Kuutazama Ulimwengu
Wanawake Wanapata Hasara
“Wanawake maskini wa sehemu za mashambani ndiyo watu wenye kupata hasara zaidi ulimwenguni,” chasema kichapo cha Umoja wa Mataifa, UN Chronicle. “Wao huwa wagonjwa na hawajui kusoma zaidi kuliko wanaume na hukosa nafasi nzuri ambazo wanaume huwa nazo ili kuwa na hali njema zaidi.” Chunguzi mbili maalumu kuhusu umaskini ulimwenguni katika 1990 zilizofanywa na mashirika mawili ya maendeleo ya kimataifa, yaani Programu ya Maendeleo ya Umoja wa Mataifa na Benki ya Dunia, zimefikia mkataa huo usiopendeza. “Wanawake kama nusu milioni, asilimia 99 wakiwa katika ulimwengu unaositawi, hufa katika kuzaa kila mwaka,” charipoti UN Chronicle.
Daraka la Mazingira
“Sisi binadamu tumekuwa hatari kwetu sisi wenyewe. Lazima tuchukue hatua bila kuchelewa.” Maneno hayo yenye kutoa onyo yanafanyiza sehemu ya daraka la mazingira lililochukuliwa na wasimamizi wa vyuo vikuu kutoka nchi 22 za Afrika, Esia, Ulaya, na Amerika ya Kaskazini na Kusini. Walidiriki kuwa shule zao zitafundisha zaidi kuhusu mambo ya mazingira kuliko hapo mwanzoni na kuongeza vifaa vya shule vya kufanyia utafiti wa kimazingira. Maofisa hao, waliokutana kwa mjadala katika Talloires, Ufaransa, Oktoba 1990, walitangaza pia miradi sawa “kwa wakati ujao wenye kusitawisha mazingira.”
“Kipimo Kilichopunguzwa” cha Miujiza
Ukame ulilazimisha kwamba “maji ya miujiza” kutoka kwa kidimbwi maarufu cha Lourdes katika Ufaransa yapunguzwe kipimo, ikileta hali ya wasiwasi kati ya wageni wenye kutafuta maponyo ya kimuujiza. Wenye mamlaka wa kidini waliwaruhusu kila mmoja wa wapilgrimu nusu painti tu ya maji hayo kutoka kwa kijito hicho, ambacho, kulingana na mila, kilibubujika katika 1858 baada ya mzuka wa Madonna. Machupa yote yaliyopita kiasi yalitwaliwa, na maji yayo yakamwagwa tena kwenye kidimbwi hicho. “Katika makanisa yote ya Ufaransa, wanaomba kwa Bikira wa Mvua, bila mafanikio. Lakini kwa vyovyote vile, yeye hangeweza kufanya inyeshe Lourdes peke yake,” gazeti Corriere della Sera lilisema.
Matatizo ya Wanyama-Vipenzi
Hali inayoongezeka ya watu wengi kutunza mbwa kama wanyama vipenzi wa nyumbani imekuwa jambo la kuhangaisha miongoni mwa wenye mamlaka wa miji na afya katika Ufaransa. Gazeti la kila juma la Kifaransa L’ Express laripori kwamba kila siku tani 20 za kinyesi cha mbwa hukusanywa kutoka kwenye barabara na vijia vya Paris kwa gharama ya zaidi ya dola 70 za U.S. kwa kilo moja. Lakini zaidi ya kuongezea gharama hiyo na udhia, jambo baya hata zaidi limegunduliwa. Kinyesi cha mbwa huwa chanzo cha ugonjwa unaosababishwa na kiini Toxocara canis. Nusu ya sehemu za kuchezea za watoto na visanduku vyao vya mchanga katika Paris zilikuwa zimeambukizwa na mayai madogo mno yenye kukinza ya kiini hicho, ambayo huingizwa nyumbani kwa wayo za viatu na kwenye miguu ya wanyama-vipenzi wa nyumbani. Kuwapo kwacho ndani ya binadamu kulikuwa kumekisiwa kimakosa kuwa chini kuliko ilivyo. Uchovu, maumivu ya tumbo, kudhuriwa na maumbile fulani, matatizo ya moyo na arteri ni viishara vya mapema vya ugonjwa huo.
Upungufu Makanisani
Idadi ya washiriki katika yale madhehebu makubwa ya Kiprotestanti katika United States inaendelea kupungua, kulingana na kichapo 1990 Yearbook of American and Canadian Churches. Ingawa kitabu mwaka hicho, kilichochapishwa na Baraza la Kitaifa la Makanisa, chaonyesha kwamba katika visa vingi upungufu huo hauzidi asilimia 1, umekuwa ukiendelea bila kubadilika tangu miaka ya katikati ya 1960. Kanisa la Disciples of Christ, Episcopal Church, Presbyterian Church (U.S.A.), United Church of Christ, United Methodist Church, Evangelical Lutheran Church in America, na American Baptist Churches in the U.S.A. yote yamepata upungufu. Hata hivyo, ripoti hiyo iliorodhesha Mashahidi wa Yehova kuwa moja ya dini zenye kupata ongezeko katika hesabu. Mashahidi wa Yehova katika United States walikuwa na ongezeko la asilimia-3 katika 1989 na ongezeko zaidi la asilimia-4 katika 1990.
Habari Mbaya kwa Wavutaji Sigara
Katika Septemba 25, 1990, Vitovu vya Udhibiti wa Maradhi katika United States vilitoa ripoti “Faida za Kiafya za Kuacha Kuvuta Sigara: Ripoti ya Mpasuaji Mkuu, 1990.” Baadhi ya maamuzi makuu yaliyofikiwa ni: “1) Kuacha kuvuta sigara kuna faida kubwa za papo hapo kwa watu wa umri wote . . . ; 2) walioacha kuvuta sigara huwa na maisha marefu zaidi kuliko wale wenye kuvuta bila kukoma; 3) kuacha kuvuta sigara hupunguza hatari ya kupatwa na kansa ya mapafu na aina nyingine ya kansa, pigo la ghafula la moyo, kifafa, na maradhi ya muda mrefu ya mapafu.”
Uuzaji wa Tumbaku kwa Wasovieti
Hivi karibuni katika Muungano wa Kisovieti, kundi lenye kasirani ya wavutaji sigara walikaribia kufanya ghasia kwa sababu ya upungufu wa sigara katika nchi hiyo. Kampuni mbili za United States ziliahidi kuondoa hali hiyo ya upungufu. Hizo zapanga kuuzia Wasovieti kiasi kinachozidi muda wa mwezi mmoja, sigara elfu milioni 34. Jambo linalovuta uangalifu ni kwamba, wawakilishi wa wa kampuni hizo za Amerika walisema kwamba sigara hizo zingekosa onyo la afya la mpasuaji mkuu kuhusu kansa na maradhi mengine yanayoshirikishwa na utumizi wa tumbaku.
Kulamba Ute wa Chura Wenye Sumu
Dakt. Alan Emery wa Hifadhi ya Mambo Asili ya Kanada aliliambia The Globe and Mail kwamba kumekuwa na ongezeko kubwa la vyura wa mianzi kuzunguka ulimwengu katika miaka kumi iliyopita. Chura wa mianzi, au Bufo marinus, “hufanyiza umaji-maji mweupe wenye sumu ambao Shirika la U.S. la Kukabiliana na Madawa ya Kulevya huuita bufotenini.” Katika Queensland, Australia, chura huyo amekuwa tatizo kubwa sana hivi kwamba serikali “imeorodhesha ute wa chura kuwa kitu kisicho halali kupatana na Sheria inayohusu Utumizi Mbaya wa Dawa za Kulevya.” Ute unaofanyizwa na chura huyo wa mianzi ni sumu na “husababisha kuona maono, kutapika sana na kupatwa na ugonjwa wa ghafula.” Globe iliripoti kwamba Wakanada wawili waliolamba vidole vyao baada ya kugusa chura-kipenzi waliugua vibaya sana na iliwabidi kulazwa hospitalini.
Usingizi kwa Ajili ya Akili
Kwa nini sisi tunahitaji usingizi? Katika mjadala wa hivi majuzi katika Strasbourg, Ufaransa, nadharia yenye ujadili ilitokezwa. Ilisemwa kwamba usingizi ni wa faida ndogo kwa mwili kuliko ulivyo kwa akili, ambayo hupata nguvu mpya kwa usingizi baada ya kutenda mchana mzima. Majaribio yanaoyesha kwamba hali “utendaji mwingine wa mwili wa kibinadamu ukiendelea bila kudhuriwa hata baada ya siku kadha wa kadha bila usingizi,” yaripoti Die Zeit, “akili ni tofauti.” Katika visa vya majaribio, watu waliugua kutokana na “kukosa mtazamo na kutoweza kukazia mambo akili, kumbukumbu lililodhoofika, kufikiri kulikopunguzwa mwendo, na matatizo ya kujielekeza vema” waliponyimwa uzingizi.
Kujengwa Upya kwa Babuloni Kwasimamishwa
Babuloni wa kale, mji wenye sifa na mashamba yao yaliyotungikwa ya Mfalme Nebukadreza, ulianguka baada ya kuvamiwa na wenye washindi miaka zaidi ya 2,500 iliyopita. Babuloni ulio mdogo zaidi uliendelea kuwako hadi karibu karne ya nne W.K., wakati ulipokuja kuwa magofu kabisa. Iraq ya siku za leo hivi karibuni ilipanga kujenga upya ngome ya awali ya taifa kubwa lenye kumiliki ifikie utukufu wake wa zamani. (Ona Amkeni! la Julai 8, 1989, ukurasa 30.) Hata hivyo, matukio ya kisiasa ya hivi karibuni katika Mashariki ya Kati yameweka kuzuizi kwa mipango kama hiyo ya ujenzi, yaripoti The New York Times. Isaya 13:19, 20 huonyesha unabii wenye kupendeza kuhusu angamizo la Babuloni, ikisema kwamba “hautakaliwa na watu tena kabisa, wala watu hawatakaa ndani yake tangu kizazi hata kizazi.”
Kodi ya Kanisa ya Ujerumani
Katika Jamhuri ya Muungano ya Ujerumani, makanisa hupata utegemezo wa kifedha kwa njia ya kodi ya kanisa, ambayo waajiri kazi hukata kutoka kwa mishahara. Mwajiri kazi mmoja alikataa kupeleka kodi ya kanisa iliyokatwa kutoka kwa mishahara ya wafanyakazi wake. Kwa nini? Katika 1664 babu zake walishtakiwa na uchawi na waliteswa na kuchomwa hadi kufa, naye hulaumu kanisa kwa hilo. Alipelekwa mahakamani, ambapo ilipatikana kwamba kitendo chake hakikuwa cha haki. “Tofauti na hivyo,” yaripoti gazeti Polizei, “yeyote ambaye babu zake walitaabika isivyo haki . . .angeweza kukataa kufanya wajibu alioulizwa kufanya” na Serikali.
Muziki Mwendo-pole
na Kunywa
Uchunguzi uliofanywa katika mabaa ambayo hucheza muziki wa kizamani wenye kupendwa na wengi na ule wa ki-siku-hizi ulipata kwamba “muziki unapopunguza mwendo, watu wanakunywa zaidi,” yaripoti jarida Psychology Today. Utafiti huo ulifanywa katika muda wa kipindi cha miaka miwili na kilihusisha vikundi 2,000 vya wanywaji. James Schaefer, mtafiti katika mradi huo, alisema kwamba “wenye kunywa sana hupendelea kusikiliza muziki wa mwendo wa polepole, wenye vilio, wenye upweke, na wa kujihurumia.” Kama vile Schaefer adokezavyo: “Inaelekea wateja mara nyingi huishi maisha ya nyimbo wanazotaka wachezewe.”