Wakati Ambapo Ukubwa Haufai
“Nguo zangu hazinitoshi tena,” akaomboleza Rosa, mwenye umri wa miaka 35. “Sasa nina uzito wa kilo 86, na sikupata kuwaza kwamba ningekuwa mkubwa jinsi hiyo!”
SI ROSA peke yake anayehangaikia uzito wake unaoongezeka. Katika Marekani, ambapo yeye huishi, karibu thuluthi ya watu wa taifa hilo ni wanene kupita kiasi.a Uwiano wa watu wazima wanene kupita kiasi katika Uingereza ulirudufika kwa miaka kumi. Na katika Japani—ambapo uzito wa kupita kiasi ulikuwa nadra—unene wa kupita kiasi unakuwa jambo la kawaida.
Idadi yenye kuongezeka ya watoto ni wazito zaidi ya wapaswavyo kuwa. Vijana Wamarekani wapatao milioni 4.7 kati ya umri wa miaka 6 na 17 ni wenye uzito wa kupita kiasi sana, huku asilimia 20 ya watoto Wakanada wakiwa wanene kupita kiasi. Katika miaka ya hivi majuzi unene wa kupita kiasi wa utotoni umeongezeka mara tatu katika Singapore.
Katika nchi fulani-fulani, kuwa mkubwa kutokana na kuongeza uzito huonwa kuwa uthibitisho wa ufanisi na afya, hali inayotamaniwa zaidi kuliko umaskini na kutopata lishe ya kutosha. Lakini katika nchi za Magharibi, ambapo chakula chapatikana kwa urahisi, kuongeza uzito kwa kawaida hakuonwi kuwa jambo la kutamaniwa. Kinyume cha hilo, kwa kawaida ni jambo linaloleta hangaiko kubwa. Kwa nini?
“Ingawa watu wengi waamini kwamba unene wa kupita kiasi ni tatizo la jinsi mtu anavyoonekana,” asema Dakt. C. Everett Koop, aliyekuwa ofisa mkuu wa afya wa Marekani, “kwa hakika ni maradhi mabaya sana.” Mtaalamu wa tezindani F. Xavier Pi-Sunyer wa New York, aeleza hivi: “[Kunenepa kwa Wamarekani] kunafanya watu wengi zaidi wawe hatarini mwa kupatwa na ugonjwa wa kisukari, msongo wa juu wa damu, mshtuko wa akili, maradhi ya moyo, na hata aina fulani za kansa.”
Uzito Zaidi, Hatari Zaidi
Fikiria uchunguzi mmoja wa wauguzi wa kike 115,000 wa Marekani, ambao walifuatiwa kwa miaka 16. Uchunguzi huo ulipata kwamba watu wazima waongezapo uzito hata kilo tano hadi nane, hilo hutokeza hatari kubwa zaidi ya maradhi ya moyo. Uchunguzi huu, uliochapishwa katika jarida The New England Journal of Medicine la Septemba 14, 1995, ulionyesha kwamba thuluthi moja ya vifo vya kansa na nusu ya vifo vya maradhi yanayohusiana na moyo vilisababishwa na uzito wa kupita kiasi. Kulingana na ripoti moja katika jarida The Journal of the American Medical Association (JAMA) la Mei 22/29, 1996, “asilimia 78 ya msongo wa juu wa damu katika wanaume na asilimia 65 katika wanawake yaweza moja kwa moja kusababishwa na unene wa kupita kiasi.” Shirika la Kansa la Marekani lasema kwamba wale ambao ni “wazito sana kupita kiasi” (asilimia 40 au zaidi kuliko uzito ufaao) “wamo katika hatari kubwa zaidi ya kupatwa na kansa.”
Lakini si kuongeza tu uzito zaidi ambako ni hatari; kusambazwa kwa mafuta ya mwili pia huathiri hatari ya maradhi. Wale walio na mafuta mengi zaidi kwenye fumbatio kwa hakika wamo hatarini zaidi kuliko wale walio na uzito zaidi katika nyonga na mapaja yao. Mafuta katika eneo la tumbo hushirikishwa na hatari inayoongezeka ya ugonjwa wa kisukari, maradhi ya moyo, kansa ya matiti, na kansa ya mji wa mimba.
Vivyo hivyo, vijana wenye uzito kupita kiasi huugua msongo wa juu wa damu, viwango vya juu vya kolesteroli, na dalili za mapema za ugonjwa wa kisukari. Na mara nyingi huja kuwa watu wazima wanene kupita kiasi. Gazeti The New York Times, likitumia habari iliyochapishwa katika jarida la kitiba la Uingereza The Lancet, liliripoti kwamba “watu waliokuwa wanene walipokuwa watoto walikufa mapema zaidi na waliugua maradhi mengi zaidi wakiwa katika miaka ya uchanga kuliko watu wote kwa ujumla.”
Miongozo Mipya ya Uzito
Serikali ya Marekani, ikiwa imesadikishwa kuhusu tatizo zito la uzito, ilikaza zaidi miongozo ya uzito iliyopendekezwa katika 1995. (Ona sanduku kwenye ukurasa ufuatao.) Miongozo iliyorekebishwa hutambulisha “uzito ufaao kiafya,” “uzito wa kupita kiasi kidogo,” na “uzito wa kupita kiasi sana.” Miongozo hiyo hutumika kwa wote watu wazima wanaume na wanawake, haidhuru umri wao ni upi.
Miongozo ya 1990 iliandaa nafasi kwa ukuzi wa mwili wa katikati katika umri wa makamo, mara nyingi uitwao mpanuko wa umri wa makamo. Miongozo mipya haiandai nafasi hiyo, kwa kuwa inaonekana kwamba watu wazima hawapaswi kuongeza uzito kwa kuendelea.b Hivyo, mtu ambaye hapo awali alionwa kuwa wa uzito wa kawaida huenda akajipata katika kikundi cha wale wenye uzito wa kupita kiasi. Kwa kielelezo, mtu mwenye kimo cha sentimeta 168 kati ya umri wa miaka 35 na 65 ambaye alikuwa na uzito wa kilo 75 angekuwa katika kiwango cha uzito ufaao kiafya kulingana na miongozo ya 1990. Lakini katika miongozo mipya, yeye angekuwa na uzito wa kupita kiasi wa kilo tano!
Tulikujaje Kuwa Wakubwa Sana?
Vitabia vya urithi vyaweza kuathiri mwelekeo wa mtu wa kuwa mnene kupita kiasi, lakini si hivyo vinavyosababisha kuongezeka kwa uzito katika nchi za Magharibi. Ni jambo jingine linalosababisha tatizo hilo.
Wataalamu wa afya wanakubali kwamba kula mafuta kwaweza kutufanya tuwe wanene. Nyama nyingi na bidhaa za kutokana na maziwa, vitu vya kuokwa, vyakula vya kutayarishwa haraka, vyakula vyepesi, vyakula vilivyokaangwa katika mafuta, michuzi mizito, michuzi rojo, na oili vimejaa mafuta mengi sana, na kuvila kwaweza kusababisha unene wa kupita kiasi. Jinsi gani?
Kula kalori nyingi katika chakula kuliko zitumiwazo na mwili wetu hufanya tuongeze uzito. Mafuta yana kalori tisa kwa gramu moja, zikilinganishwa na kalori nne katika gramu moja ya protini au gramu ya kabohaidreti. Kwa hiyo tunapata kalori nyingi zaidi tunapokula mafuta. Lakini kuna jambo jingine kuu—jinsi ambavyo mwili wa kibinadamu hutumia nishati inayoandaliwa na kabohaidreti, protini, na mafuta. Mwili hutumia kabohaidreti na protini kwanza, kisha mafuta. Kalori za mafuta ambazo hazikutumiwa hugeuzwa kuwa shahamu. Kwa hiyo kupunguza vyakula vyenye mafuta mengi ni njia muhimu ya kupunguza uzito.
Hata hivyo, wengine wanaoamini kwamba wamepunguza ulaji wao wa mafuta hupata kwamba bado miili yao inanenepa. Kwa nini? Sababu moja ni kwamba wanakula chakula kingi. Mtaalamu fulani wa lishe katika Marekani asema: “Sisi hula kupita kiasi kwa sababu kunaandaliwa chakula kingi sana. Kinapopatikana, twakila.” Watu pia huelekea kutumia kupita kiasi vyakula visivyo na mafuta mengi au visivyo na mafuta kabisa. Lakini mtaalamu mmoja afanyaye kazi na shirika la kutoa shauri kwa viwanda vya vyakula la Marekani aeleza hivi: “Bidhaa zilizopunguzwa mafuta mara nyingi hujazilia ladha kwa kuongeza kiwango cha sukari [chenye kalori nyingi mno].” Hivyo, gazeti The New York Times liliripoti: “Miwili ya mielekeo ya miaka ya 1990—kupata kingi kadiri iwezekanavyo kwa fedha zinazotumiwa na kula vyakula visivyo na mafuta mengi, au visivyo na mafuta kabisa—imeleta ulafi,” hivyo ikiongoza kwenye kuongeza uzito.
Mtindo-maisha wa kukaa-kaa pia huendeleza kuongeza uzito. Uchunguzi mmoja katika Uingereza ulipata kwamba zaidi ya thuluthi ya watu wazima katika nchi hiyo hufanya mazoezi ya chini ya dakika 20 kila juma. Wasiozidi nusu hujihusisha katika michezo yenye utendaji mwingi. Usafiri wa gari umechukua mahali pa kutembea katika nchi nyingi za Magharibi, na ongezeko la kutazama televisheni hutia moyo uvivu na ulafi. Katika Marekani, watoto huketi na kutazama televisheni kwa saa zilizokadiriwa kuwa 26 kila juma, bila kutaja wakati uliotumiwa katika michezo ya vidio. Wakati huohuo, ni asilimia 36 tu ya shule ambazo bado zina somo la mazoezi ya mwili.
Pia kuna sababu za kisaikolojia za kuwa na uzito wa kupita kiasi. “Twala kutokana na mahitaji ya kihisia-moyo,” asema Dakt. Lawrence Cheskin, wa Johns Hopkins Weight Management Center. “Twala tunapokuwa na furaha, twala tunapokuwa na huzuni. Tumekua tukiamini kwamba chakula ni kibadala cha mambo mengine mengi.”
Je, Twaweza Kufanikiwa?
Masuala ya kuwa na uzito wa kupita kiasi yana utata. Kila mwaka Wamarekani wakadiriwao kuwa milioni 80 hufuata utaratibu maalumu wa chakula ili kupunguza unene. Lakini karibu wote hurudia njia yao ya zamani ya kula mara tu baada ya kupunguza uzito fulani. Kwa kipindi cha miaka mitano, asilimia 95 hurudisha uzito waliopunguza.
Kinachohitajiwa ili kupunguza uzito na kutouongeza ni mabadiliko ya mtindo-maisha. Mabadiliko hayo huhitaji jitihada na uwajibikaji, pamoja na msaada kutoka kwa familia na marafiki. Katika visa fulani msaada wa wataalamu wa afya huenda ukahitajiwa pia.c Hata hivyo, ili jitihada zako zifaulu, kichocheo chanya ni jambo la lazima. Ni vyema kujiuliza, ‘Kwa nini nataka kupunguza uzito?’ Jitihada zako za kupunguza uzito zitaelekea zaidi kufaulu ikiwa tamaa ya kuepuka hatari za afya zinaambatana na tamaa ya kuhisi vizuri na kuonekana vizuri na kuboresha ubora wa maisha yako.
Waweza kula chakula kingi kitamu na chenye kutosheleza ambacho kina lishe na vilevile kisicho na kalori nyingi. Lakini kabla ya kuzungumzia chakula kiwezacho kukusaidia kupunguza uzito, acheni tuchunguze jinsi sehemu nyingine za ulaji ziwezavyo kuwa hatari za afya.
[Maelezo ya Chini]
a Unene wa kupita kiasi mara nyingi hufafanuliwa kuwa asilimia 20 au zaidi kupita uzito unaoaminiwa kuwa ufaao.
b Miongozo ya 1995 hutumika kwa vikundi vingi vya umri lakini si vyote. “Kuna mwafaka wa jumla kwamba miongozo mipya ya uzito yaelekea haitumiki kwa watu walio na umri wa zaidi ya miaka 65,” asema Dakt. Robert M. Russell katika jarida JAMA la Juni 19, 1996. “Uzito wa kupita kiasi kidogo tu katika mtu mwenye umri mkubwa zaidi waweza hata kunufaisha kwa kuandaa hifadhi ya nishati kwa vipindi vya ugonjwa na kwa kusaidia kuhifadhi misuli na tishu za mifupa.”
c Kwa madokezo ya kupunguza uzito, ona Amkeni! la Mei 8, 1994, ukurasa wa 20-22; Januari 22, 1993, ukurasa wa 12-14; na Mei 8, 1990, ukurasa wa 3-12.
[Chati katika ukurasa wa 6]
Je, wewe uko katika sehemu ya “uzito ufaao kiafya,” “uzito wa kupita kiasi kidogo,” au “uzito wa kupita kiasi sana?” Grafu iliyoonyeshwa hapa itakusaidia kujibu swali hilo
Miongozo ya Uzito ya 1995 kwa Wanaume na Vilevile Wanawake
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
Kimo *
cm 198
190
180
170
160
150
kg 30 40 50 60 70 80 90 100 110
Uzito†
Takwimu zategemea: U.S. Department of Agriculture, U.S. Department of Health and Human Services
*Bila viatu.
†Bila nguo. Uzito wa juu zaidi watumika kwa watu walio na misuli na mifupa zaidi, kama ilivyo na wanaume wengi.