Kokwa Yenye Jina Jipya
NA MLETA-HABARI ZA AMKENI! KATIKA BOLIVIA
KUTOKA katika misitu mizito ya mvua ya Amazonia yatoka kokwa (aina ya tunda) tamu iliyo na lishe bora. Jina layo la awali, “kokwa ya Brazili,” halifai tena kwa kuwa kufikia nusu yayo sasa yatoka katika misitu iliyo nje ya Brazili, hasa kutoka Bolivia.
Kwa kufaa, mnamo Mei 18, 1992, Baraza la Kimataifa la Kokwa liliamua kubadili jina la kokwa hiyo, ambayo awali iliitwa kokwa ya Brazili, kokwa-krimu, kokwa-siagi, castana do Pará, Paranuss, na noix du Brésil. Sasa itaitwa kokwa ya Amazonia.
Masimulizi ya Mkusanya Kokwa
Sikiliza yale Cornelio, mkusanya kokwa tangu awe na umri wa miaka sita, asemayo kuhusu kukusanya kokwa hiyo ya msitu iliyo geni sana:
“Kokwa nyingi zaidi za Amazonia hukusanywa mwituni. Ni lazima tuingie ndani kabisa ya msitu ili tuzipate. Mito inayojipinda-pinda ndiyo njia ya pekee ya kufikia huko. Mwana wangu mwenye miaka 19 nami twasafiri kwa siku kadhaa kwenye mashua ya mto yenye orofa.
“Ili tutumie kikamili mwanga wa mchana, twaamka saa 10:30 alfajiri na tayari tuko safarini kufikia mapambazuko. Vijia huingia ndani kwa kilometa kadhaa tu kufikia sehemu za kukusanya kokwa; tokea hapo na kuendelea ni lazima tuendelee mbele, tukikata magugu mazito ya msitu kwa panga. Hakuna viishara vya kukuongoza njia. Ni lazima tujue jinsi ya kutumia jua likiwa kiongozi chetu, ama sivyo tutapotea.
“Msitu una hatari nyingi sana kwa mtu yeyote anayetafuta hazina yao. Kunayo maradhi, kama vile malaria, na hatari iliyoko nyakati zote ya nyoka. Hatuogopi wale boa-mbanaji (aina ya chatu)—hawatusumbui—lakini kuna nyoka wadogo-wadogo waliojificha chini ambao ni wenye sumu kwelikweli. Rangi zao na michoro yao huwaficha kabisa. Umo lao si chungu mara ya kwanza, lakini polepole yule aliyeumwa apooza kwa sumu. Nyoka wadogo-wadogo wenye rangi ya kijani waliojificha katika matawi ni hatari kadiri iyo hiyo.
“Twaweza kupata kwa urahisi miti yenye kuvutia inayotokeza kokwa iitwayo almendros, kwa kuwa ina vimo vya kuanzia meta 30 hadi 50 kupita mingi ya miti mingine ya msitu. Mara nyingi shina haliwi na matawi mpaka lipite kimo cha miti mingine ya msitu. Cocos hukua katika miisho kabisa ya matawi, hizo huwa ni maganda magumu yenye umbo la duara na yaliyo na kipenyo cha sentimeta 10 hadi 15. Maganda hayo huwa na kokwa 10 hadi 25 zilizojipanga kwa visehemu kama katika chungwa, kila moja ikiwa katika ganda layo lenyewe.
“Cocos hizo huanguka chini katika majira ya mvua, ambayo hutokea kuanzia Novemba hadi Februari. Ni lazima zikusanywe mara hiyo, ama sivyo zitaharibika. Cocos zinazoanguka kutoka kimo cha jengo lenye orofa 15 hutokeza hatari nyingine kwa uhai. Ni lazima tufanye kazi haraka, tukiweka cocos katika rundo mbali kutoka kwenye mti almendro ili kupunguza hatari. Lakini jihadhari na nyoka! Wanapokuwa wamelala, wakiwa wamejikunja na kuweka vichwa vyao juu, wanafanana sana na tunda la coco. Wafanyakazi fulani wamewahi kushika nyoka na kumtupa, wakidhania ni tunda la coco.
“Kukata coco huhitaji ustadi. Mikato kadhaa kwa nguvu zote kwa upanga mahali pafaapo tu ndiyo inayohitajiwa kuondoa kokwa bila kuziharibu. Upesi twarudi kambini, tukibeba magunia mazito ya kokwa. Hatutumii magari wala wanyama wa kubeba mizigo. Ni lazima mkusanyaji awe mwenye nguvu na kakawana, hasa kwa sababu mavuno hufanywa katika kipindi chenye joto zaidi na mvua zaidi katika mwaka.”
Baada ya Kukusanya
Kokwa zina rangi ya kijani-kibichi zinapokusanywa, jambo linalomaanisha kwamba zaweza kuharibika upesi kwa sababu ya kuwa na maji mengi (karibu asilimia 35). Ili zisiharibike, ni lazima zigeuzwe na koleo ili zile zilizo chini ya rundo zikauke. Kokwa nyingi za Bolivia hutayarishwa kwa ajili ya kusafirishwa nje. Huchukua muda wa miezi sita ili kutayarisha mavuno hayo.
Matayarisho huanza kwa kuweka kokwa katika sufuria kubwa ya mvuke. Joto hugawanya kokwa kutoka kwa ganda layo. Kwa hiyo, kokwa zinapotolewa kwenye maganda, nyingi zayo hutoka zikiwa nzima-nzima.
Kisha kokwa hizo huwekwa kulingana na ukubwa wazo, kuanikwa kwa sinia za waya, na kuwekwa katika tanuu ili kupunguza maji yawe kati ya asilimia 4 na 8. Maganda hutumiwa kama kuni ya kuwasha tanuu hizo. Kupunguza maji kwafanya kuwezekane kuhifadhi kokwa hizo kwa mwaka mmoja au kwa miaka kadhaa zikiwa zimewekwa katika barafu. Ili kuhifadhi ubora wazo na ladha yazo, kokwa hizo huhifadhiwa katika hali isiyo na hewa katika karatasi za aluminiamu ili zisafirishwe.
Kokwa za Amazonia huliwa na mamilioni ya watu ulimwenguni kote kwa njia nyingi tofauti-tofauti. Watu fulani hula kokwa pamoja na nafaka za kiamsha-kinywa. Wengine huzipendelea zikiwa zimewekewa chokoleti au zikichanganywa na matunda yaliyokauka. Wakati mwingine ulapo kokwa hiyo iliyo tamu, kumbuka kwamba ina jina jipya—kokwa ya Amazonia!
[Picha katika ukurasa wa 15]
Kokwa za Amazonia na mti uzitokezazo