Bata-Makelele Mwenye Fahari
Na mleta-habari za Amkeni! katika Uingereza
MAJI ya Ziwa Grindon—lililo kati ya vilima Northumbrian vyenye kuteremka, si mbali na mpaka ulio kati ya Uingereza na Scotland—yaliangaza rangi za hudhurungi na kahawia za vilima vyenye mjimbi. Nilipokuwa nikitazama, mabata-mwitu walikuwa wakidonoa magugu-maji kando ya makundi ya vitwitwi, vitwitwi-kishungi, na vitwitwi-dhahabu.[1]
Kwa ghafula, ukungu ulipoanza kuondoka, nilisikia sauti ya ndege-mwitu. Ulikuwa wimbo wa utarumbeta wa mabata-makelele wakiruka kimo kifupi juu ya vilima. Walikuwa na uzuri wa upeo walipopita kwa ulaini kupiga maji chubwi kwa mabawa yazidiyo urefu wa meta 2.5.[1a] Oktoba katikati mabata hawa hurukia kusini kutoka Urusi, Iceland, na kaskazini mwa Ulaya wakati maji ya kaskazini yagandapo.[2] Hapa wao hupata chakula—mimea ya majini, makonokono, mbegu, na wadudu.[3]
Wale mabata 29 ziwani mbele yangu walinipendeza nilipolenga darubini zangu juu ya sehemu manjano-manjano chini ya midomo yao. Walionekana wenye fahari sana kwa kuinua vichwa kwa shingo zilizonyooka.[4]
Wakati mmoja bata-makelele alikuwa ndege mwenye kuongezeka Uingereza lakini akatokomea karne ya 18. Hadi sasa hajajiimarisha tena.[5] Mabata-makelele ni ndege wa vita sana wakati wa kuotamia, huku wakilinda vikali kiota chao cha mayai matano hadi saba, na baadaye makinda yao, dhidi ya adui wawezao kutokea.[6]
Wazazi mabata-makelele hushirikiana kujenga kiota cha vijiti vilivyovunjika, ama kisiwani ama moja kwa moja juu ya maji ambapo wao hujenga kisiwa kieleacho kilicho madhubuti kutegemeza binadamu. Hapo yale mayai ya manjano huotamiwa kuanzia siku 35 hadi 42. Wazazi wote wawili hutunza makinda kabla hayajaweza kupuruka kwenda zao baada ya karibu majuma kumi.[7]
Jua lilipokuwa likishuka kwa utukufu wa urujuani-mwekundu nyuma ya magofu ya ngome ya Kiroma ya Vercovicium na kupaka ziwa hilo na mabata yalo uzambarau mwanana, nilitua kufikiria uzuri wa maisha na uajabu wa uumbaji huo mwadhamu.