Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g95 5/22 kur. 3-7
  • Mamilioni ya Uhai Yakitokomea Moshini

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Mamilioni ya Uhai Yakitokomea Moshini
  • Amkeni!—1995
  • Habari Zinazolingana
  • Sigareti—Je, Wewe Huzikataa?
    Amkeni!—1996
  • Wauzaji wa Kifo—Je! Wewe Ni Mnunuzi?
    Amkeni!—1990
  • Watetea Tumbaku Waanzisha Puto la Hewa-Joto
    Amkeni!—1995
  • Makampuni ya Tumbaku Yamo Motoni
    Amkeni!—1996
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1995
g95 5/22 kur. 3-7

Mamilioni ya Uhai Yakitokomea Moshini

NDIYO bidhaa yenye kuuzwa sana ulimwenguni. Hutawala halaiki ya wanunuzi washikamanifu na hufaidika kutokana na soko layo yenye kupanuka haraka. Makampuni yanayoibuni hujishaua kwa faida kubwa, na uwezo mkubwa wa kumiliki, na umaarufu. Tatizo pekee ni kwamba, wateja wayo bora zaidi huendelea kufa!

The Economist lilionelea hivi: “Sigareti ni miongoni mwa bidhaa zenye kuuzwa sana zenye faida mno ulimwenguni. Na pia ndizo peke yazo (zenye uhalali) ambazo, zikitumiwa kama zilivyonuiwa, hufanya wengi wa wavutaji wazo kuwa waraibu na mara nyingi kuwaua.” Hili humaanisha faida kubwa kwa makampuni ya tumbaku lakini hasara kubwa kwa wateja wao. Kulingana na Vitovu vya Kudhibiti Maradhi na Kuzuia vya Marekani, yapata miaka milioni tano ya uhai hukatwa kutoka kwenye uhai wa wavutaji sigareti wa Marekani kila mwaka, yakadiriwa kuwa dakika moja ya urefu wa maisha kwa kila dakika inayotumiwa kuvuta sigareti. “Kuvuta sigareti huua Wamarekani 420,000 kwa mwaka,” laripoti gazeti Newsweek. “Hiyo ni mara 50 zaidi kuliko dawa za kulevya.”

Ulimwenguni pote, watu milioni tatu kwa mwaka—watu sita kila dakika—hufa kutokana na uvutaji sigareti, kulingana na kitabu Mortality From Smoking in Developed Countries 1950-2000, kilichotangazwa na Wakf wa Kiserikali wa Utafiti wa Kansa wa Uingereza, WHO (Shirika la Afya Ulimwenguni), na Sosaiti ya Kansa ya Marekani. Uchanganuzi huu wa tabia za uvutaji sigareti ulimwenguni, unaofahamika zaidi kufikia kipindi cha sasa, hushughulika na nchi 45. “Katika nchi zilizo nyingi,” aonya Richard Peto wa Wakf wa Kiserikali wa Utafiti wa Kansa, “hali itaendelea kuwa mbaya zaidi. Ikiwa mwelekeo wa sasa wa uvutaji sigareti utaendelea, basi kufikia wakati mvutaji sigareti mchanga wa leo atakapofikia umri wa makamo ama uzeeni, kutakuwa na karibu vifo milioni 10 kwa mwaka kutokana na tumbaku—kifo kimoja kwa kila sekunde tatu.”

“Kuvuta sigareti ni afa lisilolinganika,” akasema Dakt. Alan Lopez wa WHO. “Hatimaye litaua mmoja kati ya kila wavutaji sigareti wawili.” Martin Vessey wa Idara ya Afya ya Umma kwenye Chuo Kikuu cha Oxford asema vivyo hivyo: “Uchunguzi huu kwa kipindi cha zaidi ya miaka 40 uliongoza kwenye mkataa wenye kuogofya kwamba nusu moja ya wavutaji sigareti hatimaye watauawa na zoea lao—ni wazo lenye kuogofya kwelikweli.” Tangu miaka ya 1950, watu milioni 60 wamekufa kutokana na kuvuta sigareti.

Pia ni wazo lenye kuogofya kwelikweli kwa makampuni ya tumbaku. Ikiwa watu milioni tatu ulimwenguni pote kila mwaka wanakufa kutokana na visababishi vinavyohusiana na uvutaji sigareti, na wengine wengi huacha sigareti, kisha watumiaji wengine wapya wapitao milioni tatu ni lazima wapatikane kila mwaka.

Chanzo kimoja kimezuka kwa sababu ya kile makampuni ya tumbaku hushangilia kuwa uhuru wa wanawake. Uvutaji sigareti wa wanawake umekuwa uhakika uliotimizwa kwa miaka kadhaa katika mabara ya Magharibi na sasa waenea kwenye maeneo ambapo uvutaji sigareti na wanawake ulionekana kama mwiko. Makampuni ya tumbaku yanuia kubadili hayo yote. Wanataka kuwasaidia wanawake washerehekee wingi na uhuru walioupata. Aina za kipekee za sigareti zinazodaiwa kuwa zenye kiasi kidogo cha tumbaku na nikotini ya kiasi cha chini hushawishi wanawake wanaovuta sigareti na wanaopata moshi kama huo kuwa usio mbaya sana. Sigareti nyingine zimewekwa uturi au zina ubuni mrefu na mwembamba—umbo ambalo wanawake huenda watumaini kulifikia kwa uvutaji wa sigareti. Matangazo ya kibiashara ya tumbaku katika Asia huonyesha violezo vya kuigwa vya visichana vya Kiasia vikiwa vimevaa kwa ushawishi katika mvalio wa Magharibi.

Hata hivyo, viwango vya vifo vinavyohusiana na uvutaji sigareti, vyaenda sambamba na “uhuru” wa wanawake. Idadi ya majeruhi wa kansa ya mapafu miongoni mwa wanawake imerudufika katika miaka 20 iliyopita katika Uingereza, Japani, Norway, Poland, na Sweden. Katika Marekani na Kanada, viwango vimeongezeka kwa asilimia 300. “Umefanya maendeleo makubwa, kisura!” lapiga mbiu tangazo moja la kibiashara la sigareti.

Mashirika mengine ya tumbaku yana mbinu zao za kuvutia. Kampuni moja ya Filipino katika nchi hiyo ambayo idadi kubwa ni Wakatoliki iligawa kalenda za bure zenye picha ya Bikira Maria na shime yao ya sigareti ikiwa chini ya picha hiyo ya kiabudiwa. “Nilikuwa sijapata kuona jambo kama hili mbeleni,” akasema Dakt. Rosmarie Erben, Mwasia mshauri wa afya wa WHO. “Walikuwa wakijaribu kuhusianisha nia ya kiabudiwa hicho na tumbaku, ili kuwafanya wanawake Wafilipino wasiwe na wasiwasi kuhusu uvutaji sigareti.”

Katika China kadirio la asilimia 61 ya wanaume watu wazima huvuta sigareti, ilhali asilimia 7 tu ya wanawake wanavuta sigareti. Makampuni ya Magharibi ya tumbaku huelekeza uangalifu wao kwa eti “uhuru” wa wanawake hawa wenye kupendeza wa Mashariki, mamilioni yao kwa muda mrefu walinyimwa “anasa” za dada zao wa Magharibi wenye kuvutia. Ingawa hivyo, kizuizi kimoja kwa maoni ya makampuni ya Magharibi ni: Makampuni ya tumbaku yanayomilikiwa na serikali huandaa nyingi za sigareti hizo.

Hata hivyo, makampuni ya Magharibi polepole huingiza bidhaa zao nchini. Wakiwa na fursa chache mno za kutangaza bidhaa zao, kampuni nyingine za sigareti hutafuta mbinu ya kujipendekeza kwa watakaokuwa wateja wao kwa njia ya ujanja. China huleta filamu kutoka Hong Kong, na nyingi zazo, waigizaji hulipwa ili kuvuta sigareti—ushawishi mwanana!

Kukiwa na uhasama unaozidi kukua katika nyanja za nyumbani, makampuni ya tumbaku yenye ufanisi ya Marekani mishiko yayo ili kunasa majeruhi wapya. Uhakika waonyesha kwamba wamechukua hatua yenye kufisha kwenye mataifa yanayositawi.

Maofisa wa afya ulimwenguni kote watoa onyo. Vichwa vya habari vyatangaza: “Afrika Yapigana na Msiba Mpya—Uvutaji Sigareti.” “Moshi Wageuka Kuwa Moto Katika Asia Soko la Sigareti Lizidipo Kupanda.” “Viwango vya Kiasia vya Uvutaji Sigareti Vitaongoza kwa Ambukizo la Kansa.” “Vita Vipya vya Ulimwengu wa Tatu Vi juu ya Tumbaku.”

Kontinenti ya Afrika imeharibiwa na ukame, vita vya kiraia, na ambukizo la UKIMWI. Hata hivyo, asema Dakt. Keith Ball, Mwanatiba wa moyo Mwingereza, “Isipokuwa vita vya nyuklia ama njaa, uvutaji wa sigareti ndio tisho lililo kubwa kuliko lolote la wakati ujao la afya ya Afrika.”

Kampuni zenye uwezo huwalipa wakulima wenyeji kukuza tumbaku. Wakulima hufyeka miti inayohitajiwa sana kwa ajili ya kupika, kupasha joto, na kujenga na kuitumia kwa moto ili kukausha tumbaku. Wao hukuza mimea ya tumbaku yenye faida badala ya mimea ya kuliwa isiyo na faida nyingi. Waafrika maskini kwa kawaida hutumia kiasi kikubwa cha mapato yao duni kwa sigareti. Hivyo familia za Kiafrika hunywea kutokana na utapiamlo ilhali makampuni ya tumbaku ya Magharibi wa kiwanda kutokana na faida.

Afrika, Ulaya Mashariki, na Amerika ya Kilatini zote zimelengwa shabaha na makampuni ya tumbaku ya Magharibi yanayouona ulimwengu unaositawi kuwa fursa kubwa ya biashara. Lakini Asia yenye idadi kubwa ya watu, ndiyo kwa ulinganisho shabaha kubwa ya tamaa yao wote. China peke yake kwa sasa ina wavutaji sigareti wengi kuliko idadi nzima ya watu wa Marekani—milioni 300. Wao huvuta jumla yenye kumakisha ya sigareti trilioni 1.6 kwa mwaka mmoja, thuluthi moja ya jumla itumiwayo katika ulimwengu!

“Wanatiba wasema madhara ya kiafya yanayosababishwa na mweneo wa biashara ya tumbaku katika Asia kwa hakika yaogofya,” laripoti The New York Times. Richard Peto akadiria kwamba kati ya vifo milioni kumi vya uvutaji sigareti vinavyotazamiwa kila mwaka katika miongo miwili au mitatu ijayo, milioni mbili vitakuwa katika China peke yake. Watoto milioni 50 wa Kichina walio hai leo yawezekana wafe kutokana na maradhi yanayohusiana na uvutaji sigareti, asema Peto.

Dakt. Nigel Gray aliweka hivi hali hiyo kwa mhutasari: “Historia ya uvutaji sigareti kwa kipindi cha miongo mitano iliyopita katika China na Ulaya Mashariki yashitaki nchi hizo kwa maambukizo ya maradhi makubwa ya tumbaku.”

“Je, bidhaa ambayo ni kisababishi cha vifo vya mapema 400,000 kila mwaka katika Marekani, bidhaa ambayo Serikali ya Marekani inajaribu iwezavyo ili kusaidia raia wake kuiacha, imekujaje kuwa kitu kisichodhuru ng’ambo ya mipaka ya Marekani?” akauliza Dakt. Prakit Vateesatokit wa Kampeni ya Kupinga Uvutaji Sigareti ya Thailand. “Je, afya imekuwa isiyo na maana wakati bidhaa hiyo inapelekwa nje katika nchi nyingine?”

Biashara zinazositawi za tumbaku zina uvutano wenye nguvu katika serikali ya Marekani. Pamoja wamepigana ili kupata mizizi ng’ambo, hasa katika masoko ya Kiasia. Kwa miaka sigareti za Kimarekani zilikuwa zimewekewa kizingiti cha kibiashara katika Japani, Taiwan, Thailand, na nchi nyingine, baadhi yazo serikali ilikuwa na usimamizi juu ya bidhaa za tumbaku. Vikundi vya kupinga uvutaji wa sigareti viliandamana dhidi ya uingizaji wa sigareti za Kimarekani, lakini usimamizi wa Marekani ulibuni silaha yenye kushawishi—vizuizi vya kibiashara.

Kutoka 1985 na kuendelea, chini ya msongo mkali kutoka kwa serikali ya Marekani, nchi nyingi za Asia zimefungua milango yao, na sigareti za Kimarekani zimemiminwa ndani kwa wingi. Upelekaji nje wa sigareti za Marekani katika Asia umepanda kufikia asilimia 75 katika 1988.

Labda majeruhi walio hatarini zaidi wa vita vya tumbaku ni watoto. Uchunguzi ulioripotiwa katika The Journal of the American Medical Association wasema kwamba “watoto na matineja hufanyiza asilimia 90 ya wavutaji sigareti wote wapya.”

Makala katika U.S.News & World Report yakadiria idadi ya matineja wavuta sigareti katika Marekani kuwa milioni 3.1. Kila siku 3,000 wapya huanza kuvuta sigareti—1,000,000 kwa mwaka mmoja.

Tangazo moja la kibiashara huonyesha katuni ya ngamia mwenye kupenda raha, mwenye kutafuta anasa, mara nyingi sigareti ikining’inia kwenye midomo yake. Tangazo hili la sigareti lashutumiwa kwa kushawishi vijana kwenye utumwa wa nikotini, kabla hawajang’amua hatari za kiafya zihusikazo. Kwa muda wa miaka mitatu ya utangazaji huu, kampuni ya sigareti ilipata ongezeko la asilimia 64 katika mauzo kwa wabalehe. Uchunguzi kwenye Koleji ya Kitiba ya Georgia (Marekani) ulipata kwamba asilimia 91 ya wenye umri wa miaka sita waliochunguzwa waling’amua katuni huyu avutaye sigareti.

Picha nyingine maarufu ya sigareti ni macho cowboy mwenye kutembea ambaye ujumbe wake ni, kulingana na tineja mmoja, “Unapovuta sigareti, hakuna yeyote anaweza kukuzuia kufanya utakalo.” Inasemwa kwamba bidhaa yenye kuuza zaidi katika ulimwengu ni sigareti ambayo hudhibiti asilimia 69 ya soko miongoni mwa wavuta sigareti matineja na ni aina iliyotangazwa kupita zote. Kama kichochezi cha ziada, fomu huambatanishwa na kila pakiti, ili kubadilishwa na dangarizi, kofia, na nguo za michezo zilizo maarufu sana kwa vijana.

Vikitambua uwezo mkubwa wa matangazo ya kibiashara, vikundi vya kupinga uvutaji wa sigareti vimefaulu katika kufanya matangazo ya kibiashara ya tumbaku kupigwa marufuku katika televisheni na redio katika nchi nyingi. Hata hivyo, njia moja ambayo watangazaji wajanja wa tumbaku wameshinda mfumo huo, ni kwa mbinu ya kuweka vibandiko kwenye pindi za michezo. Hivyo basi, wonyesho wa televisheni wa mchezo wa mpira, ukiwa na halaiki kubwa ya vijana, waweza kuonyesha wachezaji wao mashuhuri wakiwa tayari utendaji na vibandiko vya sigareti vikiwa huko nyuma.

Kwenye maeneo ya ndani ya mji au mbele ya shule, wanawake waliovalia kwa ujanja nguo fupi ama mavazi ya kigaidi ama safari suti wawapa matineja wenye uchu ama tamaa ya kuonja sigareti bila malipo. Kwenye vyumba vya michezo ya video, disko, na maonyesho ya roki, sampuli za sigareti hugawanywa bila malipo. Mkakati fulani wa kampuni ya uuzaji uliofunuka kwa waandishi wa habari ulionyesha kwamba aina hiyo ya sigareti katika Kanada ulinuiwa kwa ajili ya wanaume wanaosema Kifaransa wenye umri wa kutoka miaka 12 hadi 17.

Ujumbe wenye kushawishi ni kwamba kuvuta sigareti huleta raha, kuwa sawa, ukomavu, na umaarufu. “Mahali nilikuwa nikifanya kazi,” akasema mshauri wa utangazaji wa kibiashara, “tulijaribu sana kuathiri watoto waliokuwa na umri wa 14 kuanza kuvuta sigareti.” Matangazo ya kibiashara katika Asia huonyesha kijana mwenye afya, mwanariadha Mmagharibi akicheza-cheza kwenye bichi na nyanja za mpira—bila shaka, akivuta sigareti. “Violezo na mitindo-maisha ya Magharibi hubuni viwango vyenye kuvutia vya kuigwa,” likasema jarida la biashara ya uuzaji, “na wavuta sigareti Waasia hawatosheki.”

Baada ya kutumia mabilioni ya madola kwa utangazaji, wanasoko wa tumbaku wamepata mafanikio makubwa. Ripoti maalumu ya Reader’s Digest ilionyesha kwamba kule kupanda kwa idadi ya wavutaji sigareti wachanga kwastaajabisha. “Katika Filipino,” yasema ripoti hiyo, “asilimia 22.7 ya watu walio chini ya miaka 18 sasa wavuta sigareti. Katika baadhi ya majiji ya Amerika ya Kilatini, kiwango cha matineja ni asilimia 50 yenye kumakisha. Katika Hong Kong, watoto walio wadogo kufikia umri wa miaka saba wavuta sigareti.”

Hata hivyo, hata tumbaku inaposherehekea ushindi wayo ng’ambo, kwa huzuni makampuni ya sigareti yanajua dhoruba inayojikusanya dhidi yayo nyumbani kwayo. Kuna uwezekano gani kwa tumbaku kuibuka kwa mafanikio kutokana na dhoruba hiyo?

[Blabu katika ukurasa wa 3]

Wateja bora zaidi huendelea kufa

[Blabu katika ukurasa wa 5]

Asia, nyanja za tumbaku zilizo mpya kabisa za kuulia

[Blabu katika ukurasa wa 6]

Asilimia 90 ya wavutaji sigareti wote wapya—watoto na matineja!

[Sanduku katika ukurasa wa 4]

Muungo Wenye Kufisha—Ni Viungo Gani Vilivyoko Katika Sigareti?

Zaidi ya viungo mbalimbali vya kikemikali 700 vyaweza kutumiwa na watengeneza sigareti, lakini sheria huruhusu makampuni kuziweka orodha zao siri. Ingawa hivyo, vinavyotiwa ndani miongoni mwa vikolezo, ni metali nzito, visumbufu, na viua wadudu. Viungo vingine ni vyenye sumu hivi kwamba ni kinyume cha sheria kuvitupa katika marundo ya takataka. Huo moshi uzungukao wa sigareti huchukua yapata dutu 4,000, kutia ndani asetoni, buteni, kaboni monoksaidi, na sanidi. Mapafu ya wavuta sigareti na watu wanaokuwa karibu nao yana uelekeo wa kuzoa angalau dutu 43 zijulikanazo kusababisha kansa.

[Sanduku katika ukurasa wa 5]

Wasiovuta Sigareti Hatarini

Je, wewe waishi, kufanya kazi, ama kusafiri na watu wavutao sigareti bila kiasi? Ikiwa ndiyo, huenda ukawa kwenye hatari iliyoongezeka ya kansa ya mapafu na maradhi ya moyo. Uchunguzi wa 1993 uliofanywa na Shirika la Ulinzi wa Kimazingira (EPA) la Marekani lilikata kauli kwamba moshi wa tumbaku katika mazingira (ETS) umebainishwa katika daraja la Kikundi A kiambukizacho kansa, kilicho hatari zaidi. Ripoti chungu zima zilichanganua matokeo ya chunguzi 30 zilizohusisha moshi utokao kwenye ncha ya sigareti pamoja na moshi uliopulizwa na mvutaji.

EPA yalaumu moshi wa tumbaku ya kimazingira kwa ajili ya vifo 3,000 vya kansa ya mapafu kila mwaka katika Marekani. Shirika la Kitiba la Marekani katika Juni 1994 liliunganisha mikataa hiyo na uchunguzi lililouchapisha ukionyesha kwamba wanawake ambao hawavuti sigareti kamwe lakini walio katika mazingira ya ETS wana asilimia 30 kubwa zaidi ya kupatwa na kansa ya mapafu kuliko wale wengine ambao maishani mwao hawajapata kuvuta sigareti.

Kwa watoto wachanga, kuwa katika mazingira ya moshi wa sigareti hutokeza visa 150,000 hadi 300,000 vya mchochota wa mirija ya mapafu na mchochota wa mapafu kila mwaka. Moshi wa sigareti huchochea dalili za pumu kwa watoto 200,000 hadi 1,000,000 kila mwaka katika Marekani.

Shirika la Moyo la Marekani lakadiria kwamba vifo vingi kufikia 40,000 kwa mwaka hutukia kutokana na magonjwa ya moyo na mishipa ya damu yasababishwayo na ETS.

[Picha katika ukurasa wa 7]

Kiolezo fulani chenye kuvutia cha Kiasia, na zile shabaha

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki