Mwaka wa 2000—Je, Kuvurugika kwa Kompyuta Kutakuathiri?
IMESEMWA kwamba wakati kompyuta ilipojitokeza kwenye mandhari ya ulimwengu, ilikuwa ndio uvumbuzi mkubwa zaidi tangu mwanadamu alipoanza kutumia umeme. Leo, miongo kadhaa baadaye, watu wengi hushangaa jinsi walivyoweza kuishi bila kompyuta. Hili gazeti unalolisoma lilitayarishwa kwa kutumia kompyuta. Kompyuta zaweza kuweka habari zilizohifadhiwa katika vifaa vyao vya kuhifadhia habari na kuzipata tena mara moja. Aha, kompyuta zinazostaajabisha! Jinsi zilivyo za ajabu sana! Ulimwengu ungekuwaje bila hizo?
Katika maeneo yaliyositawi ya ulimwengu, kompyuta inaathiri karibu kila jambo katika maisha ya watu. Ikiwa unategemea malipo ya uzeeni, hundi za serikali za kulipwa pesa kwa sababu ya kutojiweza, malipo ya kodi na bima, au malipo mengine mengi kama hayo, kupokea hayo yote kwategemea kompyuta. Ikiwa umeajiriwa kazi, kuna uwezekano mkubwa kwamba hundi za mshahara wako huhifadhiwa katika kompyuta. Kompyuta huhifadhi rekodi ya pesa zinazowekwa akiba katika mashirika ya benki na riba inayolipwa. Hizo huendesha mashine nyingi, kama zile za kuzalisha umeme au za kusafisha maji, katika nyumba za kisasa. Hizo zimefaidi sana madaktari, kliniki, na hospitali katika kutambua matatizo ya kiafya—na kuokoa uhai. Kompyuta hutumiwa kuchunguza hali ya hewa na kuzuia ndege zisigongane angani.
Zina Akili Kadiri Gani?
Kompyuta hazina akili kushinda binadamu anayezitengenezea programu. Kompyuta hutatua tu mambo magumu kulingana na ilivyoagizwa. Hiyo haina uwezo wa kujifanyia maamuzi mazuri na sahili. Inapokosea, huwa tu inaonyesha kutokamilika kwa wanadamu ambao wameitengenezea programu au kuiunda. Ifanyapo vizuri, mwanadamu ndiye husifiwa. Huenda kompyuta ikafanya kazi haraka zaidi kuliko mwanadamu, lakini haiwezi kuandaa majibu kwa mambo magumu isipokuwa mwanadamu awe ameipa njia ya kutokeza majibu.
Kwa mfano, mwanadamu hakufikiria sana wakati ujao alipotengeneza programu ya kompyuta fulani kwa mara ya kwanza miaka ya 1950 na 1960. Kwa kuwa vifaa vya kuhifadhi habari katika kompyuta vilikuwa ghali wakati huo, wenye kutengeneza programu za kompyuta walitafuta njia za kuokoa nafasi katika vifaa hivyo. Katika kompyuta kila herufi au nambari hujaza nafasi. Hivyo, ili kuokoa nafasi tarehe zinapohifadhiwa, watengenezaji wa programu ya kompyuta wa mapema walibuni mfumo wa maandishi yaliyofupishwa ambao uliziruka nambari mbili za kwanza za tarehe za mwaka. Kwa mfano, mwaka 1965 ukafupishwa kuwa “65,” mwaka 1985 ukawa “85,” mwaka 1999 ukawa “99,” na kadhalika. Wakati wa kuchapisha tarehe, lilikuwa jambo rahisi kuongeza “19” kwa “85” ili kupata 1985. Kwa miongo kadhaa iliyopita, mamilioni ya programu za kompyuta zimeandikwa kwa kutumia njia hiyo ya mkato. Kati ya wenye kutengeneza programu za kompyuta, ni wachache waliofikiri kwamba njia hiyo ya mkato iliyoonekana kuwa haina madhara ingetokeza magumu mazito. Ilikuwa hivyo kwa sababu hawakuwazia kwamba programu zao zingetumika hadi mwanzoni mwa karne ya 21. Hata hivyo, programu kadhaa zilizofanyizwa kwa njia hiyo ya mkato zingali zatumika, nazo zitauhifadhi mwaka wa 2000 kama “00.”
Kompyuta fulani zitaufasiri “00” kama mwaka wa 1900! Sasa wazia juu ya mvurugo unaotokea katika programu ya kompyuta wakati kompyuta inapopiga hesabu ya mkopo wa miaka mitano unaoanza mwaka wa 1999 na kupanga kwamba kiasi cha mwisho cha mkopo huo kitalipwa mwaka wa 1904! Katika visa vingine, hesabu ya tarehe itaifanya programu ya kompyuta isimame ikiwa na onyo la kuonyesha kuna kosa, na katika visa vibaya zaidi, programu hiyo itavurugika kabisa.
“Ingawa mikrochipu imetuletea mapinduzi ya viwanda ambayo yanalingana na kubuniwa kwa umeme,” likaandika gazeti la Toronto Star, “hiyo pia imetuweka katika hali ya kuweza kudhuriwa kuliko vile wabuni wake wangeweza kuwazia.” Gazeti hilo Star pia lilisema: “Ulimwenguni pote kunayo mifumo ya kompyuta na mikrochipu ambayo haiwezi kutofautisha baina ya mwaka 1900 na mwaka wa 2000. Mifumo hii isipotambuliwa na kubadilishwa, huenda kukatokea machafuko ya tufeni pote.”
Mambo Yanayotabiriwa na Wataalamu Fulani
“Kila mtu, kutia ndani mimi, anakisia matokeo yatakuwa mabaya kadiri gani,” akasema Seneta Robert Bennett, wa jimbo la Utah, Marekani. “Na hakuna mtu atakayejua hadi Siku ya Mwaka Mpya 2000 au juma moja au majuma mawili baadaye.” “Kwa kweli kuna msingi fulani wa kusema . . . kutakuwa na matokeo yatakayokuwa magumu sana kwa uchumi na magumu sana kwa watu,” akasema msaidizi mmoja wa rais wa Marekani.
“Tunahangaishwa na kuvurugwa kwa mfumo wa nyaya za kupitisha umeme, mawasiliano ya simu, na huduma za benki,” akasema msemaji wa Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA). Kulingana na ripoti kutoka ulimwenguni pote, tayari kompyuta kadhaa zimetatizika wakati tarehe katika kompyuta zilipofikia mwaka wa 2000 na kuendelea.
“Wataalamu wanatabiri juu ya kutokea kwa matatizo zaidi katika sekta ya afya,” likaripoti U.S.News & World Report, “kwa sababu rekodi za kutayarisha malipo na bima za wagonjwa katika hospitali au Mashirika ya Huduma za Afya (HMO) zinaweza kudhuriwa. Vifaa fulani vinavyotumiwa hospitalini, kutia ndani mashine za kupima wagonjwa, viko pia katika hatari ya kupata hitilafu. Kwa kuwa kampuni nyingi za umeme zimechelewa kulirekebisha tatizo, kuna tisho la kukatizwa kwa umeme.” Gazeti fulani la Kanada pia latoa maoni ya hofu kama hayo: “Hospitali na tekinolojia zetu za kitiba zote zategemea mikrochipu iliyoenea kotekote, kwa hivyo watu wanaweza kufa kutokana na kushindwa kwa mfumo wa kompyuta.” “Kwa sababu ya ile kazi tunayofanya,” akalalamika msimamizi mmoja wa hospitali, “tunaathiriwa kwa njia mbaya zaidi. Viwanda vingine huenda visiwe katika hali ya kufa na kupona.”
Wataalamu fulani wa kompyuta wanaotazamia mabaya zaidi wanatabiri kuporomoka kwa masoko ya hisa, kushindwa kwa biashara ndogo-ndogo, kutolewa kwa haraka kwa pesa zilizo katika mashirika ya benki na wateja wenye kuhofu. Nchini Marekani, waziri mdogo wa ulinzi aliiita kasoro hii ya kompyuta ulimwenguni pote kisawe cha kielektroni kinacholingana na hali ya hewa ya El Niño na kusema: “Nitakuwa wa kwanza kusema kwamba bila shaka tutakuwa na mambo mabaya ya kushangaza.”
“Matokeo kwa shughuli za kibiashara nchini Urusi yatakuwa yenye msiba ikiwa kompyuta hazitakuwa zimerekebishwa kufikia Januari 1 mwaka wa 2000,” akasema msimamizi wa Chama cha Wafanyabiashara wa Marekani. Shirika la habari la Reuters laripoti: “Makampuni ya Ujerumani yanazubaa kuhusiana na ule msiba wa kompyuta wa milenia utakaolipuka kama bomu, na matokeo yanatisha kusababisha machafuko katika Ulaya yote.” Mkurugenzi mmoja wa uchunguzi alisema “uchambuzi huo pia waweza kuelekezwa kwa Austria, Uswisi, Hispania, Ufaransa na Italia.”
Pia, gazeti la Bangkok Post lavuta uangalifu kwa tatizo la kompyuta nchini Thailand: “Ofisi za kitaifa za takwimu katika eneo hili zakabili tatizo la milenia lenye pande mbili: kuzuia lile tatizo la mwaka wa 2000 (Y2K) katika mifumo yao ya kompyuta, na kujitayarisha kufanya tena sensa mpya za watu, kulingana na Shirika la Habari la Umoja wa Mataifa.” Australia, China, Uingereza, Hong Kong, Ireland, Japani, na New Zealand zote zakabili matatizo hayohayo. Kwa kweli, ni tatizo la ulimwenguni pote linalohitaji utatuzi.
Gharama ya Kushangaza
Wataalamu fulani wamekadiria gharama kubwa ya kushangaza ya kurekebisha matatizo ya kompyuta. Kwa mfano, Ofisi ya Usimamizi na Bajeti ya Marekani, yakadiria kwamba itahitaji dola bilioni 4.7 ili kurekebisha makosa katika kompyuta za serikali kuu ya Marekani pekee. Kikundi kimoja cha wataalamu chasema kwamba kadirio halisi la kurekebisha kompyuta zote za serikali kuu lingekuwa dola bilioni 30. Je, itagharimu kiasi gani kurekebisha kompyuta ulimwenguni pote? Kiasi cha kushangaza cha “dola bilioni 600 ili kurekebisha programu za kompyuta na dola trilioni moja za kesi zitakazowasilishwa mahakamani zikiwa tokeo la marekebisho fulani ambayo yatakosa kufaulu,” likaripoti gazeti New York Post. Kikundi kingine cha wataalamu kimekadiria kwamba “gharama za marekebisho, mashtaka, na kupoteza kazi huenda zitafikia jumla ya dola trilioni 4.” “Tatizo la Mwaka wa 2000,” likaandika gazeti New York Post, “linaibuka kuwa lenye gharama kubwa sana katika historia yote ya binadamu.” Ripoti nyingine ililifafanua tatizo hilo kama “labda ndio mradi mkubwa zaidi, wenye hatari zaidi, wenye gharama kubwa zaidi ambao binadamu wamewahi kuukabili.”
Maoni Hutofautiana
Hilo litakuathirije? Ikitegemea unakoishi na juhudi zinazofanywa na mashirika unayoshughulika nayo, huenda lisiwe na athari zozote kwako au liwe lenye kukuudhi kidogo tu au liwe jambo gumu sana, hasa katika majuma machache ya kwanza baada ya Januari 1, 2000. Ikiwa kuna maeneo yanayokuhangaisha, kama vifaa maalumu unavyotumia kwa huduma za afya, tafuta msaada kutoka kwa kampuni au shirika ambalo hutoa utumishi huo na uulize jinsi ambavyo vifaa au utumishi unaotolewa huenda vikaathiriwa na tatizo la mwaka wa 2000.
Kwa kipindi cha miaka michache iliyopita, mengi sana yamesemwa kuhusu tatizo la mwaka wa 2000. Watu fulani husema kwamba tatizo hilo ni baya sana; wengine hubisha wakisema kwamba hilo limetiwa chumvi mno. Kunao wanaosema kwamba benki zitaporomoka, ilhali wataalamu wa mambo ya benki husema kuwa kufikia mwaka wa 2000, mengi ya matatizo yao yatakuwa yamerekebishwa. “Hakuna aaminiye kwamba mfumo wa simu unaelekea kuporomoka vibaya,” akasema mkuu wa Tume ya Mawasiliano ya Serikali Kuu ya Marekani. Hata hivyo, alikubali kwamba kutakuwa na matatizo ya simu mwanzoni mwa karne ijayo, lakini akasema hayo hayatakuwa yenye kutokeza msiba, bali yenye kuudhi tu. Mashirika mengi tayari yanafanya majaribio ya kuigiza tarehe katika maabara. Hilo huenda likazuia matatizo mengi. Ingawa hivyo, itabidi ulimwengu ungojee ili kuona tatizo la mwaka wa 2000 litakuwa zito kadiri gani.