Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g94 4/22 kur. 20-23
  • Diski-Songamano—Hiyo Ni Nini?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Diski-Songamano—Hiyo Ni Nini?
  • Amkeni!—1994
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Kurekodi kwa Tarakimu—Ni Nini?
  • Ni Nzuri Kadiri Gani?
  • Diski-Songamano na Kompyuta
  • Zawadi ya Muziki
    Amkeni!—2011
  • Kutoka kwa Wasomaji Wetu
    Amkeni!—1994
  • Kishikizo cha Samaki Anayeitwa Remora
    Je, Ni Kazi ya Ubuni?
  • Ni Nini Hufanya Kibao cha Muziki Kiuzwe Sana?
    Amkeni!—2011
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1994
g94 4/22 kur. 20-23

Diski-Songamano—Hiyo Ni Nini?

TANGU ianze kuuzwa kwa wingi katika miaka ya mapema ya 1980, diski-songamano ya tarakimu inayosomwa na miale ya leza imesifiwa kuwa maendeleo makubwa zaidi katika kurekodi sauti tangu Edison avumbue santuri yenye silinda ya mkebe katika 1877 au tangu sauti ya stirio ivumbuliwe katika miaka ya mapema ya 1960.[1]

Katika United States, ripoti moja katika jarida moja la kibiashara Billboard yaonyesha kwamba katika 1992, watengenezaji waliuza diski-songamano zaidi ya milioni 414 lakini wakauza sahani za santuri milioni 22 tu.[1a] Diski-songamano zinauzwa sana kiasi cha kwamba baadhi ya makampuni yameacha kutengeneza sahani za santuri.[2] Lakini, watu wengi wangali hawaelewi diski hiyo ndogo. Sauti yenye kutokezwa na tarakimu ni nini? Je! kweli hiyo ni nzuri jinsi inavyodaiwa? Diski hufanyaje kazi? Na je, ufundi kama huo ungeweza kutumiwa kuhifadhi na kutoa habari nyingi, kama vile kutoka kwenye Mnara wa Mlinzi na Amkeni!?

Kurekodi kwa Tarakimu—Ni Nini?

Ili tuelewe kurekodi kwa tarakimu ni nini, kwanza ni vizuri tujue kimsingi jinsi ya kurekodi kwa njia ya zamani. Katika sahani za santuri zijulikanazo, muziki hurekodiwa ukiwa mfuo wenye kuendelea wenye vibonde, ukiwa picha, au mfano wa wimbi la sauti. Ili kutoa muziki, sindano ya santuri huwekwa kwenye mfuo wa sahani inayozunguka. Sindano hiyo hufuata huo mfuo, na mfuo hujongea ukisababisha sindano iruke-ruke. Sindano hiyo nayo yatokeza ishara ndogo-ndogo za kiumeme zinazofanana na sauti zile zilizonakiliwa na kikuza sauti katika jumba la kurekodi muziki. Kisha ishara hiyo inakuzwa—na muziki watokea!

Kurekodi kwa tarakimu hufanywa kwa njia tofauti. Chombo cha kurekodi kwa tarakimu hujaribu na kupima ukubwa wa ishara kila baada ya muda fulani—makumi ya maelfu kwa kila sekunde moja—na kurekodi zile ishara kwa namna ya nambari, au tarakimu.[3] Vipimo hivyo hurekodiwa vikiwa kwa namna ya nambari za binari—katika lugha za kikompyuta—zenye tarakimu zinazofanyizwa na 0 na 1 pekee. Basi, nambari hizo, ama tarakimu, huchanganushwa na kompyuta, na mara nyingi kuhifadhiwa katika tepu ya sumaku. Ili muziki uchezwe baada ya kurekodiwa, kompyuta husoma tarakimu na kutengeneza tena ishara kama ile ya awali. Kisha ishara hiyo inakuzwa na—mara nyingine tena—muziki watokea!

Njia hiyo ya kurekodi muziki haiathiriwi sana na mapungukio ya mashine za kurekodi na kufanyiza muziki kuliko jinsi kurekodi kwa sahani za santuri kunavyoathiriwa. Kufanya hivyo hakutokezi kelele sana, sauti bandia, na mambo mengine machache yanayoharibu ubora wa muziki uliorekodiwa.[4] Kwa kuongezea, habari zilizo kwa hali ya tarakimu zaweza kuhifadhiwa katika hali iliyosongamana sana na ni rahisi kutolewa. Huenda mmoja akasema kwamba kurekodi kwa njia ya tarakimu, ni tokeo la asili la muungano baina ya kompyuta na santuri.

Kwa miaka mingi makampuni ya kurekodi muziki yamekuwa yakirekodi muziki kwa njia ya tarakimu katika majumba yayo ya kurekodi.[5] Lakini ule mfumo wa kucheza muziki baada ya kurekodiwa ni tata sana kuweza kutumiwa katika mifumo ya muziki ya nyumbani. Kwa maoni ya wanunuzi, maendeleo makubwa zaidi katika kurekodi muziki kwa njia ya tarakimu yalitokea kwa kutengenezwa kwa mfumo wa kucheza muziki baada ya kurekodiwa ambao haukuwa ghali na ambao haukutatanisha sana mtumiaji wa kawaida wa nyumbani. Matokeo yakawa diski-songamano ya tarakimu (CD) na chombo cha kuichezesha.

Zile nambari za binari, au nambari ziwezazo kuchaguliwa, hubadilishwa ziwe mfululizo wa mashimo madogo-madogo sana na nafasi tambarare kwenye uso wa diski ya plastiki yenye tabaka inayong’aa ya aluminiamu. Diski hiyo ina kipenyo cha milimeta 120. Ile tabaka ya aluminiamu hufunikwa na tabaka nyingine ya plastiki isiyo na rangi.[6] Ili kucheza muziki, ile diski yenye kung’aa kama fedha huingizwa katika chombo cha kuchezesha diski-songamano. Badala ya kuwa na sindano, miale ya leza hufuata kwa usahihi sana yale mashimo madogo-madogo. Miale hiyo inapogonga mashimo hayo, hutawanywa, lakini inapogonga sehemu tambarare, hurudishwa pamoja kwenye sensa.[7] Kwa njia hiyo yale mashimo na sehemu tambarare zilizopo kwenye uso wa diski-songamano hugeuzwa kuwa mapigo ya kiumeme yatakayofumbuliwa na mifumo tata ya kielektroni katika chombo hicho cha kuchezesha muziki.

Ni Nzuri Kadiri Gani?

Lakini je, kweli diski-songamano ni nzuri kuliko sahani za santuri? Naam, ebu fikiria: Kwa kuwa diski-songamano huchezeshwa kwa kutumia miale ya nuru badala ya sindano ya almasi, diski hiyo haichakai hata ichezeshwe mara ngapi. Hata alama ndogo-ndogo kwenye uso wa diski haitaathiri sana ubora wa sauti kwa sababu ile miale ya leza hukazwa kwenye yale mashimo wala si kwenye uso wa diski.[9] Zile kelele na mikwaruzo yenye kukera ambayo kila mtu aliyepata kusikiliza sahani kubwa za santuri (santuri zenye kucheza muda mrefu) aifahamu vizuri hutoweka. Hayo yote yafanya diski-songamano iwe na udumifu ambao sahani za santuri haziwezi kufikia. Inasemekana kwamba diski-songamano yaweza kudumu milele—ikitengenezwa vizuri na kutunzwa vizuri.

Mafaa mengine ya diski-songamano ni kwamba hiyo inaweza kucheza kwa muda mrefu na ni ndogo zaidi. Inaweza kugeuza muziki kwa muda unaozidi saa nzima bila mtu kuja kubadili upande mwingine wa sahani! Tena diski-songamano ni rahisi kutunza na kuhifadhi kwa sababu hiyo ni ndogo mara tano kuliko sahani kubwa za santuri.[12] Kwa kuongezea, kwa sababu vyombo vya kuchezesha diski-songamano hufanya kazi kama kompyuta, vyombo vingi vyaweza kupangiwa kucheza sehemu zitakikanazo za diski-songamano kwa mfuatilio wowote ule unaotakikana au kurudia muziki fulani. Vyombo vingine pia vina uwezo wa utafutaji ambao waweza kutumiwa kutafuta sehemu yoyote ya muziki haraka sana. Mafaa kama hayo hupendwa sana na watumizi wengi wa diski-songamano.[13]

Lakini vipi juu ya ubora wa sauti? Karibu kila mtu anayesikiliza diski-songamano kwa mara ya kwanza hustaajabia jinsi inavyotokeza sauti ya wazi na iliyo halisi. Muziki huimba kutoka kwenye hali ya ukimya sana kwa njia idhihirishayo mambo madogo-madogo sana. Sababu moja inayotokeza jambo hilo ni kwamba katika diski-songamano ile tofauti baina ya muziki wa pole zaidi na ule wenye sauti ya juu zaidi uwezao kurekodiwa—ambayo huitwa tofauti-kuu—ni kubwa zaidi ya ile tofauti iliyoko kwenye sahani kubwa za santuri za kawaida. Jambo hilo, pamoja na ukosefu wa kelele na ubadilifu wa sauti, hufanya muziki uwe halisi zaidi katika diski-songamano.

Kwa upande mwingine, diski-songamano ya kawaida yaweza kuwa ghali sana kuliko sahani kubwa ya santuri.[16] Lakini, yaweza kusemwa kwamba diski-songamano imeletea umma muziki wenye hali ya juu sana ambao ni wapenzi wachache sana wa muziki aina ya hi-fi wamefurahia nyakati zilizopita.[20]

Diski-Songamano na Kompyuta

Hivi karibuni, diski-songamano imeanza kutumiwa kwa njia nyingine tofauti kabisa kwa sababu ufundi uleule waweza kutumiwa kuhifadhi habari nyingi sana, au data. Habari kama hizo katika diski-songamano zaweza kupatikana kwa urahisi kwa kutumia kompyuta yenye chombo cha kusoma diski-songamano au iliyoshikanishwa na chombo hicho. Kama vile sehemu yoyote ya muziki ya diski-songamano yaweza kufikiwa haraka sana katika chombo cha kuichezesha, kukiwa na aina tofauti ya chombo cha kusoma diski-songamano, sehemu yoyote ya habari zilizohifadhiwa zaweza kusomwa, kutafutwa, au kunukuliwa kwa sekunde chache tu kupitia programu zilizotengenezwa vizuri za kompyuta.

Diski-songamano ina uwezo mkubwa sana wa kuhifadhi habari. Tukitumia lugha ya kikompyuta, yaweza kuhifadhi zaidi ya megabaiti 600, hiyo yatoshana na disketi ndogo 1,000 au kurasa zilizochapwa 200,000.[29] Kwa maneno mengine, seti kumi za mabuku 20 za ensaiklopedia zikiwa zimebadilishwa kuwa tarakimu zaweza kuhifadhiwa katika diski-songamano moja tu! Lakini uwezo huo si manufaa yayo pekee.

Kufikia karibu 1985, diski-songamano za kutumiwa katika kompyuta zilianza kuuzwa.[30] Diski hizo ziliitwa CD-ROM, ufupi wa maneno ya Kiingereza yanayomaanisha diski-songamano ya kusomwa tu. Mara nyingi hizo zilikuwa na habari za marejezo, kama vile ensaiklopedia, kamusi, vitabu vya majina na anwani, orodha za vitu, habari za vitabu na watungaji, habari za kiufundi, na hati za zamani au kumbukumbu za kila aina. Zilipotengenezwa mara ya kwanza, zilitumiwa sanasana katika maktaba na vyuo vingine vya masomo au vya serikali kwa sababu zilikuwa ghali sana. Kwa kweli, diski ambayo miaka michache iliyopita ingegharimu mamia kadhaa ya dola sasa zaweza kununuliwa kwa kiasi kidogo zaidi.

Haikuchukua muda mrefu kwa utengenezaji wa diski ya kusomwa tu kutumiwa zaidi ya kuwa kitu tu cha kuhifadhi habari. Katika miaka michache iliyopita, diski za kusomwa tu zenye picha za rangi na zenye kutoa sauti zilianza kuuzwa. Sasa unaweza kusoma juu ya maisha ya mtu fulani na kuona picha yake na vilevile kusikia hotuba ya mtu huyo. Na bila shaka, kuna michezo ya aina yoyote ile ya kompyuta yenye kutokeza sauti na picha zenye rangi zinazosonga. Vyombo hivyo viitwavyo mifumo yenye kuhusiana ya vyombo vya habari, vinavyounganisha kompyuta na vitumbuizo vya nyumbani, vyaonekana kuwa ndivyo vitu vitakavyopendwa zaidi wakati ujao.[31]

Kwa kweli diski-songamano ya tarakimu ni ufundi wa hali ya juu uwezao kuwa na manufaa kimasomo na kitafrija. Tutaona kama itaendelea kufanya maendeleo hata zaidi.

[Sanduku katika ukurasa wa 21]

Ulimwengu Mdogo wa Diski-Songamano

Jina diski-songamano lafaa. Kuna mashimo madogo-madogo bilioni tano hadi sita yaliyopangwa na kuzunguka kwa njia ya parafujo kwenye diski hiyo inayong’aa yenye ukubwa wa kiganja.[21] Ikinyooshwa, kamba hiyo yaweza kupita umbali kilometa 5.6 ikinyooshwa.[22] Vijia hivyo vikiwa vimekunjwa kwa mizunguko 20,000 vikitokea sehemu za ndani kuelekea nje, vinasongamana sana hivi kwamba vijia 60 vyaweza kutoshea mfuo wa sahani kubwa ya santuri (santuri zenye kucheza muda mrefu).[23] Imekadiriwa kwamba ikiwa kila shimo lingekuwa na ukubwa wa mchele mmoja, hiyo ingehitaji diski yenye ukubwa unaoshinda uwanja wa meta 21,560 za mraba.[32]

Kwa sababu ya vipimo vyayo vidogo-vidogo sana, ni lazima diski-songamano zitengenezwe katika vyumba safi ambamo hewa imechujwa kabisa.[24] Kipande kimoja tu cha vumbi la wastani, ambacho ni kubwa kushinda shimo moja katika diski-songamano mara tano, chaweza kufuta nambari kadhaa na kusababisha makosa katika kurekodi.[25] “Ukilinganisha viwango vyetu vya usafi,” asema mhandisi mmoja, “chumba cha kufanyia upasuaji ni kama zizi la nguruwe.”[26]

Kwa kuwa diski hiyo huzunguka kufikia mizunguko 500 kwa dakika moja inapochezwa, ni ajabu kwamba leza inaweza kukaziwa yale mashimo na kudhibitiwa isikengeuke kutoka kwenye kijia chake kilichozunguka.[27] Ili kutimiza jambo hilo, mwali wa leza unadhibitiwa na mfumo tata wa kuongoza miendo yao.[28]

[Sanduku katika ukurasa wa 23]

Maktaba ya Watchtower—Diski-Songamano ya Kusomwa Tu

Nyakati zote Watchtower Society imechagua kutumia maendeleo yafaayo ya kiufundi katika kueneza masilahi ya Ufalme. Katika nyakati zilizopita Sosaiti ilikuwa mojayapo mashirika ya kwanza kutumia picha zenye kusonga za rangi za sinema, stesheni za redio, santuri yenye kubebeka katika kutangaza habari njema. Sasa, Watchtower Society imetokeza kwa umma Watchtower Library—1993 Edition kwa Kiingereza. Tuna hakika kwamba hicho kitakuwa chombo kizuri ajabu cha funzo na utafiti wa Biblia.

Kwa kweli toleo hilo jipya ni maktaba kubwa. Ina maandishi, katika namna ya kielektroni, ya New World Translation of the Holy Scriptures—With References, mabuku yaliyojalidiwa ya Mnara wa Mlinzi ya kila mwaka tangu 1950 hadi 1993 na Amkeni!, (kwa Kiingereza) kutokea 1980 hadi 1993, mabuku mawili ya ensaiklopedia ya Biblia Insight on the Scriptures, na vitabu, vijitabu, broshua, na trakti nyinginezo nyingi zilizochapishwa na Watchtower Society tangu 1970. Kwa kuongezea, ina faharisi inayotia ndani vichapo vyote vya Watchtower kutokea 1930 hadi 1993.

Pamoja na uwezekano huo wa kupata habari kwa haraka, diski hiyo ya kusomwa tu huandaa programu ya utafutaji ambayo ni rahisi kutumiwa itakayokuwezesha kutafuta neno, fungu la maneno, au Andiko ambalo limetajwa katika kichapo chochote kilichopo katika Watchtower Library. Waweza pia kufungua kichapo chochote moja kwa moja, kwenye sura fulani, makala, au ukurasa. Matokeo ya utafutaji wako yaweza kuonwa katika kiwambo cha kompyuta au kunakiliwa katika maandishi yako yatumiwe katika hotuba au barua. Programu hiyo pia ina sehemu ya kupanga mambo ya funzo la kibinafsi na ya kuandika mambo yako mwenyewe.

Tunatumaini kwamba kwa kutumia chombo hiki kipya, wengi zaidi wataweza kudumu katika kutazama “sheria kamilifu iliyo ya uhuru” na kubarikiwa kwa kufanya hivyo.—Yakobo 1:25.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki