Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g94 7/8 kur. 20-23
  • Gari-Moshi Lenye “Meno”

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Gari-Moshi Lenye “Meno”
  • Amkeni!—1994
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Kwa Nini Yahitajiwa?
  • Ujenzi Mgumu
  • Mapito ya Kustaajabisha Sana
  • ‘Ni Salama Kuliko Nyumbani Mwako Mwenyewe’
  • “Reli ya Kichaa” ya Afrika Mashariki
    Amkeni!—1998
  • “Utepe wa Chuma” Unaounganisha Bahari Mbili
    Amkeni!—2010
  • Reli Inayoenea Kotekote India
    Amkeni!—2002
  • Reli Iliyochukua Zaidi ya Miaka 120 Kujengwa
    Amkeni!—2008
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1994
g94 7/8 kur. 20-23

Gari-Moshi Lenye “Meno”

Na mleta-habari za Amkeni! katika Ugiriki

JIWAZIE ukiwa katikati ya kibonde chembamba kilichoinama sana na kujawa na miti yenye usitawi mwingi, kukiwa na miamba mikubwa iliyoning’inia juu kwa njia hatari, na mto wenye kupindapinda ukitiririka kwa fujo chini ya kibonde hicho. Mara tu uanzapo kuhisi kwamba uko pwekepweke, kwa ghafula wasikia kwa mbali mvumo wa kukereza na kugotagota. Lo, hata hungetazamia kamwe kuona kisafirio chochote cha ki-siku-hizi mahali hapa papweke, ambapo paonekana hapawezi kufikiwa wala kuguswa na mwanadamu. Lakini pasipo shaka unafahamu mvumo huo—gari-moshi linakuja!

Mvumo huo ukaribiapo, watambua gari-moshi dogo kati ya ile miti mirefu, likiwa na mabehewa mawili tu na kichwa cha dizeli katikati, huku ikifanya kibarua kigumu kupanda polepole ule mwinuko wa mlima ulioinama sana. Unakaribishwa kwenye Reli ya Mtambo wa Meno Sambamba ya Dhiakoptón-Kalávrita, ambayo ni mojapo reli zenye kupendeza na kutazamisha zaidi katika Ulaya, iliyo katika mkoa wa Peloponnisos wa Ugiriki. Kwa Kigiriki reli hii hurejezewa kuwa odontotós, ambayo kwa uhalisi humaanisha “yenye meno,” jina linalofaa sana, kama utakavyoona.

Kwa Nini Yahitajiwa?

Mji wa Kalávrita, ulio katika Peloponnisos ya kaskazini, ndicho kituo cha kiuchumi na usimamizi cha eneo linalozunguka. Pia ni mahali pa upendezi wa kidini na kihistoria kwa sababu ya makao fulani maarufu ya watawa yaliyo karibu. Kwa kuwa mji huo umekaa vizuri katika bonde la mlima, una umaarufu pia kwa sababu ya uzuri wao wa kiasili, misitu inayouzunguka, chemchemi zao nyingi, na tabia ya nchi yenye kupendeza.

Wakati historia ya mji huo ilipokuwa ikivuma sana, katikati ya karne ya 19, mji huo ulikuwa na idadi ya watu 6,000. Lakini ulitenganishwa na miji na vijiji vya pwani na eneo la mawemawe la mlimani. Hakukuwa na barabara zozote zilizotandazwa vizuri wala njia nyingine yoyote ya uwasiliano, na usafiri wa kwenda na kutoka mjini ulihitaji saa nyingi za usafiri wa kutaabisha sana wa mikokoteni ya kuvutwa na farasi au punda. Njia iliyofaa zaidi ya kufika pwani ilikuwa ya kufuata bonde kubwa la kina kirefu lenye Mto Vouraikós sehemu ya chini, mto huu ukiishia kijiji cha Dhiakoptón.

Kabla ya mwanzo wa karne hii, iliamuliwa kwamba hii ingepasa kuwa ndiyo njia ya reli yenye mafaa na ya kupendeza, pito lenye kuleta utendaji mwingi kwenye miji ya pwani. Hata hivyo, uchunguzi mbalimbali uliofanywa na wahandisi ulifunua kwamba njia ambayo ilikuwa lazima reli hiyo ipite ilikuwa pia na miinamo yenye kulala sana. Basi kulihitajiwa reli ya mtambo wa meno sambamba.

Reli ya mtambo wa meno sambamba au ya meno-magurudumu ni nini? Ni reli iliyoundwa kupita katika eneo lenye miinamo iliyolala sana; kati ya zile fito za mapito ya kawaida, ina ufito wenye meno—ufito wa mtambo wa chuma-cha-pua—ambamo gia ya mviringo katika kichwa cha gari-moshi yaweza kuingizwa. Hii huzuia gari-moshi lisiteleze kinyumenyume linapopanda wala kuteleza mbele linaposhuka.

Kwa habari ya Reli ya Mtambo wa Meno Sambamba ya Dhiakoptón-Kalávrita, kila meta 7 zina mwinuko wa meta 1, na hii hutokea mahali tofauti patatu njiani. Hivyo, kwa sehemu tatu hizi za reli, dreva wa gari-moshi ni sharti asimamishe gari, atie gia katika mtambo wa meno, na kuendelea kwa mwendo wa chini uliodhibitiwa.

Ujenzi Mgumu

Kwa sababu ya eneo gumu ambalo reli ililazimika kuvuka, kuijenga kulikuwa tendo kubwa la uhandisi hodari. Kazi hiyo ilipewa kampuni moja ya Italia, iliyoanza kazi katika 1891. Ili kurahisisha ujenzi, reli ya mtengano mwembamba (sentimeta 75) ilichaguliwa.

Miaka mitano baadaye, katika 1896, tani nyingi za mawe zikawa zimeondolewa. Handaki tisa zikawa zimetobolewa kupitia mwamba wa mlima, na madaraja sita yakawa yamejengwa. Mwanzoni madaraja yote yalikuwa ya tabaka za mawe yaliyopangwa kwa namna ya matao, lakini miaka kadhaa baadaye nafasi ya baadhi yayo ilichukuliwa na madaraja ya chuma-cha-pua. Reli mpya kabisa, yenye kupanda mwendo wa kilometa 23 hadi mwinuko wa meta 720 ikawa tayari kutumiwa. Kwa kuwa sasa wajua simulizi la gari-moshi hilo, je, ungependa kulipanda na kufurahia mapito yalo ya kusisimua?

Mapito ya Kustaajabisha Sana

Acheni tupande gari-moshi la asubuhi, Na. 1328, kutoka Dhiakoptón ya pwani. Mwendo waanza kwa ulaini na polepole tupitapo kijijini. Ingawa tumejawa na tazamio lenye hamu nyingi, wanakijiji, ambao yaonekana wametumia gari-moshi hili mara nyingi, hata hawajisumbui kugeuka walitazame. Lakini sisi twaendelea tukiwa na msisimuko usiokwisha.

Baada ya dakika chache, twaona mwingilio wa kibonde cha kutisha. Ni mwono wa kustaajabisha sana. Ule mto wenye kupita kwa nguvu uko kushotoni mwetu, na mawe makubwa yamening’inia juu yetu kwa njia ya kutisha, misunobari ikiwa imetia mizizi juu yayo kwa njia hatari. Ule mto wenye kupindapinda umejikunja kwa uzuri kupita katika miamba.

Uoto umeshikana na kusitawi sana. Gari-moshi letu laonekana likipenya katika misitu ya mikuyu-mwitu na miti ya ufuo, ambayo matawi yayo karibu yaguse behewa letu. Ingawa reli hii imefanya kazi muda wa karibu karne moja sasa, sehemu fulani za genge hili ni kama hazifikiki kabisa, na uzuri wazo huonekana na msafiri peke yake.

Twafika kwenye kituo cha kwanza cha gari-moshi, kiitwacho Niámata, ambapo wakulima wachache wa hapo washuka ili watembee kwa miguu hadi kwenye mashamba yao. Tuendeleapo, eneo lazidi kuinama. Kwa ghafula gari-moshi lasimama. Bila shaka, hakuna kasoro lakini sasa dreva ni sharti atumie reli ya katikati iliyo na mitambo ya meno sambamba ili aendelee kwa tahadhari. Twahisi gia ya kichwa cha gari-moshi ikiumana na mtambo wa meno sambamba, jambo ambalo laimarisha zaidi mwendo wa behewa. Tujapopewa uhakikishio na abiria mzoefu aliye karibu nasi kwamba hakuna wasiwasi, sisi twahangaika kidogo tuangaliapo ule mpando wenye kuinama sana.

Kandokando ya kuta za sehemu zilizo wazi zaidi za kile kibonde, twaona mapango makubwa yatumiwayo na watu wa hapo kuwa mazizi ya kondoo. Katika upande wa kushoto, kuna mapango madogo zaidi yenye mawe stalaktiti na stalagmiti. Maporomoko makubwa ya maji yaanguka kutoka pande zote, na mvumo wayo, ukichanganyikana na mwangwi wayo, waongezewa nguvu na muundo wa lile genge. Hapa, kushotoni, ndipo penye mabomoko ya ardhi ambayo yamefanyiza maporomoko ya maji yasiyo ya kudumu sana ambayo hatimaye yatafagiwa na ule mto wenye kutiririka kwa fujo. Twawapita watu wenye maungo kabambe walioamua kutembea badala ya kupanda gari-moshi.

Lile bonde kubwa na mto vyaongezeka kina tupitapo juu ya daraja lenye kimo kirefu. Mahali pamoja, lile genge ni jembamba sana—lapungua kidogo tu meta mbili kwa upana—na lile gari-moshi ni sharti lipite katika handaki lililo sambamba na ule mwinamo uliolala sana.

Baada ya sisi kupita mahandaki na madaraja zaidi, lile genge lafunguka pole kwa pole na mwishowe lawa bonde jembamba, na punde si punde twafika kituo cha pili, kijiji cha Káto Zakhloroú. Ishara iliyowekwa kwenye kituo kidogo hicho yaonyesha mwinuko wa meta 601 juu ya usawa wa bahari. Nyumba chache zilizo katika kijiji hiki zimejengwa pande zote mbili za bonde, zikiwa zimefichika katikati ya mikuyu-mwitu mikubwa na mijozi. Waweza kuhisi ule unyevunyevu mzito katika hewa, na ukiwauliza wanakijiji, watakubali kwa utayari kwamba katika bonde hili lenye giza, hawajapata mwanga mwingi wa jua maishani mwao. Kwa sababu ya muundo wa lile bonde na ushikano wa ile miti, jua huonekana muda wa saa chache tu kila siku—na hata muda mchache zaidi katika majira ya baridi.

Lile gari-moshi laendelea kusonga mbele baada ya Káto Zakhloroú, likijipindapinda kama nyoka kwa kufuata mapito ya kawaida zaidi, sasa likisindikizwa na bonde tambarare la mto wa Vouraikós, unaopita kati ya miti ya wilo na yukaliptasi. Baada ya dakika 65 za kusafiri mwendo wa kutazamisha katika gari-moshi hilo, twaweza kuyaona majengo ya Kalávrita katika ukungu wa asubuhi. Ingawa mji huu una wakaaji karibu 3,000 tu, huo huvutia watalii wengi kila majira ya mwaka. Baadhi yao huja kufurahia tafrija ya kuteleza barafuni iliyo karibu, hali wengine huja kuonja tabia-nchi yayo nzuri na mapishi matamu ya huko.

‘Ni Salama Kuliko Nyumbani Mwako Mwenyewe’

Tushukapo gari-moshi, twapiga domo na Ioanní, yule dreva wa gari-moshi aliyetupandisha mahali hapa kwa ulaini na usalama sana. “Sikuzote mimi hufurahia mwendesho huu,” yeye asema kwa uradhi mtulivu. Akiinua macho yake, kama kwamba anakumbuka jambo fulani, aongezea hivi: “Lakini mambo huwa magumu katika majira ya baridi. Wajua, gari-moshi halijai sikuzote, na mtu huhisi upweke sana katikati ya kibonde hiki cha kuogofya. Halafu kuna yale maporomoko ya ardhi, theluji, baridi, na ukungu mzito usiokwisha. Lakini singekubali kubadilishana mapito haya kwa mapito yoyote ‘ya kikawaida.’”

Tuulizapo juu ya usalama wa reli hii, Ioanní ashikilia sana maoni yake kwamba: “Una usalama mwingi zaidi katika gari-moshi hili kuliko nyumbani mwako mwenyewe!” Kwa kweli, ni kasoro moja ndogo tu, isiyokuwa na majeraha makubwa, ambayo imepata kutukia muda wote wa ile historia ya karibu miaka 100 ya reli hii.

Katika miaka ya 1940 na 1950, gari-moshi hili lisilo na kifani ndiyo njia iliyotumiwa kuwaletea “habari njema” ya Ufalme wa Yehova wakaaji wa mji wa ndanindani wa Kalávrita na vijiji vya kandokando vyenye kufikiwa kwa shida. (Marko 13:10) Leo, tokeo ni kwamba kuna kutaniko dogo lakini lenye bidii la Mashahidi wa Yehova katika Kalávrita.

Kwa hiyo ukipata kuzuru Ugiriki, mbona usitie Odontotós ya Dhiakoptón-Kalávrita, lile gari-moshi lenye “meno,” katika pitapita yako ya kuona nchi? Bila shaka, ungefurahia tukio la kuthawabisha—litakalokumbukwa kwa muda mrefu!

[Sanduku katika ukurasa wa 21]

“Chumba cha Mahakama”

Hili ndilo jina ambalo wenyeji wameita mojapo mapango makubwa zaidi yaliyo kandokando ya mapito ya ile reli. Kwa nini? Ni kwamba, maumbo ya stalaktiti na stalagmiti katika pango hili yafanana ajabu na chumba cha mahakama. Upande wa nyuma waweza kuwaona “mahakimu” wamekalia jukwaa lao—maumbo yenye taadhima ya stalagmiti nzito. Pande zote mbili, stalagmiti zaidi, zilizo “mashahidi” na “mawakili,” zatazama kesi ikiendelea. Mwishowe, kwenye kinywa cha pango, mtu aweza kuwaona “washtakiwa,” waliohukumiwa na kuuawa, wakining’inia kwenye dari ya pango wakiwa ni stalaktiti ndefu mbili.

[Ramani katika ukurasa wa 22]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Njia ya lile gari-moshi lenye “meno”

GREECE

Dhiakoptón → Káto Zakhloroú → Kalávrita

[Picha katika ukurasa wa 23]

Picha ya ndani juu: Kituo cha gari-moshi cha Mega Spileon

Chini: Lile gari-moshi lenye “meno,” likipanda kigongo chembamba cha ardhi

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki