Maadili ya Tumbaku?
“Kampuni ‘B.A.T. [British American Tobacco] Uganda 1984 Ltd.’ haiamini kwamba uvutaji wa sigareti unadhuru afya.” Taarifa hiyo, iliyotiwa katika barua kwa Wizara ya Afya katika Entebbe, Uganda, imesababisha mjadiliano mkali katika Uingereza huku kukiwa na mashtaka ya kutiliwa shaka kwa maadili na viwango maradufu katika biashara. Kwa nini?
Maonyo ya serikali juu ya madhara kwa afya ni lazima yawepo kwenye pakiti za sigareti katika nchi za Magharibi ambako sasa tabia ya kuvuta sigareti inapungua kwa asilimia 1 kila mwaka. Hata hivyo, katika nchi zinazositawi, matakwa ya sheria kama hayo mara nyingi huwa hayapo, na mahali ambapo yapo, huenda maonyo hayo yasionwe ikiwa wanunuzi hununua sigareti zao moja moja, badala ya katika pakiti. Mauzo katika nchi hizo yanaongezeka kwa asilimia 2 kila mwaka. Lakini hiyo ni sehemu tu ya tatizo lenyewe. Tumbaku yenye lami nyingi “ambayo ni hatari mno kwa [nchi za Ulaya] hata wasiweze kuzivuta wenyewe” hupelekwa nje kutoka Ulaya kuelekea Afrika na nchi nyinginezo zinazositawi, adai Dakt. Roberto Masironi, mkuu wa programu ya Tumbako au Afya ulio chini ya WHO (Shirika la Afya Ulimwenguni).
Mauzo yenye bidii pia yanaendeleza chapa za sigareti mpya, zenye nguvu, na zenye bei za chini. Katika Zimbabwe, ambako nusu ya idadi ya watu ni chini ya umri wa miaka 16 na hakuna umri wa mwisho uliowekwa wa ununuzi wa tumbaku, inahofiwa kwamba watoto wadogo watakuwa wazoevu wa tabia ya kuvuta sigareti. Dakt. Timothy Stamps, waziri wa afya wa Zimbabwe, pia alionyesha wasiwasi kuhusu “ujumbe wenye hila unaoelekezwa kwa wanawake vijana” kuwafanya wawe wazoevu wa nikotini, ambayo imeitwa “dawa ya kulevya yenye kutenda haraka zaidi katika ulimwengu wa Magharibi.” Akihutubia mkutano wa WHO (Shirika la Afya Ulimwenguni), ofisa mkuu wa tiba wa Uingereza alisema hivi: “Nashindwa kuelewa jinsi mtu yeyote anaweza kujitokeza kuendeleza tabia hii hatari.”
Dhidi ya mapingamizi kama hayo, mbona jitihada za kuongeza mauzo ya tumbaku hazishindwi? Kuna sababu mbili za msingi. Kwanza, zikishindwa, maelfu ya nafasi za kazi zitapotezwa katika viwanda vya tumbaku katika Ulaya. Pili, kuna ufikirio wa uchumi wa nchi ambako tumbaku huuzwa. Kwa mfano, Kenya hupata asilimia 5 ya mapato yote ya serikali kutokana na ushuru na mapato ya kodi ya mauzo ya tumbaku. Utegemezo wa kifedha ambao hupewa harakati za michezo na viwanda vya tumbaku huchangia pia ukuzi wa mauzo ya tumbaku.
Kwa sasa, matatizo ya afya ya ulimwengu wa Magharibi sasa yananyemelea nchi za Kiafrika. Zikiendelea kupiga vita dhidi ya maleria na maradhi mengine mengi ya kwao, nchi hizo hupata mapato yao madogo yakitumiwa hadi mwisho kusaidia magonjwa yanayosababishwa na uvutaji.
Kampuni za tumbaku sasa zinaangalia Esia likiwa ndilo soko linalofuata. Huko, mauzo ya sigareti yanatazamiwa kupanda kwa angalau asilimia 18 katika miaka kumi ijayo. China inatarajiwa kukubali hatimaye tumbaku ya Magharibi. Tayari imejulikana kwamba asilimia 30 ya sigareti zote ulimwenguni huvutwa na watu wa China. Mstadi wa kansa wa Uingereza Profesa Richard Peto atabiri kwamba kati ya watoto wote wa China walio hai leo, milioni 50 hatimaye watakufa kwa maradhi yanayotokana na tumbaku, laripoti The Sunday Times la London.
Kimoja cha vitabia vinavyotambulisha Mashahidi wa Yehova—wakiwa zaidi ya milioni nne ulimwenguni pote—ni kwamba hawatumii tumbaku. Hata ingawa, wengi wao walikuwa wavutaji sana. Waliacha walipotambua kwamba uvutaji haupatani na imani ya Kikristo. (Mathayo 22:39; 2 Wakorintho 7:1) Ikiwa kwa kweli unataka kuwacha uzoevu wa tumbaku, tafuta msaada na shauri kwa mmoja wa Mashahidi wa Yehova. Yeye atafurahi kukusaidia.