Vifo Ambavyo Vyashindana na Vita
MARILYN mwenye miaka 23 alipopoteza uzito na kuhisi kunyong’onyea, alidhani lingeweza kuwa ni jambo fulani lililohusiana na mimba yake ya hivi karibuni. Pia alikuwa na kikohozi kilichodumu, ambacho alikitaja kwa daktari wake. Daktari alisema kwamba hilo lilikuwa ambukizo katika sehemu ya juu ya mrija wa kupumua akamwagizia viuavijasumu. Baadaye, alipoanza kutokwa jasho sana usiku, Marilyn aliogopa kwelikweli. Alirudi kwa daktari wake, ambaye alifanya mpango apigwe eksirei ya kifua.
Alama nyeusi katika picha ya eksirei ilihitaji hatua ya haraka, lakini Marylin hakuweza kupatikana kwa njia ya simu. “Daktari huyo alimpata mama yangu na kumwambia kwamba nilikuwa mgonjwa kwelikweli,” alisema Marylin. “Mama yangu alikuja kunitafuta, akaniambia niende kwa [daktari] mara moja. Daktari alinipeleka hospitali ambapo nilipigwa eksirei nyingine, nikalazwa.”
Marilyn alishtushwa sana kujua kwamba alikuwa na kifua kikuu. Alifikiri angekufa, lakini baada ya matibabu ya kutumia dawa za kutibu kifua kikuu, alipona baada ya muda mfupi.
Mshangao wa Marilyn wa kuwa na kifua kikuu unaeleweka. Hadi hivi karibuni, hata wataalamu wengi wa afya walifikiri kwamba kifua kikuu kimeshindwa katika nchi zilizoendelea. “Nilifikiri kilikuwa kimeng’olewa,” alisema msaidizi wa kliniki katika kituo cha matibabu katika London. “Lakini nilipokuja kufanya kazi hapa, niligundua kwamba kilikuwa kinaendelea na kusitawi na kuendelea kwa kasi kuelekea katikati ya jiji.”
Katika maeneo ambayo kifua kikuu kilikuwa kimekwisha, kimerudi tena; kilipobaki, kimekuwa kibaya zaidi. Badala ya kuangamizwa, kifua kikuu ni muuaji aliye sawa kabisa na vita na njaa. Fikiria:
◼ Japo maendeleo ya ajabu katika dawa za kisasa, kwa kipindi cha miaka mia moja iliyopita kifua kikuu kimewapeleka kaburini watu karibu milioni 200.
◼ Watu karibu bilioni mbili—thuluthi moja ya watu wote duniani—tayari wameambukizwa basila ya kifua kikuu, aina mojawapo ya bakteria. Kwa kuongezea, mtu mwingine anaambukizwa kifua kikuu kila sekunde!
◼ Katika mwaka 1995 idadi ya watu waliokuwa na kifua kikuu kilichokomaa ilikuwa karibu watu milioni 22. Karibu watu milioni tatu walikufa, wengi wao katika nchi zinazoendelea.
Kukiwa na dawa zenye nguvu sana zinazopatikana katika kupambana na kifua kikuu, kwa nini ugonjwa huu unaendelea kuwasumbua wanadamu? Je, utashindwa wakati wowote? Je, kuna njia yoyote ya kujikinga? Makala zifuatazo zitajibu maswali haya.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 3]
New Jersey Medical School—National Tuberculosis Center