Keratotomia ya Nusu-Kipenyo Ni Nini?
KERATOTOMIA YA NUSU-KIPENYO (kufanya mikato midogo-midogo katika konea ili kurekebisha jicho liache kuwa na mwono wa karibu [mwono mfupi]) imetangazwa zaidi hivi majuzi katika nchi fulani-fulani kupitia televisheni, makala za magazeti, na redio. Imekuwa habari kuu ya mazungumzo kwenye makongamano ya kimataifa ya utaalamu wa macho miaka miwili iliyopita. Ingawa utaratibu huu umefanywa kwa zaidi ya miaka 20 na umeelezwa na watafiti wa kitiba kwa miaka kadhaa kabla ya hapo, umeanza kupendwa na wengi majuzi tu. Idadi inayoongezeka ya wapasuaji wa macho wanahudhuria warsha mbalimbali na kujifunza kufanya utaratibu huo.
Mamilioni ya watu ama huzaliwa wakiwa na mwono wa karibu ama huja kuwa hivyo. “Kuwa na mwono wa karibu” kwamaanisha nini? Kwamaanisha kutoweza kuona vitu vya mbali bila msaada wa miwani au miwani ya ndani ya macho. Kwa kawaida, watu wenye mwono wa karibu waweza kusoma bila miwani lakini mara nyingi hushika visomwa karibu-karibu ili macho yaone sawasawa.
Keratotomia ya nusu-kipenyo ni utaratibu wa upasuaji ujaribuo kupunguza au kukomesha uhitaji wa kuvaa miwani ili kuona mbali wakati ufanywapo kwa watu wenye mwono wa karibu. Upasuaji huo huunda konea upya ili taswira (picha) ionwayo ianguke juu ya retina (sehemu ya nyuma ndani ya jicho) badala ya kuanguka mbele yayo, kama vile ilivyo katika mwono wa karibu. Mikato hiyo hufanywa kwa kukata konea kwa marefu ya nusu-kipenyo kuelekea ukingo wa lile eneo la mwono ili kufanya kitovu cha mwono kiwe safi. Mikato hiyo huwa ya kina, urefu, na wingi unaotofautiana.
Si Upasuaji Mpya
Wachina wa kale walijaribu kutatua tatizo la mwono wa karibu kwa kulala wakiwa wameweka mifuko ya mchanga juu ya macho yao. Matokeo yalikuwa ya muda mfupi tu. Hata mapema ya 1894, majarida ya kitiba yaliripoti juu ya hatua za upasuaji za kurekebisha au kuunda konea upya. Tangu wakati huo, wapasuaji katika Amerika Kusini, na baadaye katika Japani, walieleza juu ya mbinu za kubadili umbo la konea kwa kuipasua ili kutokeza mwono safi. Maarifa waliyopata Wajapani yalichochea mpasuaji Mrusi aunde upya njia yake na kuifanikisha zaidi.
Kadiri matokeo yalivyothibitika kuwa ya kutegemeka, wapasuaji kadhaa kutoka nchi nyinginezo walifuata upasuaji huo. Walirudi pindi kadhaa kuyatazama matokeo kisha wakaanzisha upasuaji huo ndani ya nchi zao. Kufikia 1979, ripoti zilikuwa zikiandikwa kueleza mbinu hiyo, matokeo, na mambo yaliyohitaji kuundwa upya kuongezea mafanikio. Kwa hiyo ingawa huenda utaratibu huu ukawa mpya kwako, si mpya kwa taaluma ya upasuaji.
Ili kulinda umma, uchunguzi ulifanywa Marekani kwenye vitovu kadhaa vya utafiti kuthibitisha kufanikiwa au kutofanikiwa kwa njia hii ya upasuaji, na matokeo yalichapishwa miaka ya 1980 katika ule ulioitwa uchunguzi wa PERK. Ndipo Chuo cha Marekani cha Utaalamu wa Macho kilipokubali mbinu hii kuwa mfikio wenye mafanikio wa kupunguza maiopia (mwono wa karibu).
Je, Yafaa Wewe Ufanyiwe Keratotomia ya Nusu-Kipenyo?
Kwa kuwa sasa tuna habari kidogo juu ya usitawi wa keratotomia ya nusu-kipenyo, waweza kujuaje kama hiyo ni mbinu uwezayo kufikiria kufanyiwa? Uchunguzo kamili wa macho ndiyo hatua ya kwanza. Ikiisha kuamuliwa na tabibu kwamba macho yako yafaa kufanyiwa utaratibu huo, uelekeo wa mafanikio waweza kuonyeshwa na kadiri ya maiopia (mwono wa karibu) uliyo nayo. Mafanikio ya maiopia kali zaidi yanapungua.
Ikiwa uchunguzo wa macho umethibitisha kwamba wewe wafaa kufanyiwa keratotomia ya nusu-kipenyo, utataka kutafuta mpasuaji wa keratotomia ya nusu-kipenyo aliye na uzoefu wa kutosha. Katika yaliyo mengi ya majiji makubwa, kuna angalau mstadi mmoja mwenye miaka kadhaa ya uzoefu. Kwa kuhudhuria warsha, kupitia rekodi za uzoefu, kuongea na waliokuwa wagonjwa na wataalamu wengine wa macho, labda wewe waweza kupata mtaalamu wa macho aliye na kawaida ya kupata matokeo mema.
Kati ya 1991 na 1992, katika Marekani, idadi ya wataalamu wa macho wenye kufanya upasuaji huo iliongezeka kutoka asilimia 13 kufika asilimia 25. Hii yamaanisha kwamba wengine ni wapya kwenye uwanja huo, lakini pia yaonyesha utaratibu huo unazidi kukubaliwa. Sasa wastadi wanasihi kwamba wapasuaji wapya wapate mazoezi ili waweze kuyaepuka matatanisho waliyopata-pata wale wapasuaji wa mapema.
Kabla hujaamua kupasuliwa, yafaa uwe umejielimisha juu ya ule utaratibu ili uweze kuuliza maswali uhitajiyo kujua. Wapasuaji wenye mafanikio waweza kuchanganua kila mgonjwa na kuurekebisha upasuaji ili kudhibiti matokeo. Wao hushughulikia kila kisa kulingana na hali zacho chenyewe, wakipatanisha upasuaji na mtu mwenyewe. Utafiti umehakikisha kwamba wingi wa mikato, kina chayo, na urefu wayo ndio huamua matokeo. Mambo mengine yafikiriwayo ni umri wa mtu, jinsia yake, msongo wa nguvu za macho yake, na umbo la macho. Huenda mpasuaji wako akafikiria hali nyingine tofauti ili apange na kurekebisha matokeo kulingana na hali.
Kujua ni miaka mingapi mpasuaji amekuwa akifanya upasuaji huu na amefanya visa vingapi hukupa kionyesho cha uzoefu wake. Makala za hivi majuzi katika majarida ya kitiba zimedokeza kwamba kiwango cha kuamua ubora wa uangalifu ni kwamba mpasuaji wa kurekebisha mwono awe na kipiga-taswira cha vidio ya kompyuta kiitwacho Topografia. Kadiri kifaa hicho kilivyo kizuri zaidi, ndivyo upasuaji wako utakavyoelekea zaidi kupata matokeo mema.
Ule Utaratibu
Ukiamua kwamba wataka kufanyiwa utaratibu huu, waweza kutarajia nini? Kuna kazi nyingi ya uangalifu ifanywayo kabla ya upasuaji ambayo hutia ndani uchunguzi wa macho, kutumia nguvu za mawimbi ya sauti ili kuona taswira ya macho na unene wayo, kupima uviringo wayo, kupima nguvu za msongo wa macho, na labda kufanya topografia ya vidio itumiayo kompyuta. Habari zote hizi zipatikanapo, upasuaji wako hupangwa. Baada ya kuelewa na kutia sahihi fomu ya idhini, kwa kawaida wewe hupewa dawa ya kutuliza.
Kuhusu fomu hiyo ya idhini, acheni tuzifikirie hatari zilizotajwa katika fomu. Upasuaji huu hufanywa katika tabaka za nje ya macho. Athari za kando zilizo za kawaida kutokana na upasuaji huo ni kusumbuliwa na mwangaza, kuona mianga ikimulika kama nyota, mwono wenye kubadilikabadilika, kuhisi ni kama jicho limeingiwa na kitu, macho makavu, na hisia ya kufikirifikiri sana kuhusu hali ya jicho, ambayo yaweza kuendelea muda wa saa nyingi, siku nyingi, majuma mengi, au miezi mingi. Jicho hudhoofishwa na mikato. Muda ambao jicho hudhoofishwa huwa tofauti kwa kila mtu. Matatanisho mengi yaweza kuondolewa kwa kutumia vitone vya macho vya baada ya upasuaji na kwa kufuata maagizo ya kujizuilia utendaji mbalimbali. Mgonjwa mtiifu huongezea asilimia ya mafanikio.
Kwa kuwa sasa uko tayari kupasuliwa, iweje? Mnamo dakika 30 za kutumia kiasi kidogo cha dawa ya kutuliza, watembea kwenda vyumba vya upasuaji wa keratotomia ya nusu-kipenyo. Kope zako zasafishwa, na kitambaa safi chawekwa juu ya uso wako. Huenda vipimo vya mwisho vikafanywa wakati huu, na vyombo vya upasuaji vyakaguliwa chini ya hadubini kuhakikisha usahihi. Jicho lako latiwa vitone vya kugandisha hisia. Jicho likiisha kugandishwa hisia, kitenganishi cha kope za macho chawekwa kuzuia kupepesa macho. Wewe wakaza macho kwenye nuru fulani, na kitovu cha mwono wako chatiliwa alama ili mpasuaji aanze kazi hapo. Kisha kiolezo chawekwa juu ya jicho kutia alama ya mahali upasuaji utapitia, halafu upasuaji waanza.
Katika muda upunguao dakika 20, upasuaji wamalizwa. Kwa kawaida jicho hufunikwa kwa muda fulani, lakini mnamo saa 24 waweza kuanza kuona nafuu ya mwono wako wa karibu. Mnamo saa nyingine 24, mwono huwa mzuri sana. Mabadiliko makubwa katika mwono hutukia siku 7 hadi 30 zifuatazo. Ni mabadiliko madogo tu yatukiayo baada ya miezi mitatu, na mwaka mmoja ufikapo huwa kuna utulivu wa kiasi. Kwa miaka 20 ifuatayo, karibu 1 kati ya wagonjwa 4 ataona mabadiliko zaidi kwenye mwono.
Si kwa Kila Mtu
Tumeongea kidogo juu ya matatanisho. Sasa acheni tuongee kidogo zaidi juu ya athari za kando—zitarajiwazo na zisizotarajiwa. Keratotomia ya nusu-kipenyo hairekebishi namna zote za maiopia. Husaidia karibu kila kisa, lakini haiwafai watu fulani wenye maiopia. Wengine hupatwa na mwono wa kubadilika-badilika. Hii yamaanisha kwamba asubuhi mwono huwa tofauti na jioni. Hii huonwa hasa katika watu waketio mbele ya kiwambo cha kompyuta mchana kutwa. Walio wengi kati ya wagonjwa wa keratotomia ya nusu-kipenyo hawapatwi na hilo daima, lakini asilimia ndogo hupatwa. Wengi hulalamika juu ya kusumbuliwa na mwangaza usiku baada ya upasuaji wa keratotomia ya nusu-kipenyo, lakini hapo tena, walio wengi hawalalamiki kuwa na hali hiyo daima. Wale waliokuwa na macho makavu na labda wakaacha kutumia miwani ya ndani ya macho kwa sababu hiyo watapatwa na ukavu zaidi kwa muda wa kufikia miezi sita. Wengine wamerekebishiwa maiopia yao kupita kiasi, hiyo ikiwanyang’anya mwono wa karibu na yaweza pia kufanya wasiwe na mwono mzuri wa mbali bila miwani ya ndani ya macho au miwani ya kawaida. Hili si jambo la kawaida sana lakini hupata wagonjwa fulani wa keratotomia ya nusu-kipenyo.
Katika miezi mitatu ya kwanza baada ya upasuaji, mwono waweza kuathiriwa na matatizo ya kijumla ya afya, msononeko wa hisia-moyo, mimba, dawa, mabadiliko ya kazi, kawaida za mazoezi, mabadiliko ya ulaji, na hasa ukosefu wa pumziko. Mpasuaji mmoja wa keratotomia ya nusu-kipenyo ameona kwamba watu wanyanyuao vitu vizito kwa ukawaida huhitaji mipasuo ya kurudiwa-rudiwa kwa kawaida ili wafikie kiwango kitarajiwacho cha mwono. Kuna mambo mengi yawezayo kuathiri mwono wa kila siku, hasa katika miezi mitatu ya kwanza. Ni lazima mgonjwa awe tayari kwa mabadiliko ya mwono anapokuwa akipona.
Keratotomia ya nusu-kipenyo haifanywi kwa ukamili kabisa hivi kwamba sikuzote yaweza kuwa badala ya miwani au miwani ya ndani ya macho, kwa kuwa miwani hiyo yaweza kurekebishwa kulingana na mahitaji yako hususa. Upasuaji wa keratotomia ya nusu-kipenyo ni mfikio wa jumla, na ni mara chache wagonjwa wa keratotomia ya nusu-kipenyo huchagua kuvaa miwani baada ya upasuaji. Yawezekana pia kurekebishiwa jicho moja tu ili uwe na jicho moja kwa mwono wa mbali na moja kwa mwono wa karibu. Upasuaji zaidi waweza kufanywa baada ya upasuaji wa keratotomia ya nusu-kipenyo ikiwa mwono haukufikia mradi uliotarajiwa na ikiwa kuna mengi zaidi yawezayo kutimizwa. Hii yataka mpasuaji mwenye uzoefu mwingi kujua ni upasuaji kadiri gani zaidi uhitajiwao.
Chunguza, Kisha Amua
Ushauri bora zaidi ikiwa unafikiria upasuaji huu ni kupata habari nyingi kadiri uwezavyo, kwa kuwa wahitaji kuuliza maswali yafaayo ili upate majibu manyoofu. Halafu endea wapasuaji kadhaa wa keratotomia ya nusu-kipenyo kabla ya kuamua ni mfikio gani utakao kufuata. (Mithali 15:22) Huenda ukapata kwamba una matazamio ya kufanikiwa sana katika upasuaji na kuboresha sana mwono wako.
Hivi majuzi kwenye mkutano mmoja katika Salt Lake City, Utah, Marekani, ripoti ilitolewa juu ya uchunguzo wa wagonjwa wa keratotomia ya nusu-kipenyo waliokuwa wataalamu wa macho pia. Wagonjwa hawa karibu wote kwa jumla walijibu kwamba walifurahia matokeo ya upasuaji—ni asilimia 2 ambao hawakufurahia, lakini asilimia 98 kati yao walifurahi.
Ni jambo zuri kama nini kuamka na mwono safi kila asubuhi bila kunyoosha mkono kuchukua miwani! Karibuni, hili litatendeka, si kwa upasuaji, bali kwa nguvu ya kimungu. Mfumo mpya wa Mungu utaleta mwono safi huko kwa wote waliovaa miwani wakati mmoja, lakini mwono mpya utawasisimua hasa wale ambao hawajapata kamwe kuwa na mwono! “Ndipo macho ya vipofu yatafumbuliwa.”—Isaya 35:5.
[Michoro/Picha katika ukurasa wa 25]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
Athari za Kawaida za Upasuaji wa Keratotomia ya Nusu-Kipenyo
Jicho la kawaida huleta mwono safi wa taswira mbalimbali juu ya retina
Retina
Mwono Safi
Jicho lenye mwono wa karibu ni refu mno hivi kwamba taswira hazifiki kwenye retina
Retina
Mwona wa kiwikiwi
Kigezo cha mikato minane ya nusu-kipenyo huifanya konea iwe tambarare kidogo
Jicho, baada ya upasuaji wa Keratotomia ya Nusu-Kipenyo, huwezesha mwono uliokaziwa uangalifu uifikie retina, likifanya kuwe na mwono safi
Retina
Mwono safi
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 22]
The Complete Encyclopedia of Illustration/J. G. Heck