Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g94 2/22 kur. 4-7
  • Kusaidia Watu Kujua Kusoma

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kusaidia Watu Kujua Kusoma
  • Amkeni!—1994
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Ukosefu wa Fursa
  • Mfano wa Mtu Mzima Anayejifunza
  • Wasaidie Wanafunzi Wako wa Biblia Wafikie Ubatizo
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova (Funzo)—2021
  • Jinsi ya Kumsaidia Mwanafunzi wa Biblia Afikie Hatua ya Ubatizo—Sehemu ya Pili
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova (Funzo)—2020
  • Jinsi ya Kumsaidia Mwanafunzi wa Biblia Afikie Hatua ya Ubatizo—Sehemu ya Kwanza
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova (Funzo)—2020
  • Kazia Uangalifu ‘Ufundi Wako wa Kufundisha’
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2008
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1994
g94 2/22 kur. 4-7

Kusaidia Watu Kujua Kusoma

MAMILIONI hao wasiojua kusoma na kuandika ni akina nani? Wao hasa ni wakazi wenye madaraka na wenye kufanya kazi kwa bidii. Katika nchi zinazoendelea, wao huandaa chakula, mavazi, na makao kwa idadi kubwa ya watu. Katika nchi zenye utajiri, wao hufanya kazi ambazo hakuna mtu mwingine angekubali kufanya—kazi zinazochosha sana, zenye kurudiwa-rudiwa, na za hali ya chini, lakini ambazo bado ni muhimu kwa jumuiya.

Mara nyingi, sababu inayofanya watu wasiwe na ustadi wa kusoma na kuandika ni ukosefu wa fursa ya kujifunza. Wakiwa kikundi, watu wasiojua kusoma na kuandika si wajinga, wasiojua kitu, au wasioweza kutimiza mambo. “Sina tatizo la kutumia akili,” akasema mtu wa kawaida anayejifunza. “Tatizo langu ni kusoma tu.”

Ukosefu wa Fursa

Kwa watu wengi, kutojua kusoma na kuandika hufungamanishwa na umaskini. Katika familia, umaskini hufanya watu wahangaikie kupata chakula kuliko wanavyohangaikia kupata elimu. Watoto wahitajiwapo kufanya kazi nyumbani, basi hawaendi shuleni. Na wengi wanaoenda shuleni hawaendelei na masomo.

Umaskini huleta madhara katika nchi nzima pia. Nchi zinazoendelea zenye mzigo mkubwa wa madeni ya mataifa mengine hulazimishwa kutumia kiasi kidogo zaidi cha fedha kwa ajili ya elimu. Kwa kielelezo, katika Afrika matumizi yote juu ya elimu yalipunguzwa kwa karibu asilimia 30 katika kipindi cha kwanza cha miaka ya 1980. Huku mataifa matajiri yakitumia zaidi ya dola 6,000 kwa mwaka kwa kila mmoja wa watoto wao wa shule, baadhi ya nchi maskini katika Afrika na Asia Kusini hutumia dola 2 tu kwa kila mtoto. Basi kunakuwa na shule chache zaidi na walimu wenye kufundisha watoto wengi zaidi.

Vita na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe huchangia pia kutojua kusoma na kuandika. Shirika la Hazina ya Watoto la Umoja wa Mataifa lakadiria kwamba watoto wapatao milioni saba wamo katika kambi za wakimbizi, ambamo vifaa vya masomo huwa havitoshi. Katika nchi moja pekee ya Afrika, watoto milioni 1.2 wenye umri wa chini ya miaka 15 hawajapata kwenda shule kwa sababu ya vita ya wenyewe kwa wenyewe inayowakumba.

Wale ambao hukosa fursa ya kujifunza kusoma na kuandika wakati wa utotoni nyakati nyingine huwa na fursa ya kufanya hivyo baadaye maishani, lakini si wote wanaoona kwamba yafaa kufanya hivyo. Kitabu Adult Education for Developing Countries chasema hivi kuhusu mkazi wa mashambani asiyejua kusoma na kuandika: “Mtu mzima ambaye amefanikiwa bila kujua kusoma na kuandika haelekei sana kuwa na tamaa ya kusoma na kuandika, ila tu kwa hali za kipekee. . . . Ingawa lingekuwa kosa kabisa kukata kauli kwamba yeye ameridhika kabisa na hali yake, huenda asijali sana kurekebisha hali yake.”

Lakini, wengi huwa na tamaa kubwa ya kufanya maendeleo. Bila shaka makusudi ya kutaka kufanya maendeleo hutofautiana. Wengine hutaka tu kufanyia elimu yao maendeleo na kujihisi kuwa watu wa maana. Wengine huchochewa na sababu za kifedha. Wale ambao hawana kazi hufikiri kwamba kujua kusoma na kuandika kutawasaidia kupata kazi; wale walio na kazi wanaweza kutafuta kazi nzuri zaidi.

Zikitambua uhusiano wa karibu uliopo kati ya kujua kusoma na kuandika na maendeleo ya mtu mmoja-mmoja na ile ya taifa zima, serikali na mashirika yameanzisha programu za kufundisha watu wazima wajue kusoma na kuandika. Hiyo ni kazi ngumu inayohitaji hisia-mwenzi kwa walimu na vilevile kuelewa tabia za kipekee za mtu mzima anayejifunza.

Mfano wa Mtu Mzima Anayejifunza

Wale wanaofundisha watu wazima wapaswa kutambua tofauti zilizopo kati ya watu wazima wanaojifunza na watoto wanaojifunza. Utu, tabia, mitazamo, na mapendezi zimekazwa kikiki kwa watu wazima kuliko katika watoto, jambo linalofanya watu wazima wawe wagumu sana na wasio wepesi sana kufanya mabadiliko. Kwa upande mwingine, watu wazima wana maono mengi ambayo wao waweza kutegemea na pia wanaweza kwa urahisi kuelewa mambo na mawazo yanayoweza kuvuruga akili za watoto. Mara nyingi wao hawana wasaa kama watoto. Tofauti nyingine kubwa ni kwamba watu wazima wanaojifunza wanaweza kukomesha elimu yao wakati wowote, jambo ambalo ni tofauti na watoto.

Watu wengi wazima ambao hawajui kusoma na kuandika wana vipawa vya kipekee na wamefaulu katika sehemu fulani za maisha; wao hawajasitawisha tu stadi zao za kusoma na kuandika. Mwalimu wa kufundisha watu wazima ahitaji kuwatia moyo watumie uwezo wao wa kubadilika na hali, ubuni wao, na uvumilivu wao ambao wametumia katika sehemu nyinginezo za maisha yao.

Moyo mkuu huhitajika kwa mtu asiyejua kusoma na kuandika kukiri upungufu wake na kuomba msaada. Ingawa hali na watu vilevile hutofautiana, watu wengi wazima huogopa mazoezi ya kujifunza kusoma na kuandika na wao hukosa uhakika. Baadhi yao huenda wana historia ndefu ya kutofanikiwa kimasomo. Wengine huenda wakahisi kwamba wao ni wazee mno wasiweze kujifunza mambo mapya. “Ni vigumu kujifunza kutumia mkono wa kushoto uzeeni,” yasema mithali moja ya Naijeria.

Walimu waweza kujenga uhakika na kuendeleza upendezi kwa kuwa wepesi kuona maendeleo na kutoa pongezi. Masomo yapaswa yafanyizwe kwa namna ya kupunguza hali ya kushindwa kujifunza na pia kwa namna ya kuhakikisha kwamba miradi ya kujifunza itatimizwa kwa mafanikio kila mara. Kichapo Educating the Adult chaeleza hivi: “Mafanikio ndiyo labda jambo kuu zaidi ya mengine yote ya kitia-moyo chenye kuendelea.”

Kwa kawaida watu wazima hujua jambo wanalotaka kutokana na maono yao ya kielimu na wanatamani kuona maendeleo ya mara hiyo kuelekea miradi hiyo. Profesa mmoja wa elimu ya watu wazima katika Afrika alisema hivi: “Wao wanataka waanze kujifunza, wajifunze jambo wanalohitaji kujua haraka iwezekanavyo na kumaliza masomo yao.”

Nyakati nyingine mwanafunzi huweka miradi mikubwa kupita kiasi. Tokea mwanzo mwalimu apaswa kusaidia mwanafunzi aweke miradi midogo ya kutimizwa upesi na kumsaidia mwanafunzi kuitimiza. Kwa kielelezo, tuseme kwamba Mkristo ajiandikisha katika darasa la kujifunza kusoma na kuandika kwa sababu anataka kujifunza kusoma Biblia na vichapo vya Biblia. Hiyo ni miradi ya muda mrefu. Katika kuitimiza, mwalimu anaweza kutia moyo mwanafunzi aweke miradi ya muda mfupi kama vile kujua vizuri herufi, kutafuta na kusoma maandiko yaliyoteuliwa, na kusoma kutokana na vichapo vya Biblia vilivyorahisishwa. Kutimiza miradi kwa kawaida huendeleza kichocheo na kufanya mwanafunzi aendelee kujifunza.

Walimu wenye matokeo wanaweza kufanya mambo mengi ili kuchochea tamaa kwa kuwatia moyo na kuwapongeza wanafunzi na kwa kuwasaidia kufanya maendeleo kuelekea miradi ifaayo na iwezayo kutimizwa. Lakini, ili watu wazima wafanye maendeleo, wao wasitazamie kufanyiwa kila kitu. Wanahitaji kuwa tayari kuchukua madaraka yao wenyewe na kutia bidii katika kujifunza. Katika kufanya hivyo, watajifunza kusoma na kuandika, na stadi hizo zitabadili maisha zao.

[Sanduku katika ukurasa wa 6]

Miongozo ya Kufundisha Watu Wazima Kujua Kusoma na Kuandika

1. Ni muhimu kuchochea tamaa ya mwanafunzi. Kutokea masomo ya kwanza, kazia mafaa ya kujifunza kusoma na kuandika, na kutia moyo mwanafunzi aweke miradi ifaayo ya kutimizwa baada ya muda mrefu na ya kutimizwa baada ya muda mfupi.

2. Ili kufanya maendeleo mwanafunzi apaswa kufundishwa mara kadhaa katika juma. Haitoshi kumfundisha mara moja kwa juma. Mwanafunzi apaswa kufanya mazoezi ya kusoma kati ya vipindi vya masomo.

3. Usiwe mwenye kudai mno au kumpa mwanafunzi mambo mengi mno katika kipindi kimoja cha masomo. Jambo hilo laweza kumvunja moyo na kumfanya akome kuhudhuria masomo.

4. Uwe mwenye kutia moyo nyakati zote na mwenye kutazamia mambo yafaayo. Stadi za kusoma na kuandika hukuzwa polepole na hatua kwa hatua. Mwanafunzi apaswa aridhike na maendeleo yake.

5. Tia moyo mwanafunzi atumie maishani mwake mambo anayojifunza haraka iwezekanavyo.

6. Usipoteze wakati kwa mambo ya ziada. Watu wazima wana shughuli nyingi. Tumia vipindi vya masomo kwa njia bora zaidi kwa kufundisha mambo ya maana tu.

7. Mheshimu mwanafunzi nyakati zote, ukimpa staha astahiliyo. Usimwaibishe wala kumshushia heshima.

8. Uwe chonjo kuona matatizo ya mtu mmoja-mmoja. Huenda mwanafunzi asiweze kusoma maandishi madogo kwa sababu anahitaji miwani. Huenda mwingine asiweze kusikia vizuri na hivyo huenda akapata ugumu wa kusikia matamshi sahihi.

9. Mwanafunzi apaswa ajifunze kuandika herufi moja-moja (zilizochapwa) kabla ya kujaribu kuziandika zikiwa zimeshikana. Ni rahisi zaidi kujifunza na kuandika herufi, na herufi hizo hufanana sana na zile zilizochapishwa.

10. Njia nzuri ya kufundisha namna ya kuandika herufi ni kumfanya mwanafunzi azifuatishe herufi hizo kwa kuzinakili mahali zilipoandikwa. Aweza kunakili juu ya herufi fulani mara kadhaa kabla ya kujaribu kuiandika kando bila kunakili juu yayo.

11. Mara nyingi maendeleo hufanywa haraka zaidi katika kusoma kuliko katika kuandika. Usikawize masomo mapya ya kujifunza kusoma ikiwa mwanafunzi hawezi kuandika. Kwa upande mwingine, kumbuka kwamba mwanafunzi hujifunza na kukumbuka kwa urahisi zaidi herufi mpya wakifanya mazoezi ya kuziandika.

12. Ingawa mtu mzima aliye mwanafunzi huenda akaweza kufanya kazi za kustaajabisha kwa mikono yake, kuandika kwa kalamu au penseli kwaweza kuwa jambo gumu sana na lenye kumfadhaisha sana. Usisisitize kwamba ni lazima herufi ziandikwe kikamili.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki