Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g94 5/8 kur. 20-22
  • Naweza Kupunguzaje Uzito?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Naweza Kupunguzaje Uzito?
  • Amkeni!—1994
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Kula Mno, Kujizoeza Kidogo
  • Mtego wa Kupunguza Uzito kwa Kujinyima Chakula Mno
  • Njia Salama ya Kupunguza Uzito
  • Kubadili Mpango Wako wa Kula na Mtindo-Maisha Wako
  • Wakati Ambapo Ukubwa Haufai
    Amkeni!—1997
  • Ninaweza Kupunguzaje Uzito?
    Vijana Huuliza
  • Nifanye Nini Ikiwa Sipendi Umbo Langu?
    Maswali Ambayo Vijana Huuliza—Majibu Yafanyayo Kazi, Buku la 2
  • Ni nini suluhisho la Kunenepa Kupita Kiasi?
    Amkeni!—2004
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1994
g94 5/8 kur. 20-22

Vijana huuliza...

Naweza Kupunguzaje Uzito?

“JAMBO baya kabisa ambalo lingeweza kutendeka katika maisha ya mvulana tineja ni kuwa na mafuta mengi mno.” Hivyo ndivyo alivyoomboleza mvulana tineja jina lake Judd.[1] Ikiwa uzito wako umezidi mno, wewe waweza kujua jinsi yeye ahisivyo hasa.

Hata hivyo, mafuta mengi mno mwilini yaweza kuwa na madhara mengi kuliko yale ya kuharibu uzuri wa sura yako tu. Kuwa na mafuta mengi mno kwaweza kukutia katika hatari ya kupatwa na lindi la matatizo ya afya—shida nyingi za muungano, maradhi ya kupumua, na ugonjwa wa sukari, na pia magonjwa yenye kuua kama ugonjwa wa moyo na kansa ya utumbompana ambayo yaweza kukusumbua baadaye maishani.a[2]

Bila shaka, ikiwa wewe ni mnene-mnene, hiyo haimaanishi kwa lazima kwamba wahitaji kupunguza uzito. Wengine wetu ni kwamba tu tumerithi muundo wenye maungo manene; sisi huonekana wazito kuliko vile tungependelea hata tukiwa na uzito wetu wa kawaida.b[4] Lakini ikiwa daktari wako ameamua kwamba wewe una mafuta mengi ya mwili kuliko yale ya afya, huenda mambo mengine kadhaa yakahusika. Chasema hivi kitabu The Healthy Adolescent: “Utendaji wenye kasoro za tezindani kama kongosho, kikoromeo, na adrenali . . . umeshirikishwa na kuwa na mafuta mengi mno katika watu fulani.”[5]

Kula Mno, Kujizoeza Kidogo

Katika visa vingi, kuwa na mafuta mengi mno ni tokeo la tabia mbaya tu za ulaji na kukosa mazoezi. Judd mchanga akumbuka hivi: “Kwa kuwa mama yangu alilazimika kwenda kazini ili kutupa riziki, mimi na ndugu yangu . . . tulijilisha. Tulikula pakiti za pipi, tukiziteremsha kwa chupa za soda ya lita mbili.”[8] Je! lasikika jambo la kawaida?

Ingawa hivyo, vijana wengine hawali ili waondoe njaa bali ili watimize uhitaji wao wa kuhisi wanapata malezi na faraja. Vijana hao huenda wakala mno kwa jaribio la maoni mabaya kwamba wanapunguza mkazo, kama talaka ya wazazi, kifo cha mpendwa, au tukio jingine lenye kuuma sana.[9]

Tatizo la kula mno huongezewa mara nyingi na ukosefu wa mazoezi. Kichapo A Parent’s Guide to Eating Disorders and Obesity chatoa maoni haya: “Televisheni si kwamba hutaka mtu ajikalie kitako tu bila utendaji wa kimwili, bali pia programu na matangazo yaliyomo hufanya mtu aelekee kula . . . na kula . . . na kula zaidi.”[10]

Mtego wa Kupunguza Uzito kwa Kujinyima Chakula Mno

Watu fulani hudai kwamba 1 kati ya kila Waamerika 4 amejipangia programu fulani ya kupunguza uzito kwa kujinyima chakula kwa kadiri fulani.[11] Hata hivyo, zaidi ya asilimia 90 ya watu wapunguzao uzito kwa kujinyima kadiri fulani ya chakula hurudiwa na uzito huo.[12] Kasoro hutokea wapi?

Mwili wako ni kama tanuri; ubongo wako ndicho kirekebisha-joto. Wewe ulapo, mfumo wako wa kujenga na kuvunjavunja kemikali mwilini huchoma kile chakula ili kufungulia nishati zilizomo. Wakati mwili utwaapo joto jingi kuliko lile uhitajilo, joto hilo huwekwa akibani likiwa mafuta.[13] Sasa, ukijinyima chakula mno ili upunguze uzito, utapunguza uzito—pale mwanzo. Lakini upesi mwili wako huingia haraka katika ‘hali ya kukabiliana na hatari’ na kupunguza nguvu za mfumo wako wa kujenga na kuvunjavunja kemikali mwilini. Hapo wewe huanza kuongeza uzito tena, hata kama unajinyima chakula mno, na kingi cha chakula ulacho huwekwa akibani kikiwa mafuta. Wewe hurudiwa na kila ratili uliyopunguza, hata zaidi ya hiyo. Kwa kuvurugika, wewe waanza tena kujinyima chakula kwa kadiri fulani. Lakini kadiri uzidivyo kupunguza—ndivyo uzidivyo kuongeza.[14]

Basi waweza kuona ni kwa nini mbinu za kujinyima chakula kwa kadiri fulani hazifui dafu. Vibonge vya kupunguza hamu ya kula huenda vikazuia hamu yako kwa muda, lakini mwili hujirekebisha haraka kujipatanisha navyo kisha hamu yako hurudi. Au mfumo wako wa kujenga na kuvunjavunja kemikali mwilini hupunguza mwendo nawe huongeza uzito wa mwili vyovyote vile. Tena kuna yale matokeo ya ziada ambayo yamewapata watu fulani, kama kizunguzungu, msukumo mwingi mno wa damu, mitukuto mikali ya wasiwasi—na uzoelevu wa kujinyima. Yaweza kusemwa hivyohivyo juu ya vibonge ambavyo huondoa maji au kuharakisha mwendo wa mfumo wako wa kujenga na kuvunjavunja kemikali mwilini. Dakt. Lawrence Lamb hueleza hivi bila kuficha: “Hakuna kitu kama kibonge salama, chenye matokeo ya kukusababisha upunguze mafuta yako ya mwili.”[15]

Kwa kuwa wewe ni kijana, mwili wako wahitaji wingi wa kalori na vijenga-mwili vya kutosha kila siku. Kujinyima chakula mno ili kupunguza uzito kwaweza kudumaza ukuzi wako kikweli.[16] Fikiria, pia, lile Biblia isemalo juu ya Mfalme Sauli kwenye 1 Samweli 28:20: “Wala hakuwa na nguvu yo yote; kwa maana hakula chakula mchana kutwa, wala usiku kucha.” Vivyohivyo, kulingana na tabibu mmoja, vijana wajaribuo kujinyima chakula mno waweza kupatwa na “uchovu mwingi, . . . mshuko wa moyo, ubaridi wa mwili, kupunguza mafanikio ya masomo shuleni, kufunga choo, wasiwasi, kukosa hedhi, na ugoigoi wa akili.”[17]

Njia Salama ya Kupunguza Uzito

Njia salama ya kupunguza uzito huanza na kuchunguzwa sana na tabibu wa familia yenu. Yeye aweza kuchunguza kama kuna matatizo yoyote ya afya ambayo yangeweza kuzuia mafanikio ya mpango sahili wa kupunguza uzito kwa kula kidogo. Aweza pia kukusaidia uweke mradi wenye kiasi wa kupunguza uzito na kupanga mbinu fulani ya kutimizia mradi huo muda wa kiasi kifaacho.[18]

Biblia husema hivi: “Mwanadamu hapati jema kupita kula na kunywa, na kuiburudisha roho yake kwa mema katika kazi yake.” (Mhubiri 2:24) Kwa hiyo mpango wa kujinyima chakula kwa kadiri fulani ambao wakuondolea ile shangwe ya kula hautaelekea kufua dafu hatimaye.[19] Zaidi ya hilo, kula mno ndiko Biblia hulaumu vikali. (Mithali 23:20, 21) Hapa, basi, pana madokezo machache ya kukusaidia uwe ‘mwenye kiasi’ katika kula kwako.—1 Timotheo 3:11, Habari Njema kwa Watu Wote.

Usikose kifungua-kinywa! “Njaa na hisia ya kwamba unanyimwa kitu fulani hukuzidia,” chaonya The New Teenage Body Book. “Utakuwa na mwelekeo wa kujijaza chakula—tena kalori nyingi—baadaye wakati wa mchana.”[20]

Kunywa bilauri kubwa ya maji kabla ya kila mlo. Itajaza tumbo lako. Kunywa maji ya kadiri za kutosha yaonekana husaidia pia kupunguza mjazano wa mafuta mwilini. Kwa hiyo madaktari hupendekeza kunywa angalau bilauri nane za maji kwa siku.[21]

Usile na kutazama televisheni. Asema hivi Dakt. Seymour Isenberg: “Unapokuwa ukishughulika kutazama televisheni . . . , [waweza kuanza] kula kama mashine.”[22]

Sali kabla ya kula. Kumbuka: “Mungu aliviumba [vyakula] vipokewe kwa shukrani na walio na imani wenye kuijua hiyo kweli.” (1 Timotheo 4:3) Akikumbuka uhusiano wake wa karibu na Muumba, kijana mwenye kuhofu Mungu hatataka kujitia katika kula mno kufikia hatua ya kujifanya goigoi katika mawazo na vitendo. Sala yaweza kutia nguvu azimio lako la kula kwa kiasi.

Kula polepole. Ni muda wa karibu dakika 20 ambao tumbo huchukua ili kuupa ubongo ishara ya kwamba limejaa.[24] Hivyo kula polepole kutakusaidia ‘kula ushibe,’ na basi!—Mambo ya Walawi 25:19.

Tafuta mambo yenye afya yawe badala ya kula—iwe hivyo hasa ikiwa umekuwa katika tabia ya kula wakati wowote shughuli za maisha zikuchoshapo, ubanwapo na hangaiko, uwapo mpweke, au kushuka moyo. Ongea na mtu fulani ambaye wamwamini. Nenda utembee, au ufanye mazoezi. Fanya kipendezi chenye kuburudisha. Sikiliza muziki.[25] Hata zaidi, jaribu kutosheleza hamu yako ya kiroho. (1 Petro 2:2) Ingawaje, chakula hakijengi imani. (Linganisha Waebrania 13:9.) Lakini kusoma Biblia hufanya hivyo, na hilo huenda likasaidia kuondoa akili yako kwenye hamu yako ya kula.

Kubadili Mpango Wako wa Kula na Mtindo-Maisha Wako

Mabadiliko huenda yakawa ni lazima yafanywe katika kile ambacho umekuwa ukila. Sheria ya Musa ilikataza kula mafuta. (Mambo ya Walawi 3:16, 17) Ingawa hiyo ilikuwa kwa sababu za kidini, kuepuka vyakula vya mafuta-mafuta—kama mikate ya kubandika jibini au vyakula vilivyokaangwa katika mafuta—ni njia nzuri ya kupanga ulaji wa kadiri. Vinywaji kama soda na vitumbua vyenye sukari-sukari havijengi mwili sana na vina kalori nyingi pia. Na ingawa chumvi nyingi juu ya kipande cha nyama isiyo na mafuta sana huenda kikawa na ladha nzuri, husababisha mwili wako uhifadhi maji.[26]

Walio wengi wa wataalamu wa kupanga ulaji hukubaliana kwamba kula vyakula uvipendavyo sana mara kwa mara hakutakudhuru.[27] Lakini ikiwa kweli wataka kupunguza uzito, ni lazima usitawishe upendezi wa vyakula vyenye afya zaidi kama matunda, njugu, nafaka zisizoondolewa maganda, na mboga.[28] “Ule unamnanamna wa vyakula ili usikose upendezi,” apendekeza mtaalamu mmoja wa kupanga ulaji. Eti wasema si wewe hupika katika familia yenu? Basi ongea na mama yako uone kama aweza kusaidia. Kwa kweli, familia nzima itanufaika mabadiliko mazuri yakifanywa katika ratiba ya mapishi ya kila siku.

Ingawa ni jambo la maana kula ifaavyo, hutapunguza uzito usipoutendesha kazi “kirekebisha-joto” cha ubongo wako. Jinsi gani? Kwa kujitia kwa kiasi katika mazoezi ya kukufanya upumue sana kwa karibu dakika 20 angalau mara tatu kwa juma.[30] (1 Timotheo 4:8) Jambo sahili kama kutembea haraka au kupanda ngazi za ghorofa huenda likatosha.[31] Mazoezi hukusaidia uonekane umepunguza mafuta kidogo na mwembamba vizuri hata kama una uzito au mwili wa namna gani.[32] Wakati mazoezi yawashapo lile tanuri la mfumo wa kujenga na kuvunjavunja kemikali mwilini mwako, kalori zachomeka, na mafuta yachomeka. Waweza kurekebisha utendaji wa kemikali za mwili wako kupitia mazoezi. Waweza kuongeza ukubwa wa misuli yako, na misuli yaweza kuchoma kalori hata ukiwa umelala![33]

Waweza kushinda pigano lako dhidi ya uzito wa kupita kiasi kwa kudumisha jitihada na kupiga moyo konde.c Ni kweli, kupunguza kilo chache hakutatatua matatizo yako yote, lakini huenda ukawa na sura nzuri zaidi na kuhisi vizuri zaidi. Huenda hata ukaanza kuhisi vizuri zaidi juu yako mwenyewe.

[Maelezo ya Chini]

a Karibu asilimia 80 ya vijana wenye mafuta mengi mno hubaki na mafuta mengi mno wakiwa watu wazima.[3]

b Ona “Vijana Huuliza . . . Mbona Mimi Ni Mnene Sana?” katika toleo la Aprili 22, 1994 la Amkeni!

c Watu mmoja-mmoja wenye kasoro zitokanazo na kula huenda wakahitaji msaada wa kitaalamu ili kukabiliana na msononeko wao.

[Picha katika ukurasa wa 21]

Mazoezi na milo yenye usawaziko na ya kujenga ndio ufunguo wa njia salama ya kupunguza uzito

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki