Kuutazama Ulimwengu
Reli Yalazimika Kubadili Nia
Wakati reli kubwa katika Brazili ilipoanzisha programu mpya ya kuzoeza walinzi wayo kutumia bunduki, wawili kati ya waajiriwa wao walikabili tatizo la dhamiri. Kwa kuwa Mashahidi wa Yehova huishi kwa kufuata mwongozo wa Biblia ‘kutojifunza vita tena kamwe,’ walishikilia kwamba lingekuwa kosa kwao kukubali mazoezi ya kutumia silaha za kuua. (Isaya 2:4) Walifutwa kazi moja kwa moja kwa “kutonyenyekea” kwao kwa kuchukua msimamo huo. Reli hata ilikataa ombi lao la kwamba wabaki katika vyeo vyao vya zamani na wasipewe tu ile programu ya mazoezi na upandaji cheo ulioambatana nayo. Hata hivyo, Katiba ya Brazili hutaarifu: “Uhuru wa dhamiri na ibada haupasi kuvunjwa, kwa kuwa kuna uhakikishio kamili wa kufuata dini kwa hiari, kwa namna ya sheria.” Mahakama ya Jimbo ya Wafanyakazi iliipata reli kuwa na hatia ya kufuta watu hao kazi bila “sababu ya haki” ikalazimisha kampuni hiyo iwalipe ridhaa yao ya haki.
Maradhi ya Chagas na Biashara ya Damu
Maradhi ya Chagas, yasababishwayo na kimelea na kushindwa kwa moyo baada ya hayo kulala bila athari zozote, kwa sasa umeambukiza watu kama milioni 18 wa Amerika ya Latini. Mara nyingi maradhi hayo huambukizwa kupitia mitio-damu mishipani ambayo haikuchunguzwa vya kutosha. Hivi majuzi Bolivian Times lilieleza hivi: “Mojapo sababu ambazo labda hufanya damu isichunguzwe sana katika visa vyote ni ule ubiashara wayo ufanywao ulimwenguni pote. Kuchunguza na kuchanganua damu kutafuta maradhi yoyote huipunguza faida ipatikanayo.” Siku ya Desemba 24, 1993, El Diario la La Paz lilitaarifu hivi: “Asilimia 50 ya mitio-damu mishipani iliyofanywa nchini ina viini vibaya vya maradhi yanayofuata: Chagas, malaria, mchochota-wa-ini, kaswende, na UKIMWI, ukaonya hivyo Msalaba Mwekundu wa Bolivia.”
Hatari Zipatazo Watoto Wachanga
Hivi majuzi, Japani imeona ongezeko kubwa katika idadi ya watoto wachanga “wa hatua ya kutambaa” wakimeza sumu, ndivyo iripotivyo Wizara ya Afya na Masilahi. Karibu nusu ya vitu vyote vyenye sumu vilivyomezwa na watoto wachanga katika 1992 vilihusu sigareti. Wengine walikunywa michango ya vitako na vijivujivu vya sigareti, vilivyokuwa vimeachwa katika mikebe ya vinywaji au katika vyombo vya jivu la sigareti vyenye umajimaji. Vitu vingine hatari vilivyomezwa na watoto wachanga, kulingana na mfuatano wa kumezwa kwavyo, vyatia ndani dawa, vichezeo, sarafu, vitu vya kuliwa, vipambo vya kupaka ngozi na nywele. Visa kadhaa vilitokeza ugonjwa mahututi. Wizara yaonya kwamba asilimia kubwa ajabu ya matukio haya hutukia kati ya saa 11:00 jioni na saa 3:00 usiku wakati washiriki zaidi wa familia wawapo nyumbani na iwapasapo kuweza kuwachunga watoto.
Bishano Kuhusu Ubatizo
Colorado Springs, Marekani, ambacho kimekuwa kimojapo vitovu maarufu vya Jumuiya ya Wakristo vya kueneza evanjeli, kilihusika majuzi katika bishano kuhusu njia za kuongoa watoto. Kulingana na The Denver Post, Kanisa la Kibaptisti la Jiwe-la-Pembeni hutumia kikundi cha basi 16 kupekua-pekua eneo hilo wakitafuta watoto. Ahadi za kuwapa watoto pipi, soda, na sherehe ya ufurahisho huwatia hamu ya kupanda basi hizo. Wazazi wengi huacha watoto wao waende lakini hugutuka wakati watoto hao wajapo nyumbani na hadithi za kubatizwa. Kwa kawaida “waevanjeli” hawa huambia wazazi watie sahihi fomu ya idhini kabla ya kuwabatiza watoto wao, lakini sera hiyo imelegea mara kwa mara. Kulingana na Post, mhudumu wa kanisa hilo asema hivi juu ya ile fomu ya idhini: “Hiyo hutupunguzia mwendo.”
Kupenda Mpira wa Miguu Kupita Kiasi
Mashabiki fulani wa mpira wa miguu (soka) katika Uingereza wamejibidiisha kuhusiana na mpira wa miguu kupita kiasi kile cha kawaida: Wao watoa ombi la kwamba wafapo, majivu yao yatawanywe juu ya uwanja wa kuchezea wa kikoa chao wakipendacho. Kikoa kimoja kipendwacho hupokea kufikia maombi 25 kama hayo. Zoea hilo limeenea sana hivi kwamba Shirika la Uingereza la Mpira wa Miguu limelazimika kuvitolea onyo vilabu vya mpira wa miguu juu ya jinsi hasa mabaki hayo ya kibinadamu yapasa kuondolewa mbali. Kulingana na The Medical Post, ushauri wao watia ndani unaofuata: “Hakuna uhitaji wa kunyunyiza majivu yote. Waweza kutawanya sampuli ndogo tu. Rundo kubwa lingeweza kuziua nyasi. . . . Fagia-fagia majivu hayo huku na huku kwa kifagio kuhakikisha yametandazwa juujuu tu na kwa mweneo unaolingana.”
Dini ya Tao Yavuma
“Msherehekeo mkubwa zaidi katika historia.” Hivyo ndivyo gazeti China Today lilivyoueleza msherehekeo wa Septemba 1993 wa Mwadhimisho wa Sala Kuu ya Luotion, ambao ni mwadhimisho wa dini ya Tao. Mwadhimisho huo ulifanywa kwenye Hekalu la Wingu Jeupe katika Beijing, na washiriki walikuja kutoka mahekalu ya Tao katika Australia, Hong Kong, Kanada, Marekani, na Taiwan. “Shabaha kuu” ya mwadhimisho, kulingana na gazeti hilo, “ilikuwa kuomba mbingu iwape watu furaha ulimwenguni pote.” Madhabahu 11 zilisimamishwa, maandiko yakatajwa-tajwa, na ibada zikatolewa kwa mamia ya miungu—kutia ndani mungu “mwokozi” ambaye husemekana kuokoa watu katika shida zao maishani. Msimamizi wa watawa wa kiume katika hekalu la Hong Kong aliliambia kusanyiko kwamba Dini ya Tao ina kiwango cha juu kilichopita tabia ya ulimwengu na haihusiani hata kidogo na siasa. Mwenyekiti wa hekalu moja la Tao katika Taiwan aliambia waandishi wa majarida kwamba Dini ya Tao hutetea uzalendo na udugu.
Gharama ya Kuepusha Msiba
Ingegharimu kiasi gani kuepusha badiliko lenye msiba la taratibu za hali ya hewa duniani pote ambalo wanasayansi wengi wahofu? Klaus-Peter Möller, kiongozi wa Taasisi ya Eduard Pestel ya Utafiti wa Mfumo katika Hannover, Ujerumani, alikadiria kwamba hilo lingeweza kufanywa kwa kutumia tekinolojia ya sasa. Kulingana na gazeti la Ujerumani Süddeutsche Zeitung, mpango wa Möller ungetaka punguzo la asilimia 75 la viwashio vya masalio kama makaamawe, mafuta, na gesi, na badala ya hivyo kutumia viwashio vingine visivyotoa kaboni dayoksaidi. Namna gani ile gharama? Kulingana na makadirio ya Möller, kiasi cha jumla kingekuwa dola trilioni 22.5, au karibu dola 4,000 kwa kila mwanamume, mwanamke, na mtoto aliye hai leo. Kama vile gazeti hilo limaliziavyo, kazi hiyo “ingetaka wanadamu kwa jumla wafanye tendo hodari lililo kubwa ajabu.”
Nani Alimwona Kwanza?
Papa John Paul 2 alitetea hivi majuzi pokeo moja la kukisia kwamba “baada ya ufufuo, Yesu alimtokea Madonna (Bikira Maria) kwanza kabla ya mtu mwingine yeyote, kabla ya yule malaika kutangazia wanawake jambo hilo,” yataarifu Corriere della Sera. Maoni haya, yasiyoungwa mkono hata kidogo na zile Gospeli, yameamsha fadhaiko kubwa miongoni mwa wengine. Akieleza juu ya maoni ya papa na daraka la Maria katika pokeo la Kikatoliki, mwandikaji Mkatoliki wa Italia Sergio Quinzio alisema kwamba “ujitoleaji wa watu wengi” kwa Maria umeelekea sikuzote kuongoza Wakatoliki wafuate “hata mambo yanayozidi yale ambayo Maandiko Matakatifu yametupokeza.” Aliongezea kwamba, “taarifa hii ya kimamlaka” iliyotolewa majuzi sana “hulazimisha maandiko yaseme vile yasivyosema.”
“Kuvuta Moshi wa Chura” Kwafuatia “Kuramba Chura”
Yasemwa kwamba, kwa muda mrefu watumizi fulani wa dawa za kulevya wanajua kwamba vyura fulani hutoa katika ngozi yao kemikali iitwayo bufotenini ifanyayo watu wapatwe na maono ya mang’amung’amu. Hata hivyo, kemikali hiyo ina sumu pia—sumu ya kadiri ya kwamba nyakati fulani huua mbwa wawashikao na kuwaua vyura hao. Kwa hiyo, laripoti The Wall Street Journal, watumizi fulani wa dawa za kulevya wameogopa wakaacha “kuramba chura” na badala ya hivyo wameingilia “kuvuta moshi wa chura.” Wao hukausha ule mtokotoko wa chura wenye sumu na kuvuta moshi wao, wakiwaza kwamba lile joto litaondoa vijisumu katika mtokotoko huo. Vyovyote vile, sasa ni haramu kuwatumia vyura vibaya. Bufotenini imo katika orodha ya dawa za kulevya zilizo hatari na haramu Marekani. Angalau mwuzaji mmoja amekamatwa. Vyura wake, laripoti Journal, walikamatwa na wenye mamlaka.
Kansa Yaongezeka Miongoni mwa Wanawake Wafaransa
Katika Ufaransa wanawake zaidi wanavuta sigareti kuliko wakati mwingine wowote. Miongoni mwa wavutaji wabalehe, sasa wasichana ni wengi kuliko wavulana, na idadi ya wanawake walio wavutaji wa kupindukia (sigareti zaidi ya 20 kwa siku) imekuwa zaidi ya maradufu tangu 1977. Haishangazi kwamba idadi ya wanawake wanaopatwa na kansa zinazohusiana na kuvuta sigareti inaanza pia kuongezeka sasa. Gazeti la Paris Le Figaro laripoti kwamba kuna visa vipya 20,000 vya kansa ya mapafu katika Ufaransa kila mwaka, na zaidi ya 800,000 duniani pote. Vifo kutokana na kansa ya kikoromeo katika wanawake vimeongezeka mara tatu katika Marekani na Kanada na vikawa zaidi ya maradufu katika Uingereza, Japani, na Sweden. Kwenye mkutano mmoja uliofanywa Paris hivi majuzi kuhusiana na kansa za kupumua, madaktari walikazia kwamba kwa kadiri kubwa “silaha yenye matokeo zaidi dhidi ya kansa zinazohusiana na kuvuta sigareti ni kuacha kuvuta sigareti.”
Kupungua kwa Kanisa Katika Uholanzi
Maelekeo ya sasa yakiendelea, robo tatu za Waholanzi hawatakuwa wa kanisa lolote kufikia mwaka 2020, kulingana na Staatscourant, gazeti rasmi la serikali ya Uholanzi. Uchunguzi mmoja wa hivi majuzi wenye kichwa “Kuingiza Uulimwengu Katika Dini Uholanzi 1966-1991” wapata vikundi vikubwa vinne miongoni mwa halaiki ya Waholanzi: asilimia 28 hawajawa na malezi yoyote ya kidini; asilimia 33 wamekuwa na malezi hayo lakini tangu hapo wakaliacha kanisa; asilimia 28 wamekuwa na malezi ya kidini lakini sasa huhudhuria kanisa mara chache au hawahudhurii kamwe; na ni asilimia 11 tu wahuhudhuriao kanisa mara nyingi. Staatscourant lasema kwamba mpeperuko huo wa kuacha makanisa umekuwa mwingi zaidi miongoni mwa Wakatoliki wa Roma na laeleza hivi: “Maoni ya Wakatoliki wa Roma yaonekana kutofautiana na yale ya viongozi wao wa kidini. Mtu hupata wazo la kwamba mamlaka yao yapuuzwa na washiriki wa kanisa.”