Kuutazama Ulimwengu
Tahadhari ya Kifua-Kikuu
Shirika la Afya Uliwenguni (WHO) limetangaza kwamba ugonjwa wa kifua-kikuu ni maradhi ya dharura ulimwenguni pote, likionya kwamba zaidi ya watu milioni 30 watakufa kutokana na maradhi hayo katika miaka kumi ijayo isipokuwa jambo fulani lifanywe kuzuia mweneo wayo. Ingawa kifua-kikuu chaweza kuzuiwa na kutibiwa, hesabu ya visa vyacho imeongezeka sana katika miaka ya karibuni. Sasa, watu milioni nane hushikwa na maradhi hayo kila mwaka. Kulingana na WHO, kuinuka tena kwa maradhi hayo kwa sehemu kwatokana na kupuuzwa kwa sera za umma na pia programu za kuyadhibiti yasiyosimamiwa vizuri. Jambo jingine lenye kusababisha ongezeko ni uhusiano wa karibu uliopo kati ya kifua-kikuu na ambukizo la HIV (ile virusi iletayo UKIMWI). Mtu aliyeambukizwa HIV ana uwezekano wa mara 25 wa kushikwa na aina hatari ya kifua-kikuu chenye kuua. Zaidi ya asilimia 95 ya vifo vya kifua-kikuu hutokea katika ulimwengu unaositawi.
Sehemu za Biblia Katika Lugha Zaidi ya 2,000
Shirika la United Bible Societies (UBS) lilitangaza kwamba katika kipindi cha 1992, sehemu za Biblia zimetafsiriwa katika lugha 31 nyinginezo zaidi; kwa hiyo jumla ya hesabu ya lugha ambazo angalau kitabu kimoja cha Biblia chapatikana imefikia 2,009. Upesi hesabu hiyo itaongezeka zaidi kwa sababu shirika la UBS linatafsiri sehemu za Biblia katika lugha 419 nyinginezo zaidi. Biblia kamili sasa zapatikana katika lugha 329 na “Agano Jipya” katika lugha nyinginezo 770. “Makadirio ya jumla kuu ya lugha zote za ulimwengu,” laandika Ecumenical Press Service, “ni kati ya 5,000 hadi 6,500.” Kwa kupendeza, kufikia 1993, jumla kuu ya Biblia zilizotokezwa zikiwa kamili au kwa sehemu na Watchtower Bible and Tract Society of New York, Inc., zilikuwa zaidi ya milioni 83.
Magurudumu ya Zamani Yenye Mafaa
Katika Brazili, ni lazima magurudumu milioni 17 ya magari yabadilishwe kila mwaka. Hata hivyo, gazeti Superinteressante laripoti kwamba magurudumu hayo ya zamani yaweza kutumika vizuri, yaani, kutengeneza tena mpira na kuuchanganya na lami ngumu (asfalti) ambayo imekusudiwa kumwagwa katika barabara zilizo kuu. Ingawa wazo la kutengenezwa upya kwa magurudumu ya mpira si jipya, matumizi ya magurudumu katika asfalti ni wazo jipya. Inatumainiwa kwamba utaratibu huo “utapunguza kabisa ile milima mikubwa ya takataka inayorundamana [duniani].”
UKIMWI Katika Kusini mwa Afrika
Mweneo wa UKIMWI katika maeneo ya Afrika yaliyo kusini zaidi waendelea bila kukoma. Katika kipindi cha 1992, watu zaidi ya 50 walikuwa wakipatikana kuwa wameambukizwa na virusi ya UKIMWI kila siku katika Afrika Kusini. Na kwa sababu hesabu hiyo haitii ndani wale wanaoishi katika majimbo yaliyo huru yenye wakazi wengi sana, hesabu ya kila siku ya watu walio katika hatari zaidi ya kupatwa na UKIMWI ni ya juu zaidi. Gazeti The Star la Johannesburg, Afrika Kusini, laripoti kwamba “mweneo wa kasi wa Ukimwi kotekote kusini mwa Afrika waonwa na watu wengi kuwa moja ya matatizo makubwa zaidi ya miongo ya miaka inayokuja.”
Kichaa cha Mbwa Charudi
Maradhi ya kichaa cha mbwa, kilichokuwa kimeondolewa kabisa kutoka mkoa wa Natal wa Afrika Kusini, sasa kinaongezeka sana. Katika Natal na nchi jirani Msumbiji, watu wengi wametoka mashambani na kuhamia sehemu za majiji, wakileta wanyama-vipenzi vyao pamoja nao. Programu za chanjo hazijaweza kuwafikia watu hao wote wenye kukosa makao. Katika 1992 zaidi ya visa 300 vya kichaa cha mbwa viliripotiwa katika eneo hilo. Vingi vya vifo 29 vilivyotokea vilihusu watoto. Paul Kloeck, mkurugenzi wa eneo hilo la huduma za wanyama, asema hivi kihuzuni: “Ni vigumu sana kufikia watu wengi wanaoishi katika makao ya muda waliyohamia.” Yeye asema hivi: “Jeuri ya kisiasa, makatazo ya kitamaduni na woga wa makusanyiko huzuia programu zetu.”
Ubuddha Pamoja na Jazz
Katika mchanganyiko wenye kushangaza, maelfu ya makuhani wa Buddha kutoka kotekote Japani walikusanyika pamoja na wachezaji mashuhuri wa muziki aina ya jazz katika Nippon Budokan ya Tokyo iliyo kubwa sana ili kutoa wonyesho wa muziki wa shomyo na jazz. Kwa msingi shomyo ni nyimbo za kutungwa papo hapo za wasutra, mtindo wa Kihindi, ambazo hazifanani kabisa na muziki wa Magharibi. Hata wakiwa na muziki wao wa aina tofauti, wanamuziki wa jazz hawakuwa na ugumu wowote wa kupatanisha muziki wao na ule wa kisutra. “Nafikiri mtungo wa papo hapo wahusiana kikaribu kwa njia fulani na kuamka tena kiroho kwa dini,” The Daily Yomiuri lilimnukuu mpiga kinanda maarufu wa jazz kuwa akisema maneno hayo. Yeye aliongezea hivi: “Nyakati fulani mimi huhisi kwamba mimi sichezi kinanda cha piano bali kwamba kuna nguvu fulani ya kiajabu kutoka katika ulimwengu tofauti inayocheza.”
Hofu ya Uhalifu Katika Ujerumani
Wajerumani 2 kati ya 3 huona vikundi vyenye siasa kali kuwa tisho kwa demokrasia katika nchi hiyo. Watu wengi zaidi ya nusu ya idadi yote ya watu wangependa serikali ya Taifa ichukue hatua zaidi katika kushughulika na waandamanaji wenye jeuri. Karibu asilimia 50 ya watu wakubali kwamba polisi wapaswa kutumia kwa ukawaida zaidi marungu na gesi ya kutoa machozi. Na kuhusu kupigana na uhalifu wenye kupangwa kwa utaratibu, kari-bu asilimia 60 wakubali kutumiwa kwa vifaa vya kusikiliza kisiri mazungumzo katika makao ya faragha. Hayo yalikuwa matokeo ya maoni ya watu wapatao 3,000 walioombwa maoni mwishoni mwa 1992 na Taasisi ya Emnid na kuripotiwa na gazeti Frankfurter Allgemeine Zeitung.
Hadithi ya Mapenzi ya Aina Tofauti
Hadithi za mapenzi zenye kushughulika na “mahaba” kati ya wanaume zimekuja kupendwa sana katika Japani katika miaka miwili ambayo imepita. Wasomaji wazo wenye bidii sana ni wanawake, hasa kutokea matineja hadi wenye umri wa miaka ya mapema ya 20. Gazeti Asahi Evening News chasema kwamba mwelekeo huo katika vitabu vya hadithi unaudhi wagoni wa jinsia-moja katika nchi hiyo. Lilimnukuu mwandikaji mmoja ambaye ni mgoni wa jinsia-moja, Masaki Sato, kuwa akisema hivi: “Katika maelezo ya kingono ya [hadithi hizo za mapenzi], wanaume wanakuwa shabaha ya udadisi wa wanawake.” Yeye alilalamika zaidi hivi: “Wanawake hupinga picha za wanawake zinazoonyeshwa na wanaume katika vitabu vya hadithi za kipornografia. Sasa wagoni wa jinsia-moja wamo katika hali kama hiyo.”
Watoto Wanaopotea
Mamia ya watoto hupotea bila kupatikana kila mwaka katika Italia. Wengi huondoka nyumbani asubuhi kwenda shule na huwa hawarudi tena. Katika 1992 pekee, watoto 734 walipotea, wakiwa 245 zaidi ya mwaka uliotangulia. Kulingana na ripoti iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Italia, jumla kuu ya visa vipya ilikuwa 3,063. Wasichana wengi hupotea kuliko wavulana.
Ni Nini Hukufanya Uwe Mwenye Furaha?
Kwa wazi, kuwa na fedha zaidi hakufanyi watu kuwa na furaha zaidi. Lasema gazeti Psychology Today: “Mara mapato yapitapo kiwango cha umaskini, kwa kushangaza ongezeko katika mapato hayahusiki na furaha ya binafsi.” Inasemwa kwamba mambo haya yanayofuata huwa muhimu katika kuwa na furaha: kuwa na mtazamo unaofaa wenye kuona mambo kihalisi; kuwa mwenye urafiki na kufanya marafiki; kuwa na hisia ya kudhibiti maisha yako, kunakotia ndani “kusimamia vyema wakati wako”; na kuwa na “imani ya kidini yenye utendaji.”
Si Kuchelewa Mno Kuweza Kuacha
Kadiri utakavyoacha kuvuta sigareti upesi iwezekanavyo, ndivyo hutaelekea sana kufa kutokana na kansa ya pafu. Uchunguzi wa karibuni wa Waamerika 900,000, laripoti The Lancet, ulifunua yafuatayo. Miongoni mwa watu wasiovuta sigareti, idadi ya watu waliokufa kutokana na kansa ya pafu kabla ya kufikia umri wa miaka 75 ilikuwa chini ya watu 50 kwa kila watu 100,000. Kwa wanaume walioacha kuvuta sigara wakiwa katika miaka yao ya 30, kiwango cha vifo vyao kiliongezeka kwa karibu watu 100 kwa kila watu 100,000. Kwa wale walioacha kuvuta sigara wakiwa katika miaka yao ya 60, vifo vyao viliongezeka kufikia watu 550 kwa kila watu 100,000. Miongoni mwa wavutaji ambao hawakuacha kamwe kuvuta sigara, hesabu ya vifo vya kansa ya pafu ilikuwa 1,250 kwa kila watu 100,000. Viwango vya vifo vya kansa ya pafu katika wanawake vilikuwa chini zaidi lakini vilionyesha kigezo icho hicho.
Makosa Katika Maabara
Mamia ya maelfu ya watu hufa au kuwa wagonjwa sana kila mwaka kwa sababu ya makosa yafanywayo katika maabara za kitiba, laeleza Shirika la Afya Ulimwenguni. Maabara huwa na fungu muhimu katika kupima damu na mnofu wa kibinadamu ili kugundua na kuthibitisha kuwapo kwa maradhi. Matokeo yasiyo ya kweli ya kupimwa yaweza kuongoza kwenye ugunduzi mbaya na tiba yenye kosa. Katika Aprili zaidi ya wastadi 90 kutoka ulimwenguni pote walikutana Geneva, Uswisi, ili kujadili tatizo hilo.
“Majiji Makubwa Zaidi”
“Kufikia mwisho wa karne hii, kutakuwa na ‘majiji makubwa zaidi’ 21 yenye idadi ya watu milioni 10 au zaidi,” lasema gazeti Time. “Kati ya hayo, 18 yatakuwa katika nchi zinazoendelea, kutia ndani baadhi ya mataifa maskini zaidi ulimwenguni.” Nchi 13 zimeorodheshwa kuwa tayari na watu milioni kumi au zaidi katika maeneo yazo ya majijini. Tokyo laongoza, likiwa na wakazi karibu milioni 26, likifuatwa na São Paulo, Jiji la New York, Jiji la Meksiko, Shanghai, Bombay, Los Angeles, Buenos Aires, Seoul, Beijing, Rio de Janeiro, Kalkutta, na Djakarta. Majiji fulani katika Afrika yanakuwa kwa kiwango cha asilimia 10 kila mwaka—kiwango cha kasi zaidi cha mweneo wa majiji kilichopata kurekodiwa—yasema Benki ya Dunia. Idadi kubwa zaidi huambatana na ongezeko la uchafuzi na tisho la maradhi.
Madai kwa Titanic
Wamilikaji wa vitu walipewa miezi mitatu ya kudai kitu chochote kati ya vile vitu 1,800 vilivyotolewa ndani ya meli Titanic, miaka saba baada ya meli hiyo iliyozama kupatikana katika maji baridi karibu na Newfoundland. Kwa sababu meli hiyo ilizama ikiwa katika safari yayo ya kwanza katika 1912, inaelekea kwamba wadai wengi watakuwa warithi wa wale watu 687 waliookoka msiba huo au wa wale watu 1,513 waliokufa. Mkusanyo huo watia ndani saa na johari za kila aina, sarafu, vitu vyenye kutengenezwa kwa ngozi, na vifaa vya kutengeneza nywele. Hata hivyo, kuthibitisha umilikaji kutakuwa jambo gumu kwa sababu ni vitu vichache vimeandikwa majina. Isitoshe, mtu yeyote atakaye kumiliki tena kitu fulani na aweza kuthibitisha kwamba yeye ndiye mmlikaji apaswa kuchangia gharama za dola milioni 5.5 za U.S. za msafara huo uliookoa vitu hivyo, kwa kutegemea bei ya sasa ya kitu hicho. Vitu ambavyo havitadaiwa vitakuwa mali ya shirika lililodhamini mradi huo. Kwa kushangaza, hakuna kitu chochote kati ya vitu hivyo vya maisha ya kila siku kilichotengenezwa kwa plastiki.