Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g94 7/8 kur. 24-27
  • Usiku Mmoja Kwenye Opera

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Usiku Mmoja Kwenye Opera
  • Amkeni!—1994
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Kwenye Opera
  • Ni Mambo Gani Huendelea Nyuma ya Jukwaa?
  • Opera Zenye Msingi wa Biblia
  • Jioni ya Kusisimua
  • Kujifunza Kuimba Opera
    Amkeni!—2008
  • Opera—Katika Msitu
    Amkeni!—1997
  • Vikaragosi Vinapotumiwa Kuigiza
    Amkeni!—2008
  • Imeandikwa Kwamba Nitamwona
    Amkeni!—2004
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1994
g94 7/8 kur. 24-27

Usiku Mmoja Kwenye Opera

Na mleta-habari za Amkeni! katika Italia

MVUMO ulio kawaida ya okestra ikipiga muziki wa kujaribia ala za muziki wakoma kwa ghafula, na mianga yazimika. Yule kiongozi, kwa kukaribishwa na makofi ya muda mfupi, ashika njia kwenda jukwaani, akiwainamia wahudhuriaji kwa shukrani ya makofi yao. Halafu, baada ya kimya kingi, ainua mikono yake kisha atoa ishara ya kuamrisha okestra ianze mipigo ya utangulizi. Je! wewe umepata kuwa na wasaa wa kusisimua jinsi hiyo, mwanzo wa opera? Je! ungependa kuupata? Opera ni nini hasa, na ilianzaje?

Opera ni tamasha ya tamthilia au maigizo ya kuchekesha yaliyopangiliwa muziki na kugawanywa kuwa na sehemu moja au zaidi; wahusika huigiza sehemu zao kwa kuimba. Opera hufanyizwa na mambo mbalimbali: maneno ya mchezo wa kuigizwa, au libreto, (kazi ya mwandikaji au mshairi); muziki ulioandikwa na mtungaji; kuimba; kucheza dansi; mandhari; na mavazi. Vipindi vya muziki hufanana na opera lakini hizo huwa na mtindo wa mambo mepesi kidogo. Labda wewe umeona filamu, kama West Side Story au Oklahoma, ambamo waigizaji huimba nyakati fulani badala ya kusema.

Kuna unamna-namna mwingi sana wa opera: Zile za Wolfgang Amadeus Mozart na Gioacchino Rossini zimeelezwa kuwa bora sana; zile za Giuseppe Verdi, kuwa za motomoto na za kugusa hisia; za Richard Wagner, zenye utata, za polepole, na kavu za hisia; za Georges Bizet, za mavutio mengi na uchangamshi; za Giacomo Puccini, za kusisimuka-sisimuka.

Muziki na wimbo ni kama ulianza wakati mmoja na historia ya kibinadamu. (Mwanzo 4:21; 31:27) Ala nyingi sana za muziki zimetengenezwa muda wote wa kuwako kwa wanadamu, na karibu na karne ya 11, mfumo fulani wa kuandika muziki ulianza kufuatwa. Vichapo vya marejezo vyasema kwamba opera ilianzia Florence, Italia, mwishoni mwa karne ya 16. Maneno mengi sana ya Kiitalia hutumiwa katika lugha nyingine nyingi kueleza mambo ya namna hii ya mtungo (opera, libreto, soprano, tenori), kutoa ushuhuda wa mianzo ya opera. Opera ilipokuwa ikienea sehemu mbalimbali za Ulaya, ilipatwa na mabadiliko mengi. Leo, nyumba za maonyesho ya opera zapatikana kotekote ulimwenguni.

Ili tujifunze mengi zaidi, acheni tusikilize maongezi kati ya Antonello, aishiye Milan, na Max rafiki yake, anayezuru kutoka Uswisi. Antonello na Max wanastareheka na kuchochewa isivyo kawaida jioni moja kwenye La Scala, Milan, mojapo nyumba za opera zilizo maarufu zaidi.

Kwenye Opera

Max: Nilisoma katika kitabu cha mwongozo ulichonipa kwamba La Scala ilizinduliwa katika 1778, na baada ya kuharibiwa vibaya kwa kupigwa kombora katika Vita ya Ulimwengu 2, ikajengwa upya na kuzinduliwa tena katika 1946. Kitabu hicho chasema pia kwamba yaweza kuchukua wasikilizaji zaidi ya 2,000.

Antonello: Sawasawa. Kama uwezavyo kuona, ilijengwa kwa muundo sanifu wa nusu-mviringo ulioanza kufuatwa na nyumba za opera zilizo nyingi kufikia karne za 17 na 19. Kuna tabaka sita za magawanyo ya sehemu zilizo kama masanduku za kukaliwa kuzunguka mahali pote; kuna nafasi iitwayo shimo ya kukaliwa na okestra mbele ya jukwaa. La Scala siyo nyumba ya opera iliyo ya zamani zaidi wala kubwa zaidi ulimwenguni. Umaarufu wayo watokana na uhakika wa kwamba maonyesho ya kwanza ya opera kadhaa yalifanywa hapa, na viongozi na waimbaji wengi maarufu wamefanya maonyesho hapa. Miongoni mwao alikuwako Arturo Toscanini aliyekuwa kiongozi maarufu, ambaye angeweza kuongoza bila kusoma maandishi ya muziki. Yasemekana usafiri wa miangwi ya sauti jumba La Scala ni safi kabisa, na huo ndio ubora wa msingi kwa nyumba ya opera, ambamo muziki wala sauti hazikuzwi na maikrofoni na vipaza-sauti.

Max: Je! waweza kunieleza jambo fulani juu ya waimbaji wa opera?

Antonello: Kuna sauti za namna sita. Tatu za kiume—bezi, baritoni, na tenori—na sauti tatu za kike zinazolingana—kontralto, mezo-soprano, na soprano. Bezi na kontralto ndizo nzito zaidi, hali tenori ndizo za wembamba wa juu zaidi katika kila kikundi. Baritoni na mezo-soprano ndizo sauti za katikati.

Ili mtu awe mwimbaji mzuri wa opera, ni lazima kwanza awe na kipawa cha sauti nzuri kisha ajifunze miaka mingi kwenye shule maalumu. Bila masomo hayo, ambayo hufundisha mwanafunzi jinsi ya kutumia hali bora za sauti yake kwa ukamili, hakuna mtu ambaye angeweza kuwa mwimbaji wa opera. Muda si muda utawaona waimbaji-peke. Utaona kwamba ingawa nyakati fulani wao huigiza sehemu za wavulana na wasichana halisi wenye mapenzi, hao wote, isipokuwa wachache, ni watu wakomavu, wenye maungo manene sana. Je! wajua sababu ni nini?

Max: La, ningetaka kuisikia sababu.

Antonello: Ni kwa sababu wao huanza kuvuma katika kazi-maisha yao wakiwa wamekomaa na lazima wawe na mwili wenye siha kuweza kuimba opera. Kupuliza na kupiga milio thabiti ya sauti za juu kwa kipindi kirefu si mchezo. Imesemwa kwamba Maria Callas yule mwimbaji maarufu wa sauti ya soprano, ambaye mara nyingi aliimbia hapa La Scala miaka ya 1950, alianza kuzorota baada ya kujinyima sana chakula ili akonde kidogo. Kwa hiyo, Max, badala ya kukengeushwa fikira na sura ya nje ya wale waimbaji-peke, wapaswa kuthamini sauti zao. Tazama! kiongozi ndiye yule anatokea. Chukua darubini za kuona opera ili uweze kuona vizuri zaidi waimbaji na maonyesho yote. Ingawa hivyo, nakushauri hivi: Ili ufaidike kabisa na opera, kaza fikira juu ya muziki na wimbo wenyewe kama tulivyofanya kuhusu kitendo cha kwanza.

Ni Mambo Gani Huendelea Nyuma ya Jukwaa?

Max: Makofi ni marefu wee! Waimbaji wana sauti za kuvutia kwelikweli. Sasa basi kipindi cha katikati kina urefu gani?

Antonello: Karibu dakika 20. Lakini wajua kinachoendelea nyuma ya pazia wakati wa kipindi hicho cha pumziko?

Max: Sijui.

Antonello: Ni pirikapirika nyingi ajabu! Kwa kuongozwa na msimamizi wa jukwaa, wasaidizi walio wataalamu wa jukwaa, waendesha-mashine, wanaumeme, maseremala, na wafanyakazi wengine wabomoa mapambo ya jukwaani kwa usawia mzuri ajabu na kuweka mandhari mpya mahali payo. Leo, nyumba za opera zina ufundi wa ki-siku-hizi wa kubadili mandhari upesi, nyakati fulani hata maonyesho yanapoendelea. Majukwaa yenye kuendeshwa na nguvu za mvuke, mitambo ya upandishaji, na mashine nyinginezo hutumiwa kuinua na kushusha sehemu za jukwaa. Nyumba zote za opera zina vifaa vya kufanya maajabu ya kimandhari—vifaa vitokezavyo mvuke kuchochea mawingu au ukungu, moshi, kelele ya mvua au upepo, au hata mfyatuko wa radi. Mfumo wa vimulikaji vya nguvu tofautitofauti waweza kufanyiza mandhari za namna-namna na miale ya nuru ya rangi za kustaajabisha.

Max: Tukiwa tumeketi hapa, twaiona na kuisikia opera. Lakini ni nini kinachoendelea nyuma ya jukwaa wakati wa maonyesho?

Antonello: Hilo ni jambo la kupendeza, Max. Tunapokuwa tukiyafurahia maonyesho kwa kustareheka, jeshi dogo la wafanyakazi linaendelea na shughuli zao nyuma ya jukwaa na kwenye mabapa ya jumba. Wazia ni nini lingetukia kama mwimbaji fulani, kikundi cha waimbaji, au wacheza-dansi hawangefanya miendo yao kwa wakati ufaao. Nyuma ya jukwaa, msaidizi au wasaidizi wa meneja wa jukwaa wafuatilia wimbo unaopigwa kwa kuangalia maandishi ya kimuziki ili wajue okestra imefika wapi, kisha wawatolea waimbaji ishara ya kwenda jukwaani kwa wakati ufaao. Kiongozi wa kwaya afanya hivyohivyo na kile kikundi cha waimbaji.

Kuna mwelekezi wa waigizaji katikati ya jukwaa, akiwa amefichwa asionwe na wahudhuriaji katika lile sanduku. Mwelekezi huyo (mwanamume au mwanamke) afuatilia miendo ya kiongozi wa okestra kwa kutazama televisheni ya mfumo wa ndani iliyowekwa karibu naye, kisha mwelekezi wa waigizaji atazama maandishi ya libreto na kuyatamka maneno yapasayo kufuatwa, akiwatangulia kidogo waimbaji-peke, ili mwimbaji fulani asije akasahau maneno fulani.

Mwishowe, mwelekezi wa maonyesho asimamia mabadiliko ya mandhari na miingio ya idadi kubwa za waigizaji na pia yuko macho kuwaangalia mafundi wa nguvu za umeme ili miale ya nuru ya rangi ielekezwe sehemu zifaazo za jukwaa kwa wakati ufaao. Mipango imefanywa ili jumba La Scala liwe na majukwaa mawili yenye kuzunguka au ya kupandisha watu juu kama nyumba za opera nyinginezo ili kurahisisha matayarisho ya mandhari na kufanya iwezekane kuandaa zaidi ya onyesho moja kwa wakati mmoja.

Max: Lo! watu hao wote na kazi zote hizo ili kuonyesha opera! Jamani!

Antonello: Eh ndiyo! Nyumba kubwa za opera zina kikundi cha kudumu cha okestra, kwaya, na dansi—mamia ya wasanii. Halafu tena kuna watu wengine wengi ukihesabu mafundi wote wa sanaa, wa cherehani, wa viatu, wa useremala, wasanii wa mapambo ya sura, mafundi wa nguvu za umeme, na mwanamandhari mmoja au wawili wa kutokeza na kupamba mandhari. Zaidi ya haya, wafanyakazi wahitajiwa kwa ajili ya usalama, usimamizi wa kazi, na huduma nyinginezo.

Opera Zenye Msingi wa Biblia

Max: Je! kuna opera zozote ambazo zimefanyizwa kutokana na Biblia?

Antonello: Ndiyo, nyingi. Opera imetumia mambo mengi—historia ya watu wa kale, hadithi za ubuni, hekaya za zile enzi za katikati, maandishi ya William Shakespeare na waandikaji wengine. Utungo uitwao Nabucco, ambao ni ufupisho wa “Nebukadreza,” uliotungwa na mtungaji Mwitalia Giuseppe Verdi, huwataja Wayahudi wakihamishwa Yerusalemu wakawe watumwa Babiloni. Gioacchino Rossini, mtungaji mwingine Mwitalia, alipanga utungo uitwao Mosè (Musa) uambatane na muziki naye mwanamuziki Mfaransa Charles-Camille Saint-Saëns akatunga Samson et Dalila, (Samsoni na Delila). Mawazo makuu ya drama hizi hayafuatilii Biblia kwa uangalifu mwingi, lakini inapendeza kujua kwamba opera tatu hizi zina jina la Mungu, Yehova.

Max: Kweli? Najua kwamba jina hilo limetajwa katika mitungo ya Handel na Bach, lakini sikujua kwamba limo pia katika tungo za muziki wa opera.

Antonello: Mwishoni mwa Nabucco, kile kikundi cha waimbaji chaimba juu ya ‘Yehova Mkuu,’ na kuhani mkuu Zekaria ataja jina la Mungu. Katika opera ya Rossini, Musa amwomba ‘Iehova’ amsaidie, hali katika Samson et Dalila, ‘Iehova’ au ‘Jehova’ atajwa mara kadhaa.

Max: Inapendeza sana.

Antonello: Halafu kuna opera nyingine kadhaa zilizofanyizwa kutokana na Biblia. Kati yazo kuna Salome, iliyotungwa na Richard Strauss; Moses und Aron (Musa na Haruni), iliyotungwa na Arnold Schönberg; na Debora e Jaele (Debora na Yaeli), iliyotungwa na Ildebrando Pizzetti. Lakini ebu tazama! Kitendo cha mwisho kiko karibu kuanza.

Jioni ya Kusisimua

Antonello: Je! uliifurahia opera?

Max: Ndiyo, hasa kwa sababu tayari nilikuwa nimefuata dokezo lako nikawa nimeisoma libreto na hivyo ningeweza kufuata wazo kuu la utungo. Ama sivyo huenda ikawa ingalikuwa vigumu kuelewa.

Antonello: Kwa kweli, haiwezekani kuelewa maneno yote yaimbwayo na waimbaji-peke na kile kikundi cha waimbaji, kwa kuwa nyakati fulani muziki huwa na mvumo mkubwa kuliko sauti za waimbaji, na nyakati fulani huwa ni vigumu kuzitofautisha sauti iwapo mipigo ni ya kiwango cha juu. Katika nyumba nyingi za opera sasa, wao huandaa vichwa vidogo au vichwa vya utangulizi ili wasikilizaji waweze kuelewa vizuri zaidi wazo kuu la utungo.

Max: Lilikuwa onyesho bora kabisa, Antonello. Kweli muziki na uimbaji mzuri hutufanya tumthamini Muumba, aliyempa mwanadamu zawadi ya sauti na uwezo wa kutunga, kupiga, na kuthamini muziki. Asante kwa kunipangia jioni ya kufurahisha na kusisimua jinsi hiyo.

[Picha katika ukurasa wa 24]

Jumba la La Scala

[Hisani]

Lelli & Masotti/Teatro alla Scala

[Picha katika ukurasa wa 25]

La Scala, Milan, Italia

[Hisani]

Lelli & Masotti/Teatro alla Scala

[Picha katika ukurasa wa 26]

Juu: Mandhari kutoka kwenye opera “Samson et Dalila”

[Hisani]

Winnie Klotz

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki