Nyumba za Muundo wa Mkate-Tangawizi za Haiti
NA MLETA-HABARI ZA AMKENI! KATIKA HAITI
NYUMBA za kuvutia za muundo wa mkate-tangawizi za Haiti si za kihadithi tu. Ni halisi. Lakini zikiwa zimepakwa rangi ya kijani, manjano, nyekundu, samawati, na nyekundu nzito, upendezi wao wa kizamani na uzuri wa kiajabu huzifanya zisisimue sana.[1]
Nje-nje zimesaniiwa kwa ujenzi wa mtindo wa kuvutia pamoja na muundo madhubuti uwezao kuwa wa mbao, matufali, au mchanganyiko wa vyote viwili.[2] Nyingine zina madirisha makubwa yaelekezayo kwenye roshani zilizotokeza nje zikiwa zimefunikiwa na paa na kukalia viguzo vya mbao kama kwamba zimekalia vitegemezo. Nyakati fulani nguzo za saruji au mbao zenye vitovu vya chuma hupamba veranda ndefu zifikazo kwenye mabustani. Kila kitu hupambwa kwa mbao laini, zenye mapindo maridadi, na madirisha madogo ya mviringo, vipima-upepo vya muundo wa jogoo, na makuba huongezea usisimuko.[3]
Miaka ya mapema ya 1900, nyumba za muundo wa mkate-tangawizi zilipendwa na jamii ya tabaka ya kati ya bara hili la West Indies.[4] Gharama ya kuingiza nchini vifaa kama matufali manjano, vigae vya asbesto, msunobari-lami wa Amerika ilifanya visinunulike kwa watu wa kawaida.[5] Leo, hivyo ni vionyesho vya kihistoria vya kuvutia watalii waende Port-au-Prince na majiji mengine.[6] Wageni huvutiwa na mapambo yaliyochongwa katika mbao kama lile la Seremala Gothic. Mtindo huu wa mkate-tangawizi wenye madoido ulisitawi katika mabara ya Amerika baada ya kuwezeshwa na uvumbuzi wa kikerezo cha kuzungusha mbao.[7]
Athari ya Kifaransa
Akionyesha athari nyingine katika usitawi wa nyumba za muundo wa mkate-tangawizi katika Haiti, msanii wa majengo Paul Mathon, ambaye León, baba yake, alikuwa mtangulizi wa usanii wa majengo ya muundo wa mkate-tangawizi, aliambia Amkeni! wakati mmoja: “Chanzo cha majengo hayo hakijulikani hakika, ingawa huenda hiyo ikaonekana ajabu kwa majengo ya muda unaopungua karne moja. Ingawa hatuwezi kukana kwamba yameathiriwa na mtindo wa Seremala Gothic, ni lazima tutafute kisababishi katika shule za sanaa bora ziendwazo na wale waendeshao shughuli za majengo ya nyumba-tangawizi. Athari ya Kifaransa yaelekea kuonekana wazi sana, ingawa rekebisho lilifanywa kufuata maisha, utamaduni, na tabia-anga ya Haiti.”[8][9]
Wasanii wa ujenzi wa Haiti waliozoezwa Ufaransa walianzisha mtindo huu wa kujenga katika Haiti.[10] Paul Mathon alisema: “Walizoeza wahandisi na wanyapara kutekeleza michoro yao ya ujenzi. Shule za useremala zilitokeza wastadi katika kazi ya mbao. Pia roho ya usanii ilienea ikasaidia kusambaa kwa namna hii ya usanii wa ujenzi. Baada ya muda, yote haya yalififia. Majengo ya kuiga yamekuwa hafifu.”[11]
Usanii wa ujenzi umefanyizwa vizuri uandae makao ya ubaridi wa kutosha katika tabia-anga ya tropiki. Dari zilizoinuka mara mbili za majengo ya ki-siku-hizi huandaa nafasi kubwa zaidi ya mweneo wa hewa, ikirahisisha kupungua kwa joto. Milango na madirisha mapana yenye vifungio vya muundo wa Venetia huwezesha hewa kupitapita katika kila chumba.[12] Mbao tele zilizotumiwa sakafuni na mitandazo ya ukutani hutoa uzuizi mzuri pia dhidi ya joto la nje. Na bado ujenzi wa nyumba hizi unazidi kupungua kwa kufuata mitindo mipya zaidi.[13]
Vikale vya Kukumbukwa
Ni wazi kwamba kuingia kwa urekebisha-joto wa ki-siku-hizi kumepunguza kiasi fulani cha uvutio wa nyumba za muundo wa mkate-tangawizi. Majengo ya saruji hupendelewa kwa udumifu wayo, kwa kuwa majengo ya mbao huja kuwa magofu pole kwa pole, kwa kuliwa na mchwa. Bila shaka, wasanii fulani wa ujenzi huongeza mitindo ya nyumba za muundo wa mkate-tangawizi ndani ya nyumba mpya hizi, zenye kudumu zaidi, na wengine wanarudisha nyumba za zamani za muundo wa mkate-tangawizi, wakitumia saruji kufanya muungo udumu zaidi.
Hata hapo, nyumba za muundo wa mkate-tangawizi hazitarudia fahari yazo ya zamani, ingawa baadhi yazo zaendelea kuwa makao yenye adhama. Yaonekana hatimaye zitabaki zikiwa vikale vya maonyesho—vikumbusho vya uvutio wa ujenzi wa kale wa usanifu wa Haiti usio na kifani.[14]