Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g94 4/8 kur. 23-25
  • Je! Suluhisho Ni Kujiua?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Je! Suluhisho Ni Kujiua?
  • Amkeni!—1994
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Sababu Inayofanya Wengine Wahisi Hivyo
  • Msononeko wa Familia
  • Visababishi Vingine vya Huzuni
  • Kupata Msaada
  • Kukabiliana na Hali
  • Kujiua—Pigo la Vijana
    Amkeni!—1998
  • Kwa Nini Nisijiue?
    Amkeni!—2008
  • Tatizo la Ulimwenguni Pote
    Amkeni!—2001
  • Kwa Nini Watu Hukata Tamaa ya Kuishi?
    Amkeni!—2001
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1994
g94 4/8 kur. 23-25

Vijana Huuliza. . .

Je! Suluhisho Ni Kujiua?

“Nimechoka kuamka kila asubuhi. Nimevurugika. Nimekasirika. Moyo wangu waugua. . . . Kwa hiyo nafikiria kwenda. . . . Sitaki kwenda, lakini nahisi ni lazima niende. . . . Nitazamapo wakati ujao, ninaona tu giza na maumivu.”—Taarifa ya kujiua kutoka kwa Peter mwenye miaka 21.a

WASTADI wanadai kwamba vijana wengi wapatao milioni mbili wamejaribu kujiua katika United States. Kwa huzuni, karibu 5,000 kati yao hufaulu kujiua kila mwaka. Lakini kujiua miongoni mwa vijana hukutokei United States pekee. Katika India vijana wapatao 30,000 walijiua katika mwaka wa 1990. Katika nchi kama Finland, Israel, Kanada, New Zealand, Thailand, Ufaransa, Uhispania, Uholanzi, na Uswisi, idadi ya vijana wanaojiua imepanda.

Lakini vipi ikiwa mtu anahisi amemezwa na huzuni—au akihisi amenaswa na uchungu mwingi sana wa kihisia-moyo na haoni njia ya kuepa uchungu huo? Inaweza kuonekana kwamba suluhisho rahisi ni kujiua, lakini kwa uhalisi wa mambo kujiua ni potezo lenye msiba mkubwa sana. Kujiua huacha nyuma huzuni na uchungu wa moyo kwa marafiki na familia. Hata wakati ujao uwe usio na tumaini kwa kadiri gani na matatizo yaonekane makubwa kama nini, kujiua si suluhisho.

Sababu Inayofanya Wengine Wahisi Hivyo

Ayubu mwadilifu alijua maana ya kutamauka. Baada ya kupoteza familia yake, mali zake, na afya yake nzuri, yeye alisema hivi: “Nafsi yangu huchagua kunyongwa, na kuchagua kifo kuliko maumivu yangu haya.” (Ayubu 7:15) Vijana fulani leo wamehisi vivyo hivyo. Mwandikaji mmoja analitaja jambo hilo hivi: “Mkazo wa akili . . . huleta maumivu (hisia za umizo na hofu) [ambazo] hutokeza kinga (jaribio la kuepa maumivu).” Kwa hiyo kujiua ni jaribio lisilofaa la kuepa maumivu yaonekanayo kuwa hayawezi kuvumilika.

Ni nini husababisha maumivu kama hayo? Maumivu hayo yaweza kutokezwa na tukio fulani, kama vile ugomvi mkali na wazazi, rafiki mvulana, au rafiki msichana. Baada ya kuachana na rafiki yake msichana, Brad mwenye miaka 16 alitamauka sana. Lakini, yeye hakusema na mtu yeyote juu ya hisia zake. Yeye alijiua kwa kujinyonga.

Sunita mwenye miaka 19 alishuka moyo sana wazazi wake walipogundua kwamba alikuwa anaendeleza uhusiano usio wa kiadili pamoja na rafiki yake mvulana. “Nilijua kwamba sikutaka kuendelea kuishi jinsi nilivyokuwa nikiishi,” yeye akumbuka. “Na kwa hiyo nilikuja tu nyumbani usiku mmoja, na kuanza kumeza tembe za aspirin. Nikaanza kutapika damu asubuhi iliyofuata. Sikutaka kumaliza uhai wangu bali nilitaka kumaliza mwenendo wa maisha yangu.”

Shule yaweza pia kuwa chanzo cha mkazo mkali. Akisukumwa na wazazi wake awe daktari (ambao wenyewe ni madaktari), kijana Ashish alianza kukosa usingizi na kuanza kujitenga. Akishindwa kutimiza matazamio ya wazazi wake shuleni, Ashish alimeza tembe nyingi kupita kiasi za usingizi. Tukio hilo lamkumbusha mtu juu ya Mithali 15:13 katika Biblia: “Kwa huzuni ya moyo roho hupondeka.”

Msononeko wa Familia

Mvurugo wa familia—kama vile talaka au kutengana kwa wazazi, kifo cha mtu wa familia, au kuhamia mahali papya—ni jambo jingine linalofanya baadhi ya vijana wajiue. Kwa kielelezo, Brad aliyetajwa juu, alipoteza marafiki wawili wa karibu na mtu wa ukoo katika aksidenti ya gari. Kisha familia yao ikaanza kupata matatizo ya kifedha. Brad alishindwa kabisa na hali hiyo. Huenda alihisi kama mtunga zaburi aliyelia hivi: “Nafsi yangu imeshiba taabu. . . Yamenisonga yote pamoja,”—Zaburi 88:3, 17, NW.

Idadi kubwa yenye kugutusha ya vijana inatiwa chini ya mkazo wa akili wa aina nyingine: kutendwa vibaya kimwili, kihisia-moyo, na kingono. Jimbo la Kerala, India, lina idadi ya juu zaidi ya vijana wanaojiua katika nchi hiyo. Idadi fulani ya wasichana matineja wamejaribu kujiua kwa sababu ya kutendwa vibaya na baba zao. Aina mbalimbali za kutenda watoto vibaya zimeongezeka sana ulimwenguni pote, na kwa hao wanaotendwa vibaya, msononeko unaweza kuwa mkali sana.

Visababishi Vingine vya Huzuni

Lakini si hisia zote za kutaka kujiua husababishwa na mambo ya nje. Ripoti moja ya utafiti juu ya matineja waseja yasema hivi: “Wanaume na wanawake waliojiingiza katika ngono na unywaji wa vileo walikuwa katika hatari kubwa zaidi [ya kujiua] kuliko wale walioepuka vitendo hivyo.” Mwenendo mbaya wa Sunita ulifanya apate mimba—ambayo alikomesha kwa kuitoa. (Linganisha 1 Wakorintho 6:18.) Akisumbuliwa na hatia, alitaka afe. Brad vilevile alikuwa akijaribia vileo tokea awe na miaka 14, akilewa chakari kwa ukawaida sana. Naam, kileo kikitumiwa vibaya, chaweza ‘kuuma kama nyoka.’—Mithali 23:32.

Hisia za kujiua zaweza kutoka hata kwenye “mawazo yenye kufadhaisha.” (Zaburi 94:19, NW) Madaktari wasema kwamba nyakati nyingine mawazo yenye kusababisha kushuka moyo yaweza kutokana na visababishi kadhaa vya kimwili. Kwa kielelezo, Peter, ambaye alitajwa mwanzoni, aligunduliwa kuwa alikuwa na kasoro ya usawaziko wa kemikali katika ubongo wake kabla hajajiua. Hisia za kushuka moyo ambazo hazishughulikiwi zaweza kuongezeka sana; na suluhisho laweza kuonekana kuwa ni kujiua.

Kupata Msaada

Lakini, kujiua kusifikiriwe kuwa suluhisho. Tuwe tunajua ama tusijue, sisi sote tuna ile ambayo wastadi wa akili Alan L. Berman na David A. Jobes huita ‘misaada ya ndani na ya nje ya kukabiliana kwa mafanikio na mikazo yetu ya akili na mahitilafiano yetu.’ Msaada mmoja waweza kuwa familia na marafiki. Mithali 12:25 yasema: “Uzito katika moyo wa mtu huuinamisha; bali neno jema huufurahisha.” Naam, neno jema kutoka kwa mtu mwenye kuelewa hali laweza kubadili sana hali!

Kwa hiyo mtu yeyote akihisi ameshuka moyo au ana mahangaiko, haifai asumbuke akiwa peke yake. (Mithali 18:1) Mtu huyo anayeugua anaweza kumwaga yaliyo moyoni mwake kwa mtu anayemtumaini. Kusema na mtu mwingine hupunguza uzito wa hisia za mtu, na kwaweza kumpa mtu mtazamo mpya ili kukabiliana na matatizo yake. Mtu akivunjika moyo kwa sababu ya kupoteza rafiki au mpendwa katika kifo, huyo apaswa kusema jambo hilo na msiri wake. Mtu huyo hufarijika wakati uchungu wa mapotezo hayo yanapokiriwa. (Mhubiri 7:1-3) Yaweza pia kusaidia mtu huyo akiahidi kwamba atasema na msiri wake ile misukumo ya kujiua irudipo.

Ni kweli kwamba huenda ikawa vigumu kumtumaini mtu. Lakini kwa sababu uhai wenyewe umo hatarini, je, si afadhali kusema tu naye? Yaelekea kwamba msukumo wa kujiumiza utatoweka mambo yakizungumzwa. ‘Yakizungumzwa na nani?’ huenda wengine wakauliza. Kama mtu ana wazazi wanaomhofu Mungu, mbona asijaribu ‘kuwapa moyo wake’? (Mithali 23:26) Huenda wakaelewa vizuri kuliko vile wengi wanavyofikiri na huenda wakaweza kusaidia. Ikionekana kama msaada zaidi wahitajika—kama vile uchunguzi wa daktari—wanaweza kupangia hilo.

Washiriki wa kutaniko la Kikristo ni chanzo kingine cha msaada. Wazee wa kiroho katika kutaniko waweza kutegemeza na kusaidia wale wanaosononeka. (Isaya 32:1, 2; Yakobo 5:14, 15) Baada ya kujaribu kujiua, Sunita alipata msaada kutoka kwa mhudumu wa wakati wote (painia). Sunita asema hivi: “Alishikamana nami kwa kila hali. Kama si yeye, ningerukwa na akili.”

Kukabiliana na Hali

Kuna misaada ya kutoka ndani pia inayoweza kutumiwa. Kwa kielelezo, je, unasumbuliwa na hatia kwa sababu ya kosa fulani? (Linganisha Zaburi 31:10.) Badala ya kuacha hisia kama hizo ziongezeke, mtu anapaswa anyooshe mambo. (Isaya 1:18; linganisha 2 Wakorintho 7:11.) Hatua ifaayo ni kuungama kwa wazazi wako. Ni kweli kwamba huenda wakaudhika kwanza. Lakini yaelekea watazingatia kutoa msaada. Twahakikishiwa pia kwamba Yehova ‘husamehe kabisa’ wale wanaotubu kikweli. (Isaya 55:7) Dhabihu ya fidia ya Yesu hufunika dhambi za wale wanaotubu.—Warumi 3:23, 24.

Wakristo wana imani, ujuzi wa Maandiko, na uhusiano wao pamoja na Yehova Mungu unaoweza kuwasaidia pia. Katika pindi kadhaa mtunga zaburi Daudi alisononeka sana hivi kwamba alisema: “Adui . . . ameutupa chini uzima wangu.” Yeye hakushindwa na tamauko. Aliandika hivi: “Kwa sauti yangu nitamlilia BWANA, kwa sauti yangu nitamwomba BWANA dua.” “Nimeyatafakari matendo yako yote; naziwaza kazi za mikono yako.”—Zaburi 142:1; 143:3-5.

Tamaa ya kujiumiza ikiwa yenye nguvu sana, mtu apaswa kumwita Yehova kwa sala. Yeye anaelewa maumivu yanayohisiwa na anataka mteswa aishi! (Zaburi 56:8) Anaweza kuandaa “nguvu ipitayo iliyo ya kawaida” ili ukabiliane na maumivu hayo. (2 Wakorintho 4:7, NW) Mtu apaswa kufikiria pia juu ya maumivu ambayo kujiua kutaletea familia, marafiki, Yehova mwenyewe. Kufikiria mambo kama hayo kwaweza sana kumsaidia mtu asijiue.

Kwa maana ingawa huenda ikaonekana kwa wengine kwamba umizo hilo halitatoweka kamwe, wanaweza kuhakikishiwa kwamba kuna wale ambao wamevumilia maumivu kama hayo. Wanaweza kusema kutokana na maono yao kwamba mambo yanaweza kubadilika na hata hubadilika. Wengine wanaweza kutoa msaada ili kuvumilia wakati huo wenye maumivu. Watu walioshuka moyo wanapaswa kutafuta msaada unaohitajika wanaostahili kupata—na waendelee kuishi!

[Maelezo ya Chini]

a Baadhi ya majina yamebadilishwa.

[Picha katika ukurasa wa 24

Ni vizuri kusema na mtu juu ya hisia zako zenye maumivu

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki