Muungano Hatari
MNAMO 1959, matabibu katika Marekani walitabiri kwamba ugonjwa wa kifua kikuu ungeondolewa kabisa karibuni. Na kwa kweli, katika miaka iliyofuata maradhi hayo yalipunguka haraka sana hivi kwamba watu wengi wakadhani yalikuwa yamedhibitiwa. Lakini kifua kikuu kimerudi, nacho kimepata mwenzi hatari aitwaye HIV, ambaye ni kirusi kinachodhoofisha mfumo wa kinga wa mwili na kwa kawaida kusababisha UKIMWI.
Ingawa zaidi ya watu bilioni mbili—karibu thuluthi moja ya watu wote ulimwenguni—wana bakteria ya kifua kikuu, wanapoambukizwa kwa mara ya kwanza watu hao wana uwezekano wa asilimia 10 tu wa kushikwa na maradhi hayo maishani. Ajabu ni kwamba watu wenye virusi vya HIV wana uwezekano wa asilimia 8 kila mwaka wa kuugua kifua kikuu. Basi kadiri watu wengi waambukizwapo virusi vya HIV, ndivyo iongezekavyo hatari ya kushikwa na kifua kikuu.
Dakt. Richard J. O’Brien wa WHO (Shirika la Afya Ulimwenguni) asema kwamba katika miaka ya majuzi kumekuwa na ongezeko lipatalo asilimia 15 katika visa vya kifua kikuu huko Marekani. Yeye asema kwamba hiyo “hutokea hasa kwa sababu ya muungano wa HIV na kifua kikuu.” Lakini, tisho hilo ni baya zaidi katika nchi zinazoendelea. Asilimia 90 kamili ya visa vipya vipatavyo milioni nane kila mwaka hupatikana katika nchi maskini zaidi, na wagonjwa wapatao milioni tatu kati ya hao hufa.
Ulimwenguni pote, watu wapatao milioni 4.4 wanapambana na muungano huo hatari wa virusi vya HIV na kifua kikuu. Shirika la Afya Ulimwenguni latabiri kwamba karibuni, kifua kikuu kitakuwa kikisababisha vifo milioni moja kila mwaka miongoni mwa wale ambao wana virusi vya HIV. “Magonjwa hayo mawili yameungana na kuwa tisho kubwa zaidi kwa afya ya umma katika mwongo huu,” asema Peter Piot, ambaye ni mkurugenzi mkuu wa Programu ya Pamoja ya Umoja wa Mataifa juu ya HIV/UKIMWI.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 19]
New Jersey Medical School—National Tuberculosis Center