Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g96 8/22 kur. 18-20
  • Ugemaji wa Mpira—Kazi Iathiriyo Maisha Yako

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Ugemaji wa Mpira—Kazi Iathiriyo Maisha Yako
  • Amkeni!—1996
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Maelfu ya Bidhaa za Mpira
  • Ugemaji wa Miti
  • Opera—Katika Msitu
    Amkeni!—1997
  • Tairi Zinaweza Kuathiri Uhai Wako!
    Amkeni!—2004
  • Nzumari za Nyasi za Visiwa vya Solomon
    Amkeni!—2002
  • Kuutazama Ulimwengu
    Amkeni!—1993
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1996
g96 8/22 kur. 18-20

Ugemaji wa Mpira—Kazi Iathiriyo Maisha Yako

Na mleta-habari wa Amkeni! katika Nigeria

SAA 11 alfajiri, msitu wa mvua wa Nigeria una giza na baridi. Katika nyumba ya udongo na matufali katikati ya msitu huo, John aamka na kuvaa mavazi yake. Kisha aelekea katika giza la usiku, akiwa amebeba taa, ndoo ya plastiki, na kisu kifupi kilicho na bapa lililojikunja. Kwa muda ufuatao wa saa nne, yeye husonga kutoka mti hadi mti, akikata mifuo katika gome la kila mti.

Hili ndilo tukio la kwanza katika mfululizo wa matukio ambayo huenda hatimaye yataathiri maisha yako. Jinsi gani? Kwa sababu miti anayokata John ni mipira. Na mpira ni mmojawapo rasilimali zetu zenye thamani na zenye kutumiwa sana kupita zote.

Maelfu ya Bidhaa za Mpira

Wazia tu fungu ambalo mpira huchangia katika maisha yako. Soli na visigino vya viatu vyako huenda vimetengenezwa kwa mpira. Sehemu ya chini ya zulia lako na fanicha huenda zina mpira-sifongo. Ukanda mnyumbufu katika mavazi yako yaelekea ulitengenezwa kutokana na mpira. Kunaponyesha, huenda ukachukua koti la mvua na mabuti yaliyotengenezwa kwa mpira. Je, waenda kuogelea? Mavazi ya kuogelea, miwani, na mapezi huwa na mpira. Hutaki kuogelea? Labda utapendelea kuelea tu kwenye chelezo cha mpira au kucheza na mpira wa ufuoni. Hapa na pale nyumbani mwako huenda kuna kanda za mpira, vifutaji, na gundi za mpira. Unapolala leo usiku, huenda ukapumzika kwenye godoro na mto uliotengenezwa kutokana na bidhaa za mpira. Ikiwa wahisi baridi, huenda ukakumbatia kiriba cha mpira cha maji moto.

Kando na vitu hivyo, kuna vifaa vingi ambavyo kwa hakika havingefanya kazi vizuri bila visehemu vya mpira—pete za mpira za kukazia parafujo, mikanda, gasketi, mabomba ya mpira ya kutupia maji, rola za kuchapa, au vali. Kwa kielelezo, gari la wastani lina visehemu 600 vya mpira. Kwa ujumla kulingana na The World Book Encyclopedia, bidhaa za mpira kati ya 40,000 na 50,000 hutengenezwa.

Ni nini kifanyacho mpira uwe na mafaa sana? Huo hauliki upesi, hukinza joto, hunyumbuka, hukinza maji, hubana hewa, na hufyonza mshtuko. Fikiria gurudumu, liwe la baiskeli, la gari, au la ndege. Kwa sababu ni la mpira, gurudumu haliliki haraka kwa kugusana daima na barabara, wala halitaungua kwa msuguano wa daima na barabara. Unapoendesha gari kupitia vidimbwi vyenye maji, huna haja ya kuhofu kwamba gurudumu litajaa maji na kuoza; wala halitalika. Mpira hauzuii maji kuingia ndani ya gurudumu tu bali pia huzuia hewa iliyoko ndani isitoke nje. Isitoshe, unaposafiri hali ya mpira ya kufyonza mshtuko katika magurudumu yako husaidia usihisi mshtuko kutokana na vilima vya barabara. Kwa kweli, bila mpira, itakuwa vigumu sana kwa watengenezaji kutengeneza magurudumu.

Basi yaelekea utakubali kwamba wagemaji wa mpira kama vile John huandaa utumishi wenye thamani unaoathiri maisha zetu kwa njia nzuri. Bila shaka, si mipira yote itokanayo na miti. Mipira ya sanisia, itokezwayo kutokana na kemikali, ni sehemu kubwa ya kiwanda cha mpira. Aina zote mbili za mpira zina nguvu na udhaifu wazo. Bidhaa nyingi zaweza kutumia yoyote kati yazo, na chaguo mara nyingi hufanywa kulingana na gharama. Bidhaa nyinginezo hutumia mchanganyiko wa mpira wa sanisia na wa kiasili. Magurudumu mengi ya magari yana mpira wa sanisia kuliko wa kiasili. Hata hivyo, kwa sababu mpira wa sanisia haukinzi joto sana, sehemu kubwa ya mpira wa kiasili hutumiwa katika magurudumu ya magari ya kushindana, malori, mabasi, na ndege.

Ugemaji wa Miti

Mipira hukua vyema zaidi katika tabia-nchi yenye joto na maji karibu na ikweta. Mwingi wa mpira wa kiasili hutoka katika mashamba katika Asia ya Kusini-Mashariki, hasa Malasia na Indonesia. Uliobaki hutoka Amerika Kusini na vilevile Afrika Magharibi na ya Kati.

John hagemi mti hadi unapotimia umri wa miaka sita hivi. Baada ya hapo mti utatokeza mpira kwa miaka 25 hadi 30 ijayo nao utakua kufikia kimo cha meta 20. Wakati mti wa mpira “unapostaafu” kutoka kutokeza mpira, huenda ukaendelea kukua, hadi kimo cha meta 40, nao waweza kuishi hadi umri wa uzee wa miaka 100 au zaidi.

Mpira ukitoka moja kwa moja mtini hufanana zaidi na maziwa kuliko gurudumu la gari. Dutu hii ya kimaziwa, iitwayo lateksi, huwa na chembe ndogo mno za mpira. Asilimia 35 hivi ya lateksi ni mpira. Iliyobaki ni maji hasa.

Ili kugema lateksi, John hufanya mkato wa ulalo kwenye gome. Mkato huu huenea kuzunguka nusu ya mti. Yeye huwa mwangalifu ili asikate kwa kina sana, kwa kuwa kufanya hivyo kutaharibu mti. Lateksi huanza kutiririka mara tu mkato ufanywapo; hiyo hudondoka kufuata mfuo uliofanyizwa na mkato na kumwagika ndani ya kikombe cha mwani ambacho John amekishikiza kwenye mti. Mmwagiko huo huendelea kwa muda wa saa mbili au tatu, kisha wakoma.

Siku moja au mbili baadaye, wakati John atakapougema mti huo tena, yeye atafanya mkato mwingine chini tu ya ule wa kwanza. Wakati ufuatao atakata chini ya huo. Hatimaye, kipande chakatwa kutoka gome la huo mti. Sasa John ataanza kugema sehemu nyingine ya huo mti, akiruhusu kipande hicho kipone kabisa kwa ajili ya ugemaji wa wakati ujao.

John afanya kazi haraka, akisonga kupitia msitu huo wenye ukimya akiwa peke yake, akikata miti na kufanya lateksi itiririke. Baadaye, yeye azuru tena kila mti na kukusanya katika ndoo yake lateksi iliyojikusanya. Kisha, John aongeza asidi fomi na maji katika lateksi. Hiyo huifanya iwe nzito na kuigandisha kama vile siki hugandisha maziwa. Kisha John abeba ndoo ya lateksi kichwani pake hadi kwenye barabara kuu, ambapo itachukuliwa na lori litokalo katika kiwanda cha kutengeneza mpira kilichoko karibu.

Sasa John arudi nyumbani kuoga, kula na kupumzika. Baadaye alasiri, anapoondoka nyumbani kwake tena, amevalia kinadhifu na abeba mkoba wa vitabu mkononi. Wakati huu hataenda mti hadi mti bali nyumba hadi nyumba. Akiwa mhudumu painia wa kawaida, John anashiriki kikamili katika kazi ya kuhubiri na kufanya wanafunzi.

John anapoongoza funzo la Biblia la kwanza kwa siku hiyo, lateksi aliyokusanya itakuwa imefika kwenye kiwanda cha utengenezaji. Huko mpira utatenganishwa na maji, kukaushwa, na kukandamizwa kuwa vifurushi kwa ajili ya kusafirishwa. Muda si muda utakuwa safarini kuelekea Uingereza, Japani, au Marekani. Biashara ya mpira wa kiasili ya ulimwenguni pote hutokeza zaidi ya tani milioni tano za mpira kila mwaka. Ingawa huenda isiwe hivyo, kuna uwezekano kwamba mpira katika soli za viatu vyako vijavyo utatokana na mti uliogemwa na John.

[Picha katika ukurasa wa 18]

John akiwa kazini akigema mti wa mpira

[Picha katika ukurasa wa 20]

John ashiriki katika huduma ya Kikristo

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki