“Reli ya Kichaa” ya Afrika Mashariki
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA KENYA
MIPANGO ya Uingereza, iliyofanywa miaka izidiyo 100 hivi ya kujenga reli inayovuka Afrika Mashariki haikuungwa mkono sana na kila mbunge wa bunge ya London. Mpinzani mmoja aliandika hivi kwa kukejeli:
“Gharama yake haiwezi kuelezeka;
Lengo lake hakuna akili iwezayo kuwazia;
Mahali itakapoanzia hakuna mtu awezaye kukisia;
Mahali itakapofika hakuna mtu ajuaye.
Matumizi yake hakuna mtu awezaye kuwazia;
Mizigo yake hakuna mtu awezaye kufasili;
Kwa wazi hii ni reli ya kichaa.”
Kwa kweli, mradi huo haukuwa mbaya sana kama ilivyotajwa juu. Reli hiyo ilitarajiwa kufikia umbali wa kilometa 1,000, kutoka Mombasa, bandari ya Kenya iliyo katika Bahari ya Hindi, hadi Ziwa Viktoria. Wenye kuunga mkono mradi huo walihakikisha kwamba itakapomalizika, ingeendeleza biashara na ukuzi na pia kukomesha biashara ya watumwa katika eneo hilo. Gharama ya kujenga reli hiyo ilikadiriwa kuwa dola milioni 5 (za Marekani), ambazo zingelipwa na walipa kodi Waingereza. Ilikadiriwa kwamba ingechukua muda wa miaka minne hadi mitano kujenga reli hiyo.
Na bado, mambo mengi hayakueleweka waziwazi. Wakati George Whitehouse, mhandisi mkuu, alipowasili Mombasa mnamo Desemba 1895, alikuwa na ramani ndogo tu ya njia ambayo reli hiyo ingetakikana kufuata. Habari alizopokea Whitehouse baada ya hapo zilitia hofu zaidi. Sehemu ya magharibi kabisa ya Mombasa ilikuwa yenye joto jingi na haikuwa na maji na misafara mingi iliiepuka. Ng’ambo yake, reli hiyo ingepitia kilometa 500 za pori na vichaka zilizojaa simba, mbung’o na mbu. Kisha kulikuwako eneo la milima ya kivolkano linalogawanywa na Bonde Kuu la Ufa lenye upana wa kilometa 80, na miharara yake inayoenda chini kwa meta 600. Sehemu iliyobakia ya kilometa 150 kabla ya kufika kwenye ziwa ilisemekana kuwa kinamasi. Haishangazi kwamba kujengwa kwa reli hii kungekuwa mojawapo ya matukio yenye kupendeza zaidi ya Kiafrika.
Matatizo ya Mapema
Bila shaka, wafanyakazi wengi sana wangehitajiwa kwa ajili ya mradi huo mkubwa. Kwa kuwa Mombasa ilikuwa jumuiya ndogo, wafanyakazi waliletwa kutoka India. Katika mwaka wa 1896 pekee, zaidi ya wafanyakazi 2,000 waliwasili kwa meli—waashi, wahunzi, maseremala, masoroveya, warasimu, makarani, na vibarua.
Kisha kulikuwa na kazi ya kuifanya Mombasa kuwa mahali panapofaa pa kupokea vifaa vikubwa ambavyo vilihitaji kuletwa kwa meli ili kujenga reli yenye urefu wa kilometa 1,000. Njia yenyewe ingehitaji reli 200,000, zenye urefu wa meta 9 na zenye uzito upatao kilogramu 200. Pia kulihitajika taruma milioni 1.2 (nyingi zikiwa za feleji). Kufunganisha reli na taruma kungehitaji kuletwa kwa vyuma 200,000 vya kuunganisha reli, bolti 400,000, na kabari za feleji milioni 4.8. Kwa kuongezea, magarimoshi, mabehewa ya breki, ya mizigo, na ya kubebea watu yalipaswa kuletwa. Lakini kabla ya reli ya kwanza kutandazwa, ilikuwa lazima kujenga gati, mabohari, nyumba za wafanyakazi na karakana. Upesi mji huo wa mwambao usiokuwa na utendaji mwingi ukawa bandari ya kisasa.
Whitehouse alitambua mara moja kwamba kungekuwa na tatizo la maji; visima vichache katika Mombasa vilitimiza kwa shida mahitaji ya wakazi wa huko. Lakini, maji mengi sana yangehitajika kwa ajili ya kunywa, kuoga na kwa ujenzi. “Kutokana na yale ambayo nimejionea na ninayojua kuhusu nchi hii,” akaandika Whitehouse, “siwezi kupendekeza mpango mwingine wowote isipokuwa magarimoshi yalete maji kwa kilometa za kwanza 160.” Magarimoshi hayo yatahitaji kukokota angalau lita 40,000 za maji kila siku!
Mwanzoni, wahandisi wa reli walitatua shida ya maji kwa kutengeneza bwawa na kujenga tangi la maji ya mvua. Baadaye, mashine zililetwa ambazo zilitonesha maji ya bahari.
Kazi ilianza, na kufikia mwisho wa mwaka wa 1896—mwaka mmoja baada ya Whitehouse kuwasili Mombasa—reli yenye umbali wa kilometa 40 ilikuwa imejengwa. Licha ya mafanikio haya, wachambuzi walidai kwamba reli isipojengwa haraka, garimoshi la kwanza lingefunga safari yake ya kwanza kutoka pwani hadi Ziwa Viktoria karibu mwanzoni mwa miaka ya 1920!
Kuvuka Uwanda wa Taru
Wakati huohuo, wajenzi walipatwa na maradhi. Mnamo Desemba 1896, hospitali za hema zilikuwa makao ya wafanyakazi zaidi ya 500 waliokuwa wamepatwa na malaria, ugonjwa wa kuhara damu, vidonda vya kitropiki, na nimonia. Majuma machache baadaye, nusu ya wafanyakazi hawakujiweza kwa sababu ya ugonjwa.
Hata hivyo, kazi iliendelea, na kufikia mwezi wa Mei reli zilikuwa zimetandazwa kufikia umbali wa kilometa zaidi ya 80, kwenye Nyanda za Taru zilizo kame. Ingawa mara ya kwanza mandhari ilionekana kuwa ilifaa kwa ajili ya ujenzi, Taru ilikuwa msitu wenye michongoma mikali yenye kimo cha binadamu. Mavumbi mazito mekundu yalisonga wafanyakazi. Jua lilikuwa kali sana, likikausha ardhi kabisa—eneo hilo lilijaa miiba na joto kali. Hata usiku, halijoto ilipungua kufikia digrii 40 za Selsiasi kwa nadra sana. Mwandishi M. F. Hill alisema hivi katika historia yake rasmi ya kujengwa kwa reli: “Ilikuwa kana kwamba asili yenyewe ya Afrika ilipinga kuanzishwa kwa reli ya mzungu.”
Kutishwa na Simba
Kufika mwishoni mwa mwaka wa 1898 reli ilikaribia Tsavo kwenye kilometa 195. Kisha, kwa kuongezea matatizo ya mandhari yenye hali mbaya, tatizo jingine liliibuka—simba wawili walianza kuwashambulia wafanyakazi. Simba wengi hawawindi binadamu. Kwa kawaida simba ambao hushambulia wanadamu huwa wamezeeka sana au wagonjwa wasiweze kuwinda wanyama. Simba wawili katika Tsavo, wa kiume na kike, walikuwa wa kipekee. Ingawa hawakuwa wamezeeka wala dhaifu, walikuja kimyakimya usiku na kunyakua watu.
Vibarua wenye woga walijenga vizuizi vya miiba kuzunguka kambi zao, waliwasha mioto na kuiacha iendelee kuwaka, na kuajiri walinzi ambao wangepiga mapipa matupu ya mafuta katika matumaini ya kuwazuia hao wanyama. Kufikia Desemba wafanyakazi walikuwa wametishwa sana na simba hao hivi kwamba wengine wao walisimamisha garimoshi lililokuwa likirudi Mombasa kwa kujilaza juu ya reli, kisha karibu 500 kati yao wakaingia ndani ya gari hilo. Ni wafanyakazi wapatao 48 tu waliobaki. Kwa majuma matatu yaliyofuata ujenzi ulisimama huku wafanyakazi wakijenga vibanda vya kuzuia simba.
Hatimaye, simba hao waliuawa, na kazi ikaanza tena.
Magumu Mengineyo
Kufikia katikati ya mwaka wa 1899 reli ilifika Nairobi. Kutoka hapo reli ilielekea upande wa magharibi, ikiteremka chini kwenye Bonde la Ufa kwa zaidi ya meta 400 kisha ikapanda kwenye upande mwingine kupitia misitu minene na kuvuka bonde lenye kina mpaka ikafika Mau Summit, yenye mwinuko wa meta 2,600.
Kulikuwa na magumu mengine licha ya magumu yaliyokuwako ya kujenga reli kwenye mandhari yenye mawemawe. Kwa kielelezo, wapiganaji wa maeneo fulani walikuwa wakiingia katika kambi hizo na kunyakua vifaa vya ujenzi—nyaya za simu ili kutengeneza vito, vilevile komeo, ribiti na reli ili kutengeneza silaha. Akieleza kuhusu jambo hili, Sir Charles Eliot, aliyekuwa kamishna wa Afrika Mashariki aliandika hivi: “Ebu wazia idadi ya visa vya wizi ambavyo vingetokea kwenye reli ya Ulaya ikiwa nyaya za simu zingeonwa kuwa vito vya lulu na reli kuwa bunduki za michezo za hali ya juu . . . Haishangazi kwamba [jamaa] wa huko walishawishika kuiba.”
Mkondo wa Mwisho
Wafanyakazi wa reli walipokaribia kilometa 10 za mwisho kuelekea Ziwa Viktoria, kambi yao ilivamiwa na ugonjwa wa kuhara damu na malaria. Nusu ya wafanyakazi walikuwa wagonjwa. Wakati huohuo, mvua ikaja, na kufanya ardhi iliyokuwa matope-matope kuwa kinamasi. Matuta ya reli yakawa mororo sana hivi kwamba magarimoshi yaliyokuwa yakibeba vifaa vya ujenzi yalipasa kupakuliwa yakiwa mwendoni; ama sivyo yangepinduka na kuzama ndani ya matope. Mfanyakazi mmoja afafanua garimoshi moja kuwa “likija polepole na kwa tahadhari, likitikisika upande-upande, likijongea juu na chini kama merikebu iliyo katika bahari yenye mawimbi, na likirusha matope kwa meta tatu kila upande.”
Hatimaye, mnamo Desemba 21, 1901, komeo ya mwisho ilipigiliwa katika reli ya mwisho kwenye Port Florence (sasa ni Kisumu), kwenye ufuo wa Ziwa Viktoria. Reli yote nzima yenye urefu wa kilometa 937 ilichukua muda wa miaka mitano na miezi minne kujenga na kugharimu dola 9,200,000. Zaidi ya vibarua 2,000 kati ya 31,983 walioletwa kutoka India, walikufa, wengine wakarudi India, na maelfu walibaki na kufanyiza jumuiya kubwa ya Waesia katika Afrika Mashariki ya sasa. Vituo 43 vya reli vilijengwa, pamoja na madaraja marefu 35 na zaidi ya madaraja na kalvati 1,000.
Mwandishi Elspeth Huxley aliiita “reli iliyohitaji ujasiri mwingi zaidi ulimwenguni.” Bado swali lilibaki, Je, reli hiyo ilistahili jitihada hizo, au kihalisi reli hiyo ilikuwa “reli ya kichaa,” kupotezwa kwa wakati mwingi sana, pesa na uhai?
Reli Hiyo Leo
Jibu la swali hilo lapatikana kwa kufikiria yaliyotukia katika miaka ipatayo 100 tangu reli hiyo ilipomalizika. Magarimoshi yaliyotumia kuni yalibadilishwa na magarimoshi yenye nguvu zaidi ya 200 ya kisasa ambayo hutumia diseli. Reli hiyo imepanuliwa kufikia makumi ya miji na majiji katika Kenya na Uganda. Imechangia sana katika ukuzi wa majiji makuu ya Nairobi na Kampala.
Leo reli hiyo inatimiza mambo mawili. Kwanza, inategemeka na ni salama katika kusafirisha abiria hadi mwisho wa safari zao. Pili, reli hiyo huwezesha kusafirishwa kwa shehena, kama vile simiti, kahawa, mashine, mbao, na vyakula. Shirika la Reli la Kenya linapata biashara kubwa katika kusafirisha mizigo hadi bara baada ya kupakuliwa kutoka kwenye meli.
Kwa wazi, reli hiyo imekuwa yenye thamani kubwa kwa Afrika Mashariki. Labda siku moja utafurahia kusafiri kwenye reli hii yenye sifa ambayo wakati mmoja iliitwa “reli ya kichaa.”
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 24]
SAFIRI KWA GARIMOSHI
Kwa watalii na wenyeji pia, garimoshi ni njia ya usafiri ipendwayo sana, hasa kati ya Mombasa na Nairobi. Magarimoshi ya abiria huondoka Nairobi na Mombasa saa 1:00 kamili za jioni kila siku. Ikiwa unasafiri kwa daraja la kwanza au la pili, kabla ya kuingia unatazama matangazo kwenye ubao ili kujua behewa na mahali kilipo chumba chako. Mtumishi aliyesimama karibu akuuliza kama unataka kula chakula cha jioni saa 1:15 au saa 2:30. Unapochagua anakupa kuponi inayofaa.
Unapanda. King’ora cha garimoshi kinapigwa na muziki waanza kucheza wakati garimoshi lianzapo mwendo kutoka katika stesheni.
Wakati wa chakula cha jioni ufikapo, mtu fulani hutembea kwenye kijia chembamba akicheza marimba ya mkono ili kukujulisha kwamba chakula kiko tayari. Kwenye chumba cha kulia, unaagiza chakula kilicho kwenye orodha ya vyakula; na unapokula, mfanyakazi aingia chumbani mwako ili kukutandikia kitanda.
Mkondo wa kwanza wa safari huwa usiku. Ingawa hivyo kabla ya kwenda kulala, huenda ukataka kuzima taa za chumba chako, kuchungulia nje ya dirisha lako, na kujiuliza: ‘Je, taswira na vivuli hivyo katika mbalamwezi ni tembo na simba, au ni vichaka na miti tu? Maisha yalikuwaje kulala hapa nje karibu miaka 100 iliyopita wakati reli ilipokuwa ikijengwa? Je, wakati huo ningaliogopa kulala nje? Namna gani sasa?’
Safari hiyo huchukua muda unaopungua saa 14, kwa hiyo unaweza kuona mengi baada ya machweo kuangaza mandhari ya Kiafrika. Ikiwa unasafiri kuelekea Mombasa, jua la asubuhi huchomoza juu ya msitu wa miiba, kisha baadaye juu ya minazi na kisha kwenye nyasi na nyua zilizokatwa, na majengo ya kisasa ya Mombasa. Wakulima hulima kwa mikono na watoto wasiokuwa na viatu huwapungia mkono na kuwasalimu kwa shauku abiria walio ndani ya garimoshi.
Ikiwa unasafiri kuelekea Nairobi, nuru ya kwanza hutokea unapopitia nyanda kubwa iliyo wazi. Ukiwa hapo ni rahisi kuona wanyama, hasa unapopita Mbuga ya Kitaifa ya Nairobi.
Ni jambo la kipekee kwelikweli. Ni kwenye garimoshi lipi uwezapo kufurahia kiamshakinywa huku ukichungulia dirishani na kuona kundi la punda milia au paa?
[Hisani]
Kenya Railways
[Ramani/Picha katika ukurasa wa 23]
KENYA
Ziwa Viktoria
Kisumu
NAIROBI
Tsavo
Mombasa
BAHARI YA HINDI
[Hisani]
Tufe: Mountain High Maps® Copyright © 1997 Digital Wisdom, Inc.
Ramani ya Afrika kwenye tufe: The Complete Encyclopedia of Illustration/J. G. Heck
Tandala wa kiume na wa kike. Lydekker
Magarimoshi: Kenya Railways
Simba jike. Century Magazine