Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g94 7/8 kur. 17-19
  • Ziara ya Kila Mwaka ya Kasa Majitu Wenye Migongo Minene

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Ziara ya Kila Mwaka ya Kasa Majitu Wenye Migongo Minene
  • Amkeni!—1994
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Ndio Hao Waibuka Baharini!
  • Kuyazika Mayai
  • Jitihada za Kuwahifadhi
  • Mahali Ambapo Binadamu na Kasa Hukutana
    Amkeni!—1993
  • Mfumo wa Kumwongoza Kasa
    Amkeni!—2011
  • Maajabu ya Yai la Mbuni
    Amkeni!—2002
  • Kikono cha Nyangumi Mwenye Nundu
    Amkeni!—2013
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1994
g94 7/8 kur. 17-19

Ziara ya Kila Mwaka ya Kasa Majitu Wenye Migongo Minene

NA MLETA-HABARI ZA AMKENI! KATIKA MALASIA

NI KARIBU usiku-kati. Mwezi mpevu ulio juu angani watokeza umulimuli hafifu wa kidhahabu upande hadi upande wa bahari yenye amani na utulivu. Ufuo ulioko Rantau Abang una vikundi vya watu, baadhi yao wamesimama, wengine wamechuchumaa au kukalia ule mchanga wenye ubaridi mzuri, ulio laini. Wanafanya nini hapa saa hii? Wanaingoja kwa saburi ziara ya gome kubwa lenye mikono minne—yule kasa jitu wa ngozingozi, au kasa wa ngozi nene mgongoni.

Wageni hawa wa kifumbo wakaao katika maji na nchi kavu pia wameleta umaarufu wa kimataifa kwenye ufuo huu uliokuwa ukipuuzwa. Rantau Abang iko kwenye pwani ya mashariki ya Mkono-Bahari wa Malasia, juu kidogo tu kaskazini mwa Dungun na kama kilometa 400 kutoka Singapore. Ni mojapo mahali pachache ulimwenguni ambapo kasa mwenye ngozi nene mgongoni huzuru kila mwaka kwa usafiri wenye taadhima.

Hapa yale majira ya kutaga mayai huendelea kuanzia Mei hadi Septemba hivi. Wakati wa miezi ya kilele ya Juni, Julai, na Agosti, ni rahisi sana kuona zile hatua za kutaga mayai. Kwa kawaida kasa huanza kuibuka baada ya giza kuingia. Je! wageni hawa wa kutoka sehemu zote za Malasia, Singapore, na Magharibi watakuwa wamengojea bure tu?

Ndio Hao Waibuka Baharini!

Kwa ghafula, kivuli cha umbo fulani chaonekana kikitokeatokea na kuzama katika yale maji maangavu, si mbali sana na ufuo. Umati wasisimuka! Kitu hicho kizidipo kukaribia ufuo, dude lenye umbo la kuba laanza kuibuka kutoka majini. Lo, ni kasa huyo akija ufuoni! Waongozi wachache waliopo watahadharisha watu wote watazame kwa unyamavu kadiri iwezekanavyo, ile kelele isije ikamwogopesha aende zake.

Kwanza kichwa chatokea, halafu shingo, ikifuatwa na sehemu ya mbele ya lile gome na ile mikono ya mbele, mpaka mwishowe kasa mzima afichuka ufuoni. Mwinuko mwanana wa maji wapita juu ya mkia wake na mikono ya nyuma. Lo, kweli hilo ni jitu, karibu meta mbili au zaidi kutoka puani hadi ncha ya mkia! Lifikapo hapo ufuoni lalala tuli.

Kwa haraka sana, kasa huyo ajiinua kwa mikono ya mbele na kutupa mwili wake mbele, na kupiga chini mbuu. Alala tuli kwa muda, kama kwamba arudiwe na pumzi na nguvu za kujiinua tena na kujitupa. Hivi ndivyo yeye husogeasogea katika nchi kavu. Umati pande zote mbili za kasa huyo wazuiliwa umbali fulani. Waongozi hujali sana jambo hili. Kila mara kasa huyo asogeapo mbele, umati wasonga mbele pia—lakini kwa unyamavu sana.

Yule kasa mwenye ngozi nene mgongoni achechemeapo kuupanda ufuo, ajua aendako kisilika. Ujuzi wake uliopangwa kisilika humwezesha kupata mahali ambapo mayai yake yatapata fursa kamili ya kuanguliwa kwa mafanikio. Hapo yeye aanza kuchimba shimo. Ile mikono ya nyuma yawa koleo za kuchimbia, ikichota mchanga.

Baada ya muda ambao waonekana kuwa mrefu, mmoja wa wale waongozi, ambaye ana leseni ya kukusanya mayai pia, ajitokeza mbele na kunyoosha mkono wake kuuingiza ndani ya lile shimo, ambalo lina kina kirefu sana hivi kwamba kiko cha mkono wake chapotelea ndani. Autoapo mkono wake shimoni, kila mtu atusha pumzi kwa mshangao na msisimko. Achomoa yai moja!

Yai la kasa mwenye ngozi nene mgongoni ni la rangi ya weupe hafifu. Ukubwa walo ni kuanzia ule wa mpira mdogo wa tenisi ya mezani hadi ule wa mpira wa tenisi ya kiwanjani. Kwa kawaida mayai machache ya mwisho katika kiota huwa ya ukubwa wa gololi tu. Tofauti na mayai ya ndege wa kufugwa, kwa kweli lile gome ni ngozi ngumu ambayo hubonyea kwa urahisi ifinywapo. Ajabu ni kwamba, ute wa yai hubaki ukiwa majimaji hata ukiisha kupikwa. Yasemwa kwamba ladha yao ni kali kidogo na ya kisamaki hivi. Kasa hutaga wastani wa karibu mayai 85 kwa safari moja. Lakini kiota chenye rekodi ya mayai 140 kiliripotiwa katika 1967.

Sasa umati waruhusiwa kutembea-tembea kwa uhuru. Baadhi wamgusa na kumchunguza kasa kwa woga. Wengine wampanda juu au kumwegemea ili wapigwe picha waziweke katika vitabu vya picha za familia. Kuchunguza kasa huyo kwa karibu kwafunua kwamba ute mzito wenye kupenywa na nuru kidogo tu watonatona kutoka machoni, ukiwa na punjepunje za mchanga. Yasemwa kwamba lile badiliko la kutoka majini kuja hewani ndilo husababisha jambo hili. Mara kwa mara, yule kasa afungua kinywa chake kupumua kwa mvumo wa hewa inayopulizwa.

Kuyazika Mayai

Baada ya muda mwingi, yule kiumbe aanza kusogeza mikono yake ya nyuma kuusukuma mchanga urudi ndani ya shimo. Mara tu lile shimo liishapo kujazwa, huyo kasa mwenye ngozi nene mgongoni arusha mikono yake kama vipangusa-kioo vya gari. Mchanga warushwa pande zote! Ule umati warudi nyuma haraka kulinda nyuso na miili yao. Ile mikono yaendelea kurushwa-rushwa kwa muda fulani. Lo, ni siha na nguvu iliyoje inayotumiwa! Mikono isimamapo hatimaye, umati hauwezi kuona hata dalili moja ya shimo ambalo yule kasa mwenye ngozi nene mgongoni alichimba. Kweli hiyo ni hekima ya kisilika! Lakini Muumba wa kasa huyu ni mwenye hekima kubwa kama nini isiyo na mipaka!

Kabla huyo kasa mwenye ngozi nene mgongoni hajarudi baharini, mtu mwenye leseni ya kukusanya mayai afunga ukanda kwenye mmojapo mikono yake ya mbele. Jambo hili hufanywa ili ziara zake zifuatazo za kuja nchi kavu na kuenenda katika zile bahari pana ziweze kufuatiliwa vizuri. Kila majira kasa huyo hufanya kiota kuanzia mara sita hadi tisa, kukiwa na muda wa katikati wa siku 9 hadi 14 kutoka kipindi kimoja hadi kingine cha kufanya kiota.

Kwa ghafula yule kasa mwenye ngozi nene mgongoni ajivuta kwa nguvu na kujirusha mbele. Ageuka na kurudi akielekea baharini, akichechea kwa mwendo wa haraka kuliko vile alivyowasili. Agusapo maji, kichwa chaingia ndani, halafu lile gome. Mwishowe atoweka. Wakati kichwa kitokezapo majini hatimaye, kasa huyo yuko mbali. Akata maji mbiombio kwenda kwenye bahari pana, huku mwanga wa mwezi ukimulika ncha ya juu ya pua yake. Lo, yeye ni mwepesi na chapuchapu kama nini akiwa ndani ya maji! Ni tofauti sana na mwendo wake wa chopichopi na wa polepole akiwa katika nchi kavu.

Jitihada za Kuwahifadhi

Kama vile ilivyo kwa habari ya idadi zinazoongezeka za namna nyinginezo za wanyama, kasa wa ngozi nene mgongoni watiwa hatarini na madhara ya kuchafuliwa kwa mazingira na pupa ya kibinadamu. Katika miaka ya 1970, mamia ya kasa wasiokomaa kikamili walipatikana wamefagiwa na maji wakaletwa ufuoni katika mkoa jirani wa Pahang—wakiwa wamekufa! Na mayai ya kasa hao hukusanywa ovyoovyo ili kutosheleza uchu wa watu wa kula vitu vigeni.

Tukio zuri kwa kasa hawa ni kwamba, hangaiko kubwa katika Malasia kuhusu kupungua kwa idadi yao lilisababisha kupitishwa kwa Sheria ya Kulinda Kasa katika 1951. Kukusanya mayai kibinafsi kuliharamishwa. Hata hivyo, watu mmoja-mmoja wenye uroho wa fedha hukaidi sheria hii, wakishawishwa mno na faida watakayopata. Hata hivyo, jitihada za kuwahifadhi hazijawa za bure.

Ni shangwe kuona safu za vibango vidogo sana vikiwa vimechomekwa mchangani katika ufuo wa Rantau Abang. Kila moja ni alama ya mahali palipozikwa kifungu kidogo cha mayai ya kasa mwenye ngozi nene mgongoni. Kibango hicho huonyesha hesabu ya mayai, tarehe ya kufukiwa humo, na tarakimu ya kutambulisha kiota cha awali cha mayai. Karibu siku 45 baada ya kutagwa, wavu wa waya huzungushwa kwenye kila kibango kuwazuia waanguliwa wasiponyoke. Kipindi cha kuatamia mayai ni kuanzia siku 52 hadi 61. Waanguliwa waibukapo, kwa kawaida ikiwa ni jioni baada ya jua kushuka, idadi ya kutoka katika kila shimo huandikwa. Halafu wao hutiwa katika viwekeo na baadaye huachiliwa huru kwenye ukingo wa bahari.

Programu ya kuwahifadhi imefanikiwa kutokeza maelfu mengi ya waanguliwa na kuwarudisha kwenye kao lao la majini. Lakini uwezo wao mdogo wa kuokoka, na pia hesabu inayopungua ya kasa wenye ngozi nene mgongoni wanaokuja Rantau Abang, yaendelea kuhangaisha.

[Picha katika ukurasa wa 18]

Kasa mwenye ngozi nene mgongoni, aliye na urefu wameta 1.8 kutoka kichwani hadi mkiani, hutaga mayai mengi sana. Karibu majuma manane baadaye, vitoto hutokea

[Hisani]

Kasa wa kingozi. Lydekker

C. Allen Morgan/Peter Arnold

David Harvey/SUPERSTOCK

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 17]

C. Allen Morgan/ Peter Arnold

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki