Shangwe ya Ushindi na Huzuni
“Historia ya kifua kikuu kwa kipindi cha miaka 30 iliyopita imekuwa ya shangwe ya ushindi na huzuni—shangwe ya ushindi ya wanasayansi ambao waliandaa njia za kudhibiti na hatimaye kuangamiza kabisa ugonjwa huo, na huzuni ya kushindwa kulikoenea pote kwa kutumia ugunduzi wao mbalimbali.”—J. R. Bignall, 1982.
KIFUA KIKUU kimekuwa kikiua kwa muda mrefu sana. Kiliwatesa Wainka wa Peru muda mrefu kabla Wazungu hawajasafiri kwa mashua kwenda Amerika ya Kusini. Kiliwashambulia Wamisri katika siku ambazo akina farao walikuwa wakitawala kwa fahari. Maandishi ya zamani yaonyesha kwamba kifua kikuu kilishambulia watu mashuhuri na wasio mashuhuri katika Babiloni ya kale, Ugiriki, na China.
Kuanzia karne ya 18 hadi mwanzoni mwa karne ya 20, kifua kikuu kilikuwa kisababishi kikuu cha kifo katika nchi za Magharibi. Hatimaye katika mwaka 1882, daktari Mjerumani Robert Koch alitangaza rasmi ugunduzi wake wa basila zisababishazo ugonjwa huo. Miaka 13 baadaye Wilhelm Röntgen aligundua eksirei, zikifanya iwezekane kugundua katika mapafu ya watu walio hai dalili za ugonjwa wa kifua kikuu. Kisha, katika mwaka 1921, wanasayansi Wafaransa walitokeza dawa ya chanjo dhidi ya kifua kikuu. Ikaitwa kwa heshima ya wanasayansi walioigundua, BCG (Bacillus Calmette-Guérin) mpaka sasa ndiyo chanjo pekee dhidi ya ugonjwa huo. Hata hivyo, kifua kikuu kiliendelea kusababisha vifo vingi.
Hatimaye, Ponyo!
Matabibu waliwapeleka wagonjwa wa kifua kikuu katika hospitali za magonjwa ya muda mrefu. Mara nyingi hospitali hizi zilijengwa milimani, ambapo wagonjwa wangeweza kupumzika na kupumua hewa safi. Kisha, katika mwaka 1944, madaktari katika Marekani waligundua streptomycin, kiuavijasumu cha kwanza kuwa na matokeo dhidi ya kifua kikuu. Maendeleo juu ya dawa nyingine dhidi ya kifua kikuu yalifuata kwa haraka. Hatimaye, wagonjwa wa kifua kikuu wangeweza kutibiwa, hata wakiwa nyumbani kwao.
Kadiri kiwango cha ambukizo kilivyopungua, wakati ujao ulionekana kuwa mzuri zaidi. Hospitali za magonjwa ya muda mrefu zilifungwa, na fedha kwa ajili ya utafiti wa kifua kikuu zilisimamishwa. Mipango ya kinga iliachwa, na wanasayansi na madaktari walitazamia sai nyingine za kitiba.
Ingawa kifua kikuu bado kilikuwa kikiua watu wengi katika nchi zinazoendelea, kwa hakika mambo yangekuwa mazuri. Kifua kikuu kilikuwa tatizo la wakati uliopita. Watu walifikiri hivyo, lakini walikosea.
Angamizi Larudi Tena
Katika miaka ya katikati ya 1980, kifua kikuu kilianza kurudi tena kwa njia ya kutisha na kwa kuangamiza. Kisha, katika Aprili 1993, Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) lilitangaza kifua kikuu “kuwa moja ya dharura ya duniani pote,” likiongeza kwamba “ugonjwa huo utaua zaidi ya watu milioni 30 katika mwongo mmoja ujao isipokuwa hatua za haraka zinachukuliwa kuzuia kusambaa kwake.” Lilikuwa tangazo la aina yake katika historia ya WHO.
Tangu wakati huo, hakuna “hatua ya haraka” ambayo imeweza kudhibiti kusambaa kwa ugonjwa huo. Kwa kweli, hali imekuwa mbaya zaidi. Hivi karibuni, WHO liliripoti kwamba watu wengi walikufa kutokana na kifua kikuu katika mwaka 1995 kuliko mwaka mwingine wowote katika historia. Shirika la WHO pia lilionya kwamba kufikia watu nusu bilioni wanaweza kuwa wagonjwa wa kifua kikuu katika kipindi cha miaka 50 ijayo. Kwa kuongezeka, watu wangekuwa wahasiriwa wa kifua kikuu sugu.
Kwa Nini Uangamizi Warudi Tena?
Sababu moja ni kwamba katika kipindi cha miaka 20 iliyopita, programu za kudhibiti kifua kikuu zimezorota au kupotea kabisa katika sehemu nyingi za ulimwengu. Hili limesababisha kuchelewa kugundua na kutibu wale walio na ugonjwa huo. Hilo, kwa upande mwingine, limetokeza vifo zaidi na kuenea kwa ugonjwa huo.
Sababu nyingine ya kutokea tena kwa kifua kikuu ni kuongezeka kwa idadi ya watu maskini, watu wasiopata lishe ya kutosha ambao waishi katika majiji yaliyosongamana, hasa katika majiji makubwa yenye mamilioni ya wakazi katika nchi zinazoendelea. Huku kifua kikuu kikiwa hakiko tu kwa watu maskini—mtu yeyote aweza kupata kifua kikuu—hali duni za afya na kusongamana kwa watu hufanya iwe rahisi kwa ambukizo kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mtu mwingine. Mambo hayo pia huongeza uwezekano wa kinga za mwili za watu kuwa dhaifu sana kuzuia ugonjwa huo.
HIV na Kifua Kikuu —Taabu Pande Mbili
Tatizo kubwa ni kwamba kifua kikuu kimeingia ubia wenye kuua na HIV, virusi ya UKIMWI. Kati ya watu wakadiriwao kuwa karibu milioni moja waliokufa kwa sababu ya magonjwa yenye kuhusiana na UKIMWI katika mwaka 1995, labda thuluthi moja walikufa kutokana na kifua kikuu. Hii ni kwa sababu HIV hudhoofisha uwezo wa mwili wa kuzuia kifua kikuu.
Kwa watu wengi ambukizo la kifua kikuu haliendelei kufikia hatua ya kusababisha ugonjwa. Kwa nini? Kwa sababu basila za kifua kikuu zimefungiwa ndani ya chembe ziitwazo macrophage. Huko, zimefungiwa na mfumo wa mtu wa kinga ya mwili, hasa na T lymphocyte, au chembe T.
Basila za kifua kikuu ni kama fira waliofungiwa katika vikapu vilivyo na vifuniko vilivyofunikwa kabisa. Vikapu hivyo ni macrophage, na vifuniko ni chembe T. Hata hivyo, wakati virusi vya UKIMWI vifikapo mahali hapo, hivyo huvipiga teke vifuniko vya vikapu. Hilo litokeapo, basila hutoroka na ziko huru kuvamia sehemu yoyote ya mwili.
Kwa hiyo, wagonjwa wa UKIMWI, wako katika hatari zaidi ya kusitawisha kifua kikuu kuliko watu ambao wana mfumo wa kinga ya mwili wenye afya. “Watu wenye HIV wako katika hatari zaidi,” akasema mtaalamu wa kifua kikuu katika Scotland. “Wagonjwa wawili wa HIV katika kliniki ya London walipata ugonjwa huo baada ya kukaa katika kijia ambapo mgonjwa wa kifua kikuu aliyekuwa ameketi katika gari la magurudumu alipitishwa.”
Kwa hiyo, UKIMWI umesaidia kueneza ugonjwa wa mlipuko wa kifua kikuu. Kulingana na kadirio moja, kufikia mwaka 2000, ugonjwa wa mlipuko UKIMWI utatokeza wagonjwa milioni 1.4 wa kifua kikuu ambao kinyume cha hivyo wasingepata ugonjwa huo. Jambo muhimu katika ongezeko la kifua kikuu ni kwamba wahasiriwa wa UKIMWI si tu kwamba wako katika hatari kubwa sana ya ugonjwa huo bali pia waweza kuambukiza watu wengine kifua kikuu, kutia ndani wale ambao hawana UKIMWI.
Kifua Kikuu Sugu
Sababu ya mwisho inayofanya pigano dhidi ya kifua kikuu kuwa gumu zaidi ni kutokea kwa kifua kikuu sugu. Vijidudu hivi sugu vyatokeza tisho la kufanya ugonjwa huu kuwa usiotibika tena, kama ilivyokuwa kipindi kabla ya viuavijasumu.
Kwa kusikitisha, utoaji mbaya wa dawa dhidi ya kifua kikuu ni kisababishi kikuu cha kifua kikuu sugu. Matibabu yenye matokeo ya kifua kikuu huchukua zaidi ya miezi sita na hutaka wagonjwa kutumia dawa nne kwa ukawaida bila ya kukosa. Huenda mgonjwa akalazimika kumeza vidonge vingi kama 12 hivi kwa siku. Ikiwa wagonjwa hawatumii dawa kwa ukawaida au hawamalizi matibabu, viini vya kifua kikuu sugu hutokea ambavyo ni vigumu au haviwezekani kuangamizwa. Baadhi ya viini vya kifua kikuu sugu ni vyenye upinzani kwa dawa nyingi za kutibu kifua kikuu hata kufikia saba zinazokubalika.
Kutibu wagonjwa wenye kifua kikuu sugu si kwamba ni vigumu tu, bali pia ni ghali. Gharama yaweza kuwa karibu mara 100 zaidi ya gharama ya kutibu wagonjwa wengine wa kawaida wa kifua kikuu. Kwa kielelezo, katika Marekani, gharama ya matibabu ya mgonjwa mmoja wa kifua kikuu sugu yaweza kuzidi dola 250,000!
Shirika la WHO lakadiria kwamba karibu watu milioni 100 ulimwenguni pote waweza kuwa wameambukizwa na viini vya kifua kikuu sugu, ambao baadhi yao hawawezi kutibiwa na dawa yoyote ya kutibu kifua kikuu ijulikanayo. Viini hivi vyenye kuua vyaambukiza sawa na viini vya kawaida.
Kinga na Ponyo
Jambo gani linafanywa kupambana na dharura hii ya duniani pote? Njia bora zaidi ya kudhibiti ugonjwa huu ni kuugundua na kuwatibu wagonjwa wanapokuwa katika hatua za mwanzo. Hili si kwamba linawasaidia wale ambao tayari ni wagonjwa bali pia huzuia kuenea kwa ugonjwa huu kwa wengine.
Kifua kikuu kikiachwa bila kutibiwa, huua zaidi ya nusu ya wahasiriwa wake. Lakini, kitibiwapo barabara, kifua kikuu kinatibika karibu katika kila kisa ikiwa hakikusababishwa na viini vilivyo sugu kwa dawa aina kadhaa.
Kama ambavyo tumeona, matibabu yenye matokeo hutaka wagonjwa kutumia dawa hadi wamalize kiasi kihitajiwacho. Mara nyingi, hawamalizi. Kwa nini? Kukohoa, homa, na dalili nyingine kwa kawaida huisha majuma machache baada ya matibabu kuanza. Hivyo, wagonjwa wengi hufikia mkataa kwamba wamepona na kuacha kutumia dawa.
Katika kukabiliana na tatizo hili, WHO hutia moyo programu iitwayo, DOTS, ambayo ni kifupi cha “matibabu ya kuangalia wagonjwa moja kwa moja, kwa kipindi kifupi.” Kama jina hilo lidokezavyo, wafanyakazi wa afya huangalia kuhakikisha kwamba wagonjwa wao wameza dawa zote walizopangiwa, angalau kwa miezi miwili ya kwanza ya matibabu. Lakini, hili haliwi rahisi wakati wote kulifanya kwa sababu wengi wa wale walioambukizwa kifua kikuu waishi ukingoni mwa jamii. Kwa vile mara nyingi maisha yao yamejaa msukosuko na matatizo—baadhi yao hata hawana makao—ugumu wa kuhakikisha kwamba wanameza dawa zao waweza kuwa mkubwa sana.
Hivyo je, hatimaye kuna matumaini yoyote ya kulishinda pigo hili juu ya wanadamu?
[Sanduku katika ukurasa wa5]
Habari Muhimu Kuhusu Kifua Kikuu
Maelezo: Kifua kikuu ni ugonjwa ambao kwa kawaida hushambulia na kwa kuendelea huharibu mapafu, lakini pia waweza kuenea hadi sehemu nyingine za mwili, hasa katika ubongo, mafigo, na katika mifupa.
Dalili: Kifua kikuu cha mapafu chaweza kusababisha kukohoa, kupoteza uzito na hamu ya chakula, kutoka jasho jingi wakati wa usiku, udhaifu, kushindwa kupumua, na maumivu ya kifua.
Jinsi ya kutambua dalili: Uchunguzi wa kifua kikuu wa ngozi waweza kuonyesha ikiwa mtu ameambukizwa basila. Eksirei ya kifua yaweza kuonyesha madhara katika mapafu, ambayo yaweza kuonyesha ambukizo la kifua kikuu lenye kuendelea. Uchunguzi wa maabara wa makohozi ya mgonjwa ndiyo njia yenye kuaminika zaidi ya kugundua basila za kifua kikuu.
Nani apaswa kuchunguzwa: Wale ambao ama wana dalili za kifua kikuu ama wamekuwa na ukaribu, wenye kurudia-rudia na mgonjwa wa kifua kikuu—hasa katika vyumba visivyopitisha hewa safi ya kutosha.
Chanjo: Ipo dawa ya chanjo moja tu—ijulikanayo kama BCG. Huzuia kifua kikuu kilicho kikali sana kwa watoto lakini haina matokeo sana kwa wabalehe na watu wazima. Ikiwa bora kabisa, chanjo hiyo hutoa ulinzi kwa karibu miaka 15. BCG huwalinda wale tu ambao hawajaambukizwa; haiwasaidii watu ambao tayari wameambukizwa.
[Sanduku katika ukurasa wa6]
Kifua Kikuu na Mtindo
Yaweza kuonekana kuwa jambo la ajabu, wakati wa karne ya 19, kifua kikuu kilihusishwa na mapenzi, kwani watu waliamini kwamba dalili za ugonjwa huo ziliongeza mielekeo yenye unyetivu na ya kistadi.
Mfaransa mwandishi wa michezo ya kuigiza na riwaya Alexandre Dumas karibu na mwaka 1820 aliandika katika kitabu chake Mémoires: “Ilikuwa ni mtindo kuugua kutokana na maumivu ya kifua; kila mtu alikuwa na kifua kikuu, hasa washairi; lilikuwa jambo lenye kukubalika katika jamii mtu kufa kabla hajatimiza umri wa miaka thelathini.”
Mshairi Mwingereza Lord Byron aliripotiwa akisema: “Ningependa kufa kutokana na [kifua kikuu] . . . kwa sababu wanawake wangesema, ‘Aa mwangalie Byron, apendeza kama nini afapo!’”
Mwandishi Mmarekani Henry David Thoreau, ambaye ni wazi alikufa kutokana na kifua kikuu, aliandika: “Kudhoofika na ugonjwa mara nyingi kwapendeza, kama . . . kung’aa kutokana na kifua kikuu.”
Ikitoa maelezo juu ya kuvutiwa huku kwa kifua kikuu, makala katika The Journal of the American Medical Association ilitaarifu hivi: “Fumbo hili la upendezi katika ugonjwa huu lilienea kote katika upendezi wa kibinafsi katika mtindo; wanawake walijitahidi kuwa na sura yenye kufifia, dhaifu, walitumia virembeshi vilivyofanywa vyeupe, na walipendelea kuwa wembamba, nguo za melimeli—sawa na matokeo yatafutwayo na wanawake wenye ugonjwa wa kuhofu kunenepa wenye kuonyesha mavazi leo.”
[Sanduku katika ukurasa wa7]
Je, Ni Rahisi Kupata Kifua Kikuu Leo?
“Hakuna mahali unapoweza kujificha kutokana na bakteria za kifua kikuu,” aonya Dakt. Arata Kochi, mkurugenzi wa Programu ya Kifua Kikuu ya Duniani Pote ya WHO. “Mtu yeyote aweza kupata kifua kikuu kwa urahisi sana kwa kuvuta pumzi yenye kiini cha magonjwa ya kifua kikuu ambacho mtu fulani amekohoa au amepiga chafya hewani. Viini hivi vya magonjwa vyaweza kubaki katika hewa kwa muda wa saa kadhaa; hata kwa miaka. Sisi wote tumo hatarini.”
Lakini kabla mtu hajawa mgonjwa wa kifua kikuu, mambo mawili lazima yatokee. Kwanza, lazima aambukizwe bakteria za kifua kikuu. Pili, ambukizo lazima liendelee hadi kufikia kuwa ugonjwa.
Ingawa inawezekana kuambukizwa kutokana na kuwa karibu kwa muda mfupi na mwenye kuambukiza sana, kifua kikuu chaelekea kusambaa sana kupitia kuwa karibu kunakorudiwa-rudiwa, kama vile kutokeavyo miongoni mwa washiriki wa familia waishio katika hali zenye msongamano.
Basili zivutwazo kwa njia ya hewa na mtu aambukizwaye huzaliana katika kifua. Hata hivyo, watu 9 kati ya 10 walioambukizwa hawawi wagonjwa kwa sababu mfumo wa kinga huzuia kuenea kwa ambukizo. Lakini nyakati nyingine, basili zisizo tendaji zaweza kufanywa tendaji ikiwa mfumo wa kinga umefanywa dhaifu na HIV, ugonjwa wa kisukari, tiba za kemikali za kansa, au visababishi vingine.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 4]
New Jersey Medical School—National Tuberculosis Center
[Picha katika ukurasa wa 7]
Basili za kifua kikuu zitolewazo na UKIMWI ni kama fira watolewao vikapuni