“Mti wa Uhai” Wenye Kushangaza wa Afrika
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA TANZANIA
“SIAMINI aina yake ilionekana wakati wowote ule katika sehemu yoyote ya dunia.” Ni nini alichoona Mfaransa Michel Adanson alipokuwa akizuru Senegal katika 1749? Ni mti! Wenye urefu wa meta 20 hivi, ukiwa na shina kubwa mno, na kipenyo cha meta nane. Hatimaye David Livingstone alirejezea mti huo kuwa “karoti iliyopandwa juu-chini.”
Kulingana na hekaya “ibilisi aliung’oa [mti huo], akachimbika matawi yake ardhini, na kuacha mizizi yake hewani.” Hivyo, wengi huujua mti huo kuwa “ule mti ulio juu-chini.” Katika Kilatini huitwa Adansonia digitata, ukiitwa kwa jina la mwenye kuuvumbua, lakini wengi wetu huuita mbuyu, mmoja wa miti ijulikanayo sana katika Afrika ya mashariki, ingawaje mingine inayofanana na huo na iliyo mirefu yaweza kupatikana katika Madagaska na mingine hata katika Australia.
Mti Ulio Juu-Chini
Tulikuwa tumetumia wakati mwingi kuendesha gari kupitia sehemu ya mashambani ya Tanzania. Ilikuwa furaha kuona vijiji vyenye kuvutia kwelikweli, makao yaliyo na paa za nyasi, wanawake wakibeba kuni vichwani mwao, watoto wakicheza chini ya miembe, na wachungaji wakichunga ng’ombe wao. Hatimaye twaona kile alichoona Adanson nyuma katika karne ya 18.
“Ndiyo ile pale!” Margit apaaza sauti. Ikiwa mikubwa sana, na yenye fahari, mibuyu huonekana katika hapa na pale kwenye sehemu zilizokauka zaidi za Afrika ya kitropiki. Inapatikana savanna, katika pwani, na hata kwenye miinamo ya Mlima Kilimanjaro. “Haufanani na mti wowote niliopata kuona wakati wowote ule,” aongezea mmoja wa washiriki wetu. Wenye rangi ya kijivu na mkubwa mno, mbuyu ni mmea ulio na gome lenye unene wa sentimeta tano hadi kumi. “Kwa kweli waonekana kama mti uliopandwa juu-chini!” Kwa sehemu kubwa ya mwaka, katika kipindi cha miezi sita hadi saba ya kipindi cha ukame, mti huo hauna majani kwa vyovyote. Mti huo hustahimilije? Kwa nini tusiulize mtu fulani ambaye huenda ajua.
Tukiwa twasafiri katika bara la mbuyu, hatimaye twapata kuzungumza na Shem, mwenyeji wa hapo. “Wajua,” asema mwanamume huyo, “huu ni mti ulio chupa.” Mti ulio chupa? “Ndiyo, wakati wa vipindi vifupi vya mvua, mitembo ya mti huo iliyo kama sifongo hunyonya kiwango kikubwa cha maji, ambayo huwekwa akiba katika shina kwa ajili ya kipindi cha ukame.” Kichapo Baobab—Adansonia Digitata huonelea hivi: “Utosi wa shina kwa kawaida huwa na uwazi, maji ya mvua na umande hujikusanya hapo na huenda yakawa ndiyo maji tu yapatikanayo kwa kilometa nyingi katika sehemu hiyo. . . . Shina lina kiwango cha juu cha maji. Inakadiriwa kwamba mti ulio na meta za kyubiki 200 hivi waweza kuwa na lita za maji hadi 140,000. . . . Vipande viwezekanavyo vya shina vyaweza kukatwa na kukamuliwa maji ya kunywewa.” Shem afanya mzaha hivi: “Ni mti mkubwa sana, lakini moyo wake ni laini.” Kufikia wakati huu wanakijiji zaidi wamekaribia na wanasikiliza mazungumzo kwa hamu sana. “Mlijua kwamba mbuyu ndio mti wa uhai?” auliza Emmanuel.
Ule “Mti wa Uhai”
Kwa wenyeji wengi mti huo ni zawadi kutoka kwa Mungu. Kwa nini? “Kwanza kabisa waweza kuishi kwa muda mrefu sana. Labda miaka elfu au hata zaidi,” aendelea mwanakijiji mmoja. “Hutuandalia chakula, maji, nguo, vifaa vya paa, gundi, dawa, makao, mikufu, na hata peremende kwa ajili ya watoto.” Namna gani kuni? “La, gome lake ni nyevu sana kwa maji yanayowekwa akiba ndani yake. Kwa kawaida sisi hutafuta miti mingine kwa ajili ya kusudi hilo.” Asema Daniel mchanga: “Lakini twatumia gome lake kutengenezea nyuzi na kamba zetu.” Zaidi sana ya hilo, hutumika kwa neti, mikeka, vitambaa, kofia, mitumbwi, sinia, visanduku, vikapu, na karatasi. Jivu kutoka kwenye gome laweza kutumiwa kuwa mbolea, na wengi hutengeneza sabuni kutoka kwalo. “Chipukizi changa na majani huliwa,” aongeza mmoja wa akina mama wachanga, akiwa amebeba mtoto mgongoni mwake. “Sisi pia huchoma punje zake na kuzitumia kwa kahawa. Fofota la punje hutumiwa kutengenezea pombe, na mafuta yaweza kusindikwa pia.”
Katika kipindi kifupi cha mvua, mti huo huchanua maua meupe yenye kuvutia. Lakini hayanukii vizuri kama yanavyoonekana! Huanza kufunuka kuanzia alasiri iliyosonga sana hadi mara tu baada ya mshuko-jua na kufunuka kikamili asubuhi inayofuata. Wakati wa usiku, popo wa matunda hualikwa ili kuchavusha. Wenyeji wa hapo huchanganya chavuo ya ua na maji na kuitumia kuwa gundi. Yale matunda marefu (sentimeta 40) huning’inia kwenye vikonyo. Twashika tunda hilo la rangi ya kijani, ni kama mahameli. Laonekana kama mkia wa nyani. “Aha, kumbe ndiyo sababu mti huo pia huitwa mti-mkate-wa-tumbili!” Je, tulipasue tunda na kuangalia ndani? Kwa nini sivyo!
“Mti-Hamira-Soda”
Tunda hilo lina fofota nyeupe chungu kando ya punje, yenye vitamini C nyingi sana, vitamini B1, na kalsiamu. Katika uokaji fofota yaweza kutumiwa kama kibadala kwa hamira-soda. Hiyo pia ndiyo sababu watu huuita mti-hamira-soda. Shem asema: “Nyakati fulani sisi hutengeneza vinywaji kutokana na fofota. Huonja kama limau.” Hiyo ndiyo sababu watu wengine huuita mlimau. Hutumiwa kwa nini kingine?
Shem ajibu: “Twatumia karibu kila sehemu ya mti huu. Twatumia ganda la tunda kuwa chelezo za kuvulia samaki, kata, na bakuli ya supu, na hulitumia pia kutengenezea mtego mzuri wa panya. Ng’ombe wetu wanapotatizwa na wadudu, sisi huchoma tu fofota ya tunda, na moshi huo hutumika kuwa kifukuza wadudu. Nyakati fulani twachanganya unga wa fofota na maziwa na kupata yogati bora zaidi.” Namna gani dawa? “Bila shaka mti huo ni duka letu la dawa,” acheka Shem.
Duka la Dawa la Mbuyu
Mwautumia kwa kitu gani? “Kila kitu!” Kwa sababu ya matumizi yake mengi, si ajabu kwamba wenyeji wa hapo huheshimu mti huo, kuuhofu, ndiyo, hata kuuabudu. Twagundua kuwa akina mama wanaonyonyesha huchanganya fofota iliyo ungaunga na maziwa na kuwapa watoto wao ili kuwazuia watoto wadogo wasiwe na matumbo yaliyovimba, ugonjwa wa kuhara damu, na homa. “Dawa” kutoka kwenye mti huo huuzwa katika masoko ya mahali hapo na husemekana kutibu vimbe, kuumwa kwa jino, na magonjwa mengine. Katika mahali hapo hutumiwa kutibu anemia, kuhara, influenza, pumu, matatizo ya figo, matatizo ya kupumua, na hata vidonda.
Mti huu usio wa kawaida kiasili hukumbwa na ngano na hekaya. Wengine huhisi kwamba “shamba ambalo katika hilo [mbuyu] husimama haliwezi kuuzwa, kwa kuwa kuwapo kwake huaminika kuwa dalili njema. . . . Hadithi nyingine hudai kuwa Simba atamnyafua yeyote atakayetunda bila kufikiri ua kutoka kwenye mti huo. Chipukizi hizi huaminiwa kukaliwa na roho. Yasemekana pia kuwa maji ambayo punje za mti huo zimelowekwa na kukorogwa huwa kinga kwa mashambulizi ya mamba na kwamba yule anywaye dawa ya gome la huo mti atakuwa hodari na mwenye nguvu.”—Baobab—Adansonia Digitata.
Peremende kwa Watoto
Tumejifunza mambo mengi mapya kutoka kwa wenyeji wa bara la mbuyu. Sasa, katika Dar es Salaam, twamwona Navina, Suma, na Kevin. Kisia wanachotafuna na kumumunya? Punje za mbuyu! Punje hizi nyekundu zauzwa kama peremende kandokando ya barabara, na yaonekana watoto hawa wazipenda. “Ni kali?” “Kidogo tu, lakini twapenda hivyo!” wasema watoto hao kwa sauti moja. “Tafadhali twaa baadhi yazo! Uonje!” Ndiyo, kwa nini tusionje kitu fulani kutoka kwenye “mti wa uhai” wa Afrika?
[Picha katika ukurasa wa 24]
Mbuyu, mti wenye matumizi mengi
[Picha katika ukurasa wa 24]
Punje, hutumiwa kama peremende na kuchomwa kwa ajili ya kahawa
[Picha katika ukurasa wa 25]
Chipukizi zake ni kubwa
[Picha katika ukurasa wa 25]
Hauna majani wakati wa kipindi cha ukame