazi hiyo hubadilishwa kila mwezi ili kudumisha usahihi wa upimaji huo.
Mikanda ya Usalama na Vifo Visababishwavyo na Magari
Baraza la Katiba la Mahakama Kuu ya Kosta Rika hivi majuzi liliondoa sheria iliyowalazimisha watu wafunge mikanda ya usalama, likiamua kwamba sheria hiyo ilikiuka haki ya uhuru wa kibinafsi, laripoti The Tico Times la San José, Kosta Rika. Tangu uamuzi huo ufanywe, madereva wanaotumia mikanda ya usalama wamepungua kutoka asilimia 87 hadi asilimia 44 tu, ilhali aksidenti na vifo vinavyosababishwa na aksidenti vimeongezeka. Baraza la Usalama Barabarani la Kosta Rika limeanzisha jitihada za dharura za kupunguza kiwango cha majeraha, lakini jitihada zao hazifui dafu kwa sababu abiria hawafungi mikanda ya usalama, yasema ripoti hiyo. Mwakilishi wa Baraza hilo Manfred Cervantes asema: “Tunajaribu kwelikweli kuwafundisha watu kwamba wao wanaweza kujilinda na kuokoa uhai wao wenyewe kwa kuwa madereva waangalifu.”
Vifo Vinavyosababishwa na Tumbaku
Watu wapatao bilioni 1.1 ulimwenguni pote huvuta tumbaku, asema Profesa Judith Mackay, wa Shirika la Asia la Kudhibiti Matumizi ya Tumbaku. Kama ilivyoripotiwa katika British Medical Journal, kwenye mkutano wa kumi juu ya tumbaku na afya, ilikadiriwa kwamba vifo vipatavyo milioni tatu vilisababishwa na tumbaku katika 1990. Idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka kufikia milioni kumi kati ya miaka ya 2025 na 2030. Hilo Journal lasema kwamba katika miongo mitatu ifuatayo, ongezeko la vifo vinavyosababishwa na kuvuta sigareti litaondoka katika nchi zilizoendelea hadi nchi zinazoendelea. Kulingana na Profesa Richard Peto, profesa wa takwimu za kitiba kwenye Chuo Kikuu cha Oxford, “tayari China ina vifo vingi vinavyosababishwa na tumbaku kuliko nchi nyingine yoyote.”