Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g93 12/22 kur. 20-24
  • Kielelezo cha Uaminifu cha Baba Yangu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kielelezo cha Uaminifu cha Baba Yangu
  • Amkeni!—1993
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Malezi ya Mashariki-Magharibi
  • Miaka ya Vita Yenye Maumivu
  • Burudisho la Kiroho
  • Mvunjiko wa Kuhuzunisha wa Familia
  • Mazungumzo ya Biblia ya Kukumbukwa
  • Huduma Iliyoongezwa
  • Miaka ya Mwisho-Mwisho ya Mama na Baba
  • Kukaza Macho na Moyo Kwenye Tuzo
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1996
  • Maamuzi Mazuri Yalileta Baraka za Kudumu
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2007
  • Mchukua-Nuru kwa Mataifa Mengi
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2000
  • Nilichochewa na Uaminifu-Mshikamanifu wa Familia Yangu kwa Mungu
    Amkeni!—1998
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1993
g93 12/22 kur. 20-24

Kielelezo cha Uaminifu cha Baba Yangu

ILIKUWA Julai 6, 1947, na familia yetu ilikuwa inahudhuria mkusanyiko wa wilaya wa Mashahidi wa Yehova katika London, Uingereza. Baba yangu alikuwa na machozi ya shangwe machoni mwake aliponyoosha mkono wake kunisaidia kutoka kwa kidimbwi cha ubatizo. Baba yangu nami tulikuwa tu tumetoka kubatizwa kwa wonyesho wa wakfu wetu kwa Yehova, Muumba na Mwenye Enzi Kuu. Mama yangu na ndugu zangu watatu walikuwepo kwenye pindi hii yenye furaha.

Hata hivyo, kwa kusikitisha, umoja wa familia yetu katika ibada ya Kikristo ungeharibika upesi baadaye. Lakini kabla ya kusema juu ya hilo na jinsi kielelezo cha uaminifu cha baba yangu kilivyoniathiri, acheni niseme juu ya maisha yake ya mapema.

Malezi ya Mashariki-Magharibi

Baba yangu, Lester, alizaliwa Hong Kong katika Machi 1908. Baba yake alikuwa kaimu msaidizi wa msimamizi wa bandari. Baba alipokuwa mvulana, baba yake alikuwa akimchukua waende safari kwa mashua ili kuangalia utendaji katika Hong Kong na visiwa vilivyo karibu. Kisha, baba alipokuwa na umri wa miaka minane, baba yake akafa. Baadaye, mama yake aliolewa tena, na familia ikahamia Shanghai. Katika 1920 mama yake alimpeleka baba na dada yake wa miaka kumi, Phyl, Uingereza kwa ajili ya shule.

Baba alitumia miaka yake iliyofuata karibu na Canterbury Cathedral, makao makuu ya Kanisa la Anglikana. Kuhudhuria kwake kanisa huko kulikuwa mwanzo wa mambo ya kidini. Phyl alienda kwenye shule ya bweni kaskazini mwa London, lakini yeye na baba walikuwa marafiki wakubwa sana wakati wa miaka hiyo kwa sababu walitumia likizo za shule wakiwa pamoja. Miaka mitano baadaye, katika 1925, baba alipomaliza shule, mama yake ali-rudi Uingereza na akahakikisha kwamba baba alikuwa ameanzisha biashara. Kisha, mwaka uliofuata, alirudi Shanghai akimchukua shangazi yangu Phyl.

Kabla ya mama ya baba kwenda, alimwachia nakala ya kitabu kilichoandikwa na babu. Ilikuwa hadithi ya kishairi ya maisha ya Buddha kilichoitwa “The Light of Asia.” Hili lilimfanya baba aanze kufikiri juu ya sababu hasa ya maisha. Akiwa Canterbury alipendezwa na adhama ya kanisa kuu na kawaida za mambo ya kidini, lakini ukosefu wa mafundisho ya kiroho ulimwacha na hisia tupu. Kwa hiyo alijiuliza: ‘Je! makanisa ya Mashariki yana majibu?’ Aliamua kuchunguza. Wakati wa miaka iliyofuata, alichunguza Dini ya Buddha, Dini ya Shinto, Uhindu, Dini ya Konfyushasi, na Uislamu. Lakini kila moja yazo ilishindwa kujibu maswali yake.

Baba aliishi katika nyumba ya michezo iliyokuwa ikisimamiwa na kampuni aliyokuwa akiifanyia kazi, na alifurahia kuelea na mtumbwi, kucheza mpira wa mabavu, na michezo mingineyo. Upesi akashikwa na mapenzi na Edna, msichana mwenye kuvutia ambaye alikuwa na mapendezi yaleyale ya michezo. Walioana katika 1929 na walibarikiwa kuwa na wana wanne kwa miaka kumi iliyofuata.

Miaka ya Vita Yenye Maumivu

Wakati wa miaka ya 1930, dalili za kukaribia kwa Vita ya Ulimwengu ya 2 zilikuwa zinaongezeka, kwa hiyo baba akaamua kuhama kutoka London kuelekea mashambani. Tulihama miezi michache tu kabla ya vita kuanza katika Septemba 1939.

Kuandikishwa kwa lazima kwa ajili ya utumishi wa vita kulianzishwa, na viwango vya umri viliongezwa hatua kwa hatua vita ilipoendelea. Badala ya kungoja kulazimishwa kuandikishwa, baba alijitolea kwa utumishi wa Royal Air Force na akaitwa katika Mei 1941. Ijapokuwa pindi kwa pindi aliweza kufika nyumbani akiwa likizoni, ilikuwa miaka sita kabla ya uhusiano wa kawaida wa familia kurudi. Mzigo wa kututunza sisi watoto—sisi wakubwa ambao tulikua tukiingia utineja wetu—ukawa daraka la mama akiwa peke yake.

Burudisho la Kiroho

Yapata miaka miwili hivi kabla ya baba kuachiliwa katika Royal Air Force, Mashahidi wa Yehova wawili walimzuru mama na wakaanzisha funzo la Biblia pamoja naye. Mama alimwandikia baba akamwambia jinsi alivyokuwa anafurahia mambo aliyokuwa akijifunza. Wakati mmoja alipokuwa likizoni, alimchukua kwenye funzo la Biblia la kutaniko kwenye nyumba ya faragha.

Baba aliachiliwa kutoka jeshi katika Desemba 1946 na akaanza kuhudhuria mazungumzo ya Biblia ambayo mama alikuwa nayo pamoja na wale mabibi wawili Mashahidi. Walitambua kupendezwa kwake nao wakamfanya Ernie Beavor, mwangalizi msimamizi, amtembelee baba. Kwa jioni moja tu, Ndugu Beavor alijibu kutoka kwa Biblia vipingamizi vyote vya baba. Wakati wa majuma mawili yaliyofuata, alipokuwa akisafiri kazini kuelekea London kila siku kwa gari-moshi, alisoma vitabu vitatu ambavyo Ndugu Beavor alimpatia. Ndugu Beavor alipomtembelea tena, baba alimsalimu hivi: “Hii ndiyo kweli ambayo nimekuwa nikiitafuta! Nifanyeje?”

Kuanzia hapo baba akaanza kutupeleka sisi wavulana mikutanoni. Hata hivyo, mama hakutaka sikuzote kuja nasi. Kupendezwa kwake kulianza kupungua. Hata hivyo, sisi sote tulienda mkusanyikoni katika London katika Julai 1947, ambapo baba na mimi tulibatizwa. Baadaye, mama alikuwa akija mikutanoni pindi kwa pindi.

Muda mfupi baada ya ubatizo huo, shangazi yangu Phyl akaja Uingereza kututembelea, na kwa shangwe ya baba yangu, aliikubali kweli ya Biblia na akabatizwa. Aliporudi Shanghai, alikutana na Stanley Jones na Harold King, wamishonari wawili wa Mashahidi wa Yehova ambao walikuwa wametumwa huko muda mfupi tu mbeleni. Wamishonari hao walitiwa gerezani baadaye, mmoja kwa miaka saba na mwingine kwa miaka mitano, na serikali ya Kikomunisti iliyokuwa ikitawala. Walimsaidia Phyl kiroho hadi mume wake alipostaafu kazini katika China. Kisha yeye na mume wake wakarudi Uingereza na kuishi karibu nasi.

Mvunjiko wa Kuhuzunisha wa Familia

Wakati huo, uwasiliano mzuri kati ya mama na baba ukawa tatizo. Mama aliona bidii ambayo baba alifuatia imani yake mpya, akaamini kwamba usalama wa mali ya kimwili wa familia ungekuwa hatarini, akaanza kupinga utendaji wake wa Kikristo. Mwishowe, katika Septemba 1947, alimkabili na sharti la kwamba aache imani ya Kikristo au sivyo mama aende zake.

Baba alihisi kwamba alikuwa amemtuliza mama hofu zake kwa kusababu pamoja naye kwa Maandiko, akimwonyesha kwamba hakukuwa na sababu ya kuogopa. Hata hivyo, upeo ulifika bila onyo jingine katika Oktoba 1, 1947. Baba alipofika nyumbani kutoka kazini siku hiyo, alipata nyumba tupu na mimi nimeketi kwenye ngazi za mlango na masanduku yetu. Mama alikuwa ameenda, akichukua kila kitu, kutia na ndugu zangu watatu. Nilimwambia baba kwamba nilikuwa nimechagua kukaa na yeye. Mama hakuwa hata ameacha taarifa yoyote.—Mathayo 10:35-39.

Ernie Beavor alifanya mipango ili tukae na wenzi wa ndoa wawili wazee-wazee hadi baba apate mahali pa kuishi. Walikuwa wenye fadhili sana kwetu nao wakatufariji na maneno ya mtume Paulo kwenye 1 Wakorintho 7:15: “Lakini yule asiyeamini akiondoka, na aondoke. Hapo huyo ndugu mume au ndugu mke hafungiki. Lakini Mungu ametuita katika amani.”

Hatimaye tuliwasiliana na famila yetu na tukawatembelea lakini upesi tukatambua kwamba kuridhiana imani yetu ndilo lingekuwa suluhisho pekee la kukubaliwa na mama. Tulijua kwamba kuridhiana hakungeleta baraka kutoka kwa Yehova. Kwa hiyo baba aliendelea na kazi yake ya kimwili, akimpa mama utegemezo wa kifedha kwa ajili ya ndugu zangu. Nilipoacha shule katika 1947, nilifanya kazi ya muda-muda, na katika Januari 1948, nilikubaliwa kuingia huduma ya wakati wote.

Mazungumzo ya Biblia ya Kukumbukwa

Nikiwa katika huduma ya shambani siku moja, nilipokuwa ningali na umri wa miaka 17, niliongea na mtu katika nyumba ndogo ya shamba. Nilipokuwa nikitembelea huko, Winston Churchill, kiongozi wa Uingereza wakati wa Vita ya Ulimwengu ya 2, alifika. Mazungumzo yangu yalikatizwa, lakini Bw. Churchill aliona Mnara wa Mlinzi na akanipongeza kwa kazi yangu.

Siku kadhaa baadaye nilienda kuhubiri tena nikapiga kengele ya mlango wa nyumba kubwa sana. Bawabu akafungua mlango, na nilipoomba kuongea na mwenye nyumba, aliniuliza kama nilimjua. Sikumjua. “Hapa ni Chartwell,” akasema, “makao ya Winston Churchill.” Wakati huohuo, Bw. Churchill akajitokeza. Akakumbuka kukutana kwetu wakati uliopita naye akanikaribisha. Tuliongea kidogo, alikubali vitabu vitatu na akanialika nirudi.

Baadaye, alasiri moja yenye joto, nilirudi na tena nikakaribishwa. Bw. Churchill alinipa maji ya limau na baada ya salamu fupi akasema: “Nitakupa nusu saa uniambie unafikiri Ufalme wa Mungu ni nini, lakini lazima uache nikuambie ninalouamini kuwa.” Ndivyo tulivyofanya.

Bw. Churchill alifikiri kwamba Ufalme wa Mungu utasimamishwa kupitia watu wa serikali wachaji-Mungu na kwamba wanadamu wasipojifunza kuishi kwa amani, hautakuja kamwe. Niliweza kueleze maoni ya Biblia juu ya Ufalme wa Mungu na baraka utakazoleta. Bw. Churchill alikuwa mwenye moyo mchangamfu sana na aliiheshimu kazi yetu.

Kwa kusikitisha, sikuweza kuwasiliana naye tena kamwe. Lakini nashukuru kwamba, ijapokuwa nilikuwa ningali tineja, nikiwa na mazoezi na kitiamoyo nilichopata kutoka kwa baba yangu, niliweza kumtolea ushahidi mzuri mtu mkuu hivyo katika serikali.—Zaburi 119:46.

Huduma Iliyoongezwa

Katika Mei 1950, mama alituandikia akituambia alikuwa anahamia Kanada na angemchukua John, ndugu yangu mchanga zaidi. Wakati huo ndugu zangu Peter na David walikuwa wanajitunza wenyewe. Kwa hiyo baada ya miaka 18 akiwa na kampuni yake (kutia na miaka ya vita alipowekwa kwenye orodha yao ya waajiriwa), baba alijiuzulu na akaomba utumishi wa painia wa kawaida. Alianza utumishi wa wakati wote katika Agosti 1950, aliporudi kutoka kuhudhuria mkusanyiko mkubwa wa kimataifa wa Mashahidi wa Yehova katika New York. Muda mfupi baada ya mwaka baadaye, katika Novemba 1951, baba aliwekwa kuwa mwangalizi asafirie akaanza kutembelea makutaniko kuyatia moyo. Wakati huo, katika vuli ya 1949, nilialikwa kutumikia katika ofisi ya tawi ya Mashahidi wa Yehova katika London, Uingereza.

Kisha ikaja baraka nyingine kubwa—baba na mimi tukaalikwa katika darasa la 20 la shule ya mishonari ya Gileadi katika New York. Darasa hilo lilianza katika Septemba 1952, na tukahitimu Februari uliofuata. Baadaye, nilitumikia katika makao makuu ya ulimwenguni pote ya Mashahidi wa Yehova katika Brooklyn, New York, naye baba akatumwa akiwa mwangalizi asafiriye katika Indiana.

Darasa lote la 20 lilizuiwa kwenda kwenye migawo yetu ya mishonari ili kwamba tuhudhurie mkusanyiko wa kimataifa katika Jiji la New York mnamo Julai. Nilikuja kumpenda sana mmoja wa wanadarasa wenzangu, Kae Whitson, na tukaamua kuoana. Tulipewa mgawo wa kazi ya kusafiri katika Michigan, halafu miaka miwili baadaye, tulipewa mgawo wa mishonari katika Kaskazini mwa Ailandi.

Hata hivyo, tulipokuwa karibu tu kusafiri kwa meli, Kae aligundua kuwa alikuwa na mimba. Kwa hiyo tukaanza mgawo mwingine, ule wa kulea mwana na binti watatu wawe wahudumu wa wakati wote wenye mafanikio, kama vile baba yangu alivyonizoeza kuwa. Katika Novemba 1953, baba alienda Afrika, na katika Januari 4, 1954, alifika katika mgawo wake wa mishonari Rhodesia ya Kusini (sasa Zimbabwe).

Baba alikuwa na mengi ya kujifunza—njia mpya ya maisha, desturi mpya, na majaribu mapya ya imani. Huko nyuma katika 1954, Rhodesia ya Kusini haikuwa imeathiriwa na njia za watu wa Magharibi. Baada ya mwaka mmoja katika ofisi ya tawi, baba alitumwa katika kazi ya kusafiri akiwa mwangalizi wa wilaya. Aliitwa tena katika ofisi ya tawi katika 1956 na alitumikia huko hadi kifo chake Julai 5, 1991. Aliona familia ya Betheli ikikua kuanzia 5 katika 1954 hadi zaidi ya 40, na idadi ya wahubiri wa Ufalme kutoka 9,000 hadi zaidi ya 18,000.

Miaka ya Mwisho-Mwisho ya Mama na Baba

Baba na mama hawakutalikiana kamwe. Baada ya kutoka Uingereza, mama aliishi kwa muda katika Kanada na akahamia United States akiwa na John. Ndugu zangu hawajakuwa Mashahidi. Hata hivyo, mama alifikiwa na Mashahidi katikati ya miaka ya 1960. Katika 1966, alihamia Mombasa, Kenya, ambapo alianza tena kujifunza. Lakini mwaka uliofuata akapatwa na matatizo ya mfadhaiko.

Ndugu zangu Peter na David walipanga ili apelekwe Uingereza, ambako alipata matibabu. Alipona na akaanza tena kujifunza na Mashahidi. Waweza kuwazia shangwe ya baba yangu alipomwambia kwamba alikuwa abatizwe kwenye mkusanyiko London katika 1972. Mke wangu nami tulisafiri kwa ndege kutoka United States tuwe pamoja naye wakati wa ubatizo wake.

Mwaka uliofuata baba alikuwa na likizo, na akiwa Uingereza, alikuwa na shangwe ya kufanya kazi pamoja na mama katika huduma ya nyumba kwa nyumba. Baada ya hapo alikuja kutembelea familia yetu katika United States. Baba na mama walizungumza juu ya mapatano, lakini mama akamwambia: “Tumetengana mbali kwa muda mrefu sana. Itakuwa vigumu. Tuache hadi ulimwengu mpya, wakati kila kitu kitakuwa sawa.” Kwa hiyo baba akarudi kwenye mgawo wake. Ugonjwa wa mama akiwa Kenya ulimwathiri, na mwishowe akalazwa hospitali, ambapo alikufa katika 1985.

Katika 1986, baba akawa mgonjwa sana, hivyo ndugu yangu Peter na mimi tukamtembelea nyumbani mwake Zimbabwe. Jambo hilo lilimtia moyo sana na likaonekana kama lilimpa nguvu na mtazamo mpya wa maisha. Ndugu Waafrika walikuwa na fadhili nyingi sana kwangu kwa sababu nilikuwa mwana wa Lester! Kwa kweli, mfano wa baba ulikuwa na uvutano unaofaa kwa wote waliomjua.

Sasa mimi mwenyewe ni mgonjwa. Madaktari waniambia kuwa nina wakati mfupi wa kuishi. Wanasema kwamba nina amiloidosisi, ugonjwa usio wa kawaida wenye kufisha. Hata hivyo, nina furaha kwamba watoto wangu wanafuata kielelezo changu, kama nilivyofuata kielelezo cha baba yangu mwaminifu. Wote wangali wamtumikia Yehova kwa uaminifu-mshikamanifu pamoja nasi. Ni faraja kama nini kujua kwamba iwe tutaishi au tutakufa, tuna tumaini hakika la kufurahia milele baraka nyingi za Baba yetu mpendwa wa kimbingu kwa sababu tumefanya mapenzi yake kwa uaminifu! (Waebrania 6:10)—Kama ilivyosimuliwa na Michael Davey.a

[Maelezo ya Chini]

a Mnamo Juni 22, 1993, wakati simulizi hili lilipokuwa linakamilishwa, Michael Davey alilala usingizi katika kifo.

[Picha katika ukurasa wa 21]

Kushoto: Wazazi wangu pamoja na ndugu yangu mkubwa na mimi

[Picha katika ukurasa wa 22]

Niliweza kuongea na Winston Churchill kwa upana juu ya Ufalme wa Mungu

[Hisani]

Picha ya USAF

[Picha katika ukurasa wa 23]

Baba yangu, Lester, muda mfupi kabla ya kifo chake

[Picha katika ukurasa wa 24]

Nikiwa na mke wangu, Kae

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki