“Sayansi Yajifunza kwa Vitu vya Asili”
HICHO kilikuwa kichwa cha gazeti The New York Times la Agosti 31, 1993.[1] Makala hiyo ilitaja kwamba idadi inayoongezeka ya wanasayansi wanaounda vitu vipya imejiingiza katika aina ya sayansi iitwayo biometiki. Gazeti Times lilifafanua biometiki kuwa “uchunguzi wa muundo na kazi ya vitu vya kibiolojia vikiwa vigezo kwa vitu vya kutengenezwa na binadamu.”[2]
Makala hiyo ilitaja kwamba viumbe vya hali ya chini vya baharini na buibui hutengeneza vitu bora zaidi kuliko vile vitu vinavyofanana na hivyo vinavyoweza kutengenezwa na wanasayansi. Kwa kielelezo, abaloni (aina ya konokono), hutwaa kabonati ya kalsiamu, ule ungaunga wa chokaa, kutoka majini na kutengeneza mabamba madogo-madogo sana. Kisha abaloni hushikanisha mabamba hayo kwa gamu iliyotengenezwa kwa protini na sukari. Dakt. Mehmet Sarikaya asema kwamba muundo wa kombe hizo una nguvu mara 30 kuliko kabonati ya kalsiamu ya kawaida ambayo hutengenezwa kwa maabara. “Hatuna ujuzi wa kutengeneza mabamba ya vitu yakiwa madogo-madogo sana kama yale ya kombe za bahari,” yeye akiri.[3]
Kwa njia iyo hiyo, uzi wa utando wa buibui una nguvu kuliko chuma na unadumu kuliko nailoni. Wanasayansi wanachunguza utando huo wakitazamia kutengeneza nyuzi zenye nguvu kuliko Kevlar, ambayo hutumiwa kutengeneza fulana zisizoweza kupenyezwa risasi.[4] Hata hivyo, binadamu bado hawezi kuiga ile njia ngumu sana ya jinsi buibui hutengeneza uzi wa utando.[5]
“Buibui hutengeneza uzi wa utando kwa kutumia maji yakiwa kiyeyushaji katika hewa, na katika halijoto na kanieneo zinazopatikana, na utando hupitia hatua hizo zote ili uimarike, usiweze kupenyezwa na maji na kuwa wenye nguvu sana,” akasema Dakt. Christopher Viney wa Chuo Kikuu cha Washington katika Seattle.[6] “Lakini ili utengeneze uzi mgumu kama Kevlar, ni lazima uutengeneze kwa kanieneo ya juu sana ukitumia asidi ya sulfuri.” Hivyo, mwanasayansi huyo akiri: “Bado tuna mengi ya kujifunza.”[7]
Ebu fikiria. Ikiwa ujuzi bora zaidi wa binadamu hauwezi kutokeza vitu ambavyo viumbe vya hali ya chini vya bahari na buibui viwezavyo kutokeza, je, si jambo la akili kuamini kwamba viumbe hivyo viliumbwa na mtu mwenye akili zaidi? Kwa hekima, tutampa sifa yule Mbuni Mkuu—ambaye wanasayansi wa leo wanajaribu kuiga kazi yake—kwa ajili ya ustadi wake usio na kifani akijaza dunia kwa kazi zake.—Zaburi 104:24.