Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g97 5/22 kur. 14-17
  • Opera—Katika Msitu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Opera—Katika Msitu
  • Amkeni!—1997
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Uhusiano na Mpira
  • Kuleta Mambo Fulani ya Ulaya
  • Tokea Sherehe Zenye Kufurahisha Hadi Huzuni
  • Nyakati Nzuri Sana Tena
  • Ugemaji wa Mpira—Kazi Iathiriyo Maisha Yako
    Amkeni!—1996
  • Usiku Mmoja Kwenye Opera
    Amkeni!—1994
  • Kujifunza Kuimba Opera
    Amkeni!—2008
  • Mto Mkubwa wa Amazon Unawategemeza Mamilioni
    Amkeni!—2003
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1997
g97 5/22 kur. 14-17

Opera—Katika Msitu

Na mleta-habari wa Amkeni! katika Brazili

TUKITAZAMA kupitia dirisha la ndege, twaona mito miwili inayoelekeana—mto Solimões wenye rangi ya kijivu cha kimanjano na mto Negro wenye rangi ya hudhurungi ya matope-matope. Mito hiyo ikutanapo, maji yayo hayachanganyikani kabisa mpaka baada ya kuteremka kwa kilometa kumi. Karibu na hapo, ndege yatua Manaus, ambalo ni jiji kuu la Jimbo la Amazonas katika Brazili.

“Tuna misimu miwili hapa,” ndivyo wasemavyo watu wa Manaus. “Mvua hunyesha kila siku, au hunyesha siku nzima.” Lakini mvua haiwazuii wakazi milioni 1.5 kuendelea na hekaheka zao katika jiji hili lenye mambo ya kutofautiana. Baada ya kupita viwanda vya hali ya juu kwenye barabara pana na nyumba na majengo ya makazi kwenye barabara za milimani, punde si punde twafikia msongamano wa jiji, ambako majengo marefu na majumba ya fahari yanasa fikira. Twaweza kuona ni kwa nini pindi moja Manaus liliitwa Paris la msituni. Hata hivyo, jengo moja maridadi hasa limejitokeza sana—jumba la opera.

“Kuna majumba ya opera sehemu nyingi,” asema Inês Lima Daou, mkurugenzi wa jumba hilo, “lakini hili Teatro Amazonas ni tofauti. Lipo mahali palipojitenga sana.” Jumba hilo zuri lilipataje kuwapo katikati ya msitu wa mvua ulio mkubwa zaidi ulimwenguni?

Uhusiano na Mpira

Katika 1669, Nahodha Francisco da Mota Falcão wa Ureno alijenga ngome msituni aliyoiita Fortaleza de São José do Rio Negro. Baada ya kubadilishwa jina mara kadhaa, katika 1856 iliitwa Manaus kutokana na jina la kabila la Wahindi wa eneo hilo waitwao Manáos. Kufikia 1900, watu 50,000 walikuwa wamemiminika Manaus. Ni nini kilichovutia umati huo? Ni Hevea brasiliensis, au mpira, ambao ni mti wa asili wa eneo la mito la Amazon.

Wakoloni Wareno waliowaona Wahindi wakicheza mipira mizito iliyotengenezwa kwa utomvu uliotolewa kwenye miti hiyo. Upesi, wakoloni waliona njia nyingine ya kutumia utomvu huo unaofanana na maziwa. Katika 1750, Mfalme wa Ureno Dom José alikuwa akipeleka viatu vyake Brazili ili viwekewe vitu vya kukinza maji. Kufikia 1800, Brazili ilikuwa ikisafirisha viatu vya mpira kwenda New England katika Amerika Kaskazini. Lakini, uvumbuzi wa Charles Goodyear wa kutayarisha mpira kuwa bora katika 1839 na haki ya pekee ya John Dunlop ya kutengeneza magurudumu katika 1888 uliharakisha mwendo wa ‘kukimbilia mpira.’ Ulimwengu ukahitaji mpira.

Si muda mrefu baadaye, karibu Wabrazili 200,000 walikuwa wakigema mpira, wakigema miti ipatayo milioni 80 iliyotawanyika katika msitu wa mvua karibu na Manaus.

Miaka ya kichaa cha mali ikaleta mjini umeme, simu, na hata vigari vya reli—vya kwanza katika Amerika Kusini. Matajiri wa mpira walijenga nyumba kubwa-kubwa na wakati wa mlo walitumia vitambaa vilivyotoka Ireland, na familia zao zilikuwa zikisafiri mara nyingi kwenda Ulaya na kurudi ili kufurahia utamaduni—kutia ndani opera. Punde si punde, wao walitaka jumba la opera kama yale yaliyo Ulaya.

Kuleta Mambo Fulani ya Ulaya

Tamaa ya kuwa na opera ikaanza kutimizwa katika 1881, wakati jiji hilo lilipochagua mahali kwenye mlima uliopo kati ya mito miwili, kando ya kanisa na kuzingirwa kwa msitu. Kisha, meli zilizojaa vifaa vya ujenzi zikavuka Bahari-Kuu ya Atlantiki na kuendelea kwa kilometa nyingine 1,300 kufuata Mto Amazon hadi Manaus.

Lakini ngoja kidogo! Kwa nini kuna kuba juu ya jengo hili lililoiga ujenzi wa kale? Ni kweli kwamba kuba hilo halikuwa sehemu ya jengo la awali, lakini mmojawapo wahandisi alihudhuria wonyesho fulani nchini Ufaransa, akaona kuba akalipenda na kulinunua. Karibu vigae 36,000 vya Ujerumani vyenye rangi ya kijani-kibichi na kimanjano vilitumiwa kurembesha hilo kuba.

Ukumbi huo wenye umbo la nusu duara uliweza kutoshea viti 700 vyenye viegemeo vya hinzirani kwenye jumba la chini, viti 12 katika vijumba maalumu, na viti 5 katika kila vijumba 90 vya kipekee vilivyokuwa katika roshani tatu za juu. Ili kupata vijumba vya kipekee, familia tajiri zilitoa vizuia-uso 22 vya Ugiriki, ambavyo viliwekwa juu ya nguzo kwa heshima ya watungaji, wanamuziki, na waandikaji wa tamthilia wa Ulaya.

Mng’ao ulio ndani ya jumba la opera hulifanya litazamishe kwelikweli. Katikati ya ukumbi kuna kinara cha taa kinachoning’inia kilichotengenezwa Ufaransa, na kupambwa kwa fuwele za Italia. Hicho chaweza kushushwa ili taa zibadilishwe au kufanyiwa usafi. Taa 166 za shaba zenye vifuniko 1,630 za vioo vyenye umbo la tulipu huongezea umaridadi wa kuta na kudhihirisha zaidi michoro.

Crispim do Amaral, mchoraji Mbrazili wa karne ya 19 aliyeishi Paris na kusomea Italia, alichora kwenye dari mandhari nne—opera, dansi, muziki, na msiba. Alifanikiwa katika kukufanya udhani kwamba unasimama chini ya Eiffel Tower. Katika pazia nzito kwenye jukwaa, alichora jambo lisilo la kawaida—kukutana kwa mito miwili inayofanyiza Amazon. Pazia hilo lenye miaka 100 halijikunji bali huingia moja kwa moja ndani ya kuba—na hivyo kupunguza kuharibika kwa ule mchoro.

Katika orofa ya pili kuna ukumbi wa kuchezea dansi, ambako kwenye kila upande wa chumba kuna kioo kirefu cha Ufaransa kinachoakisi vinara 32 vya taa vya Italia. Wangavu humulika michoro ya wanyama na mimea ya Amazon iliyochorwa na Domenico de Angelis, mchoraji Mwitalia. Ili kufanya nguzo zionekane kuwa nzuri, hizo nguzo za kalibu za chuma zilipigwa plasta na kuchorwa hivi kwamba zinafanana na marumaru. Gonga viegemeo vya roshani vinavyofanana na marumaru; na kumbe ni mbao. Sakafu iliyong’arishwa ilitengenezwa kwa njia ya Kifaransa, vigae 12,000 vya mbao vikiwekwa pamoja bila kushikanishwa kwa msumari au gundi. Jambo moja tu la Kibrazili lilikuwa mbao za sakafu, madawati, na meza. Tunaweza kuwazia kwamba ni lazima kila mtu alihisi amestarehe—baridi nzuri. Kwa nini?

Wajenzi walikuwa wameweka mawe ya barabara zinazozingira mahali hapo kwa kitu fulani chenye mpira. Kwa werevu jambo hilo lilifunika kelele zinazofanywa na wenye kuchelewa waliokuwa wakija katika magari ya kukokotwa kwa farasi. Pia iliruhusu milango ibaki wazi ili upepo mwanana uweze kupuliza ndani kupitia viti vyenye hinzirani na kutoa kitulizo fulani kutokana na joto.

Tokea Sherehe Zenye Kufurahisha Hadi Huzuni

Katika usiku wa ufunguzi katika 1896, vibubujisha maji vilivyo mbele ya jumba hilo la opera vilibubujisha divai milango ilipofunguliwa. Ujenzi huo ulikuwa umechukua miaka 15 na kugharimu dola milioni 10. Hilo lilikuwa jumba tukufu kwa ajili ya sauti tukufu. Katika miaka ambayo imepita watu wenye kuimba solo na vikundi vya kuimba kutoka Italia, Ufaransa, Ureno, na Hispania vilikuja kucheza La Bohème ya Puccini na Rigoletto na Il Trovatore za Verdi. Ingawa maradhi ya kitropiki kama vile kipindupindu, malaria, na homa ya kimanjano yalisababisha waimbaji fulani wasije, kukawa na tisho jingine kwa jumba hilo la opera—kuanguka kwa biashara ya mpira. Kukawa na tisho la kuanguka kwa Manaus.—Ona sanduku “Utekwa Ulioangamiza Biashara ya Mpira na Kukomesha Jumba la Opera.”

Katika 1923, hali ya Brazili ya kudhibiti mpira ilianguka. Kwa kasi sana, makabaila, wabashiri wa mambo ya kifedha, wafanyabiashara, na makahaba wakahama mji huo, likifanya Manaus kuwa mwitu wenye magugu tu. Na vipi jumba la opera? Vyumba vya ziada vikawa bohari za mpira, na jukwaa likawa uwanja wa kandanda unaochezwa ndani ya jumba!

Nyakati Nzuri Sana Tena

Baadaye, Manaus likawa mahali pa watalii wa mambo ya mazingira kujitayarishia waliokuja kuvumbua mafumbo ya msitu huo wa mvua. Wengine walikuwa wakija kwa siku chache kushika nyoka, kulisha kasuku, au kugusa-gusa mnyama aitwaye sloth. Urekebisho wa jumba la opera ungalifanya Manaus liwe uvutio wa aina tofauti!

Basi, katika 1974, jumba hilo lilifanyiwa marekebisho ghali sana ili kuhifadhi mtindo walo wa zamani na kuliboresha kiufundi. Taa, vioo, na fanicha zilisafishwa. Mafundisanifu waliweka mfumo wa hidrolia wa kusogeza jukwaa la okestra juu na chini. Sakafu mpya iliwekwa kwenye jukwaa na mfumo mpya wa sauti ukawekwa kwenye sehemu ya nyuma ya jukwaa pamoja na taa na vifaa vya vidio. Waliweka kidhibiti-halijoto kwenye chumba cha chini, chini ya viti.

Kisha okestra kubwa kutoka Rio de Janeiro ilirudisha utamaduni kwenye jumba hilo. Baadaye, mcheza-baleti wa kike aliye mashuhuri Margot Fonteyn alicheza mchezo uitwao Swan Lake na kuacha viatu vyake vya kuchezea baleti ambavyo vimeonyeshwa katika jumba la makumbusho la jumba hilo la opera.

Kwa ajili ya starehe, umaridadi, na usalama, marekebisho zaidi yalihitajika. Baada ya utafiti mwingi na plani ya uangalifu, wafanyakazi 600 na mafundisanifu 30 walimiminikia jumba hilo kwa miaka minne. Walipata ile rangi ya zamani ya waridi chini ya tabaka nane za rangi. Lile kuba lilihitaji kurekebishwa. Vigae vya zamani viliondolewa. Vilibadilishwa na vigae vipya vinavyofanana navyo ambavyo vilitengenezwa Brazili. Viti vilifanyizwa upya kwa mahameli nyekundu ya Kifaransa. Visu na burashi zilitumiwa kufanya marekebisho madogo kwenye michoro iliyokuwa rahisi kuharibika. Kwa ubaya, unyevuanga ulikuwa umeharibu michoro iliyo katika vijia, kwa hiyo vitambaa vya zari vya kijani vya Kichina vilichaguliwa kufunika paneli hizo. Isitoshe, mchwa walijaa kwenye nguzo za mbao na pia kwenye viegemeo vya roshani. Ili kuwaondosha, lita 13,790 za kiuwadudu ziliingizwa katika mbao.

Katika 1990, kulikuwa na sauti tukufu katika jumba hilo tukufu tena. Nyimbo za mwimbaji wa soprano wa Brazili Celine Imbert na nyimbo za piano za Nelson Freire ziliongezea jumba hilo fahari.

Je, hiyo ilikuwa sauti ya kengele? Ndiyo, hiyo ni kengele inayotutahadharisha kwamba wonyesho utaanza baada ya dakika tano.

“Ili kuadhimisha jumba hilo la Teatro Amazonas lenye miaka 100,” asema mkurugenzi wa jumba hilo Daou, “Tumealika mwimbaji maarufu wa sauti ya tenor José Carreras. Alivijaribu vyombo (‘akaviona kuwa bora’).” Jioni hiyo ilimalizikia kwa mchezo wa dansi katika chumba cha kuchezea dansi. Sherehe hizo ziliendelea kwa ziara ya mwongoza muziki Zubin Mehta, mwimbaji wa sauti ya tenor Luciano Pavarotti, na kikundi fulani cha Argentina kilicheza opera yenye kuvutia sana iitwayo Carmen.

Hiyo ilikuwa kengele ya kututahadharisha kwamba kungali kuna dakika tatu. Ni afadhali tuketi.

Mchana kutwa wafanyakazi 60 wamekuwa na hekaheka nyingi bila kujulikana katika kutayarisha wonyesho huo. Nao watakuwa na maonyesho zaidi—michezo ya jazi, michezo ya kitamaduni, na michezo ya kuigiza. Lakini usiku huu ni baleti.

Kengele ya dakika moja. Ukimya.

Basi utakuja lini kwenye jumba la opera katika msitu?

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa17]

Utekwa Ulioangamiza Biashara ya Mpira na Kukomesha Jumba la Opera

Katika 1876, Henry Wickham, mjasiri mmoja mchanga wa Uingereza, alifanya njama ambayo iliangamiza biashara yenye kunawiri ya mpira. Kwa msaada wa Wahindi, yeye “aliteka” mbegu bora 70,000 aina ya Hevea brasiliensis zilizokusanywa katika msitu wa Amazon, akazipakia kwenye meli, na kuzipitisha kiharamu katika forodha ya Brazili kwa kisingizio cha kwamba hizo ni “sampuli za mimea nadra sana zilizokuwa zikipelekewa Malkia Victoria.” Alizitunza katika mashua akivuka Atlantiki na kuzipeleka mbio kwa gari-moshi lililokodishwa hadi kwenye mabanda ya kukuzia mimea ya Royal Botanic Gardens kule Kew, Uingereza, ambako mbegu zilichipuka majuma machache baadaye. Kutoka huko, zilisafirishwa hadi Asia na kupandwa katika ardhi ya mabwawa ya Ceylon na Peninsula ya Malay. Kufikia 1912, mbegu hizo zilizotekwa zilikuwa zimekuwa mashamba ya mipira isiyoweza kushikwa na maradhi, na kufikia wakati miti hiyo iliweza kutokeza utomvu, chasema chanzo kimoja cha habari, “unawiri wa biashara ya mpira ya Brazili [ulikuwa umeanguka] kabisa.”

[Ramani katika ukurasa wa 14]

Manaus

[Hisani]

Mountain High Maps® Copyright © 1995 Digital Wisdom, Inc.

[Picha katika ukurasa wa 15]

Mito hii miwili hukataa kuchanganyikana

[Picha katika ukurasa wa 15]

Kuba la jumba la opera—lenye kusaidia kujua mahali ulipo

[Picha katika ukurasa wa 16]

Jengo zuri katika msitu wa mvua

[Picha katika ukurasa wa 17]

Jumba tukufu tena

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki