Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g90 3/8 kur. 6-9
  • Wauzaji wa Kifo—Je! Wewe Ni Mnunuzi?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Wauzaji wa Kifo—Je! Wewe Ni Mnunuzi?
  • Amkeni!—1990
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Kwa Nini Walivuta Sigareti?
  • Je! WEWE Ni Shabaha Yenye Kulengwa?
  • Ile Shabaha Yenye Kubagua Rangi
  • Mamilioni ya Uhai Yakitokomea Moshini
    Amkeni!—1995
  • Sigareti—Je, Wewe Huzikataa?
    Amkeni!—1996
  • Unaweza Kuyavunja Mazoea ya Tumbako
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1975
  • Maoni ya Kikristo Juu ya Kuvuta Sigareti
    Amkeni!—1990
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1990
g90 3/8 kur. 6-9

Wauzaji wa Kifo—Je! Wewe Ni Mnunuzi?

“Yule jamaa mwenye kuvuta amepewa maonyo ya namna zote kwamba kitu hiki kitakuua, nami nafikiri ivyo hivyo. Mimi nafikiri kitakuua. Nafikiri kwamba mpumbavu yeyote mwenye kuteremsha moshi katika tumbo lake atateseka. Mimi sijapata kamwe kuvuta sigareti maishani mwangu. Nimejitengenezea pesa nyingi kutokana nazo. . . . Njia moja tu tuliyotumia ili kujenga nchi hii ni kwa kuwauzia tumbako wapumbavu wale wengine wote waliomo ulimwenguni.”—James Sharp, mkuza-tumbako wa muda mrefu katika Kentucky, akiongea katika “Merchants of Death—The American Tobacco Industry,” kilichotungwa na Larry C. White.

ELEZO hilo lenye kutoboa mambo wazi lanena mengi lakini laacha maswali kadhaa bila kujibiwa. Kwa nini watu zaidi ya bilioni moja kuzunguka ulimwengu huvuta sigareti? Ni nini huwashurutisha waendelee na tabia ambayo yajulikana kuwa yenye kuua? Ingawaje, kwa msingi hali ya tumbako ni sawa na ile ya dawa za kulevya—kuna wenye kuigawa na wenye kuidai. Soko lisipoleta faida, hapo ugawanyaji hukauka. Kwa hiyo ni kwa nini watu huvuta sigareti?

Uzoelevu ndilo neno kubwa. Nikotini ikiisha kutia mzizi imara katika mwili, kila siku huwa kuna uhitaji wa kutumia kadiri fulani za nikotini kwa ukawaida. Uzoelevu huo waungana na tabia ya kuzoea. Hali fulani, zenye kukwamishwa na tabia, huchochea ile tamaa ya kutaka sigareti. Huenda mtu akafanya hivyo mara tu akiamka au huenda akafanya hivyo pamoja na kikombe cha kwanza cha chai ya asubuhi, kinywaji kifuatacho mlo wa mchana, baada ya mbano wa kazi na maongezi ya starehe kule kazini, au katika tafrija. Tabia nyingi ambazo huonekana kuwa zisizo za maana sana zaweza kuwa ndizo huchochea uvutaji.

Kwa Nini Walivuta Sigareti?

Amkeni! ilihoji watu kadhaa waliokuwa wavuta sigareti hapo kwanza ili kujaribu kuelewa kilichowasukuma kuvuta. Kwa kielelezo, yuko Ray, aliye katika miaka yake ya 50, ambaye hapo kwanza alikuwa ofisa mtumikia-manahodha katika Jeshi-Bahari la United States. Yeye alieleza hivi: “Mimi nilikuwa na karibu miaka 9 nilipovuta sigareti mara ya kwanza, lakini uvutaji wangu ulichacha nilipokuwa na miaka 12. Nakumbuka kwamba nilifukuzwa kutoka Kikosi cha Maskauti Wavulana kwa sababu ya kuvuta sigareti.”

Amkeni!: Ni nini kilifanya upendezwe na kuvuta sigareti?”

Ray: “Kuvuta kulikuwa uanaume. Wajua, mtu alionwa kuwa dume kwa kuvuta. Nakumbuka kwamba siku hizo matangazo ya kibiashara yaliwaonyesha wazima-moto na polisi wakivuta. Halafu baadaye katika Jeshi-Bahari, nikawa na kazi yenye mibano mingi ya kupeleleza bahari, nami nikahisi kwamba kuvuta sigareti kulinisaidia kuvumilia mkazo huo.

“Nilikuwa nikivuta karibu pakiti moja na nusu kwa siku [sigareti 30] nami nisingeanza siku bila sigareti yangu. Nilivuta moshi kweli kweli. Hakuna haja ya kuvuta sigareti ikiwa huvuti moshi ndani.”

Bill, msanii wa kutoka New York, ambaye pia yumo katika miaka yake ya 50, asimulia hadithi kama hiyo:

“Mimi nilianza nikiwa mtoto wa miaka 13. Nilitaka kuwa kama watu wazima. Uvutaji uliponishika kabisa, sikuweza kuacha. Kuwa na sigareti kulikuwa kama kuwa na rafiki. Kwa uhakika, kama ningekuwa nikienda kulala na ning’amue kwamba sikuwa na sigareti ndani ya nyumba, ningevaa tena na, bila kujali hali ya hewa ilikuwaje, ningeenda nje na kununua pakiti kwa ajili ya kesho. Nilikuwa nikivuta kuanzia pakiti moja hadi mbili kwa siku. Nakiri kwamba niliingiwa na uzoelevu. Tena wakati huo nilikuwa mnywaji wa kupindukia. Mambo yote mawili yalionekana yakiambatana vizuri, hasa katika mabaa ambamo nilitumia mwingi wa wakati wangu.”

Amy, ambaye ni kijana na mwenye urafiki, alianza kuvuta sigareti alipokuwa msichana wa miaka 12. “Kwanza marika ndio walinibana. Halafu, baba yangu alikufa nilipokuwa na miaka 15, na mkazo wa jambo hilo ukanisukuma mbele zaidi. Lakini nilipoongezeka umri, matangazo ya kibiashara yaliniingiza uvutano, hasa lile lenye kusema, ‘Umetoka mbali, kipenzi.” Mimi nilikuwa msichana mwenye kufuatia kazi-maisha, nikisomea uuguzi wa kupasua. Muda si muda nikawa nikivuta pakiti tatu kwa siku. Wakati wangu mzuri sana wa kuvuta sigareti ulikuwa baada ya mlo mkuu wa siku na wakati wowote nilipokuwa kwenye simu, na ilikuwa mara nyingi.” Je! yeye aliona athari zozote mbaya? “Mimi nilikuwa na kikohozi cha asubuhi na maumivu ya kichwa, na mwili wangu haukuwa tena katika hali nzuri. Kupanda tu vidato vya ngazini ili kwenda kwenye kijumba changu kulinimaliza pumzi. Nami nilikuwa wa miaka 19 tu!”

Harley, aliyekuwa mrukaji katika Jeshi-Bahari, ambaye sasa yumo katika miaka yake ya 60, alianza kuvuta wakati wa ule Mshuko wa Thamani ya Pesa akiwa na miaka 5! Kwa nini akafanya hivyo? “Watoto wote walivuta sigareti katika Aberdeen, Dakota Kusini, ambako mimi nilitoka. Mtu mwenye kuvuta alionwa kuwa kabambe siku hizo.”

Harley atoboa wazi sababu yake ya kuvuta. “Ilikuwa ili nione raha tu. Nilikuwa nikivuta moshi ule mpaka chini kwenye mapafu yangu na kuuzuilia humo. Halafu nikawa nikipenda kupuliza moshi ili uonekane ukifanyiza miviringo-viringo. Nilifikia hatua ambayo singeweza kuishi bila sigareti yangu. Nilianza siku na kuimaliza nikiwa na sigareti. Katika Jeshi-Bahari, nilikuwa nikivuta pakiti mbili hadi tatu kwa siku na sanduku la sigara (sigari) kila mwezi.”

Bill, Ray, Amy, na Harley waliacha kuvuta sigareti. Ndivyo na mamilioni ya wengine—zaidi ya milioni 43 katika United States pekee. Lakini wauzaji wa tumbako hawajaacha. Wao wanalenga shabaha kwenye masoko mapya wakati wote.

Je! WEWE Ni Shabaha Yenye Kulengwa?

Huku wavutaji wengi wa kiume wakiwa wanaacha kuvuta sigareti katika mataifa yenye maendeleo ya viwandani, kuongeza na potezo la wanunuzi kupitia kifo cha kiasili na chenye kusababishwa na uvutaji sigareti, kampuni za tumbako zimelazimika kutafuta masoko mapya. Katika visa fulani zimebadili mbinu za matangazo yazo kwa jitihada ya kuimarisha mauzo. Kudhamini matukio ya michezo, kama vile mashindano makubwa ya tenisi na golfu, ni njia yenye matokeo ya kufanya uvutaji sigareti uonekane kuwa wa kusifika. Rekebisho jingine la mbinu ya kutumia ni masoko yenye kulengwa shabaha. Je! wewe ni mmoja wa wale wawezao kuwa wanunuzi wao?

Shabaha namba moja: Wanawake. Wanawake wachache wamevuta sigareti kwa miongo ya miaka, wakisaidiwa na kutiwa moyo na kielelezo cha mabibi walio mabingwa wa kuigiza filamu kama vile Gloria Swanson, ambaye kule nyuma katika 1917 alikuwa akivuta sigareti akiwa na miaka 18. Kwa uhakika, yeye alipata moja ya nafasi zake za kwanza za kuigiza filamu kwa sababu, kama mkurugenzi alivyoliweka wazo lenyewe: “Nywele zako, uso wako, njia yako ya kuketi, njia yako ya kuvuta sigareti . . . Wewe uko kama vile nitakavyo hasa.”

Katika miaka ya 1940 Lauren Bacall, aliyeshiriki filamu mbalimbali pamoja na mume wake, Humphrey Bogart mvutaji wa kupindukia, alikuwa na umashuhuri wa kuvutia kuhusu kuvuta sigareti. Lakini sikuzote upande wa wanawake wa soko la sigareti ukaendelea kuachwa nyuma na soko la wanaume. Ndivyo na takwimu za wanawake wenye kupata kansa. Sasa zinaongezeka mbio zikaribiane na za wanaume—katika kuvuta sigareti na katika kansa ya mapafu.

Katika miaka ya majuzi kumesitawi elekeo jipya katika matangazo ya kibiashara, kwa sehemu sababu ikiwa ni lile fungu la ushindani wa wanawake katika jamii pamoja na uvutano wenye ujanja usioonekana wazi katika matangazo ya tumbako. Ni ujumbe gani ambao wanawake wanapelekewa? Kampuni ya Philip Morris, ambayo hutengeneza unamna-namna wa aina za sigareti, hufanyiza “Virginia Slims” (Sigareti Nyembamba za Virginia), ambazo hulenga shabaha kwenye mwanamke wa ki-siku-hizi. Shime ya kampuni hiyo ndiyo ilimvutia Amy: “Umetoka mbali, kipenzi.” Tangazo hilo la kibiashara huonyesha mwanamke mmamboleo wa ki-siku-hizi akiwa na sigareti kati ya vidole vyake. Lakini sasa ni lazima wanawake fulani wawe wanajiuliza wametoka umbali gani. Muda wa miaka miwili iliyopita, kansa ya mapafu imeizidi kansa ya matiti katika kadiri ya vifo vya wanawake.

Aina nyingine ya sigareti hutolea wanawake toleo hili: “5 za bure kwa kila pakiti!” “50 za bure kwa kila kartoni!” Magazeti fulani ya wanawake hata hutia ndani kuponi [hati za kujazwa] ili kupata pakiti za bure!

Ngono ni njia nyingine rahisi ya kufanya sigareti zionekane kuwa zavutia. Aina moja hutoa mwaliko huu: “Pata Raha Zaidi.” Ujumbe uliopo ni kutia na tangazo la kutaka watu, lenye kutaarifu hivi: “ATAKIWA—Mtu mrefu asiyejulikana, wa rangi iliyokolea, kwa uhusiano mrefu wa kudumu. Awe mwenye sura nzuri, na ni lazima avutie sana. Katiwa Sahihi, Kwa Hamu Nyingi ya Kutafuta Utoshelevu wa Kuvuta Sigareti.” Sigareti yenye kutangazwa huja ikiwa ‘ndefu’ na katika karatasi ya rangi iliyokolea. Je! hiyo yahusiana na ujanja fulani usioonekana wazi?

Chambo kingine ambacho hutumiwa kunasa wanawake ni njia zenye kuhusianishwa na mitindo. Aina moja ya sigareti hushangiliwa kuwa “Mtindo na ladha bora kabisa iliyofanyizwa na YVES SAINT LAURENT.” Chambo kingine hutumiwa kwa wanawake wenye kutaka sana kupoteza uzito wa mwili. Lile tangazo la kibiashara huonyesha foto ya mwanamke mwenye wembamba mzuri sana, na sigareti hizo huelezwa kuwa ni “Vivutwaji Bora Zaidi—Mtindo bora zaidi kwa wasiotaka ratili nyingi.”

Kwa nini watengeneza sigareti wanawalenga shabaha wanawake wa ulimwengu? Tengenezo la Afya Ulimwenguni latoa dokezo la wazi kwa kadirio lalo la kwamba ni “zaidi ya asilimia 50 ya wanaume lakini ni asilimia tano tu ya wanawake ambao huvuta sigareti katika nchi zinazositawi kwa kulinganishwa na karibu asilimia 30 ya jinsia zote mbili katika nchi zenye maendeleo ya viwandani.” Huko nje kuna soko kubwa sana (wanunuzi wengi) ambalo halijatumiwa bado ili kutafuta faida zenye kutokana na tumbako, bila kujali gharama ambayo huenda mwishowe ikalazimika kulipwa kwa kuharibikiwa na afya. Na wauzaji wa tumbako wanapata mafanikio. Kulingana na The New York Times, ripoti ya mpasuaji mkuu wa United States, iliyotolewa katika Januari 1989, ilitaarifu kwamba ‘watoto, hasa wasichana, wanavuta sigareti wakiwa na umri mchanga zaidi’ na hiyo yatia ndani watoto wa shule za msingi. Chanzo kingine chasema kwamba katika miaka ya majuzi hesabu ya matineja wa kike walio wavutaji katika United States imeongezeka kwa asilimia 40. Lakini si wanawake tu walio shabaha ya wauzaji hao wa kifo na magonjwa.

Ile Shabaha Yenye Kubagua Rangi

Katika kitabu chake Merchants of Death—The American Tobacco Industry, Larry C. White ataarifu hivi: “Weusi ni soko zuri la wafanyiza sigareti. Kitovu cha Kitaifa cha Takwimu za Afya chaonyesha kwamba kufikia 1986, asilimia kubwa ya weusi walivuta kwa wingi kuliko weupe [katika United States] . . . Haishangazi kwamba weusi huvuta kwa wingi kuliko weupe, kwa sababu wao ni shabaha za pekee za kuendeleza uvutaji sigareti.” Kwa nini wao ni shabaha za pekee? Kulingana na The Wall Street Journal, wao ni “kikundi ambacho hubakia nyuma ya halaiki ya watu kwa ujumla katika kuiachilia mbali tabia hiyo.” Kwa hiyo, mara nyingi mteja mweusi huwa ni mteja “mwaminifu-mshikamanifu,” ‘mpaka kifo kitakapotutenganisha.’

Kampuni za tumbako hukazaje fikira zote juu ya idadi ya weusi? Mtungaji White ataarifu hivi: “Sigareti hutangazwa sana katika magazeti yenye kuendea weusi kama vile Ebony, Jet, na Essence. Katika 1985 kampuni za sigareti zilitumia dola milioni 3.3 kuhusiana na matangazo ya kibiashara katika Ebony tu.” Kampuni moja ya tumbako huendeleza pia onyesho fulani la kila mwaka ambalo huelekezwa kwenye soko la wanawake weusi. Wao hupewa sigareti za bure. Wakati mmoja kampuni nyingine ilidhamini kwa ukawaida sikukuu fulani ya muziki wa jazi na ikaendelea kuunga mkono sikukuu za muziki ambazo hupendwa sana na weusi. Idadi ya weusi ni shabaha ya pekee kwa kadiri gani? Mnenaji mmoja wa kampuni ya Philip Morris alitaarifu hivi: “Soko la weusi ni la maana sana. Lina matokeo sana.”

Lakini kuna soko lililo la maana hata zaidi kwa mashirika ya tumbako yaliyo makubwa sana—wala si vikundi vya watu wa rangi fulani tu bali ni mataifa mazima-mazima!

[Blabu katika ukurasa wa 7]

“Kuwa na sigareti kulikuwa kama kuwa na rafiki”

[Sanduku katika ukurasa wa 9]

UVUTAJI SIGARETI na Ugonjwa wa Buerger

Kisa kimoja cha hivi majuzi katika Kanada, kilichoripotiwa na Maclean’s, chakazia ugonjwa mwingine bado wenye kuhesabiwa kuwa watokana na kuvuta sigareti. Roger Perron alianza kuvuta sigareti akiwa na miaka 13. Kufikia umri wa miaka 27, alikuwa na ugonjwa wa Buerger na akalazimika kukatwa mguu mmoja chini ya goti. Alionywa kwamba akiendelea kuvuta sigareti, ugonjwa huo ungeweza kumshambulia tena. Maclean’s yaripoti hivi: “Lakini Perron alipuuza onyo hilo, na katika 1983 madaktari wakalazimika kukata mguu wake ule mwingine. Baada ya hapo, Perron . . . mwishowe aliacha kuvuta sigareti.” Sasa yeye ana shtaka la kisheria la kutaka kampuni ya tumbako imlipe kwa hasara zilizompata.

Ugonjwa wa Buerger ni nini? Huo “hutukia mara nyingi zaidi katika wanaume wenye kuvuta sigareti. Ugonjwa huo huonyeshwa na mifuro yenye kuwasha katika mishipa-arteri, mishipa-vena, na mishipa ya fahamu, na hiyo hufanya kuta za mishipa ya damu zinenepe kwa sababu ya kupenywa na chembe nyeupe. Kwa kawaida dalili za kwanza huwa ni sura ya kibuluu katika kidole cha mguu au cha mkono na hisia yenye baridi katika kiungo chenye kuathiriwa. Kwa kuwa mishipa ya fahamu hufura na kuwasha, huenda kukawa na maumivu makali na kufinyana kwa mishipa midogo ya damu ambayo hudhibitiwa na hiyo mingine. Pia mishipa ya fahamu yenye kufinyana kupita kiasi yaweza kusababisha nyayo za miguu zitoe jasho jingi kupita kiasi, hata ingawa nyayo hizi zahisi ubaridi. . . . Vidonda na donda-ndugu lenye kuhusiana na upungufu wa damu ni matatanisho ya kawaida ya ugonjwa wenye kuendelea wa Buerger.

“Kisababishi cha ugonjwa wa Buerger hakijulikani, lakini kwa kuwa hutukia sana-sana katika wanaume vijana ambao huvuta sigareti, huo hufikiriwa kuwa ni tokezo la utendaji wa kitu fulani kilicho katika sigareti. Utibabu ulio wa maana zaidi ni kuacha kuvuta sigareti.” (Italiki ni zetu.)—The Columbia University College of Physicians and Surgeons Complete Home Medical Guide.

[Sanduku katika ukurasa wa 9]

UVUTAJI SIGARETI na Magonjwa ya Ghafula ya Moyo

“Ingawa watu walio wengi wana habari sana juu ya uhusiano uliopo kati ya uvutaji sigareti na kansa ya mapafu na magonjwa mengine ya mapafu, wengi wangali hawang’amui kwamba kuvuta sigareti ni kisababishi kikubwa cha hatari ya kupatwa na magonjwa ya ghafula ya moyo pia. Kwa uhakika, . . . ripoti ya Mpasuaji Mkuu kuhusu Uvutaji Sigareti na Afya yakadiria kwamba 225,000 kati ya vifo vya Amerika [United States] kutokana na ugonjwa wa mishipa ya moyo kila mwaka vyahusiana moja kwa moja na kuvuta sigareti—hivyo vikiwa ni vingi sana kuliko jumla ya hesabu ya vifo vyenye kutokana na kansa na magonjwa ya mapafu ambayo huhesabiwa kutokana na uvutaji sigareti.

“Mara nyingi wavuta sigareti huuliza kama sigareti zenye lami na nikotini ya kadiri ndogo hupunguza ile hatari yenye kuhusiana na mishipa ya moyo. Jibu laonekana kuwa ‘sivyo.’ Kwa uhakika, baadhi ya sigareti zenye kichungi cha vitu hivyo huongezea kiasi cha kaboni monoksaidi ambayo huvutwa ndani, hiyo ikizifanya ziwe mbaya zaidi kwa moyo kuliko zile aina zisizo na kichungi cha vitu hivyo.” (Italiki ni zetu.)—The Columbia University College of Physicians and Surgeons Complete Home Medical Guide.

[Picha katika ukurasa wa 8]

Matangazo ya tumbako yanalengwa shabaha kwenye wanawake na yanapata matokeo

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki