Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g94 3/8 kur. 15-17
  • Ile Sherehe Isiyo na Kifani ya Mnazareti Mweusi

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Ile Sherehe Isiyo na Kifani ya Mnazareti Mweusi
  • Amkeni!—1994
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Lile Andamano Kubwa Sana
  • Ni Nini Husisimua Umati Sana Hivyo?
  • Chanzo cha Msherehekeo Huo
  • Je! Yaweza Kuonwa Kuwa Ni Ibada ya Sanamu?
  • Je! Ile Sanamu Yaweza Kusaidia Wanaojitoa Sana Kuiabudu?
  • Maoni ya Kikristo Juu ya Mifano
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1988
Amkeni!—1994
g94 3/8 kur. 15-17

Ile Sherehe Isiyo na Kifani ya Mnazareti Mweusi

NA MLETA-HABARI ZA AMKENI! KATIKA UFILIPINO

SI MARA nyingi uonapo umati mkubwa kama huu. Lakini hapa Manila, tamasha hii yaweza kuonwa kila Januari 9. Mamia ya Wakatoliki wenye kujitoa sana wamesongamana katika Eneo Wazi la Miranda kwenye Kanisa la Quiapo, wakingojea Mnazareti Mweusi itokee.[1][2][3]

Eti ‘Mnazareti Mweusi?’ wewe wauliza. Ndiyo, sanamu hiyo yenye ukubwa wa mtu mzima ambayo humwakilisha Yesu Kristo akiwa amebeba msalaba ndiyo hasa hukaziwa fikira na andamano kubwa lisilo na kifani ambalo kulingana na kitabu Filipino Heritage “hakuna ubishi kwamba ndio udhihirisho mkubwa zaidi sana, wa kutazamisha zaidi sana . . . wa dini ipendwayo na wengi katika lile Taifa Moja tu la Kikristo lililo katika Asia,” yaani, Ufilipino.[4]

Lile Andamano Kubwa Sana

Malango ya kanisa yafungukapo, umati wachafuka kwa kufanya vigelegele na kulipua-lipua vibaruti. Kamba ndefu mbili zakunjuliwa ziufikie umati ili wavute kile kibebeo chenye kukokota Mnazareti Mweusi. Wafuasi wenye kujitoa wanyoosha mikono kung’ang’ania kuzishika kamba. Ni heshima kubwa kwao kufanya hivyo. Wengine washikana kwa mikono iliyonyooshwa wakijaribu kufanyiza mwanya wa kupitiwa na lile andamano. Wanaume wote ni miguu mitupu, kila mmoja akiwa amevaa T-shati na akiwa na taulo kichwani au shingoni pake.

Akiwa kwenye jukwaa lililosimamishwa karibu na lile kanisa, sasa tu mtangazaji ametoka kueleza kanuni fulani za kufuatwa na umati unaongoja. Jambo moja hususa limetajwa wazi: Katika lile andamano kuu, wanawake hawaruhusiwi. Sababu yaonekana wazi wakati Mnazareti Mweusi ivutwapo polepole kuingizwa katika lile eneo wazi; hekaheka zaanza.

Ule umati wa waabudu wenye msisimuko wanyoosha mikono, wakisukumana na kukumbana, hata kupandana juu kwa jitihada ya kufa na kupona ili kugusa Mnazareti Mweusi. Wanaume wachache wanaoendeshwa wakiwa juu ya kile kibebeo cha kukokota walazimika kusukuma chini baadhi ya wanaume hao wakijaribu kuilinda sanamu kutokana na ule umati wenye msisimuko. Wengi mno wakiruhusiwa kulipanda jukwaa kwa safari moja huenda likaanguka. Japo tahadhari hizo, nyakati nyingine kile kibebeo cha kukokota huanguka, na huchukua dakika 30 hadi muda wa saa moja kukiinua tena kwa sababu watu wengi sana hujaribu kuigusa sanamu.[5]

Watazamaji hujipanga mistari kwenye zile barabara nyembamba za Quiapo kushuhudia wakati Mnazareti Mweusi ipitapo polepole katika wilaya hiyo. Mishumaa hushikiliwa juu kuonyesha ujitoaji wao kwa ile sanamu. Wengine huleta sanamu zilizo ndogo zaidi kutoka nyumbani. Lile andamano huwa na mabango makubwa yenye maandishi ya kutambulisha vikundi mbalimbali vya wajitoaji wa Mnazareti Mweusi.

Wengine katika umati hutupa taulo na vitambaa vya mfukoni kwa mmoja wa wanaume wanaobebwa juu ya lile jukwaa pamoja na Mnazareti Mweusi. Halafu yeye hupangusa vitu hivyo juu ya ile sanamu au msalaba wayo na kuvitupa awarudishie. Halafu mwamini mwenye msisimuko hujipangusa uso kwa taulo yake. Lile andamano hufuatwa na mstari mrefu wa sanamu, nyingi zazo zikiwa ni namna ndogo zaidi za Mnazareti Mweusi. Hapo sasa ndipo mahali salama kwa wanawake kujiunga.

Kwa sasa, ndani ya kanisa, waamini, hasa wanawake, huomba Mnazareti Mweusi kwa bidii iwasaidie kwa njia nyingine. Wakiisha kuingia mlangoni, wao hujiunga na ule mstari mrefu wa wengine wanaotambaa polepole kwa magoti yao kuteremkia kijia cha kanisa hadi altare.

Ni Nini Husisimua Umati Sana Hivyo?

Sanamu ya Mnazareti Mweusi husemwa kuwa ndiyo chanzo cha miujiza mingi sana. Alberto mwenye umri wa miaka 12 alisema alienda na babu na nyanya yake kwenye sherehe hiyo kwa sababu sikuzote Mnazareti Mweusi ilimpa chochote alichoomba kupitia sala.[1] Mauricio asema alijiunga na lile andamano akitumaini kupata msamaha wa dhambi na pia kitulizo kutokana na matatizo na mikazo ya maisha ya kila siku.[5]

Mara ya kwanza ambayo Mauricio alijiunga na msherehekeo huo, alikuwa na umri wa miaka 24. Kila mwaka aliweza kuzishika kamba zivutazo sanamu. Kufikia mara yake ya tano, alikuwa na tamaa yenye nguvu kupanda hasa juu ya kile kibebeo cha kukokota. Wengine wa marafiki zake walimsaidia kupanda juu, na huko akaweza kupangusa taulo yake juu ya nyayo za Mnazareti Mweusi; halafu akajitupa chini haraka kwenye umati.[5] Kufanya hivyo huwa ndio upeo, jambo la mwisho la pekee ambalo watu walio wengi waweza kutumainia kulipata.

Chanzo cha Msherehekeo Huo

Mnazareti Mweusi husemwa kuwa ilichongwa hapo kwanza na Mhindi Mmeksiko (wengine hudai ni kazi ya mchongaji Mfilipino au Mchina) na kuletwa Manila na merikebu ya kibiashara katika karne ya 17. Wenye kuisanii waliifanya ikawa isiyo na kifani ama kwa kuichonga kutokana na mbao nyeusi ama kupaka sanamu hiyo rangi ya kahawia nyeusi, ifananayo na rangi ya Wameksiko na Wafilipino. [6][7][8][12] Katika karne ya 18, Mnazareti Mweusi ilihifadhiwa kama kitu kitakatifu katika Quiapo kwa ombi la Basilio Sancho, askofu mkuu wa Manila, aliyeipa baraka yake.[7][8] Halafu, katika sehemu ya mapema ya karne ya 19, ikapokea baraka kutoka kwa Papa Pius 7.[8]

Hata hivyo, 1923 ndipo ilipotolewa nje kwa mara ya kwanza iwe sehemu ya andamano la kidini ambalo huwa upeo wa starehe za shangwe za wilaya ya Quiapo.[8] Maandamano yameendelea muda wote tangu hapo.

Je! Yaweza Kuonwa Kuwa Ni Ibada ya Sanamu?

Kwa kawaida, Mnazareti Mweusi yaweza kuonwa ikiwa mahali payo katika dirisha moja karibu na mwingilio wa kanisa. Dirisha hilo lipo katikati hasa ya vibao viwili vyenye orodha ya zile Sampung Utos, au Amri Kumi. Kwa Wakristo fulani, huenda hilo likaonekana kuwa kinyume cha kushangaza, kwa kuwa ya pili ya hizo Amri Kumi husema: “Usijifanyie sanamu ya kuchonga, wala mfano wa kitu cho chote kilicho juu mbinguni, wala kilicho chini duniani . . . Usivisujudie wala kuvitumikia.” (Kutoka 20:4, 5) Je! Mnazareti Mweusi si sanamu ya kuchonga ambayo Wakatoliki wenye kujitoa wanaitumikia?

Wakatoliki walio wengi hawangeiona hivyo. Kichapo New Catholic Encyclopedia husema: “Kwa kuwa ibada ipewayo sanamu humfikia na kwenda mwishowe kwa mtu anayewakilishwa, namna hiyohiyo ya ibada ambayo mtu huyo aistahili yaweza kupewa kwa sanamu iwakilishayo mtu huyo.” [9] Hilo ndilo Wakatoliki wengi Wafilipino wamesema—kwamba wao huabudu, si ile sanamu, bali Yesu Kristo, ambaye sanamu hiyo yadhaniwa humwakilisha yeye. Acheni tuchunguze kidogo njia hiyo ya kuwaza.

Kwa kweli, ibada hiyo ya kadiri si ya Wakatoliki peke yao. Dini za kipagani zimekuwa zikiwaza hivyohivyo kwa karne nyingi. Kwa mfano, kulingana na Lactantius, Baba wa Kanisa la karne ya nne, wapagani hao walikuwa wakisema hivi: “Sisi hatuziogopi sanamu zenyewe, bali huogopa wenye uhai wale ambao sanamu hizo zilifanyizwa kwa mfano wao, na ambao sanamu hizo zimewekwa wakfu kwa majina yao.”[10]

Basi je! hiyo yamaanisha kwamba amri za Mungu kuhusu kuabudu sanamu hazikuwahusu wao? Je! kweli njia hiyo ya kuwaza yaweza kuwa timamu na hali yajaribu kutangua Neno la Mungu? Ingawaje, ikiwa walio wengi wa waabudu-sanamu huwaza kwa njia hiyo, basi zile amri zilikusudiwa zihusu nani?

Kumbuka kwamba Mungu alipokuwa akimpa Musa zile Amri Kumi, Waisraeli walikuwa wamesimamisha ndama ya dhahabu wakawa wakimwinamia. Huenda ikawa watu hao hawakuliona jambo walilokuwa wakifanya kuwa ibada ya sanamu hata kidogo. Katika akili zao, hiyo ndama ilimwakilisha Yehova. (Kutoka 32:4, 5) Lakini je! Mungu alipendezwa na walilokuwa wakifanya? Twasoma kwamba sasa Yehova alimwambia Musa: “Haya! shuka; kwa maana watu wako uliowatoa katika nchi ya Misri wamejiharibu nafsi zao, wamepotoka upesi kuiacha ile njia niliyowaamuru, wamejifanyizia ndama ya kuyeyusha, wakaiabudu na kuitolea dhabihu.”—Kutoka 32:7, 8.

Swali jingine ambalo lastahili kuangaliwa ni kama ni jambo la akili kuheshimu sanamu. Daima Biblia imetoboa mambo juu ya habari hiyo. Husema hivi: “Watu wa jinsi hiyo ni wapumbavu mno wasiweze kujua wanalofanya. Wao hufunga macho yao na akili zao wasiione kweli. Mwenye kuzifanya sanamu hana werevu wala akili ya kusema, ‘. . . Mimi hapa ninainamia pande la mti!’”—Isaya 44:18, 19, Today’s English Version.

Je! Ile Sanamu Yaweza Kusaidia Wanaojitoa Sana Kuiabudu?

Padri mmoja Mkatoliki aliandika hivi: “Watu ambao hutia tumaini lao hakika kwamba kuna nguvu inayoambatana na Mnazareti Mweusi ya Quiapo hawana sababu nzuri kwa tumaini lao bali ni kama tu wale wategemeao kulindwa na hirizi ya kiatu cha farasi au mguu wa sungura.”[11]

Kwa upande mwingine, Biblia husema hivi juu ya sanamu hizo: “Mtu yeyote akisali kwayo, haiwezi kumjibu wala kumwokoa na msiba.” Yehova Mungu atuambia wazi kwamba “hizo haziwezi kuwafaidi chochote.” (Isaya 46:7; Yeremia 10:5; TEV)

Hakuna shaka kwamba Wakatoliki wajitoaji ambao hupandana juu kwa matumaini ya kugusa Mnazareti Mweusi “wana juhudi kwa ajili ya Mungu,” lakini si “katika maarifa [ujuzi sahihi, NW].” (Warumi 10:2) Sisi twawatia moyo watu wote wa jinsi hiyo wapate ujuzi sahihi kwa kuchunguza Neno la Mungu, Biblia, hivyo waifuate “dini iliyo safi, isiyo na taka mbele za Mungu Baba.”—Yakobo 1:27.

[Picha katika ukurasa wa 16]

Watu humiminika ili taulo na vitambaa vya mfukoni vikapanguse ile sanamu

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki