Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g96 10/22 kur. 21-24
  • Sigareti—Je, Wewe Huzikataa?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Sigareti—Je, Wewe Huzikataa?
  • Amkeni!—1996
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Vizuizi Vyawekwa
  • Watoto—Wahasiriwa Wasio na Kinga
  • Maoni Yaliyobadilika
  • Mauzo ya Kwenda Nchi za Nje
  • Mamilioni ya Uhai Yakitokomea Moshini
    Amkeni!—1995
  • Wauzaji wa Kifo—Je! Wewe Ni Mnunuzi?
    Amkeni!—1990
  • Kwa Nini Uache Kuvuta Sigareti?
    Amkeni!—2000
  • Unaweza Kuyavunja Mazoea ya Tumbako
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1975
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1996
g96 10/22 kur. 21-24

Sigareti—Je, Wewe Huzikataa?

Taifa lililosaidia kueneza tumbaku ulimwenguni linaongoza katika kuonya juu ya hatari zayo.

“TUMBAKU,” mwanahistoria mmoja aliandika, “haikuandikwa katika historia kabla ya kuvumbuliwa kwa Amerika.” Wenyeji wa Karibea walimpa Columbus tumbaku. Jamestown, makao ya kwanza ya kudumu ya Uingereza katika Amerika Kaskazini, yalidumu kwa sababu ya kusafirisha nje tumbaku. Mauzo ya tumbaku yalisaidia kudhamini kifedha Mapinduzi ya Marekani. Na marais wa awali wa Marekani George Washington na Thomas Jefferson walikuwa wakuzaji wa tumbaku.

Katika nyakati za majuzi zaidi, sinema za Marekani zimetumia sigareti kuwa ishara ya mapenzi, uvutio, na ya kuwa mwanamume. Wanajeshi wa Marekani waliwapa sigareti watu waliokutana nao katika nchi walizokuwa wakipigana. Na inasemwa kwamba baada ya vita ya ulimwengu 2, sigareti zilitumiwa kama pesa “tokea Paris hadi Peking.”

Lakini hali ilibadilika. Mnamo January 11, 1964, ofisa mkuu wa afya wa Marekani alitoa ripoti yenye kurasa 387 yenye kuhusisha kuvuta sigareti na maradhi ya emphysema, kansa ya mapafu, na maradhi mengine hatari. Upesi sheria ya serikali ikataka kwamba onyo hili “Tahadhari: Kuvuta Sigareti Kwaweza Kudhuru Afya Yako” liwepo kwenye paketi zote za sigareti zinazouzwa Marekani. Sasa, inasemwa kuwa kuvuta sigareti kunasababisha vifo vikadiriwavyo kuwa 434,000 kwa mwaka Marekani. Hiyo inazidi idadi ya Wamarekani wote waliouawa vitani katika karne ambayo imepita!

Vizuizi Vyawekwa

Zaidi ya miaka kumi iliyopita, Aspen, Colorado, mahali papendwapo wakati wa kipupwe, ilikataza kuvuta sigareti katika mikahawa yayo. Tangu wakati huo, sehemu za watu wasiovuta sigareti zimeanza kuwa nyingi katika mikahawa, kazini, na sehemu nyinginezo za umma. Miaka kadhaa iliyopita, mtu mmoja wa California aliuliza binti yake mahali pa kupata sehemu ya wasiovuta sigareti katika mkahawa mmoja wa Virginia. “Baba,” binti huyo akajibu, “hili ni eneo la tumbaku!” Hata hivyo, kufikia wakati alipozuru tena, nusu ya mkahawa huo ilikuwa imehifadhiwa watu wasiovuta sigareti. Hivi majuzi, hakuona mtu yeyote mwenye kuvuta sigareti huko.

Lakini kutenganisha sehemu za wenye kuvuta sigareti hakujasuluhisha tatizo hilo. Mabango makubwa ya serikali kando-kando ya barabara-kuu za California yaliuliza hivi: “Je, wafikiri moshi wajua kwamba unapaswa ubaki katika sehemu ya wavutaji wa sigareti pekee?”

New York City lilipopiga marufuku kuvuta sigareti katika mikahawa yayo mikubwa, wenye mikahawa waliteta kwamba kufanya hivyo kungeondosha watalii kutoka Ulaya ambako, wao walisema, kuna sheria chache dhidi ya kuvuta sigareti. Lakini, uchunguzi mmoja uliofanywa mapema ulipata kwamba asilimia 56 ya Wamarekani walielekea zaidi kwenda kwenye mkahawa wa wasiovuta sigareti, huku asimilia 26 pekee ambao hawangeelekea kwenda huko.

Ishara moja katika reli ya chini ya ardhi ya New York City yasema: “Ujumbe u wazi katika lugha yoyote ile: Usivute sigareti wakati wowote, mahali popote, katika stesheni zetu au katika magari-moshi yetu. Asanteni.” Ishara hiyo yataja ujumbe huo si kwa Kiingereza tu bali pia katika lugha nyinginezo 15.

Je, kuvuta sigareti ni jambo zito kadiri hiyo? Ndiyo. Ikiwa watu 300 wangekufa katika msiba mmoja mkuu, jambo hilo lingekuwa habari za kutangazwa kwa siku nyingi, hata kwa majuma. Lakini makala moja katika The Journal of the American Medical Association ilisema imekadiriwa kwamba Wamarekani 53,000 hufa kila mwaka kwa sababu ya matokeo ya baadaye ya kupumua moshi wa sigareti za watu wengine. Lilisema kwamba kupumua moshi wa tumbaku kutoka kwa mtu mwingine, ni “kiongozi cha tatu katika kusababisha vifo ambacho chaweza kuzuiwa, kikifuata kuvuta sigareti na alkoholi.”

Watoto—Wahasiriwa Wasio na Kinga

Namna gani kuvuta sigareti nyumbani? Kichapo cha serikali ya Marekani, Healthy People 2000, ambacho kina lengo la kupunguza “kifo cha mapema na maradhi na ulemazo uwezao kudhibitiwa,” chasema: “Matumizi ya tumbaku husababisha zaidi ya kifo kimoja kati ya vifo sita Marekani na ndicho kisababishi kimoja kikuu ambacho chaweza kuzuiwa cha vifo na maradhi katika jumuiya yetu.”

Kiliongezea hivi: “Kuvuta sigareti wakati wa mimba hufanya asilimia 20 hadi 30 ya watoto wazaliwe wakiwa na uzani mdogo kuliko kawaida, kufikia asilimia 14 ya watoto kuzaliwa kabla ya wakati wao, na kusababisha asilimia 10 hivi ya vifo vyote vya vitoto vichanga.” Akina mama ambao huvuta sigareti, hicho kilisema, waweza kupitisha sehemu zilizo kuu za moshi wa tumbaku, si kwa kunyonyesha kitoto kichanga tu bali pia kwa “kukiweka kitoto kichanga katika chumba ambacho sigareti imevutwa punde tu.”

Akina baba wamehusika pia. Kichapo hicho-hicho kilishauri hivi: “Ikiwa ni lazima watu ambao huchangamana na watoto wavute sigareti, wanapaswa kuvuta nje au katika maeneo ambayo hayaenezi hewa hiyo mahali ambapo huenda mtoto yupo.” Madhara kwa watoto huongezeka kwa ongezeko la watu wazima wanaovuta sigareti katika chumba kilekile na kwa idadi ya sigareti zilizovutwa. Hivyo, Joycelyn Elders, aliyekuwa ofisa mkuu wa afya wa Marekani, alisema: “Watoto wako ndio wahasiriwa wasio na hatia wa uraibu wako.”

Watu wengine wamo hatarini pia. Tangazo moja la biashara lenye kudhaminiwa na serikali katika televisheni katika California lilionyesha mzee mmoja akiwa ameketi peke yake. Alisema kwamba sikuzote mke wake alikuwa ‘akimhimiza aache kuvuta.’ “Hata alinitisha kwamba ataacha kunibusu nikikataa kuacha. Nikamwambia mapafu ni yangu, na uhai ni wangu. Lakini nilikosea. Sikuacha. Sikujua kwamba uhai ambao ungepotea haukuwa wangu . . . Ulikuwa uhai wake.” Akitazama picha yake kwa huzuni, mzee huyo akasema: “Mke wangu alikuwa uhai wangu.”

Maoni Yaliyobadilika

Maonyo kama hayo yamechangia upungufu mkubwa wa uvutaji katika Marekani. Kwa kushangaza, Wamarekani wapatao milioni 46—asilimia 49.6 kati ya wale waliopata kuvuta sigareti—wameacha!

Hata hivyo, makampuni ya tumbaku yanatumia fedha nyingi sana katika matangazo ya biashara nayo yanapigana. Ule upungufu wa kuacha sigareti umepungua. Joseph A. Califano, Jr., wa Kituo cha Uraibu na Viraibishaji kwenye Chuo Kikuu cha Columbia katika New York, alisema: “Tisho kubwa zaidi kwa afya ya umma kutokana na biashara ya tumbaku [ni] matumizi yayo ya matangazo na mbinu za biashara zinazolenga watoto na matineja ambao ni waraibu wapya kwa vitu vyayo vyenye kufisha.”

Jarida The Journal of the American Medical Association lilisema: “Vijana wanaokadiriwa kuwa 3000, wengi wao wakiwa watoto na matineja, kila siku huanza uvutaji wa sigareti wa kawaida. Hiyo ni karibu wavutaji wapya milioni 1 kila mwaka ambao kwa sehemu huchukua mahali pa wavutaji wakadiriwao kuwa milioni 2 ambao ama huacha kuvuta ama hufa kila mwaka.”

Zaidi ya nusu ya wavutaji wote wa Marekani huanza kuvuta kufikia umri wa miaka 14. David Kessler, kamishna wa Usimamizi wa Chakula na Dawa wa Marekani, alisema kwamba kati ya watoto 3,000 ambao huanza kuvuta sigareti kila siku, karibu 1,000 hatimaye watakufa kutokana na magonjwa yanayohusika na kuvuta sigareti.

Ikiwa tarakimu hizo zinakushangaza, ingekuwa vizuri kukumbuka kwamba watoto wetu hufuata kielelezo tunachowawekea. Ikiwa hatutaki wavute, sisi pia hatupaswi kuvuta.

Mauzo ya Kwenda Nchi za Nje

Ingawa matumizi ya sigareti katika Marekani yamepunguka, soko la kimataifa linakua. Gazeti Los Angeles Times liliripoti kwamba “mauzo ya kwenda nchi za nje yameongezeka zaidi ya mara tatu na mauzo kutoka viwanda vya tumbaku vya Marekani yameongezeka sana.” Jarida The New England Journal of Medicine lilisema kwamba katika nchi zinazoendelea “hatari za kuvuta hazitiliwi mkazo sana,” jambo linaloruhusu makampuni ya tumbaku “kupenya masoko ya kigeni upesi.”

Lakini, Patrick Reynolds, mwana wa R. J. Reynolds, Jr., aliye pia mzao wa mwanzilishi wa kampuni inayotengeneza sigareti ziitwazo Camel na Winston, alisema kwamba kifo 1 kati ya vifo 5 Marekani husababishwa na kuvuta sigareti. Reynolds aliripotiwa pia kwamba alisema kuvuta sigareti husababisha vifo vingi kila mwaka kuliko kokeini, alkoholi, heroini, moto, ujiuaji-kimakusudi, mauaji, UKIMWI, na aksidenti ya magari zikijumlishwa pamoja na kwamba ndicho kisababishi kikuu cha kifo, maradhi, na uraibu ambacho chaweza kuzuiwa kuliko vyote katika enzi yetu.

Je, laonekana kuwa jambo lisilo la kawaida kwamba taifa lililofundisha ulimwengu kuvuta sasa limesitawisha upinzani wa kitaifa dhidi ya tumbaku? Ikiwa hivyo, ni vizuri tujiulize, ‘Ni nani ajuaye zaidi?’

Gazeti Modern Maturity lilisema juu ya mwanamke mmoja ambaye alikuwa amevuta sigareti kwa zaidi ya miaka 50. Alisema hivi: “Ukinaswa, umenaswa.” Lakini aliondolea mbali ule uvutio uliofanya aanze kuvuta sigareti mwanzoni, akaacha.

“Jaribu kuacha sigareti,” akaandika. “Utahisi vizuri sana.”

[Blabu katika ukurasa wa 21]

“Imekadiriwa kwamba katika miaka ya 1990 katika nchi zilizoendelea, tumbaku itasababisha asilimia zipatazo 30 za vifo vyote miongoni mwa watu wenye umri wa miaka 35 na 69, ikifanya hiyo kuwa kisababishi kikuu cha pekee cha vifo vya mapema katika nchi zilizoendelea.”—NEW ENGLAND JOURNAL OF MEDICINE

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 22]

MAONYO JUU YA KANSA

Maonyo yafuatayo yametolewa na broshua za Shirika la Kansa la Marekani za Facts on Lung Cancer na Cancer Facts & Figures—1995:

• “Wake wasiovuta sigareti wamo hatarini zaidi kwa asilimia 35 ya kupatwa na kansa ikiwa waume zao huvuta sigareti.”

• “Visa vya kansa ya mapafu vikadiriwavyo kuwa asimilia 90 katika wanaume na asilimia 79 katika wanawake husababishwa na kuvuta sigareti.”

• “Kwa wale ambao huvuta pakiti mbili kila siku na ambao wamevuta kwa zaidi ya miaka 40, vifo vya kansa ya mapafu vinazidi kwa mara zaidi ya 22 kuliko wasiovuta.”

• “Ulinzi bora dhidi ya kansa ya mapafu ni kutoanza kamwe kuvuta, au kuacha mara hiyo.”

• “Hakuna kitu kama sigareti isiyodhuru.”

• “Kutafuna tumbaku au kunusa ugoro huongeza uwezekano wa kupata kansa ya mdomo, zoloto, koo, na umio nako ni tabia yenye kuraibisha kabisa.”

• “Hatari zaidi ya kansa ya shavu na ufizi yaweza kuongezeka kwa karibu mara 50 miongoni mwa watumiaji wa muda mrefu.”

• “Watu ambao huacha kuvuta sigareti, hata wawe na umri gani, huishi muda mrefu kuliko wale ambao huendelea kuvuta sigareti. Wavutaji ambao huacha kuvuta kabla ya umri wa miaka 50 wana uwezo wa kuendelea kuishi kwa miaka 15 ijayo kwa asilimia 50 kwa kulinganisha na wale ambao huendelea kuvuta.”

[Sanduku katika ukurasa wa 24]

TATIZO LA MKULIMA

Kwa vizazi vingi tumbaku imetegemeza familia ambazo mashamba yao yamekuwa madogo sana kuweza kuandaa riziki kwa mazao mengine. Bila shaka, jambo hili hutokeza tatizo la dhamiri kwa watu wengi. Stanley Hauerwas, profesa wa maadili ya kitheolojia kwenye Chuo Kikuu cha Duke, chuo ambacho kilianzishwa na tajiri mmoja wa tumbaku, alisema hivi: “Nafikiri uchungu mkubwa wa watu wanaokuza tumbaku ni . . . walipoanza kuikuza, hawakujua ingeweza kuua mtu.”

[Picha katika ukurasa wa 23]

Moshi haubaki katika sehemu ya wenye kuvuta pekee

[Picha katika ukurasa wa 23]

Kuvuta wakati wa mimba husababisha asilimia 10 hivi ya vifo vyote vya vitoto vichanga

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki