Kuutazama Ulimwengu
Uhalifu—Biashara Yenye Faida
Uhalifu uliopangwa katika Italia hupata dola zikadiriwazo kuwa bilioni 200-240 kila mwaka, lasema 1997 Report of the Commercial Confederation, ambalo ni shirika la wafanya-biashara wa Italia. Angalau dola bilioni 18 yasemekana hupatikana katika ulanguzi wa dawa za kulevya, dola bilioni 11 kutoka ukahaba, na dola bilioni 15-18 kutoka riba na utapeli. “Mashirika matatu ya kibiashara kati ya kumi yanasimamiwa na watu mmoja-mmoja au makampuni yanayohusiana na mashirika ya wahalifu; asilimia 20 hadi 25 ya shughuli za benki zifanywazo kila siku zina chanzo kisichojulikana,” lataarifu gazeti la habari La Repubblica.
Kusoma Vitabu Bado Kwapendwa na Wengi
Tekinolojia ya kompyuta haijabadili mazoea ya kusoma ya Waingereza, kulingana na uchunguzi uliofanywa na Policy Studies Institute. Kama ilivyoripotiwa katika The Times, “karibu nusu ya wale waliochunguzwa walisema kwamba walikuwa wanasoma kitabu kwa ajili ya kujifurahisha, uwiano ambao umebadilika kidogo tangu 1989.” Wanawake husoma zaidi kuliko wanaume, na watu wenye umri wa zaidi ya miaka 55 ndio wasomaji sana. Vitabu vya mapishi ndivyo vipendwavyo na wengi zaidi, vikifuatiwa na hadithi za uhalifu au za kusisimua, riwaya za mahaba, na hadithi za kubuniwa za karne ya 20. Ingawa asilimia 30 ya nyumba zina kompyuta, ni asilimia 7 tu zilizo na vifaa vya kutumia CD-ROM, mshindani wa vitabu. Na tofauti na kompyuta ya kupakatwa, lasema The Times, kitabu chenye kupendeza hakiharibiwi na mchanga kwenye ufuo wa likizoni au na umati wenye kusukumana katika reli ya chini ya ardhi yenye shughuli nyingi, na kitabu kilichotokezwa vizuri chaweza kuwa “chenye kupendeza na kutuliza kama vile yaliyomo ndani yake yalivyo yenye kuandaa jambo la kufikiri.”
Kurudia Utumizi wa Maji
“Utafutaji wa muda mrefu wa kemikali ya kupambana na moto ambayo haiharibu tabaka ya ozoni hatimaye umeongoza kwenye . . . maji,” lataarifu gazeti New Scientist. “Baada ya kuzima mamia ya mioto ya majaribio, Maabara ya Utafiti wa Moto ya Norway katika Trondheim imefikia mkataa kwamba rasharasha za maji ni kibadala kifaacho cha haloni zenye kuharibu ozoni, ambazo bado zatumiwa sana katika vizimamoto.” Haloni — ambayo ni msombo wa kaboni, bromini, na florini — huzuia moto usipate oksijeni. Matone ya maji hufanya vivyo hivyo, yakifuka na kupanuka mara 1,700 ukubwa wake wa awali ili kuondosha oksijeni. Wakati tu yalipatikana kutokuwa na matokeo sana kuliko haloni ni katika mioto midogo, isiyo na miali ambayo haikufikia halijoto ya kutosha kufusha maji. Lakini vibadala vya kutengenezwa na binadamu vya haloni bado vyatafutwa, kwa kuwa maji yanatokeza tatizo: Hakuna faida nyingi ya kifedha iwezayo kupatikana kwa kuyauza.
Sasa—Mchochota wa Ini G
Madaktari katika Japani wamehakikisha kwamba kwa kipindi cha mwezi mmoja cha kupokea utiaji-damu mishipani, wagonjwa waliambukizwa kirusi cha mchochota wa ini G, aina mpya iliyotambulishwa katika 1995 Marekani. Kwa kuchunguza tena damu ya wagonjwa wa kansa ya ini waliofanyiwa upasuaji kati ya 1992 na 1994 kwenye Hospitali ya Toranomon ya Tokyo, madaktari waligundua kwamba wagonjwa 2 kati ya 55 walikuwa wameambukizwa kabla ya upasuaji na kwamba wengine 7 waliambukizwa baada ya upasuaji. Damu iliyoambukizwa ambayo kila mmoja wa wagonjwa 7 alipokea ilitoka kwa wastani wa watoaji-damu 71, madaktari hao wakasema, ikionyesha kwamba asilimia 1.4 ya ugavi wa damu uliotumiwa ulikuwa umeambukizwa kirusi hicho kipya. Ni machache sana yajulikanayo kuhusu kirusi cha mchochota wa ini G au ni asilimia ngapi ya waenezaji watakaositawisha mchochota wa ini au kansa ya ini, lasema gazeti Asahi Evening News.
“Kasoro ya Mileani”
“Ikijulikana kuwa Kasoro ya Mileani, Tatizo la Mwaka 2000, au kwa usahili ‘Y2K,’” hiyo ni “mojawapo ya kani ziwezazo kuharibu kuliko zote zijulikanazo kwa ukokotoaji wa kikompyuta wa kisasa,” lasema U.S.News & World Report. Ilianza katika miaka ya 1960 wakati kompyuta zilikuwa ghali mno na kumbukumbu zake zilikuwa chache. Ili kuhifadhi nafasi, watengenezaji wa programu za kompyuta waliandika tarehe kutumia nambari mbili tu za mwisho za mwaka. Kwa kompyuta, mwaka 1997 ulikuwa tu “97.” Tatizo ni nini? “Januari 1, 2000, asilimia 90 ya zana na programu za kompyuta za ulimwenguni ‘zitafikiri’ ni siku ya kwanza ya mwaka 1900.” Tayari makosa yamefanyika. “Katika gereza la jimbo moja, kasoro hiyo ilifanya kompyuta zihesabu kimakosa muda wa kifungo cha wafungwa kadhaa ambao waliachiliwa,” lasema Newsweek. “Kadi fulani za mkopo zimekataliwa madukani na katika mikahawa wakati tarehe za kuishia ‘00’ zilipotatanisha kompyuta. Na katika majimbo kadhaa, madereva wa lori wamegundua kwamba leseni zao za kusafiri jimbo moja hadi jingine zimebatilishwa wakati kompyuta ziliposhindwa kushughulikia maombi ya kufanya leseni upya yaliyokuwa na tarehe za baada ya mileani.” Mashirika ulimwenguni pote yatalazimika kutumia dola zipatazo bilioni 600 ili kubadili ufupisho wa tarehe — na yanatumaini kufanya hivyo katika miaka miwili inayobaki.
Wanyama Wenye Kuvunja Rekodi
Wakati wa kiangazi cha 1996, membe wa kawaida aliweka rekodi ya “mruko mrefu kupita yote uliopata kufanywa na mnyama wakati wa uhamaji” ambao tuna uthibitisho, lasema gazeti la habari la Italia Corriere della Sera. Baada ya kuondoka Finland, ambapo aliwekewa pete ya kutambulishwa, membe huyo alishikwa majuma 18 baadaye katika jimbo la Victoria katika Australia ya Kusini-Mashariki—baada ya safari ya kilometa 24,400, akisafiri wastani wa kilometa 200 kwa siku. Rekodi ya awali iliwekwa na membe wa aktiki aliyeruka kilometa 22,530 kutoka Urusi hadi Australia katika 1955. Wanyama wengine ambao katika uhamaji wao husafiri maelfu ya kilometa ni salmoni mwekundu, mikunga, vipepeo-maliki, kasa kijani, na nyangumi aina ya humpback.
Nyangumi aina ya humpback kwa kawaida huchukua siku 102 hivi kuhama kutoka Alaska hadi Hawaii, lakini watafiti wamegundua mmoja ambaye alichukua siku 39 tu kuogelea kilometa hizo 4,465! Safari hiyo yawakilisha mwendo wa wastani wa kilometa tano kwa saa. Nyangumi huyohuyo ameonwa pia katika Mexico. Nyangumi aina ya humpback huhamia Hawaii ili kuzaana kwa sababu ndama wao wana mafuta machache sana mwilini hivi kwamba hawawezi kustahimili maji yenye kuganda ya Alaska. Uhamaji wao ndio mmojawapo uhamaji mrefu sana ambao wanyama wa baharini hufanya, laripoti The Times la London.
Nzi Huyo Mhepaji!
Kwa nini ni vigumu sana kumpiga nzi? Kwa nini anaweza kutoroka haraka sana? Siri iko katika kitu fulani katika ubongo wake kiitwacho utembo mkubwa. Hii ni chembe iliyo kama utepe ambayo huwasiliana na sehemu nyingine za ubongo wa nzi kiumeme, badala ya kikemikali. Tokeo ni kwamba mkondo huo wa umeme hutiririka kwa haraka sana kwenye sehemu ya ubongo inayochochea kuruka na kupuruka, ikimwezesha nzi kutoka hatarini kwa sehemu ya elfu chache za sekunde. Kwa kielelezo, katika binadamu wa kawaida, huchukua robo ya sekunde kabla ya mkono kuitikia kitu kilichoonwa na jicho. Wakiwa na ujuzi huu wa nzi, watafiti kwenye Chuo Kikuu cha Sussex cha Uingereza wanatumaini kutokeza dawa ya kuua wadudu ambayo itakatiza kwa mafanikio itikio la nzi, laripoti The Times la London.
Tatizo la Kasa wa Baharini
Idadi ya kasa wa baharini inafikia viwango vya chini kwa njia ya hatari sana kwa sababu ya uwindaji wa kupita kiasi katika bahari za Asia-Pasifiki, laripoti gazeti The Weekend Australian. Hilo lilifanya Australia na Indonesia kudhamini kongamano katika Java kwa lengo la kuboresha njia za uhifadhi. Kwa sababu kasa huhamahama na si wa nchi fulani hususa, programu bora zaidi za uhifadhi katika nchi moja hazina maana ikiwa nchi nyingine katika njia ya uhamaji inawinda kasa bila kufikiria ugavi wa wakati ujao. “Kasa wakadiriwao kuwa 50,000 huuawa kila mwaka katika Bali pekee kwa ajili ya biashara ya watalii,” lasema gazeti hilo la habari, “na mamia ya maelfu ya mayai ya kasa yanavunwa kuwa chakula.” Papua New Guinea pia hufanya biashara ya kasa wa baharini kutia ndani loggerhead aliye hatarini mwa kutoweka na leatherback aliye hatarini na kasa wa kijani. Spishi nyinginezo zilizo hatarini ni hawksbill, flatback, na wale kasa Oliver Ridley.
Njia ya Uwasiliano ya Morse Yakaribia Kutoweka Ikiwa na Miaka 150
Zaidi ya miaka 150 iliyopita, Samuel Morse, mvumbuzi Mmarekani, alipatia kila herufi ya alfabeti ufupisho hususa wa nukta na visitari. Hiyo iliwezesha ujumbe kusikiwa kutoka kwa mawimbi ya redio kwa njia ya kifaa kiitwacho ufunguo wa Morse. Maelfu ya uhai yameokolewa baharini wakati meli zilizokuwa taabani zilipotumia ufupisho wa dharura SOS. Majeshi ya ulimwenguni pia yametumia njia hii sahili ya uwasiliano, na ndivyo na watu wengi wasio na ujuzi katika kupitisha ujumbe kwa kujifurahisha. Faida kuu ya njia ya uwasiliano ya Morse iko katika uwazi wake, jambo la muhimu wakati opareta wa redio ana lafudhi nzito au hawezi kusema lugha ya mahali ambapo yaelekea ujumbe huo utasikiwa. Lakini ujumbe wa Morse umebadilishwa kwa kuendelea na uwasiliano wa kuongea redioni na mifumo ya uwasiliano ya setilaiti. Katika 1993 njia hiyo ya uwasiliano haikuhitajika tena kwenye meli. Ufaransa iliacha mfumo wa Morse mapema mwaka huu, na kufikia 1999 utakuwa umeachwa kabisa ulimwenguni pote.