Ripoti Zenye Kupingana Juu ya Mmwagiko wa Mafuta wa Exxon
APRILI uliopita, miaka minne baada ya mmwagiko wa mafuta wa Exxon Valdez katika Prince William Sound ulioleta msiba mkubwa, hatimaye wanasayansi wa Exxon walitoa matokeo ya uchunguzi wao. Kulingana na gazeti New Scientist, Exxon ilisema kwamba “uharibifu wa kutokana na mmwagiko huo ulidumu tu kwa miezi michache na kwamba Prince William Sound ilikuwa imepata nafuu kabisa.” Tofauti sana na hayo ulikuwa ni uchunguzi mbalimbali wa wanasayansi wa serikali ya U.S. waliokuwa wamechukua miaka minne wakichunguza matokeo ya mmwagiko huo: “Ni wazi kwamba kupata nafuu baada ya muda mrefu bado hakuwezekani. Katika hali nyinginezo itachukua muda wa miaka mingi.” Wao walishtaki hivi: “Exxon inateua tu habari yenye kuifaa ili kuchunguza juu ya kupata nafuu.”[1] Madondoo ya matokeo ya uchunguzi wa mwanabiolojia wa maji ambaye pia ni mfanyabiashara ya uvuvi Rick Steiner yatoa hali za sasa katika Prince William Sound.
“Jambo lenye kutokeza zaidi ni ukosefu wa fisi-maji, bata-halikuini, muresi, ndege walaji chaza. . . . Katika maeneo ya kujaa na kupwa kwa maji, vikundi vya kome hubaki na mafuta yaliyonaswa kwa miaka minne iliyopita. . . . Wavuvi walilazimika kungoja hadi kurudi kwa samaki salmoni katika kiangazi kilichopita ili kuona kama mafuta yaliathiri uzao wa salmoni-waridi waliotokea katika wakati wa mmwagiko. Kurudi kulikuwa kwenye msiba: ni robo moja hadi theluthi moja tu ya waliotarajiwa walirudi. . . . Wanasayansi wa taifa hilo wamepata matokeo ya mafuta kwa viumbe vingi kutokea samaki hadi nyangumi—matokeo kama kuharibika kwa ubongo, kutoweza kuzaa, kuharibika kwa chembe za urithi, ulemavu wa mwili kama uti wa mgongo uliopindika, uchovu, ukuzi wa polepole wa mwili na wa uzani wa mwili, badiliko katika tabia ya ulaji, kiasi kilichopungua cha mayai, uvimbe wa macho, ongezeko la vimelea, uharibifu wa ini na tabia isiyo ya kawaida.
“Kwa wazi, hakuna kitu kama rudisho baada ya mmwagiko wa mafuta. Hatuwezi tu kurekebisha mfumo wa mazingira kama tuwezavyo kurekebisha mashine iliyovunjika. Kwa watu wengi, utambuzi huo umekuwa usiopendeza.”—National Wildlife EnviroAction.[2]
Mwanasayansi mmoja wa serikali asema hivi: “Njia ambayo uchunguzi huo unafanywa haupendelei upande wowote. Sayansi inaongozwa na mawakili wanaoamua ni uchunguzi upi utategemeza madai ya kulipwa ridhaa kwa ajili ya upotezo—au utasaidia kupinga madai yao.”[3] Gazeti New Scientist lauliza swali hili lifaalo: “Je! sayansi inategemeka wakati kuna hangaiko la kitaifa?”[4]
[Hisani ya Picha katika ukuraswa wa 31]
Wesley Bocxe/Sipa Press