Nafuu ya Uchumi wa Meksiko—Ina Mafanikio Kadiri Gani?
NA MLETA-HABARI ZA AMKENI! KATIKA MEKSIKO
ULIMWENGUNI pote, mataifa mengi yanang’ang’ana na infleshoni iliyoongezeka, kupungua kwa thamani ya fedha, ukosefu wa uthabiti, na wasiwasi wa wananchi. Baada ya mabadiliko ambayo yametukia Urusi miaka miwili iliyopita, matatizo ya kiuchumi katika nchi hiyo yaonekana yamekuwa mabaya zaidi. United States, ingawa huonwa kuwa ndilo taifa tajiri zaidi ulimwenguni, inajaribu kujikokota kutoka katika mpunguo wa hali ya uchumi. Sasa vuvumko la usitawi wa Japani limepunguza mwendo, na Wajapani ni waangalifu zaidi jinsi watumiavyo fedha zao. Kwa habari ya Amerika ya Kilatini, matatizo ya kiuchumi ni kawaida ya maisha.
Kwa kuwa ndivyo mambo yalivyo, huenda ikashangaza kusoma matangazo fulani rasmi juu ya nafuu ya uchumi wa Meksiko. Rais wa Meksiko Carlos Salinas de Gortari alitaarifu hivi: “Tumepunguza infleshoni kwa karibu asilimia 200 katika 1987 ikawa ya kiwango ambacho tayari kimefika asilimia 10 na chaendelea kushuka.” Katika hotuba yake kwa Shirika la Sera ya Kigeni katika New York, aliendelea kusema: “Tangu 1989, Wameksiko milioni kumi na tatu wameweza kuwa na nguvu za umeme, milioni kumi na moja wakawa na maji ya kunywa, na milioni nane na nusu wakawa na mfumo wa kuondoa maji machafu.”[1]
Kwa hiyo huenda maswali fulani yakatokea. Nafuu hii yahusisha nini ndani? Je! watu wa Meksiko wanaboresha kiwango chao cha maisha?
Ile Miaka ya Shida
Kabla ya miaka ya ’70, Meksiko ilionwa kuwa thabiti kiuchumi. Kwa kuwa peso yao ilikuwa na ulinganifu wa 12.50 kwa dola moja, kwa msingi uchumi ulikuwa imara, na deni la nje lilikuwa ni kama limedhibitiwa. Lakini katika miaka ya ’80, ilipoonekana kwamba kulipasa kuwako vuvumko la usitawi kwa sababu ya mafuta zaidi kupatikana Meksiko, ajabu ni kwamba shida ilisitawi, na katika 1987, Meksiko ikafikia kiasi cha juu zaidi cha infleshoni.[3]
Wakati huo ilikuwa vigumu sana kuutimiza uhitaji mkubwa wa fedha, na serikali iliendelea kuchapa fedha ambazo zilipoteza thamani kila siku. Fedha nyingi zilianza kutiririka zikipelekwa nje ya nchi hiyo ili kuwekwa salama zaidi katika benki za ng’ambo. Kushushwa kwa thamani ya peso kulilingana na kiasi cha infleshoni. Katika 1992, wakati kiwango cha ubadilishanaji-fedha kilipokuwa peso 3,110 kwa dola moja, mshusho wa thamani ya fedha ulikuwa umepita asilimia 24,000 tangu miaka ya ’70, wakati ambapo kiwango kilikuwa peso 12.50.[4]
Katika vipindi viwili vilivyotangulia vya miaka sita-sita, sehemu kubwa ya hatua iliyochukuliwa na serikali ya kutatua matatizo yaliyotajwa juu ilionekana ikijipinga na kubomoa uchumi wa Meksiko. Hali ya kutoaminiana, ndani ya nchi hiyo na pia katika nchi za kigeni, ilianza kuenea, na ikawa zaidi hivyo wakati Meksiko ilipoeleza katika 1982 kwamba haikuweza hata kulipa faida iliyotozwa juu ya deni layo la nje.[5]
Mabadiliko Makubwa Sana Katika Uchumi wa Meksiko
Mabadiliko yametukia wakati wa urais wa Carlos Salinas de Gortari, aliyeshika hatamu Desemba 1, 1988. Rais Salinas, aliye mstadi wa mambo ya uchumi na mhitimu wa Chuo Kikuu cha Harvard, akiwa amezungukwa na kikundi cha wastadi wa mambo ya fedha, alikabiliana na jukumu la kuunda upya uchumi wa Meksiko. Kulikuwa na machaguo mawili: uchumi wa mchanganyiko au uchumi wa kisoko. Uchumi wa mchanganyiko ni ule ambamo Serikali hudhibiti kwa sehemu kubwa zaidi viwanda na huduma mbalimbali, huku ikitoa fursa za biashara za watu binafsi. Uchumi wa kisoko ni ule ambamo nchi hupewa uhuru kamili, na viwanda na mashirika ya watu binafsi huruhusiwa kuendesha shughuli bila kuingiliwa sana na Serikali. Serikali ya Salinas ilichagua uchumi wa mchanganyiko, ikibadili utaratibu uliokuwa umefuatwa miaka iliyotangulia. Serikali ya hapo kwanza ilikuwa imejiwekelea biashara nyingi na mashirika ya huduma ambayo, badala ya kutokeza mazao, yalihitaji misaada ya Serikali ili yaendelee kuwapo.[6] Sasa kampuni za watu binafsi zilipewa fursa nyingi zaidi, na kwa hiyo biashara fulani za Serikali zikaanza kuuzwa—karibu 400 kufikia sasa—na hiyo ikafanya kuwe na mtiririko wa mapato ya fedha na kupunguza mzigo wenye kulemea fedha za serikali.[7]
Biashara zilipouzwa kwa watu binafsi na kukawako mwongozo wa sheria kali za kudhibiti gharama za umma, imewezekana Meksiko kupata tena fedha za kulipia deni la nje, ambalo katika 1993 lilijumlika kuwa dola zaidi ya bilioni 103. Hapo basi nchi fulani-fulani zina uhakika mwingi zaidi kwamba Meksiko ni nchi ambayo wao waweza kuweka ndani rasilmali zao.
Patano la Biashara Huru la Amerika ya Kaskazini (NAFTA)
Tangu 1990 patano la biashara huru limefanywa likihusisha Kanada, United States, na Meksiko. Katika 1993 mjadala juu ya kibali cha mwisho juu ya mwafaka huo uliendelea, hasa katika United States. Ilikuwa lazima kibali rasmi kikamilishwe kufikia mwisho wa 1993 ili patano hilo liweze kutekelezwa Januari 1, 1994. Ingawa patano hilo lilifanywa wakati wa usimamizi wa rais wa U.S. George Bush, wakati wa urais wa sasa wa Clinton kumekuwa na wapinzani wengi wasiotaka mkataba huo katika United States na katika Kanada. Mbona ubishi?
Kuna maoni tofauti juu ya matokeo yanayoweza kuletwa na NAFTA. Ni wazi Meksiko ina maoni ya kutaka matokeo mazuri. Jaime José Serra Puche, Katibu wa Biashara na Uendelezaji wa Viwanda Meksiko, alitaarifu hivi kwa kikundi cha wanabiashara Waamerika katika Detroit: “NAFTA inafaa na ina matokeo mazuri. Yaani, NAFTA itatusaidia tufanyize nafasi nyingi zaidi za kazi, itatusaidia tuwe hodari zaidi kukabiliana na wengine, na NAFTA itatusaidia kuboresha mazingira pia.” Dai hilo la mwisho latiliwa shaka na Waamerika wengi—wao wadai kwamba mazingira yamekuwa hayashughulikiwi sana na biashara za Wameksiko katika mpaka wa U.S. Pia yaripotiwa kwamba vyama vya wafanyakazi vya U.S. vyahofu kwamba NAFTA itasababisha hasara ya kukosa kazi kwa wafanyakazi Waamerika. Rais Salinas ajibu hivi: “Meksiko ndilo soko linalopanuka haraka zaidi kwa kupokea mauzo ya U.S.” Alisema kwamba Meksiko ndiyo “mnunuzi wa tatu mkubwa zaidi wa bidhaa za U.S., wenye kumzidi wakiwa ni Kanada na Japani tu.”[10]
Zaidi ya kufungulia United States na Kanada milango ya kufanya biashara pamoja, Meksiko inafungulia nchi nyinginezo pia. Japani imeonyesha inapendezwa na kuweka rasilmali katika Meksiko. Kwa kweli, moja ya shughuli za kibiashara (Teléfonos de México) iliyoruhusiwa kuendeshwa na watu binafsi ilimilikiwa kwa kutumia rasilmali ya Kijapani hasa.
Nuevo Peso (Peso Mpya) ya Meksiko
Moja ya mbinu za serikali za kudhibiti fedha vizuri zaidi ni kurekebisha fedha za Meksiko. Peso iliposhushwa thamani kwa kulinganishwa na kiwango cha dola ya U.S., peso nyingi zilihitajika kabisa kwa shughuli za kibiashara. Kufikia 1992, peso 3,150 ndizo zilizohitajiwa kujumlika kuwa dola moja, kumaanisha kwamba thamani ya dola 1,000 ilihitaji peso 3,150,000. Basi waweza kuwazia kiasi kikubwa zaidi cha fedha, kama dola milioni moja au milioni 100 kingekuwaje? Kingehitaji kuwa cha tarakimu nyingi mno hata kisifae shughuli za kibiashara. Kwa hiyo, katika 1993, iliamuliwa kuondoa sifuri tatu katika peso. Sasa kipimo kimekuwa ni peso 3.20 kwa dola moja, na utumizi wa senti ndogondogo umewezekana tena katika uchumi wa kinyumbani.
Uchumi Mpya —Matokeo ya Kinyume Nchini
Kwa miaka kadhaa sasa, kumekuwa na kubaliano katika Meksiko miongoni mwa wafanyakazi, viwanda, na mabenki kujaribu kudhibiti bei za vitu. Vyama vya wafanyakazi vimekubaliana pia kutodai kuongezwa mishahara. Hiyo imekuwa njia ya kudhibiti infleshoni. Hata hivyo, udhibiti huo umekuwa na matokeo kadiri gani? Watu fulani wafikiri kwamba ingawa ongezeko la mishahara limedhibitiwa, bei zimeongezeka. Hata ingawa infleshoni ilizuiwa isizidi asilimia 10 katika 1993, kulingana na tarakimu zilizo rasmi, watu wa kawaida, kutia na wake wakaa-nyumbani, walihisi kwamba kila siku wangeweza kununua vitu vichache zaidi kwa kiasi kilekile cha fedha. Gazeti Economist la London lilitoa muhtasari wa hali iliyopo, likisema: “Ile sherehe ya mafanikio imegeuka kuwa starehe ya kupunguza mwendo.”[10a]
Hiyo yaongoza kwenye swali hili: Je! ile nafuu ya kiuchumi imechangia nafuu ya kweli katika jamii ya watu wa Meksiko? Kwa kusikitisha, umaskini waendelea kwa fujo. Yasemwa kwamba mshahara wa chini zaidi kwa wafanyakazi, ambao huwa shida kuzidi dola 150 kwa mwezi, hufanya isiwezekane kwao kuepuka umaskini mahali pengi. Katika mikoa fulani ya Meksiko, mshahara wa chini ni mdogo hata zaidi. Mfanyakazi wa kawaida au mwashi wa kuunganisha mawe tu huenda akachuma kiasi kinacholingana na dola 200 au dola 300 kwa mwezi, jambo ambalo lafanya iwe vigumu sana kwake kuruzuku familia. Kulingana na uchunguzi mmoja wa hivi majuzi, “kati ya asilimia 91.9 ya idadi ya watu wa Meksiko wanaoishi katika umaskini, kama asilimia 30.1 wamo katika umaskini wa kupindukia.”—El Universal, Machi 31, 1993.[11]
Katika hali hiyo, Mashahidi wa Yehova zaidi ya 380,000 wanahubiri ujumbe wenye matumaini mazuri kwa Wameksiko milioni 85—kwamba karibuni umaskini na ukosefu wa haki vitaondolewa mbali ulimwenguni pote chini ya utawala wa Ufalme wa Mungu mikononi mwa Kristo Yesu aliyefufuliwa. Biblia huahidi hivi: “Maana, tazama, mimi naumba mbingu mpya na nchi mpya, na mambo ya kwanza hayatakumbukwa, wala hayataingia moyoni.” “Nao watajenga nyumba, na kukaa ndani yake; watapanda mizabibu, na kula matunda yake. Hawatajenga, akakaa mtu mwingine ndani yake; hawatapanda, akala mtu mwingine; maana kama siku za mti ndivyo zitakavyokuwa siku za watu wangu, na wateule wangu wataifurahia kazi ya mikono yao muda wa siku nyingi.” (Isaya 65:17, 21-24) Wakati huo umaskini utakoma, mahali popote ambako huenda ulikuwako.
[Blabu katika ukurasa wa 20]
“Meksiko ndilo soko linalopanuka haraka zaidi kwa kupokea mauzo ya U.S.” —Rais Salinas