Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g94 4/22 kur. 17-19
  • Mbona Mimi Ni Mnene Sana?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Mbona Mimi Ni Mnene Sana?
  • Amkeni!—1994
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Kichaa cha Kuwa Mwembamba
  • Ni Nani Asemaye Kwamba Wewe Ni Mnene?
  • Mbona Naonekana Hivi?
  • Kuridhika na Mwili Wako
  • Wakati Ambapo Ukubwa Haufai
    Amkeni!—1997
  • Nifanye Nini Ikiwa Sipendi Umbo Langu?
    Maswali Ambayo Vijana Huuliza—Majibu Yafanyayo Kazi, Buku la 2
  • Kwa Nini Mimi Ni Mwembamba Sana?
    Amkeni!—2000
  • Naweza Kupunguzaje Uzito?
    Amkeni!—1994
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1994
g94 4/22 kur. 17-19

Vijana Huuliza. . .

Mbona Mimi Ni Mnene Sana?

“Nahisi mimi ni mnene sana, lakini nikiangalia chati za kuonyesha uzito ufaao, hazionyeshi kwamba mimi ni mnene kupita kiasi.”—Patti.[1]

“Kuwa mnene . . . kwashusha sana staha yako. Nimekuwa mzito kupita kiasi tangu darasa la nne . . . Ndipo nilipoanza kubandikwa majina.”—Judd.[2]

UZITO. Hilo ni jambo linalosumbua sana vijana fulani, hasa wasichana. Kikundi kimoja cha wasichana wa kwenda shule kilipohojiwa, asilimia 58 kati yao walijiona kuwa wanene.[3]

Kulingana na uchunguzi mmoja wa U.S., asilimia 34 ya wasichana matineja walio wazito kupita kiasi wamemeza tembe za kuwafanya wapoteze uzito. Karibu 1 kati ya kila 4 ameamua kutapika chakula![4] Kitabu The New Teenage Body Book chasema hivi katika kuripoti uchunguzi mwingine: “Kwa kushangaza, karibu nusu ya watoto wenye umri wa miaka tisa na karibu asilimia 80 ya watoto wenye umri wa miaka kumi na miaka kumi na mmoja walikuwa wakipunguza ulaji wao. Asilimia ipatayo 70 ya wasichana wenye umri wa miaka kumi na mbili hadi miaka kumi na sita walikuwa wakijaribu kupoteza uzito—na asilimia 90 ya wale wenye umri wa miaka kumi na saba walikuwa wakipunguza ulaji wao ili wapoteze uzito.”[5]

Kichaa cha Kuwa Mwembamba

Kwa karne nyingi, umbo nene kidogo lilionwa kuwa zuri kwa wanaume na wanawake. Lakini katika miaka ya 1920 watengenezaji wa mitindo ya mavazi wa U.S. walifanya mabadiliko kadhaa. Kwa ghafula umbo jembamba likaja kupendwa.[6] Miongo kadhaa baadaye, umbo jembamba bado linapendwa sana. Televisheni na magazeti yamesaidia kuendeleza maoni hayo kwa matangazo yayo ya ujanja ya biashara yenye kuonyesha wanaume na wanawake wembamba wakitumiwa wakiwa violezo. Watangazaji hao hawajali kwamba violezo hao wembamba wanakaribia kufa njaa![7] Mamilioni ya vijana (na watu wazima) wamedanganywa waamini kwamba urembo watokana na kuwa mwembamba. Basi, si ajabu kwamba kwa kawaida vijana ambao si wembamba sana hujiona kuwa wanene na wasiovutia.

Mikazo kutoka kwa marika haisaidii pia. Mara nyingi vijana walio wazito kupita kiasi hufanyiwa mizaha, hudhihakiwa, na kubaguliwa nyakati zote, jambo linalotokeza kile ambacho mwandikaji mmoja alikieleza kuwa “uchungu mwingi wa kiakili”—uchungu uwezao kudumu mpaka umri mkubwa.[8]

Ni Nani Asemaye Kwamba Wewe Ni Mnene?

Kwa uzuri, suala la kama wewe kwa kweli ni mzito kupita kiasi au sivyo latia ndani mambo mengi zaidi ya jinsi uonekanavyo—angalau kwa maoni ya kitiba. Kwa kawaida madaktari husema mtu ni mnene kupita kiasi kama ana uzito wa asilimia 20 zaidi ya uzito apaswao kuwa nao.[9] Hata hivyo, chati za kawaida za kimo na uzito huonyesha wastani wa uzito, na zaweza kukupa wazo tu la uzito ambao mtu mwenye afya nzuri apaswa kuwa nao. Kwa hiyo, madaktari fulani hupendelea kupima unene wa mtu kwa kutazama mafuta ya ziada mwilini na si uzito pekee. Kulingana na A Parent’s Guide to Eating Disorders and Obesity, “mafuta yapaswa yawe asilimia 20 hadi 27 ya mwili katika wanawake na asilimia 15 hadi 22 katika wanaume.”[10]

Baadhi ya watafiti waamini kwamba ni vijana wachache tu ambao kwa kweli ni wazito kupita kiasi.[11] Tukiangalia mambo kiafya, huenda kusiwe na sababu yoyote kwako kupoteza uzito. Katika uchunguzi uliotajwa hapo mwanzoni, zaidi ya nusu ya wasichana waliohojiwa walijiona kuwa wazito kupita kiasi, lakini ni asilimia 15 tu kati yao ambao kwa kweli walikuwa hivyo.[12]

Mbona Naonekana Hivi?

Labda hutafarijika sana ujitazamapo kwenye kioo kwa sababu huenda usiwe tu na umbo uwezalo kuona kuwa la kuvutia. Msichana mmoja tineja alilalamika hivi: “Ningependa nipoteze uzito, niwe mrefu zaidi, na kuwa na umbo lenye kuvutia zaidi.”[14]

Lakini kumbuka kwamba kwa sababu wewe ni tineja, mwili wako unabadilika upesi. “Kwa kawaida, wasichana na wavulana huongeza uzito wakifikia umri wa kubalehe,” aeleza Dakt. Iris Litt. “Na ingawa wavulana huongeza hasa misuli, wasichana huongeza mafuta. Wakifikia umri wa ubalehe, msichana huongeza mafuta ya mwili kutoka asilimia ipatayo nane—wastani wa watoto wa jinsia zote—hadi karibu asilimia 22 ya mafuta ya mwili. Kwa wakati uo huo, mabadiliko ya mifupa huongeza uzito kwa wasichana. Wavulana hupanuka mabega, huku wasichana wakipanuka nyonga.”[15] Mabadiliko hayo huchukua muda. Lakini msichana mnene mwenye miaka 11 au 12 aweza kutoka kwenye umri wa ubalehe akiwa tineja mwenye umbo la kuvutia.[16] Na huenda vilevile asiwe na umbo zuri hivyo.

Ikiwa imekuwa hivyo kwako, huenda jambo hilo limesababishwa kwa sehemu fulani na chembe za urithi ulizorithi kutoka kwa wazazi wako. Madaktari fulani waamini kwamba pamoja na rangi ya ngozi yako, muundo wa nywele, na kimo, umbo la msingi la mwili wako ‘liliandikwa,’ kama mtunga-zaburi alivyoandika, katika chembe za urithi wakati wa kutungwa mimba. (Zaburi 139:16) Dakt. Lawrence Lamb, akitaja jambo hilohilo ambalo mtunga-zaburi alivuviwa kuandika, asema hivi katika kitabu chake The Weighting Game: “Ulizaliwa ukiwa na kanuni za urithi zinazoonyesha unapaswa kuwa na uzito gani, na unapaswa kuwa na mafuta kiasi gani, katika hatua mbalimbali za maisha yako.”[17]

Uchunguzi umethibitisha kwamba chembe za urithi zina uvutano kwa umbo la mwili. Watoto wa kambo huelekea kuwa na umbo la mwili la wazazi wao halisi, haidhuru wazazi wao wa kambo wawe na umbo gani.[18] Na kwa sababu mapacha huwa na chembe za urithi zinazofanana, haishangazi kwamba mapacha huelekea kuwa na uzito uleule.[19]

Hilo lamaanisha nini kwako? Kwa kielelezo, tuseme kwamba wazazi wako wote ni wanene kupita kiasi. Basi una uwezekano wa asilimia 80 wa kuwa mnene kupita kiasi. Uwezekano huo warudishwa kuwa nusu iwapo ni mzazi mmoja ndiye mnene kupita kiasi.[20] Mazoezi na ulaji wa uangalifu waweza kusaidia kwa kadiri fulani. Lakini kwa sehemu kubwa, kwa kawaida sisi hubaki tukiwa na umbo letu la msingi. Kama una mwili mdogo, basi una asili ya kuwa na mwili mwembamba. Lakini kama chembe zako za urithi zimekupa umbo la mwili mkubwa—kuwa mnene na mwenye mafuta mengi zaidi—basi wewe hukuumbwa uwe mwembamba. Hata uzito wako ukifaa kitiba, utaonekana kuwa mzito kuliko upendavyo.[21]

Kuridhika na Mwili Wako

Lavunja moyo? Labda. Lakini habari njema ni kwamba Yehova Mungu aliumba mume na mke wa kwanza, Adamu na Hawa, wakiwa na umbo kamilifu. Hata ingawa walikuja kupoteza ukamilifu na kupitishia wazao wao kutokamilika, Mungu atahakikisha kwamba upungufu wowote wa kimwili uliorithiwa utarekebishwa katika ulimwengu wake mpya wenye uadilifu.—Ayubu 14:4; Warumi 5:12; 2 Petro 3:13.[22]

Kumbuka kwamba viwango vya urembo huenda vikatokana na jamii na mapendezi ya kibinafsi. Hivyo, kile kinachoonwa kuwa urembo hutofautiana ulimwenguni kote na chaweza kubadilika baada ya muda. Kwa hiyo mbona uache “ulimwengu ukufinyange ukafanana nao”? (Warumi 12:2, Phillips)[23] Mbona ushindwe na viwango vyao na maoni yao yaliyopotoka?

Kwa kweli hakuna sababu ya wewe kujishusha au kuvunjika moyo eti kwa sababu tu wewe si mwembamba. Mungu hatuhukumu kwa kimo chetu wala kwa umbo letu. “Wanadamu huitazama sura ya nje,” Biblia yasema, “bali BWANA huutazama moyo.” (1 Samweli 16:7) Naam, ni “utu wa moyoni usionekana” ndicho kitu cha maana kwa Mungu—bali si ukubwa wa nyonga au udogo wa kiuno. (1 Petro 3:4) Na kama wewe ni mchangamfu, mwenye upole, mkarimu, na mwenye kuhangaikia wengine, kwa kawaida watu watavutiwa nawe.

Hatusemi kwamba hakuna jambo lolote uwezalo kufanya ili umbo lako liwe bora zaidi. Lakini kama umbo lako halikufurahishi sana, si lazima utese mwili wako kwa kukataa kula. Labda wahitaji tu kuwa mwangalifu zaidi kwa mitindo na rangi ya mavazi yako, ukichagua mavazi na rangi zinazositiri yale unayoona kuwa ni upungufu na yanayokazia mambo mazuri ya mwili mwako.[24]

Lakini, bado huenda ukahisi kwamba yafaa upunguze uzito kidogo tu. Au huenda ukawa na tatizo halisi ya kuwa mnene kupita kiasi na yafaa upoteze uzito kwa sababu za kiafya bali si kwamba uonekane vizuri zaidi. Jinsi uwezavyo kufanya hivyo kwa mafanikio itazungumziwa katika makala yetu inayofuata.

[Sanduku katika ukurasa wa 19]

“Mimi ni Mwembamba Mno”

Si vijana wote wanaokubali kwamba kuwa mwembamba kunavutia. “Mimi ni kijana mwenye miaka 15 ambaye ni mwembamba na anayefanyiwa mzaha nyakati zote,” alalamika Mark.[25] Kwa kawaida kuwa mwembamba huwa ni tokeo la ziada tu la kubalehe. Mwili unaokua hutumia kalori nyingi sana. Huenda kijana asianze kujaza nafasi hizo mpaka ule ukuzi wa haraka ukome.[26] Chembe za urithi huwa na fungu la kutimiza pia.[27] Bila shaka, ugonjwa au kutosawazika kwa hormoni kwaweza pia kufanya mmoja awe mwembamba kupita kiasi, na ni vizuri kumwendea daktari katika hali kama hizo.[28] Ni vizuri pia vijana kutafuta msaada wa kitiba ikiwa hawali kwa sababu wameshuka moyo ama kama wanaugua kutokana na tatizo zito la ulaji, kama vile anorexia nervosa.[29]

Haidhuru hali yako, kama unafikiri wewe ni mwembamba kupita kiasi, tafuta shauri la daktari. Huenda ikawa tu kwamba ni lazima ujifunze kukubali—na labda hata kujifunza kupenda—umbo lako.

[Picha katika ukurasa wa 18]

Wengi hudhani kwamba wao ni wanene kwa sababu hawana umbo kama wale violezo wanaoona katika magazeti ya mitindo ya mavaziy

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki