Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g93 3/22 kur. 28-29
  • Kuutazama Ulimwengu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kuutazama Ulimwengu
  • Amkeni!—1993
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Kutokea Tena kwa Ugonjwa wa Kuambukia
  • Uhalifu wa Jeuri wa Kanada
  • Nyimbo za Uchungaji
  • Siri ya Kitiba Iliyohifadhiwa Vema
  • “Msiba Juu ya Msiba”
  • Miani Inayoua
  • Kiwango cha Talaka ya Makasisi Chapanda
  • “Mshuko wa Moyo Ulio Bandia”
  • Meksiko na Kanisa Katoliki
  • Kusahihishwa kwa Halijoto ya Mwili
  • Kisasi cha Vijiumbe-Maradhi
    Amkeni!—1996
  • Magonjwa ya Kuambukiza Katika Karne ya 20
    Amkeni!—1997
  • Maji Yanapokuwa Mekundu
    Amkeni!—2001
  • Mtoto Wako Anapopata Homa
    Amkeni!—2003
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1993
g93 3/22 kur. 28-29

Kuutazama Ulimwengu

Kutokea Tena kwa Ugonjwa wa Kuambukia

“Hatari inayoletwa na magonjwa ya kuambukia haijakwisha. Inakuwa kubwa zaidi,” asema Robert Shope wa Chuo Kikuu cha Yale kuhusu ripoti iliyotolewa na Chuo cha Kitaifa cha Sayansi cha U.S. “Ikiwa hatuchukui hatua za haraka tena ili kudhibiti mambo, tungeweza kukabili hatari mpya kama ile ya mweneo wa HIV au ya mweneo wa homa ya 1918-1919.” Magonjwa manne tayari “yamezuka bila kutazamiwa, yakileta taabu kubwa na kifo,” aongeza Joshua Lederberg, mwenyekiti mwenzi wa Shope katika kamati iliyotayarisha ripoti hiyo. Magonjwa hayo ni kifua kikuu unaokinza dawa, UKIMWI, ugonjwa wa mchochota (Lyme), na aina mpya ya uambukizo hatari wa streptakoko. Ingawa madawa mengi na viuavijasumu vimesitawishwa katika muda wa miongo mitatu iliyopita, vijiumbe vimesitawisha ukinzani dhidi yazo katika njia mbalimbali. Kwa mfano, bakteria yaweza kubadilishana mata ya jeni (urithi-tabia), kutia na jeni za kukinza viuavijasumu. Kama tokeo, hospitali, vituo vya afya, na vituo vya kuandaa makao kwa wasio na makao vimekuwa vituo vyenye magonjwa mengi ya kuambukia yanayokinza madawa. Na usafiri wa kimataifa uliyoongezeka umeeneza “vijidudu vikinzani” ulimwenguni pote. Barry Bloom wa Koleji ya Utabibu ya Albert Einstein ya New York asema: “Kwa habari ya ugonjwa wa kuambukia, hakuna mahali ambapo hatuwezi kupatwa nao na hakuna mtu ambaye hawezi kuambukiwa.”

Uhalifu wa Jeuri wa Kanada

“Je! wafikiri kwamba Kanada ni mahali penye amani? Fikiri tena,” lasema The Toronto Star. “Kanada ni ya pili katika wingi wa uhalifu wa jeuri katika ulimwengu wa magharibi,” baada ya United States. Uchunguzi wa kimataifa ulionyesha kadiri ya uhalifu wa Kanada kuwa mara mbili au tatu zaidi ya ule wa Ulaya ya Magharibi, ambayo nayo, ilikuwa mara tatu zaidi ya ile ya Japani. Katika miongo ya hivi karibuni, uhalifu katika Kanada umeongezeka maradufu na hata mara tatu, huku majiji ya Vancouver, Edmonton, na Ottawa yakiwa na kiwango kikubwa zaidi cha jeuri. London, Ontario, zilifuata, zikifuatwa na Toronto na Montreal. Kulingana na mchunguzi wa uhalifu Irvin Waller wa Chuo Kikuu cha Ottawa, uhalifu wa jeuri waweza kuongezeka isipokuwa ikiwa mengi zaidi yanafanywa ili kupata kisababishi cha tatizo hilo, kama vile umaskini, ukosefu wa makao, kupuuzwa, ukosefu wa kazi, na utumizi wa vitu vinavyokuza uzoevu.

Nyimbo za Uchungaji

Wafugaji wa ng’ombe katika Japan wamekuwa wakitafuta njia bora zaidi inayochukua wakati mchache zaidi wa kukusanya ng’ombe zilizotapakaa vilimani, ambako uwezo wa kuona ni mdogo. Kwa hiyo walifanya jaribio kuona ikiwa ng’ombe wangeweza kukusanyika pamoja kwa muziki. Kwa siku 13 walicheza wimbo wa Kijapan Haru no Ogawa (Kijito Wakati wa Masika) kwa ng’ombe 16 kwa dakika tatu wakati mmoja, mara mbili hadi nne kwa siku. Punde tu baadaye, wakawapa chakula wakipendacho sana. Baada ya kukatizwa na kipupwe wakati ambao ng’ombe walizaa, ng’ombe kumi kati ya wale “waliozoezwa” walipelekwa malishoni pamoja na ndama wao tisa. Wimbo uleule ulipigwa tena. “Katika dakika mbili,” yaripoti Asahi Evening News, “mifugo wote walikuwa wamewasili, wakiletwa pamoja na muziki ambao hawakuwa wamesikia kwa karibu miezi minne.”

Siri ya Kitiba Iliyohifadhiwa Vema

Mojawapo siri zilizohifadhiwa vema zaidi za shirika la kitiba la Denmarki ilifunuliwa na Profesa Margareta Mikkelsen, tabibu. Alifunua kwamba wafanyakazi wa kitiba wanaowachunguza wagonjwa kwa ajili ya magonjwa ya kurithi hugundua kwa kawaida kwamba mtu anayesemwa kuwa baba ya mtoto hawezi kuwa baba wa asili kwa sababu ya kutopatana kwa kromosomu. Kulingana na gazeti Süddeutsche Zeitung, kati ya asilimia 5 na 8 ya baba Wadenmarki si baba wa asili wa watoto wao. Hiyo inamaanisha kwamba angalau watoto 3,000 kati ya watoto 60,000 wanaozaliwa kila mwaka wanatokana na uzinzi. Hata hivyo, wanaume hawaambiwi juu ya ugunduzi huo, ili familia isivunjike.

“Msiba Juu ya Msiba”

Semina ya hivi karibuni iliyofanyiwa Roma na Shirika la Afya Ulimwenguni na Kituo cha Kimataifa cha Utafiti na Msaada ilifunua “orodha ndefu ya mambo ya kushtua, uharibifu, na makosa makubwa ambayo mashirika ya kimataifa ya kutoa misaada huwa nayo kwa ukawaida.” lasema Economia, nyongeza la gazeti Corriere della Sera. Orodha hiyo yatia ndani peremende zilizopunguzwa kalori zinazotumwa Ethiopia yenye njaa; Mahema ya wakati wa kiangazi yaliyotumwa kufuatia tetemeko katika Anatolia, Uturuki, ambapo kipima-joto kilikuwa Sentigredi 12 za baridi; madawa yaliyokwisha nguvu; na chanjo zinazohitaji kuhifadhiwa kwa barafu zinazopelekwa sehemu zisizo na umeme. Ugavi wa misaada mara nyingi unakuwa katika mabohari bila kugawanywa au haufikii wale wanaouhitaji. Kwa nini makosa hayo makubwa huendelea? Economia lasema: “Msaada wa kimataifa ni lazima uwe na matokeo yanayoonekana, na ikiwezekana, yawe yenye kuvutia. . . . Umma unataka hivyo, kwa hiyo si kitu ikiwa, karibu sikuzote, ni kutumia pesa ovyo tu.” Wastadi wanauita “msiba juu ya msiba.”

Miani Inayoua

Wanasayansi wanasema uchafuzi wa vyanzo vya maji unaoongezeka unasababisha ongezeko la miani ya sumu inayotisha samaki ulimwenguni pote. Kulingana na ripoti moja katika International Herald Tribune, dinoflagelatesi, aina ya mwani, hutokeza sumu inayoua samaki. Kisha inajishikiza kwa vipande vya nyama ya samaki kwa kutumia shina ambalo kwalo hiyo hutoa umajimaji wenye kuyeyusha ili kufanya ile nyama iwe majimaji kabla ya kuifyonza ndani. Katika uuaji huo mkubwa wa samaki, watafiti wamehesabu miani aina ya dinoflagelatesi kufikia 175,000 katika kijiko kimoja kidogo cha maji. Dinoflagelatesi ipatayo 1,500 tu kwa kila kijiko kidogo inatosha kuweza kuua samaki katika matangi ya maji yenye samaki. Mara nyingi dinoflagelatesi huhamishiwa kwenye maeneo mapya kupitia kumwagwa kwa maji ya farumi kutoka kwa meli.

Kiwango cha Talaka ya Makasisi Chapanda

“Ndoa moja kati ya tatu katika Ujerumani huishilia kwenye talaka,” yasema The German Tribune. Na jinsi hiyohiyo, “ndoa zaidi na zaidi za wahudumu Waprotestanti zinavunjika.” Hans-Martin Heusel, katibu msimamizi wa Kanisa Protestanti katika Hesse na Nassau, akiri kwamba “kiwango cha talaka miongoni mwa wahudumu wa kiume na kike pia sasa ni cha juu kama kile cha watu wote kwa ujumla.” Ingawa kanisa hufundisha kwamba muungano wa ndoa haupaswi kuvunjwa, lasema Tribune, “uhalisi wa mambo, hata miongoni mwa wahubiri wenyewe wa kanisa, ni tofauti kabisa. Ushuhuda wa Mkristo binafsi na mafundisho ya Kanisa hupuuza kabisa talaka inayohusu mapasta.” Kukiwa na hali chache zilizo tofauti, “pasta aliyetalakana aweza kuendelea kuwa pasta ama katika cheo kilekile ama kwingineko.”

“Mshuko wa Moyo Ulio Bandia”

Idadi inayozidi kuongezeka ya wafanyakazi wa ofisi Wajapan wanaostaafu wanaugua kwa dalili za maradhi yanayoanzia kuumwa na tumbo hadi kupooza. Kadiri wakati wa kustaafu ukaribiavyo, wapenda kazi hao hupoteza uvutano kazini na hutendwa kama wasiofaa nyumbani na familia walizopuuza. “Ingawa wao hushuka moyo,” laripoti gazeti Asahi Shimbun, “wao hujaribu kuuficha kwa kujifanya wana furaha. Halafu kidogo dalili za maradhi kama vile kuumwa na tumbo huanza.” Uchunguzi huonyesha hakuna kitu kibaya kimwili. Dakt. Tooru Sekiya, aliyeita dalili hizo “mshuko wa moyo ulio bandia wa kabla ya kustaafu,” asema juu ya mgonjwa wa kawaida: “Hujibembeleza kwa kufikiri njia pekee ya kukubaliwa ingekuwa ni kuwa mgonjwa, na mara nyingi hiyo huongoza kwenye dalili mbalimbali za maradhi.” Ni nini laweza kufanywa? “Furahia mambo mengine zaidi ya kazi, kama vile kuwa na kazi za kujifurahisha,” ashauri Dakt. Takashi Sumioka, anayetibu wagonjwa wengi kama hao katika Tokyo, na “uwe na tabia ya kuthamini familia yako kila wakati.”

Meksiko na Kanisa Katoliki

Mnamo Septemba 21, 1992, baada ya mvunjiko wa zaidi ya miaka 130, Meksiko na Vatikani zilirudisha uhusiano kamili wa mashauriano. Hilo lilifuatia pendekezo la Rais Carlos Salinas de Gortari la kubadilisha Katiba na kuyapa tena makundi ya kidini haki zilizotwaliwa baada ya mapinduzi ya 1910. “Nyingi za haki hizo ziliondolewa kwanza kati ya 1856 na 1861 wakati wataka uhuru wenye kuasi, wakiwa na hamu ya kukomesha uwezo mkuu wa Kanisa Katoliki, walikatiza uhusiano wa nchi hiyo na Ofisi ya Papa,” lasema The New York Times. Hata hivyo, mengi ya makatazo hayo yamepuuzwa kwa muda mrefu. Ingawa hivyo, Katiba haikubadilishwa, kwa kuwa Wameksiko wengi bado hawakuitibari uwezo wa Kanisa Katoliki. Makanisa yote sasa yana uwezo uliokatibiwa kisheria, yana haki ya kuongoza elimu ya kidini, na yaweza kumiliki mali.

Kusahihishwa kwa Halijoto ya Mwili

Kwa zaidi ya karne moja, wastani wa halijoto ya mwili wa kibinadamu umekubaliwa kuwa Sentigredi 37, ikiwa tokeo la gazeti lililochapwa na Carl Wunderlich katika 1868, likitegemea vipimo zaidi ya milioni moja vya halijoto ya mwili katika watu wazima 25,000. Hiyo ilikuwa jitihada kubwa, kwa kuwa vipimahalijoto vya wakati ule vilichukua karibu dakika 15 au 20 kurekodi halijoto, na ilibidi visomwe hali vikiwa makwapani. Hata hivyo, Philip A. Mackowiak kwenye Chuo Kikuu cha Shule ya Tiba ya Maryland asema kwamba takwimu hiyo yapaswa kubadilishwa, kwa kuwa uchunguzi wake ulionyesha kwamba Sentigredi 37 “haikuwa halijoto ya jumla ya wastani, haikuwa halijoto ya wastani ya vipindi vyovyote vya wakati vilivyochunguzwa, haikuwa halijoto ya katikati, au halijoto yenye kurekodiwa mara nyingi zaidi.” Kwa kweli, iliwakilisha asilimia 8 tu ya mirekodio 700 iliyofanywa. Yeye asema kwamba halijoto ya mwili ya wastani, yapaswa kuwa Sentigredi 36.8.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki