Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g93 3/22 kur. 25-27
  • Mahali Ambapo Binadamu na Kasa Hukutana

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Mahali Ambapo Binadamu na Kasa Hukutana
  • Amkeni!—1993
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Kuwaona kwa Mara ya Kwanza
  • Kuwatia Kasa Alama
  • Kuyahamisha Mayai
  • Ni Lazima Binadamu Ajifunze Kujali
  • Mfumo wa Kumwongoza Kasa
    Amkeni!—2011
  • Ziara ya Kila Mwaka ya Kasa Majitu Wenye Migongo Minene
    Amkeni!—1994
  • Maajabu ya Mchanga
    Amkeni!—2003
  • Kuutazama Ulimwengu
    Amkeni!—1997
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1993
g93 3/22 kur. 25-27

Mahali Ambapo Binadamu na Kasa Hukutana

Na mleta habari za Amkeni! kutoka Australia

WAKATI bora zaidi wa kukutana na kasa wa baharini asiyefugwa ni wakati anapotaga mayai katika kiota chake kipya kwenye mchanga. Kwa hiyo je, ungependa kuja nami tunapozuru Mon Repos—ufuo wenye umbali wa kilomita 1.5 kwenye pwani ya Queensland, nchi yenye jua ya Australia? Usihangaike kwamba utasumbuliwa na jua linalochoma la nusu-tropiki, kwa kuwa ziara yetu itakuwa ya usiku. Wakati bora zaidi wa ziara fupi hiyo yenye kusisimua ni kati ya saa mbili usiku na usiku wa manane.

Inapendekezwa kwenda na kiongozi stadi na kikundi kidogo, kwa kuwa kuna mambo kadha ya kufanya na yale yasiyopaswa kufanywa ikiwa tutamwona na kumgusa kasa mkubwa wa kike. Tunapotembea kando ya ufuo juu ya mahali ambapo maji hujaa, kiongozi atuomba tuzime tochi zetu kwa sababu mwangaza huwashtua kasa. Na tunashangaa jinsi tunavyoweza kuona vizuri alama za kasa zenye upana wa mita moja kwenye mchanga hata bila mianga.

Kisha, kiongozi wetu atufahamisha juu ya mambo ya kuvutia kuhusu kasa wa baharini katika eneo hilo. Kuna aina sita tofauti katika bahari ya Australia, lakini ni aina nne tu wanaopatikana hapa katika Mon Repos, ambayo ni eneo kuu la kutaga mayai katika pwani ya Bundaberg. Wakipangwa kwa utaratibu wa wale wanaopatikana kwa wingi, aina hiyo nne ni: kasa wagomvi (Caretta caretta), kasa mgongotambarare (Natator depressa), kasa kijani-kibichi (Chelonia mydas), na kasa mgongongozi (Dermochelys coriacea).

Kuwaona kwa Mara ya Kwanza

Tunasisimka sana tunapomwona kasa mkubwa. Ni wa aina ile ya kwanza tulioorodhesha—kasa mgomvi. Tunatazama kwa ukimya huku akiendelea kutambaa kutoka majini hadi juu ya mahali maji-kujaa hufikia kwenye mchanga. Hatimaye tunaposonga karibu, tunaona kwamba amechimba shimo lenye umbo la kisahani kwa kukwaruza mchanga na mimea na kuisuku-ma kando yake. Hilo huzuia nyasi isikue juu ya kiota chake na kufungia vitoto vinapoangua katika majuma 7 hadi 12. Pia amemaliza kuchimba kiota cha umbo la pera kwa kufukua na kusukuma mchanga kwa vikono vyake vya nyuma—fukua kulia, sukuma kushoto; fukua kushoto, sukuma kulia. Yote hayo huchukua dakika kama 45.

Hadi kufikia sasa, angeliweza kushtuliwa kwa urahisi na kurudi majini, lakini aanzapo kutaga mayai, tunaruhusiwa kumgusa. Kiongozi anammulika, nasi twaweza kumpiga picha ikiwa twataka. Yule kasa aendelea kutaga mayai kwenye kiota kwa dakika 10 hadi 20, yakiwa na umajimaji mweupe ulio kama makamasi unaolinda mayai yasiharibiwe na uyoga na wadudu yanapongoja kuangua. Kasa wagomvi hutaga mayai 120 kwa wastani yenye ukubwa wa milimita 38 kwa kipenyo kwa kikundi cha mayai—kila siku 14 mara kadha kwa kipindi—kukiwa na miaka miwili hadi minne kati ya vipindi.

Tunapomgusa kasa kihalisi, tunashangaa jinsi ngozi yake ilivyo nyororo—jambo linalofanya ngozi ya kasa itamanike sana na huhatarisha kuwako kwa kasa. Gamba au kombe lake limefanyizwa kwa mabamba na linalingana na uti wa mgongo na mbavu. Sasa aanza kufunika mayai yake. Lakini kwa kuwa ameyataga karibu na mahali maji-kujaa hufika, ni lazima yahamishwe ikiwa yataokoka. Hilo litafanywa na washi-riki wawili wa kikundi cha utafiti waliojiunga na kikundi chetu.

Kuwatia Kasa Alama

Kasa wetu atatiwa alama kwenye kimojapo kikono chake cha mbele ili kusaidia katika utafiti wa kasa wa baharini. Hiyo si kazi rahisi kwa kufikiria mchanga wote anaotupatupa kila mahali. Alama hizo zimefanyizwa kwa mchanganyiko wa madini ya titani isiyopata kutu. Upande wa nyuma mna anwani, na ni jambo la maana kwa mradi wa utafiti kwamba kasa wote walioonwa waripotiwe kwa hesabu. Ni wakati tu kasa anapokufa ndipo ile alama inaondolewa na kurudishwa, pamoja na habari nyingi kuhusu mahali anapopatikana. Upande wa mbele wa alama hiyo ni nambari ya utambulisho wa kasa huyo. Kasa wetu ni T54239, lakini tunaamua kumwita Tabitha.

Kwa sababu Tabitha hajapata kutiwa alama, inaelekea kwamba hajapata kutega mayai kamwe na hivyo angeweza kuandaa habari ya maana ya kusaidia kuimarisha ulinzi wa kasa na mayai yao katika Pasifiki Kusini. Sasa, ili kupata habari hiyo, tunashuhudia upasuaji mdogo wa kasa papo hapo ufuoni! Utaratibu huo huitwa laparoskopi na hutumiwa katika kupasua wanadamu pia. Tabitha anapinduliwa polepole na kuwekelewa juu ya wilibaro. Tunamsikitikia na tunapata kwamba kumpapasa kooni kwaonekana kwamtuliza. Hayo si machozi tunayoona, bali ni mchanganyiko wa chumvi anaotoa ili kuondoa mchanga machoni pake na kuondolea mbali chumvi ya ziada anayopata kwa kunywa maji ya bahari. Hayamaanishi anaona uchungu. Ngozi yake inapanguswa juu ya kikono chake cha chini; kisha mpira unatiwa ndani kupitia sehemu ndogo iliyokatwa, na hewa kidogo inapulizwa ndani. Kwa kutazama mbegu zake, watafiti wanagundua kwamba hiki ni kipindi chake cha kwanza cha uzalishaji, na ana mayai mengine mengi yanayostawi. Habari hiyo yote inarekodiwa; kisha hewa inaondolewa kupitia kilango kwenye mpira, na sehemu iliyokatwa inashonwa.

Baada ya kugeuzwa tena kwenye mchanga, Tabitha aanza kuelekea majini kisilika. Mawimbi yamfunika Tabitha na kumchukua ndani baharini kwa kitulizo chake.

Kuyahamisha Mayai

Tunaporudi, tunaona kwamba tayari mayai yameondolewa kwenye kiota. Baada ya muda wa saa nne, yai hujishikiza kwenye sehemu ya ndani ya gamba na kufanyiza chembe za damu. Ikiwa yatageuzwa baada ya hilo, yataharibika. Kwenye sehemu ya kutagia mayai, mara nyingi muda wa saa mbili huruhusiwa kwa ajili ya kuyahamisha, na kiasi cha kufanikiwa katika kuyahamisha ni kikubwa sana. Kusudi la hilo ni kulinda kiota na mayai kutoka kwa maji na mmomonyoko. Hali-joto ya mchanga huamua jinsia ya vitoto. Visiwa vingi vina michanga yenye ubaridi kidogo na sanasana hutokeza wa kiume, hali michanga yenye joto zaidi ya Mon Repos sanasana hutokeza wa kike.

Vitoto huangua kuanzia Januari hadi Machi. Hivyo hukwaruza paa lavyo la mchanga, vikisababisha mchanga kuanguka na kuwainua juu zaidi. Ikiwa hali-joto ya mchanga si ya juu sana, wao huendelea na safari yao nje ya kiota na kuelekea baharini. Lakini safari yao ndio tu imeanza. Inaaminiwa kwamba huchukua miaka 50 ili kufikia ukomavu wa kuweza kuzaa. Ni asilimia ndogo wanaofikia hapo.

Ni Lazima Binadamu Ajifunze Kujali

Kwa kusikitisha, kutojali na kutofikiri kwa ainabinadamu kunasababisha upungufu wa aina sita ya kasa wa baharini wanaojulikana. Mara nyingi mifuko ya plastiki inayotupwa baharini hufikiriwa kimakosa kuwa yavuyavu na kuliwa na kasa. Hiyo huziba njia za uyeyushaji chakula na kuwafanya wapate njaa hadi kufa. Takataka nyingine zaweza kuwanyonga kasa. Hata majembe ya mashua yaweza kuwa hatari ikiwa nahodha hawi mwangalifu. Kuongezea hayo kuna mivujo ya mafuta na takataka za sumu zinazoweza kuangamiza uhai wote wa pwani wakati wa kipindi cha kuzalisha. Na kwa sababu ni lazima kasa aje juu ya maji kila dakika 15 ili kupata hewa, wavu wa kuvulia samaki unaomnasa kasa waweza kumfanya afe maji.

Kadiri watu wengi watambuavyo hatari hizo na kujifunza kutunza zaidi mazingira, pasipo shaka fursa zaidi zitajitokeza ili binadamu na kasa wakutane—kukimvutia na kumsisimua ainabinadamu kwa aina nyingine bado ya maajabu ya mzunguko wa kuzaa wenye kustaajabisha wa muumba.

[Picha katika ukurasa wa 26]

Juu kushoto kwenda kulia: upasuaji mdogo, kurudi baharini, mayai yakihamishwa, kikono kikitiwa alama

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki