Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g96 1/22 kur. 18-20
  • Makampuni ya Tumbaku Yamo Motoni

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Makampuni ya Tumbaku Yamo Motoni
  • Amkeni!—1996
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Mleta-habari wa Amkeni! Aripoti Juu ya Huo Mwelekeo
  • Shabaha Kuu
  • Je, Uvute Sigareti au Uendeleze Maisha Yako?
  • Watetea Tumbaku Waanzisha Puto la Hewa-Joto
    Amkeni!—1995
  • Kwa Nini Uache Kuvuta Sigareti?
    Amkeni!—2000
  • Mamilioni ya Uhai Yakitokomea Moshini
    Amkeni!—1995
  • Maadili ya Tumbaku?
    Amkeni!—1992
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1996
g96 1/22 kur. 18-20

Makampuni ya Tumbaku Yamo Motoni

KULINGANA na ripoti iliyotokea katika The New York Times la Julai 26, 1995, “Idara ya Sheria imeitisha kikao kikuu cha kisheria katika New York ili kuchunguza ikiwa makampuni ya tumbaku yalitoa habari za uwongo kwa maofisa wa Serikali wanaochunguza vifanyizo na athari mbaya za sigareti. Hiyo idara yaelekea itaitisha kikao cha pili cha kisheria hapa ili kuchunguza ikiwa wasimamizi wa makampuni walidanganya Bunge kuhusu bidhaa za tumbaku.”

Msingi wa hili ni nini? Hiyo ripoti ilieleza wazi. Katika Aprili 1994, wasimamizi wakuu wa makampuni ya tumbaku makubwa saba katika Marekani walikuwa wametoa ushahidi chini ya kiapo mbele ya halmashauri ya Bunge kwamba “hawakufikiri nikotini ilikuwa yenye kuraibisha, kwamba sigareti husababisha maradhi au kwamba makampuni yao yalifanyiza kiwango cha nikotini katika bidhaa za tumbaku.”

Baadaye mambo yote yakafunuka—madai yao ya kutokuwa na hatia yakafunuka—wakati katika Juni 1995, hati elfu mbili zenye kupasisha hatia zilipofunuliwa. Hati hizi zaonyesha kwamba watafiti wa tumbaku walikuwa wametumia miaka 15 wakichunguza athari za vifanyizo na matokeo ya madawa kwenye mwili, ubongo, na tabia ya wavutaji sigareti. Dakt. Victor DeNoble aliyekuwa awali mwanasayansi wa utafiti katika moja ya hayo makampuni, afafanua ugunduzi wa msingi wa huo utafiti: “Kampuni ilianza kutambua kwamba ingeweza kupunguza tar, na kuongeza nikotini, na bado sigareti ikubalike kwa mvutaji. Baada ya kazi yao yote ya utafiti, walitambua kwamba nikotini haikuwa ikituliza tu au kusisimua, lakini ilikuwa na athari yayo hasa, katika ubongo, na kwamba watu walikuwa wakivuta sigareti kwa ajili ya athari za ubongo.”

Kulingana na The New York Times, chunguzi za kampuni zilionyesha kwamba “haidhuru ni aina gani ya sigareti waliyovuta watu, walielekea kupata kiwango cha nikotini walichohitaji kwa kuvuta kwa kina, na kuushikilia moshi kwa muda mrefu zaidi kinywani, au kuvuta sigareti nyingi zaidi.” Watafiti wa kampuni walijaribu kutengeneza sigareti yenye kiwango kidogo cha tar kukiwa na viwango vya kutosha vya nikotini kuweza kumridhisha mvutaji.

Hizo hati zilifunua zaidi kwamba makampuni ya tumbaku yalionyesha upendezi mwingi mno katika wateja wayo. Wanafunzi wa vyuo ndio walikuwa wakichunguzwa kwa zaidi ya miaka 15. Watu katika mji mmoja wa Iowa, kutia ndani wavutaji wenye umri wa miaka 14, waliulizwa kuhusu mazoea yao ya uvutaji.

Kufunuliwa kwa hati hizi za utafiti kwaonekana kuwa manufaa kwa muungano wa mawakili wanaoanzisha mashtaka ya kikundi dhidi ya makampuni saba ya tumbaku. Wanadai kwamba makampuni ya tumbaku yalificha habari kuhusu vifanyizo vyenye kuraibisha vya nikotini na kufanyiza viwango vya nikotini ili kuchochea uraibu. Wakili mmoja alisema kwamba hakuna kikao cha kisheria ulimwenguni kitaamini kwamba makampuni haya yalikuwa yakifanya utafiti huo kama kipitisha wakati tu.

Moto uendeleapo kuongezeka zaidi katika ulimwengu uliositawi, moshi wa tumbaku waendelea kupepea kuelekea ulimwengu unaositawi. Miaka 40 iliyopita, hakuna wanawake waliovuta sigareti na ni asilimia 20 tu ya wanaume katika Kusini, au ulimwengu unaositawi, waliovuta sigareti. Lakini leo, asilimia 8 ya wanawake wote na asilimia 50 ya wanaume wote katika nchi zinazositawi ni wavuta-tumbaku—na idadi hiyo yaendelea kupanda. “Moshi,” wasema watafiti, “wapepea ukielekea Kusini.”

Mleta-habari wa Amkeni! Aripoti Juu ya Huo Mwelekeo

Mwandikaji wetu aliye Brazili atoa maelezo fulani ya jumla juu ya hiyo hali huko Kusini. Utafiti katika ulimwengu uliovuvumuka kiviwanda hutokeza picha yenye kufisha mno kwa mvutaji tumbaku. Hiyo ina athari zayo. “Nchi ambazo zimetambua umaana mkubwa wa kupasha umma habari sasa zinaona mianzo ya udidimiaji wa utumizi wa tumbaku,” laripoti Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO). “Katika Kaskazini,” laongezea Panos, shirika la habari lenye makao makuu London, “uvutaji sigareti haukubaliki tena kijamii katika nyumba nyingi, mahali pa umma na mahali pa kazi,” na watu wengi sasa wanatambua kwamba “uvutaji sigareti waweza kuwaua.” “Kiwanda cha tumbaku kinasonga kuelekea Kusini.”

Kwa utofauti, Kusini, kufungua soko jipya kwathibitika kuwa rahisi kama kufungua furushi la sigareti. Kwa biashara ya tumbaku, hali katika nchi zinazositawi ni zenye kutamanisha. Katika nchi 3 kati ya 4 zinazositawi, hakuna marufuku juu ya kutangaza uvutaji, na kwa wakati huohuo, utambuzi wa umma wa hatari za uvutaji sigareti ni wa chini. “Watu hawana habari kuhusu hatari kwa sababu hawaelezwi juu yazo,” laonelea Panos.

Ili kuwashawishi wanawake vijana—ambao ni moja ya shabaha kuu za hiyo biashara—kuwasha sigareti yao ya kwanza, matangazo ya kibiashara “huonyesha uvutaji sigareti ukiwa utendaji wenye kuvutia wa raha unaofurahiwa na wanawake walio huru.” Matangazo ya tumbaku husikika kuwa sawa kwa njia ya kutilika shaka na yale yaliyotumiwa katika ulimwengu uliovuvumuka kiviwanda nusu karne iliyopita. Wakati huo, matangazo yalifanya kazi. Kabla ya muda mrefu, chasema chanzo kimoja, mwanamke 1 kati ya 3 “alikuwa akivuta sigareti kwa idili kama ile ya kiume.”

Leo, utafutaji soko wa bidii unaoelekezewa wanawake wasiotambua kinachoendelea katika nchi zinazositawi wahakikisha kwamba “mafanikio” haya ya kutangaza ya miaka ya 1920 na 1930 yako karibu kurudiwa. Kwa hivyo, mtazamo wenye kuhuzunisha ni kwamba mamilioni ya wanawake vijana katika nchi zilizo maskini zaidi ulimwenguni kwa sasa yako katika hatari ya kuwa, kama mwanamaoni mmoja alivyosema, “wasichana warembo katika miaka yao ya mapema ya nikotini.”

Shabaha Kuu

Ingawa wanawake wanafanyiza moja ya shabaha kuu za biashara ya tumbaku, vijana ndio shabaha yayo kuu. Matangazo ya kikatuni na maneno ya shime ya sigareti kwenye vichezeo yanafanyiza faida, na ndivyo ilivyo na uthamini wa michezo.

Katika China, laripoti gazeti Panoscope, “asilimia kubwa ya vijana wanavuta sigareti.” Asilimia ipatayo 35 ya vijana wenye umri wa miaka 12 hadi 15 na asilimia 10 ya wenye umri wa miaka 9 hadi 12 ni wavutaji sigareti. Katika Brazili, laripoti Folha de S. Paulo la kila siku, vijana wakadiriwao kuwa milioni kumi ni wavutaji sigareti. Je, hawana habari kuhusu hatari? “Najua kwamba kuvuta sigareti ni kwenye madhara,” asema Rafael, mvulana Mbrazili mwenye umri wa miaka 15 ambaye huvuta pakiti moja na nusu za sigareti kwa siku, “lakini ni nzuri sana.” Matokeo ya kusababu huku kwa kutojali ni nini? “Kila siku,” laripoti Panos, “angalau vijana wengine 4,000 huanza kuvuta sigareti.”

Biashara ya tumbaku hupeleka Kusini baadhi ya bidhaa ambazo zina tar na nikotini ya juu zaidi kuliko aina ziuzwazo Kaskazini. Sababu iko wazi. “Siombi radhi kwa ajili ya nikotini,” akasema ofisa mmoja wa biashara ya tumbaku miaka kadhaa iliyopita. “Ndicho kitu kiletacho biashara yenye kujirudia. Ndicho kifanyacho watu warudi kununua zaidi.” Ina matokeo. “Kwa sababu ya viwango vya juu vya nikotini,” chathibitisha kichapo cha Kiholanzi Roken Welbeschouwd (Uvutaji Sigareti—Mambo Yote Yamekwisha Fikiriwa), “kutegemea sigareti kunatimizwa haraka zaidi, na hili hufungua fursa kwa ongezeko la utumizi na mauzo kwa kushusha viwango hivyo hatua kwa hatua.”

“Biashara ya tumbaku,” lamalizia Panos, “huona Kusini kuwa soko ambalo litafanya biashara hiyo isifilisike.”

Je, Uvute Sigareti au Uendeleze Maisha Yako?

Ikiwa unaishi katika nchi inayositawi, utafanya nini? Mambo ya hakika yako wazi. Hadi 1950, vifo vilivyotokana na maradhi yahusianayo na uvutaji sigareti havikuwa vingi, lakini leo watu milioni moja Kusini wanakufa kila mwaka kutokana na maradhi yanayohusiana na uvutaji sigareti. Hata hivyo, WHO yaonya kwamba katika kipindi cha miongo mitatu idadi ya kila mwaka ya vifo vinavyohusiana na uvutaji sigareti katika nchi zinazositawi vitaongezeka hadi milioni saba. Kinyume cha kile matangazo ya tumbaku hukuambia, sigareti ni zenye kufisha.

Unasema kwamba unatambua hatari? Sawa, lakini utafanya nini na ujuzi huo? Je, utakuwa kama mvutaji ambaye amesoma mambo mengi yenye kuogofya kuhusu uvutaji sigareti hivi kwamba ameamua kuacha kusoma? Au utakuwa mwerevu vya kutosha kuweza kuona kupita kisetiri kilichowekwa na matangazo ya tumbaku na kusema la kwa uvutaji sigareti? Ni kweli, moshi wa tumbaku unapepea kuelekea Kusini—lakini si lazima upepee kuelekea pale ulipo!

[Sanduku katika ukurasa wa19]

China—Nambari Moja

Zhang Hanmin, mfanyakazi mwenye umri wa miaka 35 katika China, akunja viganja vyake na kuwasha sigareti. “Kusema kweli,” yeye asema, “naweza kumudu bila vitu vingi lakini siwezi kumudu bila sigareti.” Yaonekana, jambo hilohilo laweza kusemwa kuhusu wengine milioni 300 kama Zhang. Tangu miaka ya 1980, China “imetokeza, kuuza na kuvuta sigareti kuliko nchi nyingineyo yote.” Katika mwaka fulani wa hivi majuzi “mabilioni ya sigareti yaliuzwa kwa watu wenye mazoea ya kuvuta sigareti,” ikifanya China kuwa “taifa nambari moja la tumbaku.”—Gazeti Panoscope.

[Sanduku katika ukurasa wa20]

Sigareti Zilizo na “Uhakikisho”?

Ingawa watu milioni tatu hufa kila mwaka kwa sababu ya maradhi yanayohusiana na tumbaku, matangazo yaendelea kuwaambia wavutaji kwamba zoea lao ni salama. Kwa kielelezo, tangazo moja la hivi majuzi katika gazeti moja la Brazili, lilivumisha habari ya kuwasili kwa aina ya sigareti ambayo “huja ikiwa na uhakikisho wa kiwandani.” Tangazo hilo latoa uhakikisho huu: “Gari lako lina uhakikisho; televisheni yako ina uhakikisho; saa yako ina uhakikisho. Sigareti yako pia ina uhakikisho.” Hata hivyo, kama mengi ya matangazo yatajavyo na kama wavutaji walio wagonjwa mno wawezavyo kutoa ushahidi, uhakikisho pekee ni kwamba “uvutaji sigareti unadhuru afya.”

[Picha katika ukurasa wa 19]

Shabaha kuu—wanawake katika nchi zinazositawi

[Hisani]

Picha ya WHO iliyopigwa na L. Taylor

[Picha katika ukurasa wa 20]

Kutotambua hatari?

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 20]

WHO

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki