Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g94 7/22 kur. 12-14
  • Mexico Yabadili Sheria Zayo Juu ya Dini

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Mexico Yabadili Sheria Zayo Juu ya Dini
  • Amkeni!—1994
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Ile Sheria Mpya
  • Mashahidi wa Yehova Wasajiliwa Kihalali
  • Je, Uhuru Zaidi wa Dhamiri Utaruhusiwa Mexico?
    Amkeni!—2000
  • Uhuru wa Kidini Wamaanisha Nini Kwako?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1997
  • Kutumikia kwa Moyo Wote Licha ya Majaribu
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2001
  • Nafuu ya Uchumi wa Meksiko—Ina Mafanikio Kadiri Gani?
    Amkeni!—1994
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1994
g94 7/22 kur. 12-14

Mexico Yabadili Sheria Zayo Juu ya Dini

MNAMO JULAI 16, 1992, SHERIA MPYA YA MASHIRIKA YA KIDINI NA IBADA YA UMMA ILIANZISHWA NCHINI MEXICO. KWA NINI ILIHITAJIWA, NA SHERIA HIYO MPYA YAMAANISHA NINI? NA TUCHUNGUZE JAMBO HILO AMBALO LIMEAMSHA MATARAJIO MENGI.

BAADA ya ushindi wa Hispania dhidi ya ile ambayo sasa ni Mexico, watu walilazimishwa kuwa katika dini ya Katoliki. Wakati ulipowadia kutunga sheria juu ya mambo ya kidini, sheria ya Hispania iitwayo Constitución de Cádiz (1812), ilitumiwa kwa sehemu; Kifungu 12 kilisema: “Dini ya Taifa la Hispania ni, na daima itakuwa Katoliki, Apostoliki, Roma, dini moja tu ya kweli iliyo ya pekee.” Baadaye, mwaka 1824, Katiba ya Mexico ilianzishwa, nayo ilisema: “Dini ya Taifa la Mexico ni, na daima itakuwa Katoliki, Apostoliki, Roma. Taifa huilinda kwa sheria za hekima na za haki, na kupinga kuwako kwa dini nyingine.” Ingawa kulikuwa na marekebisho kadhaa ya sheria hiyo ya nchi, wazo ilo hilo lilitolewa hata baadaye mwaka 1843, sheria hiyo ikiipa dini ya Katoliki mahali pa kwanza na kwa kweli ikikosa kuhusisha dini nyingine yoyote.[1]

Ilikuwa katika 1857 kwamba Benito Juárez, mwanasiasa wa Mexico alipoanza kurekebisha sheria za nchi hiyo akianzisha zile zilizoitwa Sheria za Mapinduzi Makubwa ya Kidini. Hiyo ilikuwa kwa kusudi la “kutaifisha mali za kanisa” na “kuzidisha uwezo wa kisiasa na wa kiuchumi wa Taifa hilo na kupunguza ule wa Kanisa [Katoliki].” (Historia de México, Buku 10, ukurasa 2182).[2] Katika fungu hilo la sheria la 1859, ile Sheria ya Utaifishaji wa Mali za Dini ilianzishwa, kutia na sheria iliyotaka kwamba ndoa zifungishwe na Taifa ili ziwe halali. Katika 1860 ile Sheria ya Uhuru wa Dini ilianzishwa.[3]

Sheria za mapinduzi makubwa ya kidini zilitolea watu kadiri fulani ya uhuru wa kidini, zikisema kwamba dini ya Katoliki haingekuwa tena ya pekee katika nchi hiyo. Hata hivyo, uhuru huo mpya ulikuwa na mipaka na masharti. Sheria zilikiri kwamba dini zilikuwako Mexico lakini hazikupewa utambuzi au haki zozote za kisheria. Sheria za mapinduzi makubwa ya kidini zilikusudiwa hasa kuwekea mipaka dini ya Katoliki lakini kwa njia hiyo zikatilia mipaka dini zote nchini. Hata hivyo, dini nyingine isipokuwa Katoliki zingeweza kuendeshwa kwa uhuru zaidi, na dini za Protestanti kutoka Marekani zilianza kampeni ya kueneza evanjeli nchini.

Katika roho ileile ya kuzuia dini, sheria za mapinduzi makubwa ya kidini ziliimarishwa tena katika 1917, jambo lililotokeza mnyanyaso wa makasisi na Wakatoliki. Hilo lilitokeza vita ya Cristeros katika 1926, vita ya Katoliki dhidi ya serikali iliyokuwa jaribio la kufuta zile sheria zuifu zilizosimamia dini. Vita hiyo ilikwisha katika 1929 kukiwa na makubaliano juu ya uvumilio kutoka kwa serikali, lakini sheria hizo ziliendelea bila kurekebishwa.[4]

Katika ufafanuzi juu ya sheria hizo, kitabu Una Ley Para la Libertad Religiosa (Sheria ya Uhuru wa Dini) chataja: “Twang’amua kwamba hapo awali Kifungu cha Katiba 24 katika fungu lalo la pili, na vifungu vile vingine vya katiba vilivyorekebishwa, vilikuwa ni uvunjaji wa uhuru wa kidini kwa njia ya waziwazi, kwani zilizuia mtu mmoja-mmoja asidhihirishe dini yake na hivyo kufanya udhihirisho huo uongozwe na mamlaka.

“Isitoshe, usimamizi huo wa kikatiba ulipingana waziwazi na yale yaliyoidhinishwa katika Julisho la Ulimwenguni Pote la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa (Kifungu 19) na katika Mkataba wa Marekani wa Haki za Kibinadamu (Kifungu 12), kanuni za kimataifa ambazo Taifa la Mexico lilikuwa limekubali.”[5]

Katika 1988, wakati rais mpya wa Mexico aliposhika hatamu yake ya miaka sita, viongozi wa Katoliki walialikwa kwenye sherehe ya kutawazwa kwake rasmi kuwa rais. Katika ujumbe wake, Rais Carlos Salinas de Gortari alitangaza uhitaji wa kufanya uhusiano kati ya Dini na Taifa uwe mzuri zaidi. Mfikio huo mpya uliongoza kwenye mkataa kwamba ilikuwa lazima kurekebisha sheria zilizohusu dini. Zaidi ya hiyo, nchi hiyo ilikuwa ikisitawi kuwa jamii ya kidemokrasi zaidi, na mipango ilianzishwa kwa ajili ya makubaliano ya biashara huru pamoja na Marekani na Kanada. Kwa hiyo ilikuwa jambo la muhimu kurekebisha sheria hiyo ili kuifanya ipatane na uhuru wa dini.

Ile Sheria Mpya

Ile sheria mpya, kama inavyosemwa katika kifungu chayo cha kwanza, “ina msingi wa ile kanuni ya kihistoria ya kutengana kwa Dini na Taifa, pamoja na uhuru wa itikadi za kidini . . . ”[6] Kifungu cha pili chahakikisha uhuru wa mtu mmoja-mmoja “kuwa na au kutumia itikadi za kidini ambazo yeye apendelea na adhihirishe, wakiwa kikundi au akiwa binafsi, vitendo vya ibada au njia ya kuabudu anayopendelea . . . kutotangaza itikadi za kidini . . . mtu asionewe, asilazimishwe, au kuonyeshwa uhasama kwa sababu ya itikadi zake za kidini . . . , kushirikiana na kukutana pamoja kwa amani kwa ajili ya makusudi ya kidini.”[7] Kupitia sheria hii, “makanisa na vikundi vya kidini vitakuwa halali vikiwa mashirika ya kidini mara tu yanapopata usajili unaotakwa katika Wizara ya Serikali.”[8] Pia, “mashirika ya kidini yanayofanyizwa chini ya sheria ya sasa yaweza kuwa na mali yao yenyewe inayoyaruhusu kutimiza makusudi yayo.”[9]

Mashahidi wa Yehova Wasajiliwa Kihalali

Kulingana na sheria hiyo mpya, Mashahidi wa Yehova katika Mexico walitoa ombi kwenye Ofisi ya Mambo ya Dini mnamo Aprili 13, 1993, ili wasajiliwe kuwa dini. Kabla ya wakati huo, Mashahidi wa Yehova, kama vile dini nyingine katika nchi hiyo, walikuwa wakitenda lakini bila kutambuliwa kisheria. Mashahidi wa Yehova walikuwa wamekuwa katika nchi hiyo tangu mapema katika karne ya 20. Ingawa hawakutambuliwa kisheria, mnamo Juni 2, 1930, serikali ya Mexico iliidhinisha International Association of Bible Students. Mnamo Desemba 20, 1932, jina hilo lilibadilishwa kuwa La Torre del Vigía (Mnara wa Mlinzi). Lakini katika 1943, kwa sababu ya sheria zilizozuia utendaji wa kidini nchini humo, shirika jipya la ziada lilisajiliwa likiwa shirika la umma. Kwa njia hiyo Yehova alibariki kazi ambayo Mashahidi wa Yehova walikuwa wamekuwa wakifanya muda wa miaka yote. Kwa sasa, kulingana na cheti cha tarehe Mei 7, 1993, walichopewa mnamo Mei 31, 1993, Mashahidi wa Yehova wamesajiliwa kuwa La Torre del Vigía, A. R., na Los Testigos de Jehová en México, A. R., yote mawili yakiwa mashirika ya kidini.[10]

Chini ya mashirika hayo mapya, Mashahidi wa Yehova katika Mexico, kama vile katika nchi nyingine 230 ulimwenguni, waendelea kufanya kazi kwa bidii katika kuhubiri juu ya Ufalme wa Mungu. Kuna programu kubwa ya upanuzi katika Mexico, inayotia ndani ujenzi wa Majumba ya Ufalme mapya na Majumba ya Kusanyiko mapya. Kukiwa na wahubiri zaidi ya 380,000 na wapya wengine 30,000 wakibatizwa kila mwaka, kuna kazi nyingi ya kufanya, kama inavyoweza kuonwa katika yale mafunzo ya Biblia ya nyumbani 530,000 ambayo yanaongozwa kwa sasa.

Hayo hayamaanishi kwamba matatizo yote ya Mashahidi wa Yehova nchini Mexico yametatuliwa. Watoto wao wangali wakabili mibano shuleni kwa sababu ya suala la kutokuwamo. Hata hivyo, wenye mamlaka wataka kutekeleza ile sheria mpya kwa njia isiyo ya upendeleo katika kushughulika na dini mbalimbali nchini. Kwelikweli Mexico imechukua hatua kubwa katika kutetea haki za kibinadamu na uhuru wa kidini kwa ile sheria mpya inayohusu dini.

[Picha katika ukurasa wa 13]

Vyeti vya usajili wa Mashahidi wa Yehova katika Mexico

[Picha katika ukurasa wa 14]

Kituo kipya cha elimu ya Biblia kikijengwa na Mashahidi wa Yehova nchini Mexico

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki