Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g95 5/22 kur. 8-13
  • Watetea Tumbaku Waanzisha Puto la Hewa-Joto

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Watetea Tumbaku Waanzisha Puto la Hewa-Joto
  • Amkeni!—1995
  • Habari Zinazolingana
  • Makampuni ya Tumbaku Yamo Motoni
    Amkeni!—1996
  • Kwa Nini Uache Kuvuta Sigareti?
    Amkeni!—2000
  • Jitayarishe kwa Ajili ya Magumu
    Amkeni!—2010
  • Mamilioni ya Uhai Yakitokomea Moshini
    Amkeni!—1995
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1995
g95 5/22 kur. 8-13

Watetea Tumbaku Waanzisha Puto la Hewa-Joto

KATIKA miaka ya 1940, London lilikuwa jiji lililokuwa limebambwa. Ndege za kivita za Ujerumani na mabomu mengi yalimwagwa yakisababisha hofu na uharibifu. Lakini hali haingekuwa mbaya hivyo, huenda wenyeji wangesisimuka kutokana na mandhari yenye usisimuzi.

Yakiwa yamefungwa na kebo ndefu, maelfu ya puto kubwa yalielea kwa wangavu juu yao. Kusudi lao lilikuwa kuzuia mashambulizi ya ndege ya kimo cha chini wakitumaini kunyaka mabomu machache yakiwa hewani. Kizingiti cha puto, cha kiakili kama kilivyoonekana, kilipata mafanikio machache mno.

Makampuni ya sigareti vivyohivyo yamejipata yenyewe yakiwa yamebambwa. Milki kubwa za tumbaku zenye msukosuko, wakati mmoja zilizokuwa ngome zisizoshindika za kisiasa na kiuchumi, zashambuliwa kutoka kila upande.

Jamii ya kitiba yafungua ukurasa baada ya ukurasa wa uchunguzi wenye kutoa ithibati. Maofisa wa afya wenye idili watumia hali hiyo ili kujifaidi. Wazazi wenye hasira wadai kwamba watoto wao waonewa. Watoa sheria wenye kuazimia wamekataza uvutaji wa sigareti katika majengo ya ofisi, mikahawani, kambi za kijeshi, na katika eropleni. Katika nchi nyingi, matangazo ya kibiashara ya sigareti yamepigwa marufuku katika televisheni na redio. Katika Marekani, majimbo mazima yashitaki makampuni ya tumbaku ya mamilioni ya dola katika kugharamika kwa utunzaji wa kiafya. Hata wanasheria wanajiunga na pigano hilo.

Hivyo katika jaribio la kuwapinga washambulizi wao, makampuni ya tumbaku yameanzisha puto zao za kitamathali za kujikinga. Hata hivyo, yaonekana kujawa na hewa-joto nyingi.

Mwaka jana, umma wa Marekani uliweza kujionea kabisa watoa sheria wenye karaha na maofisa wa afya wa serikali wakipanga shambulio kabambe dhidi ya biashara ya tumbaku. Katika usikizi mbele ya jopo la kikongamano la Marekani katika Aprili 1994, maofisa wakuu wa kampuni saba kubwa za tumbaku Marekani walikabiliwa na tarakimu zenye kuwatia hatiani: zaidi ya Wamarekani 400,000 wafa kila mwaka na mamilioni zaidi ni wagonjwa, wanakaribia kufa, na wenye uraibu.

Wao walikuwa na lipi la kusema kwa kujitetea? Maofisa wakuu wa makampuni washambuliwaji walitoa taarifa fulani zenye kupendeza katika utetezi wao: “Uvutaji sigareti . . bado haujathibitishwa kuwa unachangia ukuzi wa maradhi,” akataarifu msemaji wa Taasisi ya Tumbaku. Hata zaidi, zoea la kuvuta sigareti lilionyeshwa kuwa lisilodhuru kama vile utendaji wowote ule wenye kufurahisha, kama vile kumumunya peremende ama kunywa kahawa. “Kuwako kwa nikotini hakuzifanyi sigareti kuwa dawa fulani ya kulevya, ama uvutaji sigareti kuwa uraibu,” akasema ofisa mkuu mmoja wa kampuni ya tumbaku. “Ile dhana kwamba kiwango chochote kile cha nikotini katika sigareti ni chenye kuraibisha si kweli,” akataarifu mwanasayansi wa kampuni fulani ya tumbaku.

Ikiwa sigareti haziraibishi, ikauliza halmashauri hiyo, kwa nini makampuni ya tumbaku yamejaribu kuongeza viwango vya nikotini katika bidhaa zao? “Ladha,” akaeleza ofisa mkuu mwingine wa kampuni ya tumbaku. Je, kuna kitu kingine chochote kilicho kibaya zaidi kuliko sigareti isiyo na ladha? Alipoonyeshwa marundo ya utafiti kutoka faili za kampuni yao yakidokeza uraibishaji wa nikotini, alishikamana na dhana yake.

Yaonekana, yeye na wengine watashikilia maoni hayo hata makaburi yajawe na majeruhi wa tumbaku. Mapema katika 1993, Dakt. Lonnie Bristow, mwenyekiti wa Kamati ya Wadhamini ya Shirika la Kitiba la Marekani alitoa usai wenye kupendeza. The Journal of the American Medical Association liliripoti hivi: “Aliwaalika maofisa wakuu wa kampuni kubwa za tumbaku za Marekani kuandamana naye kupitia vyumba vya hospitali ili kuona mojapo matokeo ya uvutaji sigareti—wagonjwa wa kansa ya mapafu na ulemavu mwingine wa kimapafu. Hakuna mmoja wao aliyekubali mwaliko huo.”

Biashara ya tumbaku hujitutumua kwamba huandaa kazi murua katika ulimwengu wa uchumi wenye kukosa kazi. Kwa kielelezo, katika Argentina kazi milioni moja zimebuniwa na biashara hiyo, kukiwa na kazi milioni nne zaidi zinazohusiana nayo. Kodi zilizo kubwa zinazolipa zimepatia makampuni ya tumbaku upendeleo wa serikali nyingi.

Shirika moja la tumbaku, kihususa limefadhili vikundi maskini kwa michango ya ukarimu—udhihirisho unaonekana kuwa kujali raia. Hata hivyo, barua za siri za kampuni zilifunua kwamba nia hususa ya hii “bajeti ya kusitawisha eneo”—ili kufanyiza halijema miongoni mwa wanaoelekea kuwa waunga-mkono.

Kampuni hiyohiyo ya tumbaku pia imefanya marafiki miongoni mwa sanaa ikitoa michango mikubwa kwa majumba ya hifadhi za vitu vya kale, shule, shule za uchezaji muziki, na vyuo vya muziki. Maofisa wa mashirika ya sanaa wameamua kukubali fedha za tumbaku wanazozihitaji mno. Hivi majuzi, washiriki wa jamii ya sanaa wa New York City walikabili tatizo lenye kutatanisha kampuni hiyohiyo ya tumbaku ilipowaomba kuwaunga mkono katika jitihada zayo za kushawishi umma kupinge sheria dhidi ya uvutaji sigareti.

Na bila shaka, mibabe tajiri wa tumbaku hawaogopi kutapanya fedha kwa wanasiasa, wanaoweza kutumia uwezo wao dhidi ya mapendekezo yoyote yasiyofaa masilahi ya tumbaku. Maofisa wa serikali walio katika vyeo vya juu wametetea makampuni ya tumbaku. Wengine wana mahusiano ya kifedha na biashara hiyo ama wahisi msongo kuwalipa kwa ajili ya utegemezo mzuri kifedha wa uchaguzi walioupata kutoka kwa makampuni ya tumbaku.

Mbunge mmoja wa Marekani aliripotiwa kupokea zaidi ya dola 21,000 kama misaada kutoka kwa makampuni ya sigareti na kama tokeo alipiga kura dhidi ya idadi kadhaa ya masuala ya kupinga tumbaku.

Aliyekuwa mtetezi maalumu wa tumbaku mwenye kulipwa vizuri, wakati mmoja alikuwa mwakilishi katika bunge kuu na mvutaji sigareti sana, hivi majuzi aligundua kwamba alikuwa na kansa ya koo, mapafu, na ini. Sasa yuna maguno na malalamiko mengi kwamba “kulazwa na ugonjwa uliojisababishia mwenyewe” humfanya mtu ajihisi kuwa mpumbavu.

Kwa uwezo ambao fedha zinao katika matangazo ya kibiashara, mibabe wa tumbaku wanawashambulia sana wapinzani wao. Tangazo moja la kibiashara lapeperusha bendera ya kutaka uhuru, kwa udhati likionya, “Leo Ni Sigareti. Na Kesho Je?” Tangazo hilo huonyesha kwamba kafeni, alkoholi, na mikate ya kupachikwa nyama ndizo zinazokabili janga la eti waitwao wakatazaji washupavu.

Matangazo ya kibiashara magazetini yatafuta kukosoa ule uchunguzi unaonukuliwa sana wa Shirika la Ulinzi wa Kimazingira ambao uliainisha moshi wa mpwito kuwa wenye kutokeza kansa. Biashara ya tumbaku ilitangaza mipango ya kufanya pigano la kisheria. Programu fulani ya televisheni ililaumu kampuni moja kwa kuchezea viwango vya nikotini ili kutia moyo uraibu. Kampuni iliyotangaza hayo ilishtakiwa mara hiyo mahakamani na kudaiwa dola bilioni 10.

Makampuni ya tumbaku yamepigana kwa dhati, lakini mawingu ya mashtaka bado yazidi kuwa mazito. Chunguzi 50,000 zilifanywa wakati wa miongo minne iliyopita, zikitokeza rundo linalozidi kukua la uthibitisho wa madhara ya matumizi ya tumbaku.

Makampuni ya sigareti yalijaribu kuepaje lawama zilizotupiwa? Kwa unyeti wameshikilia uhakika mmoja: Wavuta sigareti huacha. Hivyo basi, wao husema, nikotini hairaibishi. Hata hivyo, tarakimu huonyesha vingine. Kweli, Wamarekani milioni 40 wameacha uvutaji sigareti. Lakini milioni 50 zaidi bado wavuta sigareti, na asilimia 70 ya hawa husema kwamba wanataka kuacha. Kati ya milioni 17 wanaojaribu kuacha kila mwaka, asilimia 90 hushindwa katika muda wa mwaka mmoja.

Baada ya upasuaji wa kansa ya mapafu, yapata asilimia 50 ya wavuta sigareti wa Marekani hurudia zoea hilo. Kwa wavuta sigareti waliopata kuwa na maradhi ya mshiko wa moyo, asilimia 38 huanza tena hata kabla ya kuondoka hospitalini. Asilimia 40 ya wavuta sigareti walioondolewa zoloto lenye kansa watajaribu kuvuta sigareti tena.

Kati ya mamilioni ya matineja wavutao sigareti katika Marekani, robo tatu walijaribu angalau mara moja kuacha lakini walishindwa. Tarakimu pia huonyesha kwamba kwa vijana wengi, kuvuta tumbaku ni kikanyagio kuelekea kwenye madawa mazito. Wabalehe wavutaji sigareti wako mara 50 zaidi kuelekea kutumia kokaine kuliko wale ambao bado hawajavuta sigareti. Mvutaji sigareti mwenye umri wa 13 akubali. “Hakuna shaka akilini mwangu kwamba sigareti ni mlango wa kuelekea kuvuta madawa mazito,” msichana huyo akaandika. “Karibu kila mtu ninayemjua, isipokuwa watu watatu tu, walianza kuvuta sigareti kabla ya kutumia madawa.”

Namna gani kuhusu sigareti zenye kiasi kidogo cha tumbaku? Uchunguzi huonyesha kwamba huenda, kwa hakika, ziwe zenye madhara hata zaidi—kwa sababu mbili: Moja, mara kwa mara mvutaji huvuta pumzi kwa uzito zaidi ili kutoa ile nikotini mfumo wake utamaniyo, hilo likifanya tishu nyingi za mapafu ziathiriwe na moshi wenye sumu; mbili, ule uelewevu usiofaa kwamba anavuta sigareti fulani “yenye afya” huenda umfanye asijitahidi kuacha kabisa.

Zaidi ya chunguzi 2,000 zimefanyiwa nikotini peke yake. Zafunua kwamba nikotini ni mojapo dutu yenye kuraibisha ijulikanayo kwa mwanadamu, na mojapo yenye kudhuru zaidi. Nikotini huongeza kiwango cha mpigo wa moyo nayo huziba mishipa ya damu. Hiyo hufyonzwa katika mfumo wa damu kwa sekunde saba—hata kasi zaidi kuliko dawa inayodungwa moja kwa moja kwenye mshipa. Hiyo hufanya ubongo utake zaidi, tamaa ambayo wengine husema ni yenye kuraibisha maradufu kuliko heroini.

Makampuni ya tumbaku, yajapokataa, je, yanajua tabia za kuraibisha za nikotini? Hakika yamejua hilo kwa muda mrefu sana. Kwa kielelezo, ripoti ya 1983 ilionyesha kwamba mtafiti wa kampuni moja ya tumbaku aliona kwamba panya wa maabara walionyesha dalili dhahiri za uraibu, kwa kawaida wakisukuma bawaba ili kupata vima zaidi vya nikotini. Inaripotiwa kwamba, uchunguzi huo ulizimwa na kampuni ya tumbaku na umejulikana hivi majuzi tu.

Mibabe wa tumbaku hawajakaa kitako bila kutenda wanaposhambuliwa kutoka pande zote. Kamati ya Utafiti wa Tumbaku katika New York City yaongoza kile The Wall Street Journal lakiita “kampeni iliyo ndefu zaidi inayotoa habari zisizo sahihi katika historia ya biashara ya Marekani.”

Chini ya dhana ya kuongoza utafiti huru, kamati hiyo imeweka akiba mamilioni ya dola ili kukabiliana na washambulizi. Yote yalianzia 1953 wakati Dakt. Ernst Wynder wa Memorial Sloan-Kettering Cancer Center alipopata kwamba kiasi kidogo cha tumbaku iliyopakwa kwenye mgongo wa panya-buku ilisababisha uvimbe. Kampuni zilianzisha kamati hiyo ili kusawazisha uthibitisho wazi uliokusanyika dhidi ya bidhaa yao, kwa kufunika uthibitisho wao wa kisayansi.

Hata hivyo, wanasayansi wa kamati wangeweza kutokezaje matokeo yaliyo kinyume hivyo na ugunduzi wa jumuiya ile iliyobaki ya utafiti? Hati zilizotolewa majuzi zilifunua hila nyingi zilizofichwa. Watafiti wengi wa kamati, wakiwa wamefungwa na mikataba iliyoandikwa na kudhibitiwa na vikoa vya wanasheria walio macho, walipata kwamba hofu ya kiafya inayozidi kukua ilikuwa na misingi thabiti. Lakini kamati, ilipokabiliwa na mambo ya hakika, kulingana na The Wall Street Journal, “nyakati nyingine ilipuuza, ama hata kukatiza uchunguzi wao wenyewe ambao ulionyesha uvutaji sigareti kuwa afa la kiafya.”

Ukitendeka kwa usiri, utafutaji wa sigareti iliyo salama zaidi ukaendelea kwa miaka. Kufanya hivyo hadharani kungekuwa kukubali bila maneno kwamba uvutaji sigareti kwa hakika hudhuru afya. Kufikia mwishoni mwa miaka ya 1970, mwanasheria wa cheo cha juu akiwakilisha kampuni fulani ya tumbaku alipendekeza kwamba jitihada za kutokeza sigareti “salama” zitupiliwe mbali kwani hazikufaulu na kwamba barua zinazoihusu ziwekwe kando.

Mambo mawili yakawa wazi kutokana na miaka ya majaribio: Nikotini kwa kweli yaraibisha, na uvutaji sigareti huua. Ingawa yakataa hakika hizi hadharani, makampuni ya tumbaku yaonyesha kwa matendo yao kwamba yanajua hakika zote vizuri sana.

Akilaumu utokezaji wa kimakusudi, David Kessler kamishna wa Usimamizi wa Chakula na Dawa (FDA) wa Marekani alisema hivi: “Baadhi ya sigareti za leo huenda, kwa hakika, zifuzu kuwa na mifumo ya hali ya juu ya kupelekea nikotini kwa kiasi hususa kilichohesabiwa . . . cha kutosha kufanyiza na kudumisha uraibu.”

Kessler alifunua kwamba makampuni ya tumbaku huwa na sera kadhaa zikithibitisha nia yao. Moja ni kwa kukuza tumbaku ikiwa na kiwango cha juu cha nikotini kijulikanacho. Utaratibu mwingine hutengeneza chujio za sigareti na makaratasi yakiwa na nikotini ili kusisimua zaidi. Hata nyingine huweka nikotini zaidi katika vuto la kwanza la mvutaji sigareti kuliko lile la mwisho. Kwa kuongezea, hati za kampuni zaonyesha kwamba misombo ya amonia huongezwa kwa sigareti ili kuruhusu nikotini kutoka kwa tumbaku. “Karibu mara mbili ya kile kiasi cha kawaida kilichovutwa huingia katika mfumo wa damu wa mvutaji sigareti,” yasema ripoti ya New York Times. FDA imetangaza kwamba nikotini ni dawa yenye kuraibisha na hudhamiria kutendesha sigareti kwa njia kali zaidi.

Pia serikali kwa njia tofauti zimetegemea sigareti. Serikali ya Marekani, kwa mfano, hukusanya bilioni 12 kwa mwaka mmoja katika kodi ya serikali na majimbo kutoka kwa bidhaa za tumbaku. Hata hivyo, Ofisi ya serikali ya Uchanganuzi wa Tekinolojia, imepiga hesabu ya dola bilioni 68 kwa mwaka mmoja kuwa hasara kwa serikali kwa ajili ya uvutaji sigareti, kwa sababu ya gharama za utunzi wa afya na hasara ya utokezo wa mazao.

Madai ya thawabu za kiuchumi na kazi nyingi, utegemezo mwafaka wa sanaa, ukataaji wa kinyeti wa madhara ya afya—kwa kweli, kampuni za tumbaku zimeweka puto za kitamathali ili kujikinga. Kama watathibitika kuwa wenye matokeo zaidi kuliko puto za ukingaji juu ya London ama sivyo yangojewa kuonekana.

Lakini ni wazi kwamba makampuni mibabe kamwe haiwezi kuficha uasilia wayo. Yamefanya mamilioni, na yameua mamilioni, lakini yaonekana kutoathiriwa na jambo la kwamba hatimaye uhai wa kibinadamu umeharibiwa sana.

[Blabu katika ukurasa wa 8]

Yaonekana kujawa na hewa-joto nyingi

[Blabu katika ukurasa wa 9]

Uchunguzi mmoja wa serikali waonyesha moshi wa mpwito kuwa wenye kusababisha kansa

[Blabu katika ukurasa wa 10]

Nikotini ni mojapo dutu ijulikanayo kuraibisha mno

[Blabu katika ukurasa wa 11]

Yamefanya mamilioni; yameua mamilioni

[Sanduku katika ukurasa wa 10]

Chunguzi 50,000—Wao Wamepata Nini?

Hapa kuna uchanganuzi mdogo wa mahangaiko ya afya uliotokezwa na watafiti katika mahusiano na utumizi wa tumbaku:

KANSA YA MAPAFU: Wavutaji sigareti hufanyiza asilimia 87 ya vifo vya kansa ya mapafu.

MARADHI YA MOYO: Wavutaji sigareti wana asilimia 70 ya hatari kubwa zaidi ya maradhi ya moyo.

KANSA YA MATITI: Wanawake wanaovuta sigareti 40 ama zaidi kila siku wana asilimia 74 kubwa zaidi ya kufa kutokana na kansa ya matiti.

ULEMAVU WA KUSIKIA: Vitoto vya mama wavutaji sigareti wana tatizo kubwa zaidi la kusikia vizuri.

MAAFA YA KISUKARI: Walio na ugonjwa wa kisukari wanaovuta sigareti ama kutafuna tumbaku wako katika hatari zaidi ya kuharibika figo na wana uendelevu wa haraka wa retinopathi (tatizo la retina).

KANSA YA UTUMBOMPANA: Chunguzi mbili zilizohusisha zaidi ya watu 150,000 zilionyesha uhusiano ulio wazi kati ya uvutaji sigareti na kansa ya utumbompana.

PUMU: Moshi wa sigareti waweza kufanya pumu iwe mbaya zaidi kwa vijana.

MWELEKEO WA KUVUTA SIGARETI: Mabinti wa wanawake waliovuta sigareti wakati wa mimba wana uelekeo mara nne wa kuvuta sigareti.

LEUKEMIA: Uvutaji sigareti waonekana kusababisha leukemia ya uboho.

MAJERAHA YA MAZOEZI: Kulingana na uchunguzi wa Jeshi la Marekani, wavutaji sigareti wana uelekeo mkubwa wa kupata majeraha wakati wa mazoezi.

KUMBUKUMBU: Vima vya juu vya nikotini huenda viharibu uwezo wa kiakili wakati mtu anapofanya kazi tata.

KUSHUKA MOYO: Wanatiba ya akili wanachunguza uthibitisho wa uhusiano kati ya kuvuta sigareti na kushuka moyo kukubwa pamoja na unyong’onyevu wa akili.

UJIUAJI: Uchunguzi wa wakunga ulionyesha kwamba ujiuaji ulikuwa mara mbili zaidi miongoni mwa wakunga waliovuta sigareti.

Hatari nyingine za kuongezea kwenye orodha ni: Kansa ya mdomo, zoloto, koo, umio, kongosho, tumbo, utumbo mdogo, kifuko cha mkojo, figo, na shingo ya mji wa mimba, mshtuko wa akili, mshiko wa moyo, maradhi yenye kusedesha ya mapafu, maradhi ya mzunguko wa damu, vidonda vya matumbo, kisukari, utasa, uzani wa chini wa mtoto-mzaliwa, kupungua kwa uzito wa mifupa, na maambukizo ya masikio. Maafa ya moto yaweza kuongezewa pia, kwani uvutaji sigareti ndio kisababishi kikubwa cha mioto ya nyumbani, hotelini, na hospitalini.

[Sanduku katika ukurasa wa 12]

Tumbaku Isiyo na Moshi—Kibadala Hatari

Kampuni ya sigareti yenye kufanikiwa zaidi katika biashara ya ugoro ya dola bilioni 1.1 kwa ujanja huwekea chambo cha ugoro uliokolezwa kwa wanaoanza kuvuta sigareti. Imekoleza aina za sigareti zilizo maarufu. Ule “msisimuo mdogo wa tumbaku” ambao wao hutwaa huridhisha lakini si kwa muda mrefu. Aliyekuwa naibu wa mwenyekiti wa kampuni hiyo ya tumbaku alisema hivi: “Watu wengi huenda waanze na sigareti zilizokolezwa zaidi, lakini hatimaye, wataifikia [aina iliyo na nguvu zaidi].” Hiyo hutangazwa kuwa, “Tafuno Lenye Nguvu kwa Wanaume Wenye Nguvu” nayo, “Huridhisha.”

The Wall Street Journal, lililoripoti mkakati huu wa kampuni hiyo na likanukuu ukataaji wayo kwamba “hubadili kiwango cha nikotini,” Journal pia lilitaarifu kwamba waliokuwa wanakemia wa tumbaku wawili wa kampuni ya tumbaku, wakizungumza juu ya mada hiyo kwa mara yao ya kwanza, walisema kwamba “ingawa kampuni hiyo haifanyizi viwango vya nikotini, hufanyiza kiasi cha nikotini ambacho mtumizi hufyonza.” Wao pia wanasema kwamba kampuni hiyo huongeza kemikali mbalimbali ili kuongeza nguvu ualkali wa ugoro wayo. Kadiri ugoro unavyokuwa na alkali, “ndivyo nikotini nyingi inavyotolewa.” Journal laongezea ubainifu huu kuhusu ugoro na tumbaku ya kutafuna: “Ugoro ambao mara nyingi huchanganyishwa isivyofaa kwa kutoeleweka na tumbaku ya kutafuna, ni tumbaku iliyokatwa vipande ambayo watumizi humumunya, hawatafuni. Watumizi wanabwia, ama ‘kuchovya,’ na kuuweka katikati ya shavu na ufizi, wakiubadili-badili kwa ulimi wao na kutema mate pindi kwa pindi.”

Aina za tumbaku zilizokolezwa hutengenezwa kwa ajili ya wanaoanza kuvuta sigareti, asilimia 7 na 22 kama zifuatanavyo huwa bila nikotini iwezayo kufyonzwa ndani ya mkondo wa damu. Aina iliyo na nguvu zaidi yaweza kumfanya mtumizi mpya kusongwa na pumzi. Tumbaku yayo iko katika muundo mwembamba kwa ajili ya wanaume “halisi.” Asilimia 79 ya nikotini yayo ni “bila nikotini,” ikiwepo kwa ajili ya ufyonzaji wa mara moja kwenye mkondo wa damu. Katika Marekani, watumizi huanza ugoro katika wastani wa umri wa miaka tisa. Na je, mwenye umri wa miaka tisa atakinza kuendelea ili kuanza kutumia aina iliyo na nguvu zaidi na kujiunga na wanaume “halisi”?

Vima vitokezwavyo na nikotini kwa hakika vina nguvu kuliko vile vitokanavyo na sigareti. Watumizi waripotiwa kuwa na uelekeo wa kupata kansa ya mdomo mara 4 zaidi, na hatari ya kupata kansa ya zoloto ni mara 50 kubwa zaidi kuliko wale wasiotumia.

Malalamishi ya umma katika Marekani kwa muda mfupi yaliwaka wakati mashtaka ya kisheria yalipotolewa dhidi ya kampuni ya tumbaku na mama ya aliyekuwa nyota wa riadha za sekondari aliyekufa kutokana na kansa ya mdomo. Alipata kibaba cha ugoro bila malipo kwenye michezo akiwa na umri wa miaka 12 na akawa mtumizi wa vibaba vinne kwa juma. Baada ya kufanyiwa pasuaji kadhaa zenye maumivu ambazo zilichonga ulimi wake, taya, na shingo, madaktari wake wakashindwa. Mvulana huyo mchanga alikufa akiwa na umri wa miaka 19.

[Sanduku katika ukurasa wa 13]

Jinsi ya Kuwa Mwacha Sigareti

Mamilioni ya watu kwa mafanikio wameacha uraibu wao wa nikotini. Ikiwa wewe ni mvutaji sigareti, hata yule wa miaka mingi, wewe pia unaweza kulibwaga zoea hili lenye kudhuru. Madokezo machache ambayo yaweza kusaidia:

• Jua kimbele kile utatazamia. Dalili za kuacha huenda zikatia ndani fadhaiko, kukasirika, kisunzi, kuumwa na kichwa, kukosa usingizi, mvurugo wa tumbo, njaa, uchu, kumakinika kusiko kamili, kutetemeka. Kwa hakika si tazamio lenye kupendeza, lakini dalili zilizo nyingi hudumu kwa siku chache tu na hutoweka polepole kadiri mwili unapokuwa hauna nikotini.

• Sasa mng’ang’ano wa uchu wa kiakili unaanza. Si kwamba tu mwili wako ulikamia nikotini bali akili yako iliongozwa na tabia zinazohusiana na uvutaji sigareti. Changanua kawaida yako ili kuona ni lini bila kukusudia uliunyoosha mkono ili kuchukua sigareti, na ubadili kitabia hicho. Kwa kielelezo, ikiwa sikuzote ulivuta sigareti mara baada ya mlo, azimia kusimama mara moja na kutembea kidogo ama kuosha vyombo.

• Wakati uchu mkubwa unapokupata, labda kwa sababu ya kipindi chenye mkazo, kumbuka kwamba hisi hiyo kwa kawaida itapita mnamo dakika tano. Jitayarishe kujaza akili yako kwa kuandika barua fulani, kufanya mazoezi, ama kula kumbwe lenye afya. Sala ni msaada wenye nguvu kuelekea kujidhibiti.

• Ikiwa umevunjika moyo kutokana na majaribio ya kuacha yasiyofaulu, jipe moyo. Jambo lililo muhimu ni kuendelea kujaribu.

• Ikiwa matazamio ya kuongeza uzito yakuzuia, weka akilini kwamba manufaa za kuacha sigareti zapita kwa wingi hatari ya kilo kadhaa za ziada. Inaweza kusaidia ukiwa na matunda au mboga karibu. Na unywe maji mengi.

• Kuacha kuvuta sigareti ni jambo moja. Kujiepusha kabisa ni jambo jingine. Weka miradi ya wakati ya kutovuta sigareti—siku moja, juma moja, miezi mitatu, daima.

Yesu alisema hivi: “Ni lazima umpende jirani yako kama wewe mwenyewe.” (Marko 12:31 New World Translation) Ili kumpenda jirani yako, acha uvutaji sigareti. Ili kujipenda mwenyewe, acha uvutaji sigareti.—Ona pia “Maoni ya Kikristo Juu ya Kuvuta Sigareti,” katika Amkeni!, Machi 8, 1990, kurasa 13-16.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki