Uhandisi wa Koa
JE! UMEWAHI kuona jinsi ilivyo rahisi kuvunja kipande cha chaki ya kuandikia katika vipande viwili? Lakini sasa, jaribu kuvunja koa la abaloni mwekundu katika vipande viwili. Huenda ukahitaji nyundo ili kuivunja. Ilhali koa la abaloni limefanyizwa kwa dutu ile ile kama chaki ya kalsiamu kaboneti. Koa limefanyizwa pamoja kwa njia tofauti-tofauti. Kwa njia tofauti sana, kwa kweli, hivi kwamba lina uwezo wa kukinza mvunjiko wa mara 40 zaidi ya chaki ya kuandika.
Abaloni huwezaje uhandisi huu hodari? Wanasayansi kwenye Chuo Kikuu cha Washington katika Seattle, U.S.A., wamegundua siri za konokono huyo wa baharini. Abaloni hutumia koa lake moja lililo kama sahani kuwa ukuta wa ulinzi dhidi ya ulimwengu wa nje. Kwa ajili ya uthabiti, koa hutokeza safu nyingi. Safu ya nje ni yenye kukwaruza na hafifu. Lakini safu ya ndani, iitwayo lulumizi, hung’aa kwa wangavu wenye kupendeza, na hapo ndipo kuna uthabiti wa koa.
Wanasayansi wa Washington wamejifunza kwamba safu hii ya ndani “ina tabaka ya muundo wa tofali-na-chokaa,” laandika Science News. Ikiwa na upana wa karibu maikroni moja tu (sehemu moja ya milioni kwa meta), matofali haya madogo mno hushikiliwa pamoja na chokaa iliyofanyizwa na abaloni mwenyewe, mgandamano wenye nguvu ambao wanasayansi bado wangali wakijaribu kuelewa. Wanasayansi wanasema kwamba safu za “matofali” madogo madogo hufyonza migongano kwa kuteleza kwenye safu zinazopakana. wakati uleule, safu za kikaboni za chokaa huunganisha kwa njia fulani mipasuko inayotokea kwa “mishipa” ya kipekee. Kwa yote hayo, koa hilo laweza kuwa na njia tano mbalimbali za kukinza mvunjiko!
Wanasayansi wanavutiwa sana na koa la abaloni lenye nguvu ya ajabu hivi kwamba wanajaribu kutokeza njia kama hizo katika kutengeneza vyombo vya kauri vyenye nguvu. Wakifanikiwa, bila shaka watasifiwa sana. Jinsi lilivyo jambo lenye kuhuzunisha kwamba Mbuni Mkuu, ambaye wanajaribu kuiga kazi yake, hukosa kusifiwa kwa ubingwa wake usio na kifani!—Ayubu 37:14.