Kifua Kikuu Charudi kwa Pigo!
TANGU miaka ya 1950, idadi ya visa vya kifua kikuu ilipunguka Marekani kwa kiwango cha asilimia 5 kwa mwaka. Hata hivyo, tangu 1985 kumekuwa na ongezeko la asilimia 18 la visa vinavyoripotiwa vya kifua kikuu. Jambo la kufadhaisha hata zaidi ni kuwapo kwa aina mpya ya maradhi hayo ambayo hayatibiwi na dawa. Sasa kifua kikuu chaua watu wakadiriwao kuwa milioni tatu kila mwaka. Kwa nini pigano dhidi ya kifua kikuu halifanikiwi?
Sababu moja ni kwamba wagonjwa wengi hawatumii dawa kamwe kwa kipindi kinachohitajiwa—mara nyingi kwa miezi sita hadi tisa. Kwa kielelezo, katika New York City uchunguzi mmoja ulifunua kwamba asilimia 89 ya kikundi cha wagonjwa 200 wenye kifua kikuu kinachoendelea kuwadhoofisha hawakumaliza kutumia dawa. “Ni vibaya sana,” asema Dakt. Lee Reichman, msimamizi wa Shirika la Mapafu la Marekani, “kwa sababu watu hao (a) hawataponywa, na (b) labda watasitawisha kifua kikuu ambacho kinakinza dawa za kawaida.” Lakini wabebaji hao wa kifua kikuu waweza kudhuru zaidi ya afya yao wenyewe. “Kwa kutotumia dawa walizopewa,” Dakt. Reichman aongezea, “wao waweza kuambukiza watu wengine.” Bila shaka hili ni jambo linalochangia visa vipya vinavyokadiriwa kuwa milioni nane vinavyogunduliwa ulimwenguni pote kila mwaka.
Wanafunzi wa Biblia watambua kwamba “tauni mahali mahali” ni sehemu za ishara kwamba twaishi katika “siku za mwisho” za huu mfumo wa mambo. (Luka 21:11; 2 Timotheo 3:1) Ni nini kitakachofuata? Dunia mpya, ambamo “hapana mwenyeji atakayesema, Mimi mgonjwa.” (Isaya 33:24) Ndiyo, Yehova Mungu aahidi, si kitulizo cha muda tu, bali kitulizo cha kudumu kutokana na ugonjwa na kifo.—Ufunuo 21:1-4.