Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g99 5/22 kur. 21-24
  • Kinga Mpya Dhidi ya Kifua Kikuu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kinga Mpya Dhidi ya Kifua Kikuu
  • Amkeni!—1999
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Sasa Kuna Habari Njema
  • Ina Mafanikio Kadiri Gani?
  • Haitumiki Sana—Lakini Kuna Maendeleo
  • Shangwe ya Ushindi na Huzuni
    Amkeni!—1997
  • Muungano Hatari
    Amkeni!—1998
  • Kifua Kikuu Charudi kwa Pigo!
    Amkeni!—1996
  • Suluhisho la Duniani Pote—Je, Lawezekana?
    Amkeni!—1997
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1999
g99 5/22 kur. 21-24

Kinga Mpya Dhidi ya Kifua Kikuu

KIFUA KIKUU ni maradhi ya kuambukizwa ambacho ni kisababishi cha kifo cha kale zaidi miongoni mwa wanadamu, na bado kingali tisho kubwa kwa afya hivi kwamba Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) lakilinganisha na bomu linaloelekea kulipuka. Kuhusu kifua kikuu, ripoti moja ya WHO yaonya kwamba “tunakimbizana na wakati.” Mwanadamu akishindwa kukomesha kifua kikuu, huenda siku moja atakabili maradhi sugu “yanayoenezwa kupitia hewa, na ambayo hayawezi kutibiwa kama vile UKIMWI.” Shirika la WHO lahimiza kwamba wakati umewadia wa kuzinduka na kutambua madhara yawezayo kuletwa na kifua kikuu. “Kila mtu anayepumua hewa . . . , anapaswa kuhangaikia hatari hii.”

Je, kusema hivyo ni kutia chumvi? La. Kwa mfano, ebu wazia jinsi ambavyo ulimwengu ungezinduka iwapo maradhi fulani yangetisha kusababisha vifo vya watu wote nchini Kanada kwa miaka kumi! Ingawa jambo hilo laonekana kama haliwezekani, lakini kwa kweli tisho hilo lipo. Ulimwenguni pote, kifua kikuu husababisha vifo vya watu kuliko jumla ya vifo vyote vinavyosababishwa na UKIMWI, malaria, na maradhi ya kanda za joto: watu 8,000 kila siku. Watu wapatao milioni 20 sasa wanaugua kifua kikuu, na watu wapatao milioni 30 wanaweza kufa kutokana na kifua kikuu kwa miaka kumi ijayo—idadi kubwa kuliko watu wote nchini Kanada.—Ona Sanduku “Kifua Kikuu Chakumba Dunia Yote,” kwenye ukurasa wa 22.

Sasa Kuna Habari Njema

Lakini, kuna tumaini leo. Baada ya kufanya majaribio kwa miaka kumi, watafiti wamepata mbinu ambayo inaweza kudhibiti kifua kikuu. Dakt. Hiroshi Nakajima, aliyekuwa mkurugenzi-mkuu wa WHO, alisema kwamba hiyo mbinu mpya “ilikuwa mojawapo ya maendeleo makubwa zaidi kuhusu afya ya umma yaliyopata kufanywa mwongo huu.” Na Dakt. Arata Kochi, mkurugenzi wa Mpango wa WHO wa Ulimwenguni Pote wa Kudhibiti Kifua Kikuu, asema kwamba mbinu hiyo inaandaa fursa ya kwanza kabisa ya “kuondoa pigo la kifua kikuu.” Ni nini inayosababisha msisimko huo wote? Ni tiba iitwayo DOTS.

Neno DOTS ni ufupi wa maneno directly observed treatment, short-course (tiba ya muda mfupi ya kuzingatia na kutazama wagonjwa). Ni njia ya tiba ambayo inaweza kutibu wengi wanaougua kifua kikuu kwa kipindi cha miezi sita hadi miezi minane bila hata mgonjwa kulazwa hospitalini kwa siku moja. Ili ifaulu, DOTS hutegemea mambo matano. Shirika la WHO lataarifu kwamba ikiwa mojawapo ya hayo mambo linakosekana, uwezo wa kutibu watu wanaougua kifua kikuu “utapotea.” Ni mambo yapi hayo?

● 1. Kuzingatia (Directly): Kifua kikuu ambacho hakijagunduliwa ndicho hatari zaidi. Basi WHO lakazia kwamba jambo la kwanza kabisa, wanatiba wanapaswa kuzingatia kazi ya kuwatambulisha watu wanaougua kifua kikuu katika jumuiya yao.

● 2. Kutazama (Observed): Jambo la pili la DOTS lafanya taasisi za kitiba—wala si mgonjwa—kuwa na daraka la kusaidia wagonjwa wapone. Wanatiba au watu waliojitolea ambao wamezoezwa, kama vile wenye maduka, walimu, watu ambao waliwahi kushikwa na kifua kikuu, huwatazama wagonjwa wakimeza kila dawa ya kifua kikuu. “Hao wenye kuwatazama wagonjwa” ni muhimu sana ili kuwe na mafanikio kwa sababu jambo kuu linalofanya kifua kikuu kidumu hadi leo ni kwamba wagonjwa huacha kumeza dawa mapema mno. (Ona sanduku “Kwa Nini Kifua Kikuu Kimeibuka—Tena?” kwenye ukurasa wa 22.) Baada ya kutumia dawa kwa majuma machache tu, wao huanza kupata nafuu na kuacha kumeza dawa. Lakini, ni lazima waendelee kutumia dawa kwa miezi sita hadi nane ili kuondoa vijidudu vyote vya kifua kikuu mwilini.

● 3. Tiba (Treatment): Katika miezi hiyo sita hadi minane, wanatiba huchunguza matokeo ya tiba na kuandika maendeleo ya mgonjwa. Kwa njia hiyo, wao huhakikisha kwamba wagonjwa wamepona kabisa na hawawezi kuwaambukiza watu wengine.

● 4. Muda Mfupi (Short-Course): Jambo la nne la mbinu ya tiba ya DOTS ni kutumia dawa zinazotakikana kwa kiasi kifaacho ili kutibu kifua kikuu, ambako huitwa tiba ya muda mfupi, kwa kipindi kinachotakikana. Tiba hiyo inayochanganya dawa nyingi ina nguvu za kutosha kuua vijidudu vya kifua kikuu.a Ni lazima dawa hizo ziwepo daima ili tiba hiyo isikatizwe.

● 5. !: Shirika la WHO lataja jambo la tano katika mbinu ya tiba ya DOTS kwa njia ya alama ya mshangao mwishoni mwa lile neno DOTS! Alama hiyo yasimamia msaada wa kifedha na sera nzuri. Shirika la WHO lahimiza taasisi za kitiba zitafute fedha kwa serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali na kufanya matibabu ya kifua kikuu yawe sehemu ya mpango wa kitiba wa nchi.

Kuhusu kutafuta fedha, tiba ya DOTS yawavutia wakuu wanaoamua kama watafadhili DOTS kifedha au la. Benki ya Ulimwengu imetaja kwamba DOTS ni “mojawapo ya njia bora zisizo na gharama zinazotumiwa kupambana na . . . maradhi.” Shirika la WHO lakadiria kwamba gharama yote ya kutumia mbinu hii katika nchi maskini ni dola 100 hivi kwa kila mgonjwa. “Si rahisi gharama hiyo izidi senti 10 (za Marekani) kwa kila mtu katika nchi zinazoendelea, ambayo ni nafuu hata katika nyakati ngumu za kiuchumi.” Hata hivyo, gharama hiyo nafuu ina manufaa tele.

Ina Mafanikio Kadiri Gani?

Wawakilishi wa WHO walitangaza mnamo Machi 1997 kwamba matumizi kidogo ya mbinu ya DOTS yalikuwa “yanafanya kifua kikuu kisiendelee kuongezeka kwa mara ya kwanza katika miongo mingi.” “Mahali ambapo DOTS inatumiwa, wenye kutibiwa na kupona huongezeka karibu maradufu.” Majaribio ya DOTS yaliyofanywa katika maeneo yaliyokumbwa vibaya na kifua kikuu tayari yanaonyesha kwamba mbinu hiyo inafanikiwa. Ebu ona mafanikio machache ambayo yanatajwa na WHO.

Nchini India “DOTS imetumiwa katika eneo lenye zaidi ya watu milioni 12. . . . Sasa wagonjwa 4 kati ya kila 5 wametibiwa kifua kikuu na kupona.” Katika majaribio yaliyofanyiwa watu milioni moja nchini Bangladesh, “asilimia 87 [ya watu wanaougua kifua kikuu] walitibiwa wakapona.” Katika kisiwa kimoja cha Indonesia, mpango wa DOTS “unatibu na kuponesha wagonjwa 9 kati ya 10 walioambukizwa.” Nchini China majaribio hayo “yalifanikiwa sana,” huku asilimia 94 ya wagonjwa wakitibiwa na kupona. Katika jiji moja la Afrika Kusini, “zaidi ya asilimia 80 ya [wagonjwa wa kifua kikuu] wanatibiwa kwa mafanikio.” Hivi majuzi, DOTS ilianza kutumiwa New York City, ikafanikiwa sana.

Dakt. Kochi amalizia kwamba matokeo ya majaribio hayo katika makumi kadhaa ya nchi yaonyesha kwamba mbinu hiyo “inaweza kutumiwa kila mahali na inaweza kutibu na kuponya asilimia 85 na zaidi ya wagonjwa.”

Haitumiki Sana—Lakini Kuna Maendeleo

Kukiwa na tiba ambayo inaweza kuondoa kabisa maradhi ya kuambukiza ambayo ni mojawapo ya visababishi vikuu vya kifo miongoni mwa wanadamu kwa urahisi na bila gharama, ungetarajia kwamba mbinu ya DOTS ingetumika sana. “Lakini,” ofisa mmoja wa WHO asema, “kwa kushangaza ni nchi chache tu ndizo zinazotekeleza mbinu hiyo ya WHO ya kudhibiti kifua kikuu ambayo imethibitishwa kuwa yenye mafanikio na isiyo na gharama.” Hata mwanzoni mwa 1996, ni nchi 34 tu ambazo zilikuwa zimetekeleza mbinu hiyo kotekote nchini.

Hata hivyo kuna maendeleo. Kabla ya mwaka wa 1993, shirika la WHO lilipotangaza hali ya dharura duniani kote kuhusu kifua kikuu, ni mgonjwa 1 tu kati ya kila 50 waliougua kifua kikuu ambao walipokea tiba ya DOTS. Leo ni mgonjwa 1 kati ya kila wagonjwa 10. Inaripotiwa kwamba katika mwaka wa 1998, nchi zipatazo 96 zilikuwa zikitumia mbinu ya DOTS. Nchi nyinginezo zikiunga mkono mpango wa DOTS, idadi ya watu wenye kuugua kifua kikuu kila mwaka ‘itapunguzwa kwa nusu kwa mwongo mmoja tu.’ Dakt. Kochi asema: “Tuna mpango wa tiba ambao umethibitishwa kuwa bora na ambao unahitaji tu kutumiwa zaidi.”

Kwa kuwa mwanadamu ana ujuzi na vifaa vya kupambana na kifua kikuu kwa mafanikio, kitu kimoja tu kinachokosekana ‘ni watu ambao watahakikisha kwamba dawa hizo zinatumiwa kote ulimwenguni.’ Si ajabu kwamba katika kichapo kilichoandikiwa madaktari na wanatiba wengine ulimwenguni kote, shirika la WHO lauliza: “Mbona hatujaanza kutumia vifaa hivyo?”

[Maelezo ya Chini]

a Dawa hizo zatia ndani isoniazid, rifampin, pyrazinamide, streptomycin, na ethambutol.

[Blabu katika ukurasa wa 21]

Kila sekunde moja, mtu fulani duniani huambukizwa kifua kikuu

[Blabu katika ukurasa wa 21]

‘Dawa zenye kuokoa uhai zinaozeana bila kutumiwa huku mamilioni ya watu wakifa.’—Dr. Arata Kochi

[Blabu katika ukurasa wa 23]

“Mbinu ya DOTS itakuwa maendeleo makubwa zaidi kuhusu mambo ya afya katika mwongo huu.”

[Sanduku katika ukurasa wa 22]

Kwa Nini Kifua Kikuu Kimeibuka—TENA?

Tiba ya kifua kikuu (TB) iligunduliwa zaidi ya miongo minne iliyopita. Tangu wakati huo, zaidi ya watu milioni 120 wamekufa kwa kifua kikuu, na karibu milioni 3 watakufa mwaka huu. Lakini, kwa nini watu wengi wangali wanakufa kwa kifua kikuu ilhali kuna tiba? Kuna sababu tatu za msingi: kupuuza, virusi vya HIV/UKIMWI, na kifua kikuu sugu.

Kupuuza. Ulimwengu umezingatia maradhi yenye kuambukiza kama vile UKIMWI na Ebola. Hata hivyo, kwa kila mtu mmoja aliyekufa kwa Ebola, watu 12,000 walikufa kwa kifua kikuu. Kwani, kifua kikuu kimeenea sana katika nchi zinazositawi hivi kwamba watu wanakiona kuwa sehemu ya maisha. Na katika nchi tajiri, kifua kikuu kimeachiliwa kitawale ingawa dawa nzuri za kukitibu zinaozeana bila kutumiwa. Upuuzaji huo ulimwenguni kote umekuwa kosa lenye kusababisha maafa. Huku hangaiko la ulimwengu juu ya kifua kikuu likizidi kupoa, vijidudu vya kifua kikuu navyo vinazidi kuimarika. Leo, vinashambulia watu wengi zaidi katika nchi nyingi zaidi kuliko wakati mwingine wowote katika historia ya wanadamu.

Virusi vya HIV/UKIMWI. Kifua kikuu huandamana na virusi vya HIV na UKIMWI. Watu wanapoambukizwa virusi vya HIV—ambavyo hudhoofisha kinga yao—wao wana uwezekano wa mara 30 wa kuambukizwa kifua kikuu kuliko wengine. Si ajabu kwamba mweneo wa sasa wa virusi vya HIV umesababisha ongezeko la wagonjwa wa kifua kikuu vilevile! Inakadiriwa kwamba watu 266,000 waliothibitishwa kuwa na virusi vya HIV walikufa kwa kifua kikuu mwaka wa 1997. “Hao ni wanaume na wanawake,” asema Peter Piot, mkurugenzi wa Mpango wa Pamoja wa Umoja wa Mataifa wa HIV/UKIMWI, “ambao hawakunufaika na dawa zisizo ghali za kifua kikuu ambazo walihitaji ili kutibu kifua kikuu.”

Kifua Kikuu Sugu. “Vijidudu sugu,” ambavyo vina kinga dhidi ya dawa zote za wanadamu, ni mambo tu ya kubuniwa na hadithi za sayansi, lakini kwa habari ya kifua kikuu, jambo hilo ni ukweli mtupu. Tayari huenda zaidi ya watu milioni 50 wameambukizwa kifua kikuu sugu (MDR). Wagonjwa wa kifua kikuu ambao huacha kutumia dawa baada ya majuma machache eti kwa sababu wanahisi nafuu, au kwa sababu dawa zimekwisha, au kwa sababu maradhi haya yanafanya mtu adharauliwe hawaui vijidudu vyote vya kifua kikuu katika mwili wao. Kwa mfano, katika nchi moja ya Asia watu 2 kati ya kila 3 wanaougua kifua kikuu huacha matibabu mapema. Wanapokuwa wagonjwa tena, ugonjwa huo waweza kuwa mgumu zaidi kutibu kwa sababu vijidudu vinavyobaki hupigana na kushinda dawa yoyote ile ipatikanayo ya kifua kikuu. Basi, mwishowe mgonjwa huyo hushikwa na kifua kikuu kisichoweza kutibiwa—wao na mtu mwingine yeyote ambaye huenda wakamwambukiza. Na vijidudu hivyo vikipata tu kuwa hewani, tunabaki tukijiuliza, Je, mwanadamu ataweza kudhibiti tena kifua kikuu sugu?

[Sanduku katika ukurasa wa 22]

Kifua Kikuu Chakumba Dunia Yote

Kifua kikuu kinazidi kuenea, kugharimu zaidi kitiba, na kuzidi kuwa hatari kila mwaka. Ripoti zilizokusanywa na Shirika la Afya Ulimwenguni laonyesha mweneo wa ugonjwa huu wenye kusababisha vifo bila kutambulikana. Hapa pana mifano kadhaa: “Pakistan hoi mbele ya kifua kikuu.” “Kifua kikuu kimerudi Thailand kwa kishindo.” “Leo, kifua kikuu ni mojawapo ya visababishi vikuu vya ugonjwa na kifo nchini Brazili.” “Kifua kikuu chaendelea kuwaponda watu wa Mexico.” Nchini Urusi “kifua kikuu chaongezeka upesi.” Katika Ethiopia “kifua kikuu kimewaka nchini kote.” “Afrika Kusini ina mojawapo ya viwango vya juu zaidi vilivyorekodiwa vya kifua kikuu ulimwenguni.”

Ingawa watu 95 kati ya kila 100 wanaougua kifua kikuu wanaishi katika nchi maskini za ulimwengu, kifua kikuu kinazidi kukumba nchi tajiri vilevile. Nchini Marekani, kuliripotiwa ongezeko kubwa la wagonjwa wa kifua kikuu mapema katika miaka ya 1990. Mwandishi wa habari Mmarekani Valery Gartseff asema kwamba kifua kikuu “kimerudi tena kuwatesa Wamarekani.” Vivyo hivyo, Dakt. Jaap Broek­mans, mkurugenzi wa shirika la Royal Netherlands TB Association alisema hivi majuzi kwamba kifua kikuu “kimeanza kuponda vibaya Ulaya Mashariki na sehemu fulani za Ulaya Magharibi.” Si ajabu kwamba jarida Science, la Agosti 22, 1997, lasema kwamba “kifua kikuu chaendelea kuwa tisho kuu kwa afya.”

[Sanduku katika ukurasa wa 24]

Ukuzi wa Vijidudu vya Kifua Kikuu Wagunduliwa

Hivi majuzi watafiti walifaulu kuandika ukuzi wote wa bakteria ya kifua kikuu. Utimizo huo ni “jambo jipya katika vita dhidi ya mojawapo ya visababishi vikuu vya kifo miongoni mwa wanadamu,” asema Dakt.  Douglas Young, wa chuo cha Imperial College School of Medicine jijini London. Shirika la Afya Ulimwenguni laripoti kwamba ugunduzi huu “waweza kuwa muhimu sana katika utafiti wa wakati ujao wa dawa na chanjo za kifua kikuu.” —The TB Treatment Observer, Septemba 15, 1998.

[Picha katika ukurasa wa 23]

Dawa hizi kwa pamoja zaweza kuua vijidudu vya kifua kikuu

aarifa ya WHO

[Hisani]

Photo supplied by WHO, Geneva

Picha: WHO/Thierry Falise

[Picha katika ukurasa wa 24]

Inagharimu dola 100 kutibu mgonjwa

[Hisani]

Picha: WHO/Thierry Falise

Photo supplied by WHO, Geneva

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 21]

Picha: WHO/Thierry Falise

Photo supplied by WHO, Geneva

Picha: WHO/Thierry Falise

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki