Mashahidi wa Yehova na Wastadi wa Tiba Washirikiana
KATIKA 1945, Mashahidi wa Yehova walitambua kwamba kutia damu mishipani kulikuwa utumizi wa damu usio wa kimaandiko. Likitiwa katika Sheria ya Musa, katazo hilo liliendelezwa katika Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo. Matendo 15:28, 29 lasema: “Kwa maana ilimpendeza [roho takatifu, NW] na sisi, tusiwatwike mzigo ila hayo yaliyo lazima, yaani, mjiepushe na vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu, na damu, na nyama zilizosongolewa, na uasherati. Mkijizuia na hayo, mtafanya vema. Wasalamu.” (Ona Mambo ya Walawi 17:10-12.) Kukataa kwa Mashahidi kukubali mitio ya damu mishipani kuliongoza kwenye mahitilafiano mengi kati yao na wastadi wa tiba.
Halmashauri za Uhusiano na Hospitali
Ili kuunga mkono Mashahidi katika kukataa kwao kupokea damu, kuondoa kutokuelewa kwa upande wa madaktari na hospitali, na kufanyiza hali ya ushirikiano zaidi kati ya taasisi za kitiba na wagonjwa Mashahidi, Halmashauri za Uhusiano na Hospitali zilianzishwa na Baraza Linaloongoza la Mashahidi wa Yehova. Zikifanyizwa na Mashahidi wakomavu waliozoezwa ili kushughulika kwa uelewano na madaktari na hospitali, halmashauri hizo zilimaliza mahitilafiano, na zikaanzisha hali ya ushirikiano mkubwa zaidi. Kuanzia halmashauri chache kama hizo katika 1979, hesabu yazo sasa imekua hadi 850 katika nchi 65. Hiyo yamaanisha kwamba utumishi wazo wenye kusaidia sasa wapatikana kwa Mashahidi wa Yehova wapatao milioni 3.5.
Wazee zaidi ya 4,500 katika makutaniko ya Mashahidi wa Yehova wamezoezwa kusema na madaktari ili kuwasaidia kuona kutoka fasihi yenyewe ya tiba mambo yote yanayoweza kufanywa bila kutumia njia ya kutia damu mishipani. Katika hali ambapo kuna uhitaji fulani wa pekee, makala zifaazo hupelekwa kwa faksi moja kwa moja kwenye hospitali ili kusaidia matabibu wawatibu Mashahidi bila kutumia damu. Au halmashauri hizo hupanga kuwaona madaktari wengine wenye kushirikiana ili kusitawisha njia za matibabu au upasuaji bila kutia damu.
Kwa kielelezo, katika visa vingi ambamo damu nyingi imepotezwa kwa sababu ya kupungua kwa chembe nyekundu za damu, ambapo madaktari walisema kulikuwa na uhitaji wa kutia damu mishipani ili kuongeza chembe nyekundu, washiriki wa Halmashauri ya Uhusiano na Hospitali wameweza kushiriki makala kutoka kwa fasihi za kitiba zinazoonyesha matokeo bora ya utibabu wa erythropoietin (EPO) iliyochanganywa kufanya jambo lilelile. Homoni hiyo iliyosanidiwa hutenda kama erythropoietin ya asili ipatikanayo katika figo zetu na huchochea uboho wa mifupa kupeleka chembe mpya zilizo bora katika mkondo wa damu.
Madaktari fulani wamehisi kwamba utibabu wa EPO hauwezi kufanya kazi haraka vya kutosha ili kutimiza uhitaji, lakini visa kadhaa vinavyohusu Mashahidi wa Yehova vimeonyesha jinsi ipatavyo matokeo haraka. Katika kisa kimoja, katika siku ileile ambayo utibabu wa EPO ulitumiwa, hesabu ya chembe mpya nyekundu ilikuwa tayari mara nne kuliko ile ya kawaida! Katika siku nyingine mgonjwa alipata nafuu kidogo, na kufikia siku ya nne, hesabu ya chembe nyekundu ilianza kupanda. Katika siku kadhaa zaidi, ilikuwa ikipanda haraka. Mgonjwa huyo aliokoka. Kwa njia hiyo madaktari na pia mgonjwa walinufaishwa na utendaji mbalimbali wa hizo Halmashauri za Uhusiano na Hospitali.
Madaktari katika Australia waliposema hawakuweza kuokoa uhai wa mgonjwa Shahidi bila kutumia damu ili kutibu maradhi fulani ya tropiki yasiyo ya kawaida, walitoa maombi kwenye Halmashauri ya Uhusiano na Hospitali ya mahali hapo kwa ajili ya msaada wowote ambao halmashauri hiyo ingeweza kuwapa katika kupata habari juu ya kutibu bila kutumia damu. Ofisi ya tawi ya Australia ya Mashahidi wa Yehova ilijulishwa juu ya uhitaji huo. Waliwasiliana na Huduma za Habari za Hospitali kwenye ofisi za makao makuu ya kimataifa ya Mashahidi wa Yehova katika Brooklyn, New York. Ilifanya utafiti kwenye kituo cha data za tiba. Makala zenye kusaidia zilipelekwa kwa faksi hadi Australia. Muda wa saa 11 tu baada ya kuondoka kwenye ofisi ya daktari, mshiriki wa Halmashauri ya Uhusiano na Hospitali ya Australia alikuwa amerudi akiwa na makala zilizohitajiwa. Hizo zikawa zenye matokeo, na mgonjwa huyo akapona. Habari za kitiba zilizopelekwa kwa faksi zimepelekwa kutoka New York hadi mbali kama Nepal.
Utafiti na Msaada Bora
Ubora wa utafiti unaofanywa na Mashahidi wa Yehova katika fasihi ya kitiba wafaa na ni wa kisasa. Muuguzi aliyehitimu ambaye ni mkurugenzi msaidizi wa huduma za kitiba kwenye hospitali moja katika Oregon, U.S.A., alisema hivi katika makala katika kichapo cha kitiba kwa ajili ya mameneja wa vyumba vya upasuaji: “Mashahidi wa Yehova . . . [wako] mbele zaidi yetu. Wao wafahamu zaidi juu ya njia isiyohusu damu na bidhaa za damu na mara nyingi hutuandalia fasihi kabla ya sisi hata kusikia juu yayo.”—OR Manager, Januari 1993, ukurasa 12.
Madaktari fulani na vituo vya kitiba vilivyo mashuhuri sana vinavyoweza kutibu bila kutumia damu nzima-nzima huwa tayari kuzungumzia mifikio yao na utaratibu wao wa tiba. Itikio lao la fadhili kwa uhitaji huu limesaidia kuokoa uhai, kama inavyoweza kuonwa katika visa vya kutibiwa kwa mafanikio kwa ajili ya leukemia na katika aina mbalimbali za upasuaji. Mara nyingi mawasiliano hayo ya kitiba yalifanywa kwa kupiga simu za kimataifa.
Ule mpango wa kuhamisha mgonjwa kutoka hospitali moja hadi nyingine, kutoka sehemu moja ya nchi hadi ile nyingine, na hata kutoka nchi moja hadi nyingine, waonyesha kadiri ambayo Mashahidi wa Yehova wamefikia ili kusaidia wale walio katika uhitaji wanapokabili hali ya kitiba yenye kutahini imani. Vielelezo fulani ni hivi: Mgonjwa aliye mtu mzima alisafirishwa kwa ndege kutoka Suriname hadi Puerto Rico; mwingine alisafirishwa kwa ndege kutoka Samoa hadi Hawaii; kitoto, kutoka Austria hadi Florida, U.S.A.
Madaktari Zaidi Washirikiana
Maendeleo katika hali ya Mashahidi wa Yehova yaweza kuonwa pia katika idadi inayozidi kukua ya matabibu wenye nia ya kushirikiana nao katika jambo hilo, kutoka karibu 5,000 miaka mitano iliyopita hadi zaidi ya 30,000 sasa katika mabara 65. Idadi hiyo ya madaktari wenye uwezo imewezesha kuwe na tukio jingine lenye kufaa—kufanyizwa kwa vituo zaidi ya 30 vya utibabu na upasuaji usiotia ndani damu katika mabara mbalimbali.
Hivyo, siku hizi, angalau katika Amerika Kaskazini, ni vigumu kusikia juu ya jitihada za kulazimisha mtio wa damu mishipani kwa mtu mzima, na mabara mengine mengi yanasitawi kuelekea jambo hilohilo. Matatizo mengi sasa yahusu watoto waliotoka kuzaliwa na hasa kuhusu wale waliozaliwa kabla ya wakati wao. Watoto hao wasiokomaa huanza na matatizo mengi yanayohusiana na viungo ambavyo havijakomaa ambavyo havitendi kazi kama kawaida, kama vile mapafu na figo. Lakini madaktari wanagundua njia za kutibu hali hizo bila kutia damu mishipani. Kwa kielelezo, mfanyizo wa mchanganyiko wenye ute-ute wapatikana ili kuondoa matatizo ya kupumua. Utumizi wa EPO wakubaliwa na wengi katika kushughulikia kupungua kwa chembe nyekundu za damu wakati mmoja azaliwapo kabla ya wakati barabara.
Msaada kwa Wafanyakazi na Maofisa wa Kitiba
Ili kusaidia matabibu wa watoto na wa wale waliotoka kuzaliwa watibu watoto wa Mashahidi wa Yehova bila kutia damu mishipani, Huduma za Habari za Hospitali imetokeza buku lenye faharisi ya sehemu tatu ya makala 55 kutoka kwa fasihi ya kitiba inayoonyesha yale yanayoweza kufanywa bila damu kwa ajili ya matatizo mengi ya wale waliotoka kuzaliwa.
Ili kufikia mahakimu, wafanyakazi wa jamii, hospitali za watoto, matabibu wa watoto waliotoka kuzaliwa, na matabibu wa watoto kwa habari juu ya kupatikana kwa njia nyinginezo zisizohusisha damu, Mashahidi wa Yehova wametokeza kihususa kwa ajili ya wafanyakazi na maofisa hao wa kitiba buku la kurasa 260 liitwalo Family Care and Medical Management for Jehovah’s Witnesses.a Ni kitabu chenye kurasa zinazoweza kuondolewa ili kiendelee kutiwa habari za kisasa. Kwa kuwa kumekuwa hali fulani za kuelewa vibaya maisha ya familia miongoni mwa Mashahidi wa Yehova, hicho pia chafanya iwe wazi kwa wastadi ule upendo ambao wazazi wanao kwa ajili ya watoto wao katika hali ambayo bila shaka ni yenye mafaa na ya kujali inayotokezwa na mtindo-maisha unaoletwa na ufundishaji wa Biblia.
Kichapo hicho kinapokewaje? Baada ya kuchunguza yaliyomo, katibu msimamizi wa hospitali moja ya watoto katika Pennsylvania, U.S.A., alisema angetazamia wafanyakazi wake wakisome na kukitumia. Yeye aliongeza hivi: “Kisiponiru-dia kurasa zikiwa zimekunjwa na kuchakaa, nitataka kujua sababu!” Tayari mahakimu fulani wamebadili amri zao za mahakama ili kuwataka matabibu watumie njia zote nyinginezo zisizohusisha damu kabla ya kutumia damu. Watoto wametibiwa bila damu na wamerudi nyumbani wakiwa wamepona.
Itikio la kawaida ni lile la hakimu mmoja wa maswala ya watoto katika Ohio, U.S.A. Alivutiwa sana na buku la Family Care hivi kwamba aliagiza nakala saba za ziada kwa ajili ya wenzake. Sasa yeye hurekebisha amri zake za mahakama ili kusawazisha kazi ya tabibu na haki ya wazazi, akitimiza hayo katika njia mbili. Yeye huonyesha kihususa katika amri yake (1) kwamba ni lazima madaktari kwanza watumie njia zote nyinginezo kabla ya kutumia damu; na (2) kwamba ni lazima matabibu wamhakikishie kwamba damu watakayotumia imechunguzwa na haina UKIMWI na mchochota-ini. Katika amri tatu alizotoa tangu alipoanza kuzirekebisha, watoto wote watatu walitibiwa kwa mafanikio bila kutia damu mishipani.
Dakt. Charles H. Baron, profesa wa sheria kwenye Shule ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Boston, alitoa insha mwaka uliopita kwenye mkutano wa wasomi katika Chuo Kikuu cha Paris. Mada yake ilikuwa “Damu, Dhambi, na Kifo: Mashahidi wa Yehova na Shirika la Haki za Mgonjwa la Amerika.” Katika insha hiyo yenyewe, fungu lifuatalo lilisema hivi juu ya kazi ya Halmashauri za Uhusiano na Hospitali za Mashahidi:
“Wao hata wameweza kufanya tiba ya Amerika ifikirie baadhi ya itikadi zayo kwa kupata uthibitisho zaidi. Katika kufanya hivyo, jamii nzima ya Amerika imefaidika. Kwa sababu ya kazi ya Halmashauri za Uhusiano na Hospitali za Mashahidi, leo si Mashahidi wa Yehova pekee wasioelekea kutiwa damu isiyohitajiwa, bali pia wagonjwa kwa ujumla. Wagonjwa kwa ujumla hufurahia uhuru mkubwa zaidi juu ya maamuzi mengi ya utunzi wa afya kwa sababu ya ile kazi iliyofanywa na Mashahidi wakiwa sehemu ya shirika kuu la haki za wagonjwa. Na kusudi la uhuru kwa ujumla na hasa uhuru wa kidini umesitawishwa na ukinzani wa kujitoa wa Mashahidi dhidi ya jitihada za kuwalazimisha kuchukua hatua zisizopatana na itikadi zao za kidini.”
Huenda utendaji huo wote wa Halmashauri za Uhusiano na Hospitali usiwe kuhubiri habari njema za Ufalme wa Mungu moja kwa moja, lakini kwa hakika unatoa jibu kwa mwito wa moja kwa moja unaofanywa dhidi ya ibada yetu katika ile ambayo baraza linaloongoza la karne ya kwanza liliita mojawapo mambo “yaliyo ya lazima” ya utumishi wetu mtakatifu. (Matendo 15:28, 29) Hata hivyo, kwa kupendeza, jitihada yetu ya ujasiri lakini yenye staha ili kuwasiliana imefungua njia kwa baadhi ya wastadi wa tiba kuitikia ujumbe wa Ufalme. Washiriki kadhaa wa Halmashauri za Uhusiano na Hospitali wameanza mafunzo ya Biblia pamoja na madaktari waliokutana nao katika utendaji wa kihalmashauri, madaktari wawili kama hao wakibatizwa hivi karibuni.
Kwa hiyo kwa msaada wa mpango wa Halmashauri ya Uhusiano na Hospitali, Mashahidi wa Yehova wanasaidiwa kutii sheria kamilifu ya Yehova juu ya kuepuka damu, bila kuridhiana uaminifu-maadili wao na bado wakipata utunzaji wa kitiba unaohitajiwa. (Zaburi 19:7) Kwelikweli kumekuwa na mafanikio mazuri yenye kuendelea katika kuziba pengo lililokuwapo wakati mmoja. Sasa madaktari na hospitali wamefahamishwa vizuri zaidi juu ya jinsi wanavyoweza kuandaa utibabu unaopatikana bila kutumia damu. Kwa wagonjwa, watu wa ukoo, washiriki wa kidini, na wafanyakazi wa hospitali, hilo hutokeza kile ambacho kila mtu hutaka—kupona kwa mgonjwa.—Imechangwa na Huduma za Habari za Hospitali kwenye makao makuu ya Watch Tower Society.
[Maelezo ya Chini]
a Katika lugha ya Kiingereza pekee.
[Picha katika ukurasa wa 25]
Halmashauri ya Uhusiano yajadiliana na daktari mmoja
[Picha katika ukurasa wa 26]
“Utunzi wa Familia”