Aligeta—Adimu, Weupe,na Wenye Macho-Samawati!
TAARIFA ifuatayo iliyotayarishwa na Curt Burnette kwa ajili ya Taasisi ya Audubon yaeleza hadithi ya wale aligeta weupe wa kutazamisha.
“Wale aligeta wenye ngozi nyeupe na macho-samawati ni mgeuko wa ghafula wa yule aligeta wa Marekani wala si jamii tofauti. Huo mgeuko wa ghafula huitwa weuo (kufanyika -eupe), kwa hiyo hawa ni aligeta wa weuo. Wale wa aina ya zeruzeru wana ngozi nyeupe na macho mekundu-meupe-njano. Wanyama wa weuo wana macho yenye urangirangi. Uzeruzeru ni haba lakini weuo ni haba hata zaidi. Ingawa weuo hutokea katika jamii nyingine chache za wanyama, wale aligeta weupe ndio wa kwanza wajulikanao kuwa waligeuka kuwa aligeta wa weuo.
“Kuna aligeta weupe 18, na wote waligunduliwa kwenye eneo la kiota kimoja mwishoni mwa Agosti, 1987. Wavuvi watatu Wakajuni waliwapata karibu na Houma, Louisiana, kusini-magharibi mwa New Orleans. Walikuwa na umri upatao majuma 1-2 wakati wale wa kwanza walipoletwa kwenye Hifadhi ya Wanyama ya Audubon siku ya Septemba 5, 1987. Zaidi ya wale weupe 18, ndugu zao 7 wenye rangi ya kawaida walitekwa, na idadi isiyotambuliwa ya walio wa kawaida wakakimbia. Kiota kilipatikana katika nchi-kavu iliyo milki ya Shirika la Louisiana la Ardhi na Uvinjari (LL&E). Ingawa eneo lenye kiota hicho limekuwa likitupiwa macho na mayai kukusanywa na kuanguliwa, hakuna aligeta zaidi weupe ambao wamepata kugunduliwa.
“Aligeta weupe wote 18 na ndugu zao 7 wa kawaida ni wa kiume. Hiyo yawezekana kwa sababu jinsia ya aligeta huamuliwa na halijoto ya kiota na kwa hiyo wote waweza kuwa wa kiume, wote wa kike, au mchanganyiko. Kufikia wakati wa kuandika habari hii, wale aligeta wanafikia kukomaa viungo vya uzazi (miaka 5-6). Ukubwa wa wale 18 watofautiana kuanzia karibu meta 1.5 na kilo 2.3-2.5 hadi meta 2.4 na kilo 11.4. Hii hutokana na mbinu tofauti-tofauti za usimamizi. Aligeta waliolelewa kwenye shamba la kutunzia aligeta la LL&E hukua upesi zaidi.
“LL&E humiliki 14 kati ya wale aligeta weupe na walifanya neema kuipa 4 Taasisi ya Audubon. Kwa sasa Taasisi hiyo huonyesha 2 kwenye hifadhi yao ya Audubon na 2 kwenye hifadhi yao ya wanyama wa majini iitwayo Hifadhi-Maji ya Mabara ya Marekani. Aligeta wawili huzungushwa kutoka hifadhi moja hadi hifadhi nyingine ya wanyama wa nchi kavu na wa majini kwa kupokezana zamu, na tayari wamekuwa katika hifadhi zaidi ya 12 katika Marekani, na moja katika Japani.
“Wale aligeta weupe wamekuwa maarufu na wenye kufurahiwa kotekote ulimwenguni. Kugunduliwa kwao kulitangazwa ulimwenguni pote na mfumo wa utangazaji-habari wa CNN. Wameonekana mara nyingi katika televisheni kutia na vipindi vya Today Show, Nashville Network, Tonight Show, CBS Morning News, Late Night chenye kuendeshwa na David Letterman, Christian Broadcast Network, MTV, na habari za kigeni na maonyesho ya asubuhi. Makala za nyusipepa na magazeti ulimwenguni pote huongea juu yao pindi kwa pindi. Miaka michache iliyopita gazeti moja la Kifaransa lilikuwa na makala moja na picha zao na halaiki ya watu ilipendezwa sana hata likaendeleza wonyesho wa kufuatisha ule uliotangulia.
“Imekuwaje kwamba kuna aligeta wachache sana weupe na kwamba hakuna mtu aliyekuwa amepata kuona yeyote? Kwanza, zaidi ya wao kuwa ni migeuko haba ya ghafula, aligeta wa weuo na wa uzeruzeru wana utofauti wenye kuonekana wazi uwezao kuwatia katika hatari ya kushambuliwa na aligeta wa kawaida. Wakati aligeta mtoto aanguliwapo, yeye huwa na urefu wa sentimeta 20-25 tu. Mama aligeta hulinda kiota kwa kitambo lakini upesi hao aligeta wadogo huanza kujitegemea. Watoto walioanguliwa wa aligeta wa kawaida huwa wenye milia ya manjano na myeusi na rangi hiyo hulingana vema na mazingira yao. Mtoto aliyeanguliwa mweupe angeonekana na kunaswa kwa urahisi na wanyemeleaji wengi tofauti.
“Mambo mawili ya mwisho yaliyo ya kupendeza na yasiyo ya kawaida juu ya aligeta weupe ni haya: madoa yao meusi na hali ya hasira yao. Ni wachache sana kati ya aligeta weupe walioanguliwa wakiwa na madoa meusi. Walio wengi hawakuwa na yoyote. Hata hivyo, walipozidi kukua, wengi zaidi walianza kusitawisha maeneo fulani meusi. Karibu madoa yote yalisitawi kuzunguka kichwa na shingo tu. Hiyo imefanya iwe rahisi zaidi kutambua mmoja kwa mwingine, ingawa wengine wao hawajapata kamwe madoa yoyote hata kidogo.
“Na mwisho, yakubaliwa na kila mtu ambaye ameshughulika na aligeta weupe kwamba wao ni chapuchapu kwa uchokozi na hasira kuliko aligeta wa kawaida. Hakuna aliye na uhakika kwa nini iko hivyo, lakini wao hutendewa kama kwamba ni mamba wenye mbio na wenye kukasirika upesi badala ya kutendewa kama aligeta wa polepole zaidi na watulivu zaidi. Hilo nalo ni fumbo jingine kati ya mafumbo mengi ya wakazi hao wa kustaajabisha wa mabwawa!”—Na Curt Burnette, Taasisi ya Audubon.[1]
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 16]
Picha: Hifadhi ya Audubon, New Orleans