Mkanju Ulio Mkubwa Kuliko Yote Ulimwenguni
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA BRAZILI
MKUBWA kuliko yote ulimwenguni? Kulingana na Guinness O Livro dos Recordes 1994, huenda ukawa. Ukiwa karibu na pwani ya Rio Grande do Norte, mkanju uliopigwa picha hapa ndio kwa hakika ulio mkubwa kuliko yote katika Brazili. Kwa kweli, mti huu peke yake hufunika eneo la jengo kubwa la jiji—lililo sawa na mikanju 70 ya ukubwa wa wastani!
Mkanju ni mti wenye majani mabichi wakati wote mwakani ambao hutofautiana kwa ukubwa kutoka kichaka kidogo hadi mti upatao kimo cha meta 20. Maua madogo ya mkanju yanatofautiana waziwazi na majani yao makubwa, magumu. Mbegu yao iwezayo kuliwa ndiyo ile korosho tamu, ambayo huonekana kana kwamba ilishindiliwa kwa nguvu ndani ya tunda lililo na umbo kama la pea linaloitwa kanju. Kwa kushangaza, mkanju una uhusiano na namna fulani ya mmea wenye sumu, na wale wanaoushika wanapaswa kuwa waangalifu sana. Korosho ina magamba mawili, na kati ya magamba haya kuna mafuta yanayoweza kusababisha malengelenge kwenye ngozi. Kwa sababu ya taratibu ya uchomaji, vifanyizo vya korosho vyenye sumu huondolewa.
Jambo lisilo kawaida ni kwamba, korosho yenye umbo la figo huonekana ikikua nje ya tunda, kana kwamba Muumba wayo alisahau hiyo korosho na kuibandika juu yalo baadaye. Kanju ndilo kikonyo cha korosho. Kwa hivyo, wengine huita korosho tunda halisi la huo mti. Viwavyo vyote, wazia tu, wakati ujao ulapo korosho, huenda ikawa unakula zao la mkanju ulio mkubwa kuliko yote ulimwenguni!