Baruti za Kutegwa Ardhini—Usumbufu wa Duniani Pote
MAELFU ya wanaume, wanawake, na watoto wasio na hatia katika nchi zaidi ya 60 huvunjwa maungo, na wengine kuuawa, kila mwezi na baruti za kutegwa ardhini. Yakadiriwa kwamba baruti za kutegwa dhidi ya wafanyakazi zimeua au zikajeruhi watu wengi kuliko vita ya kikemikali, ya kibiolojia, na ya kinyukilia. Kulingana na shirika la utafiti Human Rights Watch, watu kama 30,000 wamevunjwa maungo na baruti zilizotegwa katika Kambodia pekee.[1]
Vilipuko vidogo hivi vimetegwa ardhini katika mapigano mbalimbali, na vilivyo vingi kati yavyo havijaondolewa kamwe. Yakadiriwa kwamba baruti kama milioni 100 zabaki zimefukiwa katika nchi zaidi ya 60. Zaweza kulipushwa kwa kukanyagwa kidogo tu nazo hupendwa na wengi vitani kwa sababu hazina gharama na zina matokeo. Aina moja hugharimu dola 3 tu (za Marekani). Nyingine, ambayo hurusha vigololi 700 vya chuma-cha-pua na kuua kwa umbali wa meta 40, hugharimu dola 27 tu. Baruti hizo zatakiwa sana, laripoti The New York Times, hivi kwamba sasa mataifa 48 hutengeneza na kuuza namna 340 tofauti.[2] Na nyingi zaidi hutegwa kila siku kuliko zile zimalizwazo nguvu kwa shughuli za kung’oa baruti.
Kung’oa baruti za kutegwa ni jambo gumu na hugharimu, kwa kuwa majeshi mengi hayaweki ramani za mahali zilipotegwa; na baruti za kutegwa zinazidi kutengenezwa kwa mbao, plastiki, na vifaa vingine visivyonaswa na vigundua-madini. Seneta wa Marekani Patrick Leahy, aliyetoa wito wa kupiga marufuku upelekaji-nje wa silaha hizi, alitaarifu hivi: “Katika Uholanzi, watu wangali wakiuawa na baruti za Kijerumani zilizotegwa kuanzia Vita ya Ulimwengu 2. Fikiria jinsi hali ilivyo mbaya zaidi Afghanistan, Kambodia, Angola, Bosnia na nchi nyingine zote ambazo zimetegewa baruti nyingi.”[3]
Ni ulimwengu mpya wa Mungu tu unaokuja utakaotatua matatizo hayo. Neno lake huahidi: “[Mungu] avikomesha vita hata mwisho wa dunia; avunja uta, akata mkuki, achoma moto magari [ya vita].”—Zaburi 46:9.